KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Tuesday, April 1, 2014

SUNGURA MJANJA WA MASHAUZI ATOA KITU KIPYA


MWIMBAJI chipukizi wa tarab anayeinukia vizuri nchini, Saida Ramadhani ‘Sungura Mjanja’, ameibuka na wimbo mpya uitwao Ropokeni Yanayowahusu.

Akizungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii katika hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es Salaam, mwimbaji huyo wa kundi la Mashauzi amesema wimbo huo ametungiwa na dada yake, Isha Ramadhani.
“Dada Isha katunga, mimi nimerekodi na umekwishakamilika, ni wimbo mzuri sana, naamini utapendwa ukitoka. Na utazidi kunipandisha matawi ya juu,”alisema Saida.
Saida ameingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo za Kili mwaka huu kupitia wimbo wa Asiyekujua Hakuthamini, ambao ameshirikiana na dada yake, Isha ulioingia kwenye kipengele cha wimbo bora wa Taarab.

ISHA MASHAUZI AIBUKA NA SURA SIYO ROHOMWANAMUZIKI na kiongozi wa kundi la taarab la Mashauzi Classic, Isha Mashauzi, ametoa nyimbo mpya mbili, ambazo muda si mrefu zitaanza kusikika kwenye vituo mbalimbali vya Redio nchini.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii katika hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es Salaam wakati wa semina ya wanamuziki waliongia kwenye tuzo za Kili 2014, Isha au Jike la Simba amesema kwamba nyimbo zote ni nzuri.
Amezitaja nyimbo hizo kuwa ni Sura Siyo Roho na Mapenzi Hayana Dhamana, ambazo zote ametunga yeye mwenyewe.
“Kama kawaida, wapenzi na mashabiki wangu na mashabiki wa Mashauzi Classic kwa ujumla, wajiandae kwa kazi mpya, tutaanza na audio (sauti) baadaye itafuatia na kwenye video pia,”alisema Isha.

FATIHYA AKIWA NDANI YA MAONYESHO YA BIASHARA COCO BEACHMFANYABIASHARA Fatihya Masoud (kushoto) akifurahia jambo wakati akimueleza mteja, Farida Shekigenda, bei ya mabegi alipotembelea banda lake juzi kwenye maonyesho ya biashara ya Kariakoo yanayofanyika kwenye ufukwe wa Coco Beach kwa udhamini wa Kampuni ya Simu ya Tigo.

MFANYABIASHARA Fatihya Masoud (kushoto) akimueleza mteja, Farida Shekigenda, bei ya mabegi alipotembelea banda lake juzi kwenye maonyesho ya biashara ya Kariakoo yanayofanyika kwenye ufukwe wa Coco Beach kwa udhamini wa Kampuni ya Simu ya Tigo.

MFANYABIASHARA Fatihya Masoud akifurahia vipodozi vyake wakati wa maonyesho hayo

Sunday, March 9, 2014

UZINDUZI ALBAMU YA NYONGA MKALIA INI WAFANA


 
 

Moja ya sehemu ambayo unaweza kumtambua msanii mzuri ni pale ambapo anaweza kuimba na kucheza na mashabiki wake wanaokuja kila mara kumuangalia kwenye shoo na matamasha tofauti.

Hassan Ally alidhihirisha uzuri na umahiri wake ambao haupo tu kwenye kuimba na kutunga mashairi lakini pia kutawala jukwaa na kucheza na mashabiki wake.

Kwa wale ambao hawakufika kwenye shoo ya jana kwa sababu tofauti tofauti nakushauri ukisikia huyu jamaa anafanya shoo nyingine,nenda ukahudhurie.

Kila shoo nzuri hupambwa na muunganiko wa maelewano na sapoti baina ya wasanii,na jana Kings Modern Taarab walifanya vizuri sana kwenye kumuunga mkono mwenzao.

Walitoa burudani nzuri sana iliyowafanya mashabiki waliofika watulie huku wakisubiri Hassan Ally.Baadhi ya wasanii kutoka Kings ambao walitoa burudani ni pamoja na Amina Mnyalu,Aysher Vuvuzela,Mwanahawa Chipolopolo.

Ingawa shoo ilichelewa sana kuanza ilia baada Kings walipoanza kazi mambo yalikuwa poa,Baada ya nyimbo kadhaa za Kings ndipo Joha Kassim akapanda stejini nae akatoa shoo kali kama kawaida yake.

Ndio Hassan Ally aliingia ukumbini kwa kuwasuprise mashabiki wake kupitia geti ambalo mara kwa mara huwa linafungwa huku akisindikizwa na ngoma.

Moja ya vitu ambavyo wengi walivipenda na kumshangilia sana ni kuwashukuru watu ambao walifanikisha shoo hiyo,huku akionyesha furaha yake na upendo kwa wote waliohudhuria.

Hassana Ally alijipanga sana kiasi cha kujua afanye nini na wakati gani,sio tu katika uimbaji lakini kucheza na vijana walioandalia kufanya kazi hiyo.

Kuna muda alishuka chini ya steji na kuanza kucheza na mashabiki wake kitu kilichowafanya wengi kuancha kucheza na kumuangalia jinsi walivyokuwa wanacheza vizuri sana tena kwa umoja wao.

“Wengi hawajui kuwa mimi nina mtoto,sasa leo nataka mumuone mwanamke niliyezaa naye” Hayo yalikuwa maneno na Hassan Ally ambapo alimuita ‘Nyonga mkalia Ini’ wake,ndio zipotoka shangwe kutoka kwa mashabiki.

Kabla ya Khadija Kopa Hajapanda stejini,Hassan Ally aliimba nyimbo “Nyonga Mkalia Ini” na Mr. Pendwa Pendwa. Lady with Confidence ilikuwa ni nyimbo moja wapo ambayo Malkia aliimba.

Ingawa Bi.Mwanahawa Ally na Mc Dida hawakuwepo,lakini shoo ilikuwa nzuri na ilipangilia sana kiasi cha kufanya watu kutowaulizia hao ambao hawakuwepo. Mwanahawa Chipolopolo alichukua jukumu la U-Mc na kwa maoni yangu aliufanyia haki sana,pia watangazaji Yunis Kanumba wa City Radio na Mwanne wa Eatv walitoa sapoti pia.

IMETOLEWA BLOGU YA NAKSHI 255

THABITI ABDUL AJITOSA KWENYE MOVI

 Wengi wa wasanii wa taarab wana kipaji zaidi ya kimoja,wapo ambao wanaimba na kutunga wenyewe nyimbo zao kitu ambacho tumekizoea.pia katika tasnia hii ya taarab wapo wasanii ambao wanapiga vyombo na pia wanaimba wapenzi wengi hawjui hili.

Ukimzungumzia Thabit Abdul “Jiko la Jela” yeye amekwenda zaidi ya hapo licha ya kwamba ni muimbaji na mpiga mpiga vyombo lakini pia ni muigizaji mzuri.

Thabi Abdul kwa sasa amefanya filamu yake mwenyewe akishirikiana na baadhi ya mastaa  wa “Bongo Movies”, inayokwenda kwa jina la “Brother and Sister”.

Kwa mujibu wa mtu wa karibu na na Thabit ambaye pia ni mtengenezaji wa filamu hiyo amesema,kazi hiyo imeshakamilika na ipo katika hatua za mwisho kuingia sokoni ili wapenzi wapate kuiona filamu hiyo

Wednesday, March 5, 2014

NYONGO MKALIA INI KUZINDULIWA KESHO TRAVERTINE


MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Hassan Ally kesho anatarajiwa kufanya uzinduzi wa albamu yake mpya itakayojulikana kwa jina la Nyongo mkalia ini.

Akizungumza na Burudani juzi, Hassan alisema onyesho hilo litafanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.

Hassan alisema albamu hiyo itakuwa ya kwanza kwake kuifanya kwa kujitegemea nje ya kundi lake la Kings Modern Taarab.

Kwa mujibu wa Hassan, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya onyesho hilo yamekamilika na amewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kumuunga mkono.

Hassan alisema uzinduzi huo utasindikizwa na burudani kutoka kwa waimbaji mahiri wa muziki huo, Mwanahawa Ally, Jokha Kassim, Khadija Kopa na kundi la Kings Modern Taarab.

