KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, May 25, 2016

KHADIJA YUSUPH: SIWEZI KUONDOKA JAHAZI KWA SABABU YA LEILA RASHID


MWIMBAJI nyota wa taarab wa kikundi cha Jahazi, Khadija  Yusuph amesema kamwe hawezi kuondoka katika kikundi hicho kwa sababu ya kutokuelewana kwake na wifiye, Leila Rashid.

Khadija amesema hawezi kuliacha kundi hilo kwa sababu ya maneno ya wanadamu na kwamba kwa kuwa kazi yao ni kusema, atawaacha wafanye hivyo hadi watakapochoka.

"Mimi nipo Jahazi na nitaendelea kuwepo kama kawaida,"alisema Khadija, ambaye ni dada wa kiongozi wa kundi hilo, Mzee Yusuph.

Khadija alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali kuhusu uhusiano wake na Leila, mke wa Mzee Yusuph, ambaye wamekuwa hawaelewani kwa muda mrefu sasa.

Alisema uhusiano kati yake na Mzee Yusuph ni mzuri na wamekuwa karibu zaidi, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma,  lakini tatizo kubwa lipo kwa wifiye Leila.

Mwanamama huyo mwenye sauti ya chiriku alisema kamwe ugomvi wake huo na Leila hauwezi kuwagawa mashabiki wa kundi hilo kwa sababu kila wanapokuwa kazini, kila mmoja anaheshimu kazi yake.

Khadija alisema inawezekana hali ya kutokuelewana kati yake na Leila, imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kutokana na kufanyakazi katika kundi moja, lakini wangekuwa makundi tofauti, huenda uhusiano wao ungekuwa mzuri.

"Kaka yangu anao wake wawili, lakini siwezi kusema simpendi mke mdogo, nampenda mke mkubwa, nawapenda wote,"  alisisitiza mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la East African Melody.

"Ukewenza haukuanza kwa Leila na mke mkubwa wa Yusuph, ulianza tangu enzi ya mabibi na mababu zetu. Hata mimi niliwahi kuolewa ukewenza, lakini sikuwahi kugombana na wifi zangu wala
mkwe wangu. Ukewenza ni mume, kama mume hayupo vizuri, lazima tofauti zitazuka,"alisema.

Khadija alisema haamini iwapo wapo watu wanaomfitinisha yeye na Leila, isipokuwa huo ni uamuzi binafsi wa wifi yake kwa vile kila anapojaribu kumsalimia, amekuwa akimnunia na kukataa kumuitikia.

"Basi na ndio mpaka leo ipo hivyo, hanisalimii, simsalimii, hakuna fitina, labda yeye mwenyewe. Na hata kama yupo katika familia kweli, sawa na mimi sijamkataa kwa sababu ningemkataa, basi hata ile siku ya mwanzo aliyokwenda kuolewa ningemkataa,"alisema Khadija.

Akizungumzia uimbaji wake, Khadija alisema sauti yake imeendelea kuwa maridhawa kwa vile hatumii kilevi cha aina yoyote.

"Sauti hii ni orijino kama mashabiki wanavyoniita kwamba nina sauti ya chiriku. Situmii kitu chochote, nipo kikawaida tu. Hiki ni  kipaji kutoka kwa mama yangu, maana naye alikuwa mwimbaji
wa kikundi cha Culture,"alisisitiza.

Khadija pia alikanusha madai kuwa anapenda wanaume wenye umri mdogo kuliko wa kwake. Amesema madai hayo hayana ukweli wowote kwa sababu mara zote mbili, ameolewa na wanaume wenye umri mkubwa kuliko wa kwake.

Khadija amesema kitu pekee anachokijutia katika maisha yake ni ugomvi kati yake na Leila kutokana na kuihusisha familia yake, akiwemo mama yake mzazi.

"Mama yangu katukanwa sana. Nimelia saba kwa matusi yake. Kwa kweli najuta kuwemo katika muziki wa taarab,"alisema.

Khadija pia amekiri kuwa tangu Leila alipojifungua hivi karibuni, hajawahi kwenda kumuona mtoto aliyezaliwa.