KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Sunday, August 13, 2017

WASANII WANANE JAHAZI WATIMKIA WAKALI WAO MODERN TALADANCE

THABITI Abdul
KHADIJA Yussuf
AISHA Vuvuzela
JUMANNE Ulaya
RAHMA Machupa

HATIMAYE kikundi cha muziki wa taarab cha Jahazi, kimesambaratika baada ya wasanii wake zaidi ya wanane, kuhama na kujiunga na kikundi cha Wakali Wao Modern Taladance.

Habari kutoka ndani ya Jahazi zimeeleza kuwa, uamuzi wa wasanii hao kuhama, umelenga kuheshimu matakwa ya kiongozi wa zamani wa kundi hilo, Mzee Yussuf, kutaka jina hilo lisiendelee kutumika.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mzee Yussuf aliwaeleza wasanii wa kundi hilo kuwa, kuendelea kutumia jina la Jahazi ni sawa na kuendelea kumshirikisha na dhambi wakati alishatangaza kuachana na muziki wa taarab na kumrudia Mungu.

Miongoni mwa wasanii wa Jahazi, waliojiunga na Wakali Wao Modern Taladance ni pamoja na Khadija Yussuf, Rahma Machupa, Aisha Vuvuzela, Mwasiti, Miriam, Mgeni Kisoda, Jumanne Ulaya na Mohamed Ali 'Mtoto Pori'.

Akihojiwa na Uhuru mwishoni mwa wiki, Khadija alikiri kuondoka kwake Jahazi, akiwa amefuatana na wasanii wengine kadhaa.  Alisema wamefikia uamuzi huo kwa sababu kuendelea kwao kuwepo Jahazi ni kuzidi kumpa dhambi kaka yake, Mzee Yussuf.

"Jahazi ilikuwa Mzee Yussuf. Kwa vile ameamua kumrudia Mungu, tuliona ni bora kikundi kivunjwe ili kuepuka kumshirikisha katika dhambi,"alisema.

Aliongeza: "Nimeondoka Jahazi na kijiji changu. Mfalme Mzee Yussuf alikuwa ndiye kila kitu. Ameondoka na sasa hakuna wa kuiongoza."

Khadija alisema hajutii uamuzi wake huo kwa sababu yeye na wenzake wanajiamini kikazi na watashirikiana vyema na wenzao waliowakuta Wakali Wao kuupaisha muziki wa taarab.

"Mashabiki wetu watarajie makubwa kutoka kwetu kwa sababu ukali wetu ni ule ule, hatujatetereka kimuziki,"alisisitiza mwanamama huyo, ambaye amewahi kuimbia vikundi vya East African Melody na Zanzibar Stars.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wakali Wao Modern Taladance, Thabiti Abdul, alithibitisha kuwepo kwa muungano kati ya vikundi hivyo viwili.

Thabiti alisema awali, uongozi uliokuwa umebaki Jahazi, baada ya Mzee Yussuf kuachana na muziki, ulimfuata na kumuomba ajiunge na kikundi hicho akiwa ndiye mkurugenzi mkuu.

"Lakini baada ya majadiliano ya muda mrefu kati yetu, ikaonekana ni vizuri wasanii waliokuwa Jahazi waje kwangu ili tuwe kitu kimoja kwa kuwa mwenye bendi yake alikuwa hataki jina hilo liendelee kutumika,"alisema.

Thabiti, ambaye ni mmoja wa wapiga kinanda maarufu nchini, akitokea bendi ya Twanga Pepeta International, alisema lengo la muungano wao, ambao wameuita kwa jina la 'Mbili kwa moja', ni kuendeleza muziki wa taarab.

"Niliukubali mpango huu kwa sababu baada ya Mzee Yussuf kujitoa, Jahazi ilikuwa kama imekufa. Japokuwa ilikuwa ikiendelea na maonyesho, haikuwa Jahazi iliyozoeleka,"alisema.

Thabiti alisema mikakati waliyonayo ni kuhakikisha Wakali Wao, kinakuwa kikundi bora na maarufu katika muziki wa taarab nchini kama ilivyokuwa Jahazi enzi za Mzee Yussuf.

"Hakuna kushindwa, tunataka tushinde. Lazima tufike kule ilikokuwa Jahazi,"alisisitiza msanii huyo, ambaye pia ni mtunzi mahiri wa nyimbo za muziki huo.