Mwimbaji huyo machachari alianza kutambulika rasmi katika muziki wa taarab alipokuwa kundi la New Zanzibar Stars. Uimbaji wake maridhawa na sauti yake murua vilimwezesha kupata mashabiki lukuki.

Baadaye alihamia kundi la Kings Modern Taarab kabla ya kutua T Moto Modern Taarab, lakini hakudumu navyo kwa muda mrefu. Alirejea Kings Modern Taarab mwaka jana na amedumu na kundi hilo hadi sasa, akiwa mmoja wa waimbaji wake mahiri.

MWANAHAWA AWASHUKUA MAPROMOTA UCHWARA


MWIMBAJI mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Mwanahawa Ally ameilalamikia tabia ya baadhi ya mapromota kutumia jina na picha yake kibiashara bila idhini yake.

Mwanahawa alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, amekuwa akikerwa na tabia hiyo kwa sababu mapromota hao wamekuwa wakitumia jina na picha zake kibiashara bila kufikia makubaliano nao.

Alisema baadhi ya mapromota wamekuwa wakitengeneza matangazo ya barabarani yakiwa na picha zake na kumtaja kuwa ni miongoni mwa waimbaji watakaoshiriki kwenye maonyesho fulani wakati si kweli.

Amewataka mapromota hao kuacha tabia hiyo mara moja, vinginevyo atawachukulia hatua za kisheria ili liwe fundisho kwa wengine.

“Sitopenda kusikia au kuona jina au picha yangu inatumika kutangaza shoo bila idhini yangu au uongozi wa bendi yangu. Mimi ni msanii wa Dar Modern Taarab na nitakuwa napatikana katika kikundi hiki kila ijumaa katika hoteli ya Travertine,"alisema.

Mwanahawa ameamua kuwatolea uvivu mapromota hao kutokana na baadhi yao kutumia jina lake kuwahadaa mashabiki wa muziki wa taarab.

MASHAUZI ASEMA HANA UGOMVI NA THABITI ABDUL


 
KIONGOZI wa kikundi cha muziki wa taarab cha Mashauzi Classic, Isha Mashauzi amesema hana ugomvi wowote na mmiliki mwenzake wa zamani wa kikundi hicho, Thabiti Abdul.

Isha alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, Thabiti aliondoka Mashauzi Classic kwa hiyari yake na alitoa taarifa kwa viongozi wenzake.

“Sijui kwa nini mtu anapofanya mazuri hawaongei. Kuhusu kuwa na mgogoro na Thabit, mimi  sijui kwani nilishawahi kufanya naye kazi katika bendi yangu kwa muda mrefu, na yeye mwenyewe alituita sisi viongozi kwa pamoja na kusema anaondoka ndani ya bendi,"alisema

Kwa mujibu wa Isha, Thabiti aliwaeleza viongozi wenzake kwamba yuko tayari kushirikiana na Mashauzi Classic wakati wowote atakapohitajika kufanya hivyo, lakini kwa sasa hawamuhitaji.

"Kusema ule ukweli, kwa sasa hatuna shida naye, muda ukifika kama tutamuhitaji, tutafanya hivyo,"alisema mwanamama huyo.

“Lakini bado nashangaa kwa nini watu wanaeneza kutokuelewana baina yetu, labda mumfuate yeye mumuulize, lakini kwa upande wangu haja ya mja ni kunena, muungwana ni vitendo, kwa hiyo sioni sababu ya kuanza kujibizana," alisisitiza Isha.

Isha alisema pia kuwa, amekuwa akishangazwa na maneno yaliyozagaa mitaani na miongoni mwa wasanii wenzake kwamba, anaringa wakati hana sababu ya kufanya hivyo.

"Nimringie nani wakati mabosi zangu ni mashabiki na wapenzi wetu? Bila wao nisingekuwa hapa nilipo kwa sasa. Sisi ni mwendo wa kazi na bendi yangu, waache waongee wanavyojisikia, sisi tunachapa kazi,"aliongeza.

Mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la Jahazi amewaomba mashabiki wa Mashauzi Classic wakae mkao wa kula, kusubiri ujio wa albamu yao mpya wanayotarajia kuitoa hivi karibuni.

Saturday, February 1, 2014

KHADIJA KOPA ATIKISA MBEYA

Mwimbaji nyota wa kikundi cha taarab cha Tanzania One Theatre (TOT), Khadija Omar Kopa akiimba wakati wa onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa City Pub mjini Mbeya.
Waimbaji taarab wa TOT wakiwa kazini kwenye ukumbi wa City Pub mjini Mbeya.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Naye Nnauye naye alikuwepo. Hapa akimpongeza Khadija kwa uimbaji wake.
Mashabiki wa taarab wakiselebuka wakati kikundi cha TOT kilipokuwa kikitoa burudani kwenye ukumbi wa City Pub, Mbeya

Wednesday, January 29, 2014

ALLY J AKABIDHIWA FIVE STARS


ALIYEKUWA mmiliki wa kikundi cha muziki wa taarab cha Five Stars, Shaks amesema, ameamua kumkabidhi kundi hilo msanii Ally J.

Shaks alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, Ally J hakuwa mmiliki wa kundi hilo, isipokuwa alikuwa miongoni mwa wasanii waanzilishi na alikabidhiwa jukumu la uongozi.

"Wakati nalinunua kundi hili, Ally J alikuwa miongoni mwa wasanii niliowakuta na alikuwa miongoni mwa waanzilishi, hakuwahi kuwa mmiliki,"alisema.

Shaks alitoa ufafanuzi huo baada ya Ally J kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni akisema kuwa, Five Stars haiwezi kufa.

Majigambo hayo ya Ally J yalikuja baada ya Shaks kutangaza kulivunja kundi hilo wiki mbili zilizopita.

"Kwa sasa Ally J ana uwezo na haki ya kusema chochote kuhusu Five Stars kwa sasa nilimpa umiliki wa kundi hilo bure bila kumuuzia,"alisema Shaks.

Hata hivyo, Shaks alisema Ally J hana haki ya kuwamiliki wasanii wa kundi hilo kwa vile alishavunja mikataba yao na kuwaruhusu kujiunga na vikundi vingine.

MWANAHAWA: SIWEZI KUACHA KUIMBA TAARAB


MWIMBAJI mkongwe wa nyimbo za muziki wa taarab nchini, Mwanahawa Ally, amesema hawezi kuacha muziki huo kwa sasa kwa sababu ndio unaomwezesha kuendesha maisha yake.

Mwanahawa alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, sauti yake ndiyo kipaji alichopewa na Mungu kinachomwingizia kipato chake cha kila siku.

Mwanamama huyo, aliyejiunga na kikundi cha Dar Modern Taarab hivi karibuni alisema, ataachana muziki baada kujiona hawezi kuimba kama ilivyo kawaida yake.

"Labda itokee nimepatwa na ugonjwa ambao utanifanya nishindwe kabisa kuimba, lakini kwa sasa sifikirii kabisa kuacha muziki wa taarab,"alisisitiza.

Mwanahawa ni miongoni mwa wasanii wa kundi la Five Stars Modern Taarab waliopata ajali mwaka juzi mkoani Morogoro na kunusurika kufa. Katika ajali hiyo, wasanii tisa walipoteza maisha.

Kwa sasa, Mwanahawa na kundi lake la Dar Modern Taarab, wanajiandaa kwa uzinduzi wa albamu yao mpya, utakaofanyika Februari 14 mwaka huu.

KHADIJA KOPA KUANZISHA KUNDI LAKE LA TAARAB?KUNA habari kuwa, mwimbaji nyota wa muziki wa taarab hapa nchini, Khadija Omar Kopa, anafanya mipango ya kuanzisha kikundi chake cha muziki huo.

Habari za uhakika kutoka kwa watu wa karibu na msanii huyo zimeeleza kuwa, tayari Khadija ameshaagiza vyombo vipya vya muziki kutoka China.

Kwa mujibu wa habari hizo, vyombo hivyo vinatarajiwa kutua nchini wakati wowote kabla ya kundi hilo kuingia kambini kwa lengo la kuandaa nyimbo mpya.

Kwa sasa, Khadija ni mwimbaji na Mkurugenzi Msaidizi wa kikundi cha sanaa za maonyesho cha Tanzania One Theatre (TOT).

