KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, January 18, 2013

LAMANIA WA EAST AFRICAN MELODY AFARIKI DUNIA


MMOJA wa viongozi wa kikundi cha muziki wa taarab cha East African Melody, Lamania Shaaban amefariki dunia.

Lamania alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita akiwa usingizini, nyumbani kwake Mbagala, Dar es Salaam.

Mazishi ya Lamania yalifanyika juzi saa saba mchana Tandika kwa Maguruwe baada ya kuswaliwa katika msikiti wa Sheikh Kilembe.

Mkurugenzi wa East African Melody, Haji Mohamed alisema marehemu Lamania alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupooza kwa zaidi ya miaka mitatu.

Haji alisema Lamania alikuwa nje ya jukwaa la muziki huo kutokana na kusumbuliwa na maradhi hayo kwa muda mrefu.

Enzi za uhai wake, Lamania alikuwa mtunzi wa nyimbo na mpiga gita hodari katika nyimbo za taarab za East African Melody, kikundi kilichoanzishwa miaka ya 1992 huko Dubai katika Falme za Kiarabu.

Kwa mujibu wa Haji, marehemu Lamania alijiunga na East African Melody mwaka 1994 wakati kikundi hicho bado kikiwa Falme za Kiarabu.

Hadi mauti yalipomkuta, Lamania alikuwa mkurugenzi wa muziki wa kikundi hicho, ambacho makao makuu yake ni Mlandege, Zanzibar.

Lamania atakumbukwa kwa tungo zake mwanana, ambazo zilikipatia umaarufu mkubwa kikundi hicho na kukifanya kisiwe na mpinzani miaka ya 1990.

Miongoni mwa tungo zake, ambazo hadi sasa bado zinateka hisia za mashabiki wengi wa muziki huo ni pamoja na Tutabanana hapahapa, Utalijua Jiji, Wa Mungu uwazi, Mwanamke khulka, Nani zaidi, Viumbe wazito, Mama shughuli, Wasio haya wana mji wao.

Haji alisema kifo cha Lamania ni pigo kubwa kwa kikundi chake kutokana na utaalamu aliokuwa nao katika kutunga nyimbo, kupiga ala na pia kushirikiana vyema na wenzake.

"Tumempoteza msanii mzuri, ambaye sio siri kwamba alikuwa nguzo kuu ya utunzi katika kikundi chetu. Iliyobaki ni kumshukuru Mungu na kumuomba ampe malazi mema kwa sababu kifo ni njia ya kila mtu,"alisema.

Marehemu ameacha mke na watoto wanne.

Tuesday, January 15, 2013

KIKUNDI CHA TAIFA CHA TAARAB CHATIA FORA SHEREHE ZA MAPINDUZI ZANZIBAR

KIKUNDI cha Taifa cha Taarab cha Zanzibar juzi usiku kilitia fora kwa kutoa burdani ya aina yake ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za sherehe za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutokana na nyimbo zake zilizoisisimua hadhira.

Onyesho hilo la taarab lilifanyika katika ukumbi wa Salama Bwawani, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na mkewe, Mwanamwema Shein na viongozi wengine mbali mbali wa serikali na vyama vya siasa.

Katika onyesho hilo, kikundi hicho kilitumbuiza kwa nyimbo mbali mbali zilizoimbwa na waimbaji wake mahiri na wenye sauti za kumtoa nyoka pangoni huku wapiga ala wakionyesha uhodari wao katika kupiga ala za kiasili.

Kikundi hicho kilianza onyesho hilo kwa wimbo wa 'Rais tunakupenda' ulioimbwa kwa pamoja na Asha Ali kutoka Pemba na Sihaba Juma kutoka Unguja.

Wimbo huo ulikuwa ukimpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake katika kusimamia utawala bora na mikakati yake ya kuendeleza kiliko cha kisasa na pia kuongeza bei ya karafuu.

Wimbo huo pia ulimpongeza Dk. Shein kwa kuendelea kusimamia vyema amani na utulivu uliopo nchini, ambao ndiyo muhimili mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Nyimbo zingine za kikundi hicho zilizotia fora katika onyesho hilo ni ‘Siri ya Moyoni’, ulioimbwa na Fauzia Abdalla, Chaguo ulioimbwa na Saada Mohammed, Mpewa hapokonyeki ulioimbwa na Mtumwa Mbarouk na ’Sema’, ulioimbwa na Fatma Issa.

Mwimbaji mwingine aliyetia fora katika onyesho hilo alikuwa Makame Faki, maarufu kwa jina la Sauti ya Zege, ambaye upigaji wake wa kinanda ulitia fora na kuwafanya watu waliohudhuria waliwazike.

Mkurugenzi wa Kikundi hicho, Iddi Suwedi naye alitia fora baada ya kuimba wimbo wake wa Kinacho wasumbueni, uliotungwa na Mohammed Ahmed wakati Hilda Mohamed alitia fora aliposhuka na kibao chake cha Ninavyokupenda wakati Ali Masoud aliteka hadhira kwa wimbo wake wa Hakika nakupenda.

