KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, December 28, 2012

JAHAZI YAPAGAWISHA MASHABIKI USIKU WA DAR LIVE


Mzee Yusuf akiongea na mashabiki wake.
Bi. Leila Rashid akiendeleza makamuzi.
...Khadija Yusuf kazini.
Mwimbaji wa Jahazi Modern Taarab, Fatma Mahmoud 'Mcharuko' akiwapa raha mashabiki.

Sehemu ya nyomi iliyotia timu mahali hapo.
Wapenzi wa taarab wakijiachia kwa raha zao na Jahazi.
Mzee Yusuf akizidi kukoleza burudani ndani ya Dar Live.

Thursday, December 27, 2012

KHADIJA KOPA APAGAWISHA MASHABIKI KIVULE
Na Peter Mwenda
MALKIA wa Mipasho nchini, Khadija Kopa na kundi lake cha Tanzania One Theatre (TOT)leo kitatoa shoo kabambe kusherekea sikukuu ya Krismas kwa wakazi wa Kata ya Kivule, Ilala kusherekea sikukuu ya Krismas kwenye ukumbi wa Vegetable Garden Pub.
Akizungumza jana, Kopa alisema kikundi hicho ambacho kitamba na nyimbo kemkem za taarab zinazotingisha katika miundoko ya Pwani ukiwemo Full Stop, Stop in Town na Mjini Chuo Kikuu ameahidi kukonga nyoyo za mashabiki wake katika eneo hilo kwenye sikukuu hiyo.
Alisema TOT taarab imesheheni kila idara ikiwa na wanamuziki wenye uwezo mkubwa wa kupiga taarab yenye mahadhi yanayokubalika akiwepo mkongwe Abdul Misambano, Mwanamtama Amir, Ali Star, Rukia Juma na Kopa Junior anayeimba nyimbo za Omar Kopa.
Mkurugenzi wa Vegetable Garden Pub, Anicety Mkwaya alisema maandalizi ya burudani hiyo imekamilika na zawadi zitatolewa kwa wale watakacheza taarab vizuri na watakaovaa vizuri.
Alisema burudani katika ukumbi huo zinaendelea ambako Januari 29 bendi ya Msondo Ngoma itatoa burudami katika ukumbi huo

Friday, December 21, 2012

ALBAMU MPYA YA JAHAZI KUZINDULIWA DESEMBA 30KIKUNDI cha taarab cha Jahazi kinatarajia kupakua albamu mpya ya Wasiwasi wako katika onyesho litakalofanyika Desemba 30 mwaka huu kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.
Akizungumza na blogu ya rusha roho leo, kiongozi wa kundi hilo, Mzee Yusuph amesema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya uzinduzi huo yameshakamilika.
Kwa mujibu wa Mzee, albamu hiyo itakuwa na nyimbo sita, ambazo amejigamba kuwa zote zitakuwa moto wa kuotea mbali.
Mzee alisema tayari nyimbo zote sita zimeshakamilisha na baadhi zimeshaanza kupigwa na kusikika kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Wasiwasi wako aliouimba yeye mwenyewe, Kazi mnayo ulioimbwa na Ahmed Ally  na Sitaki Shari ulioimbwa na mahabuba wake, Leila Rashid.
Alizitaja nyimbo nyingine kuwa ni Nipe Stara ulioimbwa na Rahma Machuppa, Hata bado hamjanuna ulioimbwa na Fatma Ally na Mambo bado ulioimbwa na Khadija Yussuf.
Mzee alisema amepania kufanya mabadiliko makubwa kwenye muziki wa taarab ili kuwapa mashabiki ladha tofauti badala ya ile waliyoizoea.
"Sisi kama Jahazi tunapenda tufanye kile kitu mashabiki wanapenda, hivyo tunawaahidi mambo mapya kabisa katika albamu yetu hii mpya,"alisema.
Alisema wakati wa onyesho hilo, wanatarajia kuuza CD na DVD za albamu hiyo kwa mashabiki ili wakapate starehe zaidi majumbani kwao.
Albamu hiyo itakuwa ya tisa tangu kundi la Jahazi lilipoanzishwa mwaka 2006. Albamu zingine zilizopita za kundi hilo ni Tupendane wabaya waulizane, Wagombanao ndio wapatanao, Mpenzi chokolate, Daktari wa mapenzi, Two in one, VIP na My Valentine.

