MWIMBAJI mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Mwanahawa Ally amesema kwa sasa hategemei kurudi katika kundi lake la Jahazi kutokana na mambo waliyomfanyia.
Amesema hivi sasa anaendelea na kazi yake ya uimbaji katika kundi la East African Melody la jijini Dar es Salaam na tayari amesharekodi kibao kinachoitwa 'Rabi nilinde na wenye nia mbaya'.
Mwanahawa aliyasema hayo juzi alipozungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa makala hii na kuongeza kuwa, hataki kuendelea kufanyakazi zake kwa kutegemea Jahazi.
Alisema yeye ni mwimbaji mzoefu na anayesifika ndani na nje ya nchi na kwamba kipaji chake ni cha kuzaliwa na si cha kutegemea kundi au mtu. Alisema uwezo alionao ndio uliomfikisha hapo alipo.
"Kwangu mimi Jahazi ni kama kundi la kawaida, siwezi kulipapatikia wala sina haja nalo, kipaji na uwezo nilionao unanitosha na unanifanya nitambe,"alisema mwanamama huyo mwenye umri unaokadiwa kuwa zaidi ya miaka 60.
"Nimeanza kazi hii ya uimbaji wakati hao waimbaji wa Jahazi hawajazaliwa na hadi sasa nipo kwenye fani na ninawika, siwezi kubembeleza mtu na wala sijaona cha kubembeleza," alisema gwiji huyo wa mipasho mwenye sauti ya kuvutia.
Alisema baada ya kujiondoa Jahazi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kutoelewana na baadhi ya waimbaji pamoja na uongozi wa kundi hilo, amerudi katika kundi la East African Melody, ambako anaimba kama kibarua.
Muimbaji huyo aliyewahi kutamba na wimbo wa 'Kinyago cha Mpapure' na kujipatia umaarufu mkubwa alisema, akiwa katika kundi hilo, anafanya shughuli zake bila kuingiliwa na mtu.
Alisema kutokana na uwezo mkubwa wa uimbaji alionao, hawezi kubabaishwa na kundi lolote na anajiamini kwamba anaweza kufanyakazi sehemu yoyote.
Mwimbaji huyo, mwenye umbo kubwa na sauti ya kuvutia alisema, hajafikiria kuachana na kazi ya uimbaji kwani ni sehemu ya maisha yake na anaipenda kuliko kazi nyingine yoyote.
"Bado sijafikiria siku ya kuacha kuimba, kazi hii ndio iliyoniweka mjini hadi sasa, ninaendesha familia yangu kwa kazi hii, kwa hiyo bado ninaiheshimu sana," alisema mwimbaji huyo, anayetamba na kibao cha 'Roho mbaya siyo mtaji' alichokiimba akiwa Jahazi.
Mkongwe huyo wa mipasho pia alisema hana mpango wa kuhamia katika kundi la Fiver Stars 'Watoto wa Bongo' hata kama ataombwa kujiunga na kundi hilo.
Alisema mawazo yake ameyaelekeza kwenye makundi makongwe, likiwemo Melody kutokana na kusheheni waimbaji wenye umri unaoendana naye.
"Hata nikiombwa niende Fiver Stars, siwezi kwenda kwa sasa, watanisumbua tu, kiwango changu hakiendani nao," alisema mwimbaji huyo aliyenusurika kufa katika ajali ya gari akiwa na kundi hilo hivi karibuni.
Ajali hiyo ilitokea Machi 21 mwaka huu baada ya basi dogo aina ya Toyota Coaster walilokuwa wakisafiria kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam, kulivaa lori lililokuwa limeegeshwa kando mwa barabara na baadae kupinduka na kusababisha vifo vya wasanii 13 wa kundi la Fiver Stars, akiwemo mwimbaji nyota wa kundi hilo Issa Kijoti.
Ajali hiyo ilitokea saa 2.30 usiku, ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, umbali wa kilomita sita kutoka lango kuu la kuingia hifadhini, ambapo wasanii wengine sita waliokuwa kwenye gari hilo walijeruhiwa.
Mwanahawa aliambatana na kundi hilo kama mwimbaji mwalikwa na katika ajali hiyo, aliumia mkono na kupelekwa Kenya kwa matibabu.
Akizungumzia afya yake baada ya ajali hiyo, Mwanahawa alisema anaendelea vizuri na anafanya shughuli zake kama kawaida.
Alisema katika maisha yake hawezi kuisahau ajali hiyo, na ndio kubwa aliyowahi kukumbana nayo tangu kuzaliwa.
"Itachukua muda mrefu kuisahau ajali kama ile ambayo ilipoteza roho za wasanii wezewtu 13 kwa mpigo, ninamuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu pahala pema peponi Amina," alisema.
No comments:
Post a Comment