Kwa mujibu wa Thabiti, katika maonyesho yao, watakuwa wakiimba nyimbo zote za Jahazi, zilizoimbwa na wasanii waliopo kwenye kikundi hicho, akiwemo Khadija Yussuf.

Thabiti alisema kikundi pekee kilichokuwa kikimuumiza kichwa kilikuwa Jahazi, lakini kwa kuwa hakipo, haoni kikundi kingine kitakachomsumbua.

"Mimi na Mzee Yussuf ndio tuliokuwa tukisumbuana. Hata kwenye tuzo za wasanii bora wa muziki wa taarab, tulikuwa tukibadilishana kuzinyakua. Kwa hiyo naweza kusema kuwa, kwa sasa nimebaki peke yangu,"alisema.

Thabiti alisema kwa kuwapata wapiga ala mahiri, kina Mgeni Kisoda, Jumanne na waimbaji kina Khadija, Rahma Machupa, Mwasiti, Miriam na Mtoto Pori, anaamini Wakali Wao itakuwa kwenye matawi ya juu.

Naye Mtoto Pori alisema yeye na wasanii wengine wote kutoka Jahazi, waliojiunga na Wakali Wao, wamefanya hivyo kwa moyo safi, bila kushawishiwa na mtu.

"Tuliona kwa kuwa mwanzilishi wa kikundi hataki jina lake liendelee kutumika, tusiendelee kumbebesha dhambi. Tuliangalia upepo, tukaona ni bora tuondoke,"alisema mwimbaji huyo machachari.

Aliongeza: "Pia, tuliona hakuna anayependa kuwa masikini kwa sababu ni kitu kibaya. Unaamka asubuhi, hujui wapo pa kwenda."

Utambulisho wa wasanii hao wapya ndani ya Wakali Wao Modern Taladance, umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, kwenye ukumbi utakaotangazwa baadaye.


 

Sunday, June 25, 2017

EID MUBARAKA WASOMAJI WANGU WAPENZI WA BLOGU YA RUSHAROHO


EID MUBARAK



Mikono tupeane
Rehema tutakiane
Upendo tushikamane
Toba tuhimizane
Makosa tusameheane
Yarabi tupe baraka zako
Utukubalie swaumu zetu
Amina yarabi Amina

KHADIJA: SIKUKATAA KUMPA MKONO LEILA WAKATI WA MSIBA. ASEMA HUO NI UZUSHI, MZEE YUSSUF ASIMULIA KILICHOTOKEA



MWIMBAJI  nyota wa muziki wa taarab nchini, Khadija Yussuph, amekanusha madai kuwa alikataa kupeana mkono na mke mkubwa wa kaka yake, Leila Rashid wakati wa msiba wa mke mdogo, Chiku.

Khadija amesema madai hayo hayana msingi wowote kwa sababu asingeweza kufanya kitu kama hicho kwenye msiba na kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akihojiwa katika kipindi cha Ng'aring'ri, cha Clouds TV leo, Khadija alisema kifo cha wifi yake, Chiku, ambaye ni mke mdogo wa kaka yake, Mzee Yussuph kilimchanganya na kumpa uchungu mkubwa.

"Kumbuka kulikuwa na watu wengi na ulikuwa msiba, nisingeweza kukataa kupeana naye mkono. Ingekuwa kwenye harusi labda ingeweza kutokea, lakini sio kwenye msiba.

"Na mimi nilikuwa nimechanganyikiwa sana. Nakumbuka nilimuona kwa mbali wakati anafika, lakini sikumbuki kama alinifuata na kunipa mkono, sio kweli hata kidogo,"amesema Khadija, ambaye alikuwa akiimba kundi moja na kaka yake, Mzee Yussuph na wifi yake, Leila.

Khadija amewataka mashabiki wake wapuuze madai hayo kwa kuwa yamelenga kumchafua kwa vile bado anamtambua Leila kuwa ni mke halali wa kaka yake, ikiwa ni pamoja na kuzaa naye watoto wawili.

Aidha, amewataka mashabiki wa muziki huo kumuombea Mzee Yussuph awe na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu, ambacho mkewe amemuachia watoto wadogo wawili.

Chiku alifariki dunia wiki iliyopita baada ya kufanyiwa operesheni ya uzazi kwenye Hospitali ya Amana, Dar es Salaam. Mazishi yake yalifanyika kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Akizungumzia uamuzi wa Mzee Yussuph kuachana na muziki wa taarab na kumrudia Mungu, ikiwa ni pamoja na kwenda kuhiji Makka, Khadija alikiri kuwa anajisikia kupwaya kwa vile alizoea kuimba naye pamoja.