Monday, December 17, 2012

THABITI ABDUL AJA NA HABIBIHUWEZI kuamini, lakini ndivyo ilivyo. Baada ya kutamba katika utunzi na upapasaji kinanda kwenye nyimbo nyingi za taarab, hatimaye mwanamuziki Thabiti Abdul ameamua kujitosa kwenye uimbaji.
Mwanamuziki huyo, ambaye pia ni mahiri katika muziki wa dansi, ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Habibi.
Thabiti ameimba kibao hicho kwa kushirikiana na baadhi ya wasanii wa kundi la Mashauzi Classic, ambalo yeye ni miongoni mwa wakurugenzi wake.
Mpiga kinanda huyo amekiimba kibao hicho kwa umahiri mkubwa, akimlalamikia kimwana, ambaye amekuwa akimtesa kimapenzi.
Wakati Thabiti akijitosa kwenye uimbaji taarab, mwimbaji mkongwe wa fani hiyo, Ally Hemed Star ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Ni wewe.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ally Star kuibuka na kibao cha taarab baada ya kuwa kimya kwa takriban miaka miwili.

MASIKINI KHADIJA YUSSUF, AANGUA KILIO CHA UCHUNGU. KISA? WIFIYE LEILA RASHID!


MWIMBAJI nyota wa taarab wa kikundi cha Jahazi, Khadija Yussuf mwishoni mwa wiki iliyopita aliangua kilio wakati alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mitikisiko ya Pwani kilichorushwa hewani
na kituo cha ITV.
Sababu kubwa iliyomfanya Khadija aangue kilio ni kuzuka kwa tofauti kubwa kati yake na kaka yake, Mzee Yussuf, ambaye ndiye mkurugenzi wa kikundi hicho.
Mtangazaji wa kipindi hicho alimuuliza Khadija ni kitu kipi kinachomkera katika maisha yake. Naye bila kutafakari kwa muda mrefu alijibu kuwa, ni kile kitendo cha mtu kutoka aendako na kwenda kumzushia maneno ya uongo kwa Mzee.
"Kinachoniuma zaidi ni kwamba afadhali hayo maneno ningekuwa nimeyasema, lakini sijafanya hivyo.
Hawa watu wanapaswa kutambua kwamba kuna Mungu na mimi na Mzee Yussuf tumezaliwa baba mmoja mama mmoja, atakapozikwa Mzee Yussuf ndipo nitakapozikwa mimi,"alisema Khadija huku machozi yakianza kumlengalenga.
"Kusema kweli maisha ninayoishi na Mzee Yussuf hivi sasa ni tofauti na huko nyuma tulikotoka. Inaniuma sana,"alisema Khadija na kuangua kilio kikali, ambacho kilisababisha mtangazaji wa kipindi hicho naye machozi kumlenga.
Mapema Khadija alisema kuna kikundi cha watu ndani ya Jahazi, ambacho kimekuwa kikimchonganisha yeye na wifi yake, Leila Rashid, ambaye ni mke wa pili wa Mzee.
Alisema watu hao wamekuwa wakipeleka maneno ya umbeya kwa Leila wakidai kuwa yeye ndiye ameyasema na vivyo hivyo wamekuwa wakija kwake na kumweleza maneno kama hayo.
"Kuna wakati Leila amekuwa akinitumia meseji zenye maneno machafu. Ninapomjibu anakasirika. Sielewi tunachogombea ni kipi,"alisema Khadija.
"Binafsi sina tatizo na Leila na sioni kwa nini tugombane. Sielewi na ninashangaa. Lakini hii yote ni kwa sababu kuna watu ndani ya Jahazi wanaotuchonganisha kwa makusudi,"aliongeza.
Khadija alisema kwa sasa anajiandaa kuibuka na kibao chake kipya kitakachojulikana kwa jina la Na bado. Alisema kibao hicho kitazinduliwa katika onyesho maalumu litakalofanyika Desemba 30 mwaka huu.

