KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, March 5, 2014

MASHAUZI ASEMA HANA UGOMVI NA THABITI ABDUL


 
KIONGOZI wa kikundi cha muziki wa taarab cha Mashauzi Classic, Isha Mashauzi amesema hana ugomvi wowote na mmiliki mwenzake wa zamani wa kikundi hicho, Thabiti Abdul.

Isha alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, Thabiti aliondoka Mashauzi Classic kwa hiyari yake na alitoa taarifa kwa viongozi wenzake.

“Sijui kwa nini mtu anapofanya mazuri hawaongei. Kuhusu kuwa na mgogoro na Thabit, mimi  sijui kwani nilishawahi kufanya naye kazi katika bendi yangu kwa muda mrefu, na yeye mwenyewe alituita sisi viongozi kwa pamoja na kusema anaondoka ndani ya bendi,"alisema

Kwa mujibu wa Isha, Thabiti aliwaeleza viongozi wenzake kwamba yuko tayari kushirikiana na Mashauzi Classic wakati wowote atakapohitajika kufanya hivyo, lakini kwa sasa hawamuhitaji.

"Kusema ule ukweli, kwa sasa hatuna shida naye, muda ukifika kama tutamuhitaji, tutafanya hivyo,"alisema mwanamama huyo.

“Lakini bado nashangaa kwa nini watu wanaeneza kutokuelewana baina yetu, labda mumfuate yeye mumuulize, lakini kwa upande wangu haja ya mja ni kunena, muungwana ni vitendo, kwa hiyo sioni sababu ya kuanza kujibizana," alisisitiza Isha.

Isha alisema pia kuwa, amekuwa akishangazwa na maneno yaliyozagaa mitaani na miongoni mwa wasanii wenzake kwamba, anaringa wakati hana sababu ya kufanya hivyo.

"Nimringie nani wakati mabosi zangu ni mashabiki na wapenzi wetu? Bila wao nisingekuwa hapa nilipo kwa sasa. Sisi ni mwendo wa kazi na bendi yangu, waache waongee wanavyojisikia, sisi tunachapa kazi,"aliongeza.

Mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la Jahazi amewaomba mashabiki wa Mashauzi Classic wakae mkao wa kula, kusubiri ujio wa albamu yao mpya wanayotarajia kuitoa hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment