KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, December 26, 2014

FIVE STARS YAJA NA TATU MPYA, ISHA MASHAUZI APAKUA SURA SURAMBI
KIKUNDI cha taarab cha Five Stars, ambacho kimezidi kujiimarisha kwa kuwanyakua waimbaji wapya kadhaa, wiki iliyopita kiliingia studio kurekodi vibao vitatu vipya.

Vibao hivyo vipya ni Ubaya hauna soko kilichoimbwa na Mwanaidi Ramadhani, Kishtobe kilichoimbwa na Salha na Sina Gubu kilichoibwa na Mape Kibwana.

Kiongozi wa kundi hilo, Ally J, ametamba kuwa vibao hivyo vitakuwa moto wa kuotea mbali kutokana na kupigwa katika miondoko ya kisasa zaidi.

Wakati huo huo, kiongozi wa kundi la Mashauzi Classic, Isha Ramadhani, ameachia kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Sura Surambi.

Kibao hicho ni utunzi na uimbaji wake Isha Mashauzi na tayari kimesharekodiwa wikiendi iliyopita kwenye studio za Sound Crafters, zilizoko Temeke jijini Dar es Salaam chini ya producer Enrico.

“Sura Surambi” inategemewa kuendelea kumweka juu Isha Mashauzi kwa namna alivyoimba wimbo huo na hapana shaka itatosha kabisa kuthibitisha ni kwanini alistahili tuzo ya mwimbaji bora wa kike wa taarab.

Gita la solo katika wimbo huo limepigwa na Ramadhani Kalenga, besi limepigwa na Rajabu Kondo wakati kinanda kimepapaswa na Kalikiti Moto.

MBILI MPYA ZA WAKALI WAO MODERN TARADANCE USIPIMEKUNDI la muziki wa taarab la Wakali Wao Modern Taradance limedhihirisha kuwa ni moto wa kuotea mbali katika taarab ya kisasa baada ya kuibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Siioni thamani ya pendo.

Kibao hicho kilichotungwa na kuwekwa muziki na kiongozi wa kundi hilo, Thabiti Abdul, kimeimbwa na mwanadada Asia Mariam.

Kibao hicho na kile cha Mtu Mzima hovyo, vimerekodiwa katika studio za Marlon Linje, na vimekolezwa vikorombwezo vyenye mvuto wa aina yake.

Kibao cha Siioni Thamani ya Pendo kimepigwa katika miondoko ya taratibu, ni rhumba fulani lililokwenda shule huku ndani yake kukiwa kumechombezwa vitu fulani kutoka kwa baadhi ya nyimbo maarafu.

Kwa mfano, kipo kipande ambacho kimetoholewa kutoka kwenye wimbo wa Makumbele, uliotamba na bendi ya Orchestra Maquis Original ya hapa nchini zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Aidha utakutana pia na vipande kutoka kwa wimbo unaendelea kulitingisha bara la Afrika “Kuchi Kuchi (Oh Baby)” ulioimbwa na J’odie wa Nigeria.

Vibao hivyo vimerekodiwa siku chache baada ya kundi hilo kuzindua albamu yao ya kwanza, inayojulikana kwa jina la Kalieni Viti siyo Umbea”.

OGOPA KOPA WAJA NA TATU KALI MPYA


KUNDI jipya la muziki wa taarab la Ogopa Kopa, linaloongozwa na Malkia wa muziki huo nchini, Khadija Omar Kopa, limedhihirisha kuwa ni tishio baada ya kuibuka na vibao vipya  vitatu.

Moja ya vibao hivyo vipya ni Stop Red Card, kilichoimbwa na Anifa Maulid, almaarufu kwa jina la Jike la Chui, mwanadada mwenye sauti murua inayoleta starahamu ya aina yake masikioni.

Kibao kingine ni Chozi la mnyonge, kilichoimbwa na kijana anayechipukia katika muziki huo, Hassan Ali, ambaye amejaliwa kuwa na sauti maridhawa.

Kiongozi wa kundi hilo, Khadija Omar Kopa, naye ameibuka na kibao kikali kinachotarajiwa kubeba jina la albamu mpya ya kundi hilo, Mama mukubwa.