Alisema uamuzi huo wa Mzee Yussuph umemfanya ajihisi upweke kila anapojihusisha na muziki huo stejini kwa vile alimzoea kama kaka, kiongozi na msanii mwenzake.

Kwa upande wake, Mzee Yussuph alisema hana hakika iwapo Khadija alikataa kupeana mkono na Leila wakati wa msiba wa mkewe mdogo, Chiku.

Alisema kama ni kweli Khadija alifanya kitendo hicho ni kosa kubwa mbele ya Mungu, hivyo anamuombea msamaha kwake na kwa mashabiki wa muziki huo.

Hata hivyo, alisema katika siku za hivi karibuni, Khadija alikuwa na uhusiano mzuri na Leila, ikiwa ni pamoja na kuchati ama kuzungumza kwa simu, tofauti na miaka kadhaa iliyopita, ambapo hawakuwa wakielewana.

Kuhusu msiba wa mkewe mdogo Chiku, msanii huyo nyota wa zamani wa taarab alisema baada ya kupata taarifa za kifo chake, alichanganyikiwa kwa kuwa hakutarajia.

Alisema mara baada ya kupata taarifa hizo, alimpigia simu mkewe mkubwa, Leila ambaye naye alichanganyikiwa na kumuuliza iwapo anaruhusiwa kuhudhuria kwenye msiba.

Amesema maneno ambayo hawezi kuyasahau kutoka kwa Leila ni pale alipompa pole na kisha kutuma ujumbe mfupi kwenye simu ya mkononi ukisema 'Jamani Chiku, mbona mapema hivi.'

Sunday, June 18, 2017

MKE WA PILI WA MZEE YUSSUPH AFARIKI KWA UZAZI AMANA




Aliyekuwa mfalme wa muziki wa Taarab Alhaj Mzee Yusuf, amefiwa na mke wake wa pili, Chiku Khamis Tumbo.

Mzee Yusuf amenukuliwa katika moja ya vyombo vya habari leo akisema kuwa, mkewe alifariki jana kwenye Hospitali ya Amana, Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo wa zamani wa kundi la Jahazi, alisema alimpeleka mkewe Amana, jana saa 10 alasiri, kwa ajili ya kujifungua na kwa bahati mbaya opereshini (upasuaji) iliyofanywa jioni, haikwenda salama na ikampoteza mkewe na mtoto aliyezaliwa.

Mazishi ya Chiku yanatarajiwa kufanyika leo jioni kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam. Marehemu Chiku ameacha watoto wawili.

Wednesday, May 10, 2017

ALLY J AITOSA FIVE STARS NA KUREJEA JAHAZI MODERN TAARAB




KIONGOZI wa kundi la muziki wa taarab la Five Stars, Ally J, ameamua kuliacha kundi hilo na kujiunga na kundi lake la zamani la Jahazi.

Ally J, ambaye ni mmoja wa wapapasaji mahiri wa kinanda nchini, amesema uamuzi wake huo umelenga kukuza na kuendeleza fani ya taarab, ambayo imeanza kupwaya.

Msanii huyo alisema ni kweli kwamba, aliwahi kuapa huko nyuma kuwa hatarudi tena kwenye kundi la Jahazi, lakini kuwa na mkataba wa kufanya hivyo.

Alikiri kuwa uamuzi wa kiongozi wa zamani wa Jahazi, Mzee Yussuf, kuachana na taarab baada ya kurejea kutoka Hijja, Makka, umeudhoofisha muziki huo.

"Kwamba sitarajii kurudi Jahazi, yalikuwa maneno tu. Nilipoona wanahitaji mtu wa aina yangu na baada ya kunifuata, nilizungumza nao tukakubaliana,"alisema Ally J, ambaye pia ni mmoja wa watunzi mahiri wa muziki wa taarab nchini.

Mpiga kinanda huyo alisema yeye si mgeni katika kundi la Jahazi kwa vile aliwahi kulitumikia miaka ya nyuma, likiwa chini ya Mzee Yussuf na kwamba aliondoka kwa hiari yake bila kugombana na mtu yeyote.

Ally J alisema anamshukuru Mungu kwamba alipokelewa vizuri Jahazi na kwamba, kurejea kwake hakumaanisha kwamba kundi hilo halina wasanii wengine wazuri wa kiwango chake.

"Si kwamba Jahazi haina wapigaji wazuri, isipokuwa walitaka mtu anayeifahamu vyema mipigo ya Jahazi,"alisema Ally J.

