KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Monday, May 11, 2015

KHADIJA KOPA: NILIWAHI KUVUMISHIWA NIMEMUUA LEILA KHATIBU NA OMAR KOPA




WAKATI alipojiunga na kikundi cha taarab cha Tanzania One Theatre (TOT Plus), mwanzoni mwa miaka ya 1990, Khadija Omar Kopa, alionekana kuwa mwimbaji wa kawaida. Si mashabiki wengi wa muziki huo waliokuwa wakimfahamu.
Lakini kwa mashabiki wa taarab wa visiwa vya Zanzibar, jina la Khadija Kopa lilikuwa maarufu. Ni kutokana na uimbaji wake mahiri na sauti yake maridhawa, kupitia vibao vilivyompa sifa na umaarufu mkubwa, kama vile Kadandie, Daktari na Wahoi, alivyoviimba akiwa katika kikundi cha Culture.
Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyoufanya uongozi wa TOT Plus, kumfuata Khadija visiwani Zanzibar na kumuomba ajiunge na kikundi hicho ili kukipa sura na mwonekano mpya, tofauti na taarab iliyozoeleka Tanzania Bara.
Kwa umbo, Khadija Omar Kopa ni mnene. Rangi yake ni nyeusi yenye mng’ao. Uso wake hujawa na tabasamu muda wote utadhani hajui kitu kinachoitwa kukasirika.
Licha ya kuwa na umbile hilo, Khadija ni mwepesi wa kuunyonganyonga mwili wake atakavyo awapo stejini, akiimba nyimbo za muziki wa taarab. Sauti yake nayo ni maridhawa na yenye mvuto wa pekee.
Sifa hizo ndizo zilizomfanya mwanamama huyo apachikwe jina la ‘Malkia wa Mipasho’ nchini. Waliompa jina hilo hawakubahatisha, walitambua vyema kwamba uwezo wake katika fani hiyo ni mkubwa.
Akiwa TOT Plus mwaka 1992, Khadija ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa kundi hilo, alidhihirisha kwamba halikukosea kumfungia safari visiwani humo baada ya kuanza kung’ara kwa vibao kama ‘Tx mpenzi’, ‘Ngwinji’, ‘Wrong number’, ‘Mtie kamba mumeo’ na nyinginezo.
Hata hivyo, miaka miwili baadaye, Khadija alikorofishana na uongozi wa TOT Plus baada ya yeye na mwimbaji mwenzake, Othman Soud kuamua kuondoka kinyemela na kwenda Dubai, ambako walishiriki kuanzisha kundi la East African Melody.
Baada ya kurejea nchini kutoka Dubai, mwanamama huyo alilazimika kujiunga na kikundi cha Muungano Cultural Troupe kwa vile uongozi wa TOT uligoma kumpokea.
Kujiunga kwa Khadija na Othman katika kikundi cha Muungano, kulisababisha kuwepo kwa ushindani mkali kati ya vikundi hivyo viwili, ambavyo vilifanya maonyesho kadhaa ya pamoja kwa ajili ya kuonyeshana nani mkali.
Akiwa Muungano, Khadija aling’ara kwa vibao vyake murua kama vile ‘Homa ya Jiji’, ‘Kiduhushi’ na ‘Umeishiwa’. Pia kulizuka ushindani mkali kati yake na marehemu Nasma Khamis ‘Kidogo’, ambaye alichukuliwa na TOT kutoka Culture kwa lengo la kuziba pengo lake.
Akizungumza mjini Dar es Salaam hivi karibuni, Khadija alikiri kwamba asingeweza kufika mahali alipo bila ya kupata msaada mkubwa kutoka kwa Othman.
“Othman ndiye aliyekuwa mtunzi wa nyimbo zote nilizoimba tangu nikiwa Culture na TOT. Hata TOT waliponifuata Zanzibar, niliwaambia kwamba nisingeweza kujiunga na kikundi hicho bila ya Othman kwa sababu bila yeye nisingeweza kufanya lolote la maana,”alisema Khadija.
Kwa sasa, Othman ni askari wa Jeshi la Magereza visiwani Zanzibar na uamuzi wake wa kuacha kujihusisha na muziki wa taarab ulimfanya Khadija aanze kuchacharika na kutunga nyimbo zake mwenyewe.
Khadija anakiri kuwa ushindani wa kimuziki uliokuwepo kati ya TOT na Muungano ulisaidia kwa kiasi kikubwa kuinua hadhi ya muziki huo. Anasema haitatokea kwa vikundi viwili vya taarab nchini kuwa na ushindani kama huo.
“Kila tulipofanya maonyesho ya pamoja, kumbi zilifurika. Iwe Dar es Salaam, Morogoro au Mwanza, mashabiki walikuwa wakifurika ukumbini kutushuhudia.
“Ni ushindani uliosababisha mashabiki wetu wajenge uhasama mkubwa, lakini sisi wasanii tulikuwa kitu kimoja. Wengine walidhani mimi na Nasma  tulikuwa na uadui kutokana na nyimbo tulizoimba, kumbe tulikuwa marafiki wakubwa na tulisaidiana kwa kila hali,”alisema Khadija.
Khadija amekiri kuwa ushindani wa taarab umepungua katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kuwepo kwa utitiri wa vikundi vya muziki huo.
Aidha, alisema maonyesho ya vikundi vya taarab yamekuwa yakifanyika kuanzia Jumatatu hadi Jumapili hivyo kuwafanya wasanii wake kuchoka na kukosa ubunifu.
“Kinachosikitisha zaidi ni kuona kuwa baadhi ya vikundi vya mitaani vimekuwa vikiimba nyimbo za vikundi vingine na maonyesho yamekuwa yakifanyika bure hadi mashabiki wanachoka.
“Utakuta kikundi kimoja kinafanya onyesho mtaa huu, kingine kinafanya onyesho mtaa wa pili. Huyu akisikia mwenzake amekwenda kufanya maonyesho Lindi na mwingine naye anakwenda huko huko,”alisema Khadija.
Akizungumzia madai ya kuwepo kwa uhusiano kati ya muziki wa taarab na ushoga, Khadija alisema si kweli kwa sababu kumjua shoga kunahitaji ushahidi wa uhakika.
“Ushoga ni nafsi ya mtu kupenda kitu, si maumbile au mwonekano wake,”alisisitiza mwanamama huyo.
Mwimbaji huyo pia alieleza kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya mashabiki wa muziki huo, hasa wanawake, kucheza kwa kukata viuno na pia kuvaa mavazi yanayowaonyesha wakiwa nusu uchi.
Alisema japokuwa kukata viuno ni asili ya mwafrika, lakini uvaaji wa mavazi ya nusu uchi si wa kistaarab, umepitiliza na unachangia kushusha hadhi ya muziki huo na kuufanya uonekane kuwa wa kihuni.
“Tatizo hili halipo kwenye muziki wa taarab pekee, hata hip hop na bongo fleva, utakuta wacheza shoo wamevalishwa nguo za nusu uchi. Mbona wanaume hawavai nguo za aina hiyo, wanawavalisha watoto wa kike?” Alihoji msanii huyo.
Amesema imefikia hatua hivi sasa, mzazi hawezi kutazama televisheni akiwa na watoto wake, vinginevyo analazimika kuwa na ‘remote’ mkononi ili kukitokea tukio la aibu, aweze kuzima televisheni mara moja ama kukimbilia nje ili kuepuka aibu.
Khadija amekiri kuwa umaarufu kwa wasanii ni mzuri, lakini wakati mwingine umekuwa ukiwasababishia madhara ya aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuzushiwa mambo ya uongo.
“Binafsi niliwahi kuzushiwa kwamba nimemuua mwanangu Omar Kopa kwa lengo la kujiongezea umaarufu baada ya kuonekana amenizima. Pia Leila Khatib alipokufa, niliambiwa kwamba mimi ndiye niliyemuua,”alilalamika.
Aliongeza kuwa, mbaya zaidi siku ambayo Leila alizikwa, hakuweza kuhudhuria kwenye mazishi kutokana na yeye kufiwa na bibi yake, hali iliyozidisha uvumi huo.
“Ukiwa msanii mzuri, unageuzwa kama malaika mtoa roho. Msanii mwenzako akiumwa, unaogopa hata kwenda kumuangalia,” alisema.
Khadija amekielezea kifo cha aliyekuwa mkurugenzi wa kikundi cha TOT Plus, Kepteni mstaafu, John Komba kuwa ni pigo kubwa katika fani ya sanaa nchini.
Amesema si rahisi kwa pengo la Kepteni Komba kuzibika kutokana na vipaji alivyokuwa navyo, isipokuwa anaweza kutokea msanii atakayeleta ahuni.
“Kuziba pengo lake si rahisi, litabaki kama lilivyo,”alisisitiza msanii huyo, ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa TOT.

Miongoni mwa mafanikio ya Khadija kutokana na muziki huo ni pamoja na kutembelea nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Marekani. Pia amefanikiwa kuanzisha kundi lake linalojulikana kwa jina la Ogopa Kopa Classic Music.
Moja ya malengo yake ni kurekodi upya nyimbo zake zote alizowahi kuziimba akiwa katika vikundi mbalimbali. Kikundi hicho kinaundwa na wasanii wasiozidi 10, akiwemo mtoto wake wa mwisho wa kiume, anayefahamika zaidi kwa jina la Black Kopa.
Iwapo mipango yake hiyo itafanikiwa, Khadija amesema anatarajia kuanzisha miradi mbalimbali ya kikundi kwa lengo la kuwaongezea wasanii mapato. Pia amepanga kuwashawishi wasanii wake wajiunge na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kujiwekea akiba kwa maisha yao ya baadaye.
Khadija hakuwa tayari kuzungumzia kwa kirefu ndoa yake na mumewe, aliyefariki mwaka juzi mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, ambaye inadaiwa alikuwa na umri mdogo kuliko yeye.
Alisema halikuwa jambo la ajabu kwake kuolewa na mwanaume mwenye umri mdogo kwa sababu hata Mtume Muhammad na mkewe Khadija, walifunga ndoa wakiwa wanatofautiana kwa miaka mingi.
“Mume wangu alikuwa anajua kunitunza. Nikienda kwenye maonyesho alikuwa akinifuata, tunarudi nyumbani pamoja, sijui kama naweza kumpata mume mwingine bora kama yeye. Kama atajitokeza, itabidi nimchunguze sana,”alisema Khadija huku akitabasamu.
Khadija ametoa mwito kwa wasanii wa muziki wa taarab kuwa na umoja kama ilivyo kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya, ikiwa ni pamoja na kurekodi nyimbo pamoja.
“Inasikitisha kuona sisi wasanii wa muziki wa taarab hatuna uwezo wa kufanya hivyo. Bongo fleva wanaungana na kuimba pamoja, lakini sisi hatuna uwezo huo. Mbaya zaidi hatuna mapromota na mameneja wa kutuvusha kutoka hapa tulipo,”alilalamika.

No comments:

Post a Comment