Sunday, December 9, 2012

RAIS KIKWETE AMTUNIKIA NISHANI BI KIDUDE
RAIS Jakaya Kikwete amewatunukia nishani ya heshima ya Jamhuri ya Muungano wanamuziki watatu, msanii mmoja wa maigizo na mwanariadha mkongwe.
Wasanii na wanamichezo hao wamepewa tuzo hizo leo jioni katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.
Utoaji wa nishani hizo ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za miaka 51 ya uhuru wa Tanzania Bara, zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Wasanii na wanamichezo waliopewa nishani hizo ni kiongozi wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo, kiongozi wa zamani wa bendi ya Dar es Salaam International, marehemu Marijani Rajabu na mwimbaji mkongwe wa taarab, Fatuma Baraka 'Bi Kidude'.
Wengine ni aliyekuwa msanii maarufu wa maigizo na filamu nchini, marehemu Fundi Saidi 'Mzee Kipara' na mwanariadha mkongwe, John Steven Akwari.
Gurumo, Bi Kidude na Akwari walihudhuria hafla hiyo na kuvishwa nishani zao na Rais Kikwete wakati nishani za Marijani na Mzee Kipara zilipokelewa na watoto wao.
Nishani ya sanaa na michezo, hutolewa kwa wasanii na wanamichezo mashuhuri, ambao kazi zao za sanaa au michezo zimeipatia sifa kubwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bi Kidude hakuweza kwenda eneo la kupokea nishani kutokana na hali ya afya yake kutokuwa nzuri. Ilibidi Rais Kikwete amfuate mahali alipokuwa ameketi na kumtunukia nishani yake.
Bi Kidude, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka zaidi ya 100 ni mwimbaji taarbab mkongwe aliyedumu kwenye fani hiyo kwa zaidi ya miaka 50. Ni msanii pekee wa taarab mwenye sifa zilizotukuka kutokana na ukongwe wake na umahiri wake katika kuimba taarab.
Gurumo alianza muziki 1960 na kushiriki katika bendi mbalimbali kama vile NUTA, JUWATA, OTTU, Atomic Jacc, Kiko Kids, Jamhuri Jazz, Kilwa Jazz, Rufiji Jazz, Mlimani Park, Msondo Ngoma. Ametunga nyimbo nyingi zinazoelimisha jamii kuhusu kuheshimu na kufanyakazi kwa juhudi na maarifa, kulinda uhuru wa nchi, kudumisha usawa, haki na amani na kuwaasa wazazi kutimiza wajibu wao kwa kulea watoto na vijana kutimiza wajibu wao.
Marehemu Marijani, maarufu kama Jabali la Muziki, alifariki dunia mwaka 1995. Alitoa mchango mkubwa katika tasnia ya muziki, alishiriki kutunga na kurekodi nyimbo zaidi ya 103, ambazo zilirekodiwa RTD, nyimbo zake zilikuwa na mafunzo mengi kwa jamii na zinaendelea kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini.
Mzee Kipara mwaka 1962 alijiunga na waigizaji wa Redio Tanzania, pia ameshiriki maigizo na tamthiria nyingi za kwenye televisheni kama vile Hujafa hujaumbifa, Fukuto, Radi, Gharika, Tufani na Tetemo.
Mzee Akwari aliweka historia ya pekee nchini mwaka 1968 pale aliposhiriki mbio za marathoni za Olimpiki na kuumia goti na kutoka malengelenge, lakini aliushangaza ulimwengu alipoendelea na kumaliza mbio hizo. Alipoulizwa, alisema 'mimi sikutumwa kuja kuanza mbio, nimetumwa kumaliza mbio'. Maneno hayo yamekuwa yakitumika kama mifano duniani.