Aliongeza kuwa binafsi anazo njia zake za kimuziki kama ilivyo kwa Jahazi na vikundi vingine vya taarab, lakini hilo haliwezi kumfanya ashindwe kwenda sambamba na kundi hilo kwa wakati huu.

Alisema iwapo ataamua kubadilisha mipigo ya kimuziki ya Jahazi na kuanzisha mipigo ya Five Stars Modern Taarab, atakuwa ameiondoa kwenye reli na kufanya kitu tofauti na kile walichokizoea.

"Mimi na wenzangu kina Jumanne Ulaya na wengine niliowakuta Jahazi, tutakaa na kuona tufanye nini ili kuliendeleza kundi hili kimuziki,"alisema Ally J.

Mtaalamu huyo wa kupapasa kinanda alisema, karibu nyimbo zote alizoshiriki kupiga ala hiyo alipokuwa Jahazi ni nzuri hivyo anaamini ataendelea kutumia ujuzi wake kufanya vizuri zaidi.

Hata hivyo, Ally J amekiri kuwa uamuzi wake wa kurejea Jahazi haukuwafurahisha wasanii na mashabiki wengi wa muziki huo kwa vile kila mmoja ana mtazamo wake.

"Jambo la muhimu ni kwamba nahitaji kufikiria, sio kufikiriwa. Haya ni maisha na maamuzi yangu. Hakuna mdau yeyote wa taarab aliyewahi kunisaidia matatizo yangu ya kimaisha. Tuache maneno maneno, tupige muziki. Tutengeneze nyimbo nzuri,"alisema.

Alisema tayari ameshatunga nyimbo mbili mpya ndani ya kundi la Jahazi, ambazo ni Nataka Jibu na Jicho la Mungu, zilizoimbwa na Mwasiti na Mosi Suleiman.

Alikiri kuwa amekuwa akikumbana na changamoto nyingi katika muziki huo, lakini amekuwa akijitahidi kukabiliana nazo kadri ya uwezo wake.

"Ninachokifanya kwa sasa ni kufikiria nitoe kitu gani kitakachokubalika kwa mashabiki. Hii ni kwa sababu Jahazi imeshatoa nyimbo nyingi nzuri, hivyo mashabiki kwa sasa wanatarajia kuona mambo mapya sio yale yale waliyoyazoea,"alisisitiza msanii huyo.

Pamoja na kujiengua katika kundi la Five Stars Modern Taarab, Ally J alisema kundi hilo bado lipo na litaendelea kufanya maonyesho yake kama ilivyokuwa zamani, japokuwa kwa sasa halina wasanii wa kudumu.

Alisema Five Stars badi ipo na itaendelea kuwepo, isipokuwa yeye ndiye hayupo. Alisema binafsi itakapotokea kundi hilo kupata mwaliko wa kufanya maonyesho, atakuwa akishiriki iwapo kundi lake la Jahazi halitakuwa na kazi siku hiyo.

Thursday, January 5, 2017

LEYLA: SIPENDI KUZUNGUMZA MAMBO YANAYOMUHUSU KHADIJA YUSSUF

MWIMBAJI nyota wa taarab wa kundi la Jahazi, Leyla Rashid, amesema kamwe katika maisha yake hapendi kuzungumza mambo yanayomuhusu Khadija Yussuf.

Leila, mke wa kiongozi wa zamani wa kundi hilo, Mzee Yussuf, amesema anashangazwa na kauli mbalimbali zinazotolewa na Khadija kuhusu ndoa yake.

Mwanamama huyo amesema mumewe hajawahi kumkataza kuimba taarab ama kumtishia kumuacha kama inavyodaiwa na Khadija.

Akizungumzia wimbo mpya wa Khadija, ambao unazungumzia ndoa yake na Mzee, Leyla alisema ameusikia lakini hawezi kuuzungumzia.

"Sina mpango wa kumpa mtu kiki (kumpa ujiko) na wala sifikirii. Najali mambo yangu,"amesema Leyla.

"Ninayemjua katika maisha yangu ni Mzee, sina haja na Khadija,"aliongeza.

Leyla alisema maelewano kati yake na mumewe yanaendelea vizuri na ndoa yao imezidi kuimarika kuliko ilivyokuwa awali.

Aidha, alisema suala la talaka siyo la ajabu kwa watu wenye ndoa na kwamba linaweza kumkuta mtu yeyote.