MOJA ya matatizo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya muziki wa taarab hapa nchini ni kuwepo kwa chuki, uhasama na kupigana vijembe miongoni mwa wasanii wa fani hiyo.
Matatizo hayo kwa kiasi kikubwa yamesababisha wanamuziki wengi washindwe kupiga hatua mbele kimaendeleo, badala yake huishia njiani.
Hali hiyo imesabisha waimbaji wengi wa muziki huo waliowahi kutamba hapa nchini miaka ya nyuma hivi sasa kutoonekana tena kwenye tasinia hiyo.
Mbali na kutoweka kwa baadhi ya wasanii, matatizo hayo yamesababisha soko la muziki huo kushuka kadri siku zinavyosonga mbele. Umaarufu wa wasanii wa muziki huo umekuwa ukibaki na kuishia hapa hapa nchini.
Hali hiyo imeonekana kumgusa na kumkera sana mkongwe wa muziki huo nchini, Khadija Omar Kopa, ambaye ameeleza kinagaubaka sababu zinazochangia kuzorota kwa maendeleo ya muziki huo.
“Hakuna kingine zaidi ya waimbani kujengeana chuki, majungu na kupigana vijembe,”alisema Khadija wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Ladha za Pwani, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha C2C.
Khadija alisema katika siku za hivi karibuni, kumezuka baadhi ya waimbaji, ambao wamekuwa wakipika majungu kwa wenzao kwa lengo la kuwadhoofisha, hali inayorudisha nyuma maendeleo na maudhui ya muziki huo.
Mwanamama huyo aliyejengeka kimwili alisema, lengo la muziki wa taarab ni kuelimisha, kufurahisha na kutoa ujumbe kwa jamii na si kujengeana chuki, fitina na majungu kama ilivyozoeleka hivi sasa.
Mkongwe huyo wa mipasho aliyewahi kujizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchini alisema, kinachoshangaza ni kwamba tabia hiyo hufanywa na waimbaji chipukizi na baadhi ya vikundi vilivyoibuka hivi karibuni.
"Nawasikitikia sana hawa waimbaji chipukizi kwa kujiingiza kwenye matatizo. Badala ya kuendeleza vipaji vyao, wao wanaendeleza malumbano," alisema.
Mwimbaji huyo mwenye macho yenye mvuto na sauti ya kubembeleza alisema binafsi ameshangazwa na kukerwa zaidi na kikundi cha taarab cha Jahazi Modern kutokana na vitendo wanavyomfanyia.
Alisema baadhi ya waimbaji na viongozi wa kundi hilo wamejenga chuki za waziwazi dhidi yake, bila sababu yoyote, hali inayomweka kwenye wakati mgumu.
Khadija alisema mara kadhaa anapoalikwa kufanya maonyesho kwa kushirikiana na kundi hilo, viongozi na wasanii wake humfanyia vituko vya kila aina, ambavyo humfanya wakati mwingine ashindwe kuimba.
"Mara kwa mara ninapoalikwa kuimba pamoja na Jahazi, huwa sipewi ushirikiano. Hunifanyia vituko vingi sana,”alisema.
Mkongwe huyo wa taarab, aliyeanza kung’ara akiwa katika kundi la Culture la Zanzibar, alisema binafsi hana bifu na uongozi ama msanii yeyote wa kundi hilo na kwamba anawaheshimu.
Gwiji huyo wa kundi la taarab la Tanzania One Theatre (TOT Plus), anayetamba na wimbo wa Top in Town alisema, kutokana na vituko anavyofanyiwa na uongozi wa kundi hilo, analiona kama vile limeamua kumdhalilisha na kumvunjia heshima.
Akitoa mfano alisema, katika tamasha la Mitikisiko ya Pwani lililofanyika mwishoni mwa mwaka jana katika ukumbi wa Daimond Jubilee, Dar es Salaam, alilazimika kuimba kwa tabu baada ya Jahazi kuondoa stejini baadhi vyombo vyao.
Kwa mujibu wa Khadija, kuna siku alikodiwa na mfanyabiashara Abbas Shentemba kuimba akiwa na waimbaji wengine pamoja na kundi la Jahazi, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kuwekewa ngumu na viongozi wa kundi hilo.
"Nakumbuka nilialikwa pamoja waimbji wengi, akiwemo Mohamed Iliyas na Afua Suleiman, lakini sikuweza kuimba kutokana na kubaniwa na uongozi wa Jahazi na kila nilipokuwa namkumbusha msimamizi wa onyesho hilo, alinijibu kwa kejeli,”alisema.
"Alianza kupanda jukwaani Afua, wakati anapanda Mohamed Iliyas, nilimtuma mpiga kinanda mmoja wa Jahazi akamwambie yule msimamizi kwamba akiteremka Iliyas nipande mimi, lakini wakampa majibu ya kebehi,”aliongeza.
Akisimulia zaidi mkasa huo, nguli huyo wa mipasho alisema, siku hiyo alipata taarifa mapema kwamba hawezi kuimba na alimfuata aliyemkodi na kumuuliza, lakini alimpa majibu kwamba lazima aimbe.
Alisema baada ya Iliyas kuteremka stejini, alipanda Mzee Yusuf na kuanza kuimba na hapo ndipo alipoamini maneno aliyoambiwa mapema kwamba hawezi kuimba siku hiyo.
“Baada ya Mzee Yusuf kupanda stejini, nilimfuata aliyenialika na kumuaga na yeye akakubali, kwa maana hiyo niliondoka bila kuimba,”alisema Khadija.
"Mimi binafsi ni mtu wa watu, kwa hiyo naomba kama Jahazi nimewakosea kitu, wanambie ili niwaombe radhi na mimi kama wamenikosea waniombe radhi,”aliongeza.
"Namheshimu kila mtu, sijawahi kugombana na yeyote, naona Jahazi wanajisumbua kwa sababu kwangu ni watoto wadogo sana," alisema.
Mkongwe huyo wa mipasho amewatahadharisha waimbaji chipukizi kwa kuwataka wasibweteke na kuvamia mambo yasiyowahusu badala yake waonyeshe vipaji vyao.Alisema waimbaji wengi chipukizi wanalewa sifa na kusahau wajibu wao.
Khadija, ambaye alizaliwa miaka 47 iliyopita katika mtaa wa Makadara, Zanzibar amewahi kuimba pia kwenye vikundi vya East African Melody na Muungano.
No comments:
Post a Comment