MZEE YUSSUF AJA NA NGOMA MPYA 'MAHABA NIUE'


Huu ni wimbo mpya kabisa, umepewa jina la “Mahaba Niue” ikiwa ndio ‘singo’ mpya ya albam ijayo ya Jahazi Modern Taarab.

Ni utunzi na uimbaji wake Mfalme Mzee Yussuf, ngoma kali ambayo inakuwa zawadi nzuri ya kufungia mwaka 2014 na kufungua 2015.

Kazi hii imefanyika katika studio za Sound Crafters, Temeke jijini Dar es Salaam, chini ya producer Enrico. Ndani ya wimbo huu utakutana na mipini mikali ya Mohamed Mauji aliyetambaa vizuri na gitaa lake la solo huku kwenye kinanda kazi kubwa ikiwa imefanywa na Chid Boy.

Kama ilivyo kawaida ya Mzee Yussuf kwenye ngoma ambapo hufunika na vionjo vikali, humu nako ametisha sana, utakutana na vitu vya “Songa Ugali Tule” na vikorombwezo vingine kibao.

Je huu ndio wimbo wa mwisho wa Mzee Yussuf? Sahau kabisa hiyo kitu. Mzee Yussuf ameiambia Saluti5 kuwa lolote linaweza kutokea.

“Ningependa kuacha kuimba mwaka huu, lakini ni mapokeo ya kazi hii ndiyo yatakayoamua, nitaangalia mashabiki wanaipokea vipi, nitaangalia pia namna malengo yangu mengine yatakavyokuwa.

Ninatamani “Mahaba Niue” uwe wimbo wangu wa mwisho, lakini sisemi kuwa huu ni wimbo wangu wa mwisho,” alisema Mzee Yussuf katika maongezi yake na Saluti5

Monday, December 15, 2014

FIVE STARS MODERN TAARAB YAJA KIVINGINE, YAMNYAKUA SALHA, KUZINDUA ALBAMU MPYA DESEMBA 19 DAR

SALHA Aboud
MARYAM Aboud
MUSSA Kijoti
KIONGOZI wa Five Stars Modern Taarab, Ally J (kushoto)

MWIMBAJI nyota wa taarab nchini, Salha Abdul, amejiunga na kikundi cha taarab cha Five Stars kinachoongozwa na mpiga kinanda mahiri, Ally J.
Salha alitangaza uamuzi wake huo mwishoni mwa wiki kwa kile alichodai kuwa, umelenga zaidi kukuza kipaji chake.
Mwanadada huyo mwenye sura jamali na umbo lenye mvuto alisema amefikia uamuzi huo baada ya kushawishiwa kufanya hivyo na Ally J na pia baada ya kupata barakaa za mama yake mzazi.
"Nilipigiwa simu na Ally J akinieleza kwamba ana mazungumza na mimi na bila kusita nilimkubalia kwa sababu namheshimu sana,"alisema Salha, ambaye kabla ya kujiunga na Five Stars alikuwa kwenye kikundi cha Kings Modern Taarab.
Tayari Salma ameshaibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Kishtobe, ambacho kimeshaanza kusikika kwenye vituo mbalimbali vya redio nchini.
Kwa mujibu wa Ally J, kikundi hicho kinatarajiwa kufanya uzinduzi wa albamu yake mpya Desemba 19 mwaka huu, utakaofanyika kwenye ukumbi wa Travertine, Dar es Salaam.
Ally J alisema kikundi chake kimeamua kutoka kivingine, ikiwa ni pamoja na kuboresha mipigo yake ya taarab kwa kuweka vionjo vipya kwa lengo la kuleta mvuto kwa mashabiki.
Aliwashukuru wadau mbalimbali wa taarab, ambao wameamua kukiongezea nguvu kikundi hicho ili kiweze kuwa tishio kama ilivyokuwa wakati kilipoanzishwa.
Five Stars ilipata pigo miaka miwili iliyopita baada ya wasanii wake 11 kufariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea mkoani Morogoro.
All J alisema uzinduzi wa albamu ya kikundi hicho utapambwa na wasanii mbalimbali maarufu wa taarab nchini, wakiwemo wakongwe Khadija Omar Kopa, Mwanahawa Ally na Jokha Kassim.
Kwa upande wake, waimbaji Mussa Kijoti na Maryam Aboud walisema ujio wa albamu yao mpya utakuwa na kishindo kizito kwa vile wameamua kutoka kivingine.