Monday, January 7, 2013

MZEE YUSSUF, KHADIJA NI VILIO, MASHABIKI WASHIKWA NA SIMANZI

Richard Bukos na Shakoor Jongo
Ndugu wanapogombana shika jembe ukalime, wakipatana nenda ukavune, ngano hiyo ilidhihirika kwa kaka na dada, Mzee Yusuf ‘Mfalme’ na Khadija Yusuf ambao mwaka jana walikosana kiasi cha kunyimana salamu na kusemeana mbovu kwenye vyombo vya habari.

Mzee na Khadija, Ijumaa iliyopita kwenye onesho la uzinduzi wa albamu mpya ya Kundi la Jahazi Modern Taarab, My Valentine, waliangua vilio vilivyoambatana na machozi, walipokuwa wakiimba pamoja wimbo “Undugu Hazina Yetu.”

Ndugu hao wa damu walipokuwa wanaangusha vilio, mashabiki ambao walihudhuria onesho hilo kwenye Ukumbi wa PTA, Temeke, Dar, walitafsiri kuwa mashairi ya wimbo huo yaliwachoma, hivyo kuwakumbusha walipokuwa katika ‘bifu’ zito.

Mwanzoni mwa mwaka jana, Khadija alilikacha Kundi la Jahazi linalomilikiwa na Mzee, kisha kwenda kushiriki kuanzisha Five Stars Modern Taarab na akiwa huko, alidaiwa kumpiga madongo mengi kaka yake.

Katika tukio la Ijumaa, aliyeanza kumwaga machozi ni Khadija kabla ya Mzee kuguswa, naye kuangusha kilio chenye ujazo wa kutosha.
Wakati wawili hao wakilia, baadhi ya watu wa karibu walifika kuwasaidia ili waendelee kuimba.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Khadija ambaye machozi yalikuwa mengi kutokana na kuzidiwa na hisia za uchungu, hivyo watu hao kulazimika kumuondoa ukumbini haraka.

Khadija, alipotolewa ukumbini, alipandishwa kwenye gari ambalo liliondoka naye, kabla ya kumrejesha baada ya nusu saa kuendelea kuwajibika jukwaani.
Mwanamuziki huyo, hivi karibuni alirejea Jahazi baada ya kupata suluhu na Mzee, hivyo kuliacha Kundi la Five Stars Taarab kwenye mataa.

Awali, Mzee ndiye aliyeanza kupanda jukwaani, akamkaribisha Khadija na kuanza kuimba Undugu Hazina Yetu lakini wimbo haukufika katikati, wawili hao walikumbatiana kabla ya kuangusha vilio.

Wakizungumza ukumbini hapo, Khadija na Mzee walisema kuwa safari ndefu ya maisha yao iliwakumbusha mbali na kuwataka walimwengu kutoingilia ugomvi wao, kwani wao ni ndugu na hata wakitofautiana, mwisho wa siku wataelewana.

Tukio la Mzee na Khadija likiwa halijapoa, ukumbi wa PTA uliingia kwenye mshikemshike wa aina yake baada ya wanenguaji wawili wa Kundi la Kanga Moja kucharukiana na kupeana mkong’oto.

Tifu la wanenguaji hao ambapo mmoja wao tulimnasa kwa jina la Rehema, lilizua patashika, hasa baada ya kuwa wagumu kuamulika.
Juhudi za walinzi na waratibu wa ‘shoo’ hiyo ya Jahazi, zilisaidia kuwatuliza wanenguaji hao, lakini baada ya kuamuliwa, Rehema aliangusha kilio huku akijiapiza kulipa kisasi.

(Habari, Picha kwa hisani ya gazeti la Amani)

Tuesday, January 1, 2013

T -MOTO YAZINDUA ALBAMU YA DOMO LA UDAKU KWA STAILI YA AINA YAKE

Mashabiki wa Dar Live wakiwa na furaha ya kuuona mwaka mpya na burudani ya taarab.
Umati ukirindima kwa burudani baada ya kutangaziwa kuwa mwaka mpya 2013 umeingia
Kundi la Kings Modern Taarab likikonga nyoyo za mashabiki kabla ya kuwapisha T Moto.
Kundi la T Moto likizindua albam yake ya ‘Domo la Udaku’.
Mkurugenzi wa T Moto, Amini Salmini (kushoto) na muimbaji wa kundi hilo, Jokha Kassim (aliyevalia
shela kama bi harusi) wakiingia jukwaani kimadaha.
Wapambe walioshika shela kwa nyuma wakinogesha hafla hiyo.
Jokha akikamua.
Wacheza kiduku nao wakimrusha roho ‘bi harusi’ kwa pembeni.
Uzinduzi wa albam ukiendelea.
 Ni shangwe tupu ndani ya Dar Live.
 ‘Bi. Harusi’ akiondolewa jukwaani baada ya kumaliza kufanya makamuzi.
Muimbaji mpya wa T Moto aliyetokea Kings Modern Taarab, Ustaadh Issa Ally, akikamua.