KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, January 18, 2013

LAMANIA WA EAST AFRICAN MELODY AFARIKI DUNIA


MMOJA wa viongozi wa kikundi cha muziki wa taarab cha East African Melody, Lamania Shaaban amefariki dunia.

Lamania alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita akiwa usingizini, nyumbani kwake Mbagala, Dar es Salaam.

Mazishi ya Lamania yalifanyika juzi saa saba mchana Tandika kwa Maguruwe baada ya kuswaliwa katika msikiti wa Sheikh Kilembe.

Mkurugenzi wa East African Melody, Haji Mohamed alisema marehemu Lamania alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupooza kwa zaidi ya miaka mitatu.

Haji alisema Lamania alikuwa nje ya jukwaa la muziki huo kutokana na kusumbuliwa na maradhi hayo kwa muda mrefu.

Enzi za uhai wake, Lamania alikuwa mtunzi wa nyimbo na mpiga gita hodari katika nyimbo za taarab za East African Melody, kikundi kilichoanzishwa miaka ya 1992 huko Dubai katika Falme za Kiarabu.

Kwa mujibu wa Haji, marehemu Lamania alijiunga na East African Melody mwaka 1994 wakati kikundi hicho bado kikiwa Falme za Kiarabu.

Hadi mauti yalipomkuta, Lamania alikuwa mkurugenzi wa muziki wa kikundi hicho, ambacho makao makuu yake ni Mlandege, Zanzibar.

Lamania atakumbukwa kwa tungo zake mwanana, ambazo zilikipatia umaarufu mkubwa kikundi hicho na kukifanya kisiwe na mpinzani miaka ya 1990.

Miongoni mwa tungo zake, ambazo hadi sasa bado zinateka hisia za mashabiki wengi wa muziki huo ni pamoja na Tutabanana hapahapa, Utalijua Jiji, Wa Mungu uwazi, Mwanamke khulka, Nani zaidi, Viumbe wazito, Mama shughuli, Wasio haya wana mji wao.

Haji alisema kifo cha Lamania ni pigo kubwa kwa kikundi chake kutokana na utaalamu aliokuwa nao katika kutunga nyimbo, kupiga ala na pia kushirikiana vyema na wenzake.

"Tumempoteza msanii mzuri, ambaye sio siri kwamba alikuwa nguzo kuu ya utunzi katika kikundi chetu. Iliyobaki ni kumshukuru Mungu na kumuomba ampe malazi mema kwa sababu kifo ni njia ya kila mtu,"alisema.

Marehemu ameacha mke na watoto wanne.

No comments:

Post a Comment