Mbali na kuwa msanii wa TOT, Khadija pia amekuwa akirekodi nyimbo zake binafsi na kufanya maonyesho kwa kujitegemea.

THABIT ABDUL AIPELEKA MODERN TARADANSI STUDIO


KUNDI jipya la muziki wa taarab la Modern Taradansi, linaloongozwa na Thabiti Abdul, limeingia studio kurekodi nyimbo zake mpya tatu.

Akizungumza na Burudani wiki hii, Thabiti alisema wamerekodi nyimbo hizo kwenye studio za Sound Crafters, zilizoko Temeke, Dar es Salaam.

Thabiti, ambaye ni mtunzi na mpiga kinanda hodari nchini alisema, wamerekodi nyimbo hizo kwa lengo la kukitambulisha rasmi kikundi hicho.

Hata hivyo, Thabiti hakuwa tayari kutaja majina ya nyimbo hizo kwa madai kuwa, watazitangaza rasmi mwishoni mwa wiki hii.

Kiongozi huyo wa Modern Taradansi, pia hakuwa tayari kutaja majina ya wasanii wanaounda kikundi hicho kwa madai kuwa, watajulikana siku ya utambulisho.

"Kwa sasa ni mapema kuwataja wasanii wanaounda kundi letu na pia nyimbo zetu mpya. Tutafanya hivyo siku ya utambulisho,"alisema.

DAR MODERN TAARAB SASA INATISHA, YANYAKUA NYOTA WAPYA KADHAA

Mwamvita Shaibu
Zubeda Mlamali

BAADA ya kujiimarisha kwa kunyakua wasanii mbalimbali wapya wa taarab kutoka katika vikundi vingine, kikundi cha Dar Modern kimeingia studio kurekodi albamu yake ya pili.

Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo, zilirekodiwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye studio za Sound Crafters zilizoko Temeke, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na kikundi hicho wiki hii imeeleza kuwa, albamu hiyo mpya itakuwa na nyimbo saba zilizoimbwa na wasanii tofauti.

Kwa mujibu wa taarifa, lengo la kurekodi albamu hiyo ni kutambulisha ujio mpya wa kikundi hicho baada ya kutumia fedha nyingi kunyakua waimbaji nyota kutoka vikundi mbalimbali maarufu vya muziki huo.

"Lengo letu ni kuifanya Dar Modern Taarab itishe na iwe na kikosi kizuri baada ya kunyakua wasanii wazuri,"imeeleza taarifa hiyo iliyotiwa saini na mmoja wa viongozi wa kundi hilo, Adam Mlamali.

Miongoni mwa waimbaji wapya wanaounda kundi hilo ni pamoja na mkongwe, Mwanahawa Ally, Mwamvita Shaibu, Husna Mlamali, Zubeda Mlamali na Mossy Suleiman.

Vibao vipya vilivyorekodiwa na kikundi hicho ni Oh my honey (Hassan Vocha), Naenda kwa mume wangu (Husna Mlamali), Sikuamini macho yangu (Mwamvita Shaibu), Malipo duniani (Zubeda Mlamali), Siwanyimi uzuri (Mwanahawa Ally).

Mlamali hakutaka kutaja jina la wimbo ulioimbwa na Mossy kwa madai kuwa, wanataka iwe 'sapraisi' kwa mashabiki wao.

"Huu wimbo utakuwa sapraisi kwa mashabiki wakati tutakapozindua albamu yetu,"alisema Mlamali.
Kwa mujibu wa Mlamali, uzinduzi wa albamu hiyo umepangwa kufanyika Februari 14 mwaka huu, kwenye ukumbi wao mpya wa Dar Modern Hall ulioko Magomeni, Dar es Salaam.

Monday, January 27, 2014

KWENYE PICHA MNAPENDEZA, LAKINI MH....

Ni tangazo la Jahazi. Lakini pia picha ya wanafamilia, Mzee Yussuf, mkewe Leila Rashid na dada mtu, Khadija Yussuf. Leila ni mke wa Mzee na pia wifi ya Khadija.

Kwenye picha mnapendeza, lakini haifurahishi kusikia Khadija na Leila hawaelewani, wanagombana mara kwa mara. Haipendezi.