KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Monday, December 17, 2012

MASIKINI KHADIJA YUSSUF, AANGUA KILIO CHA UCHUNGU. KISA? WIFIYE LEILA RASHID!


MWIMBAJI nyota wa taarab wa kikundi cha Jahazi, Khadija Yussuf mwishoni mwa wiki iliyopita aliangua kilio wakati alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mitikisiko ya Pwani kilichorushwa hewani
na kituo cha ITV.
Sababu kubwa iliyomfanya Khadija aangue kilio ni kuzuka kwa tofauti kubwa kati yake na kaka yake, Mzee Yussuf, ambaye ndiye mkurugenzi wa kikundi hicho.
Mtangazaji wa kipindi hicho alimuuliza Khadija ni kitu kipi kinachomkera katika maisha yake. Naye bila kutafakari kwa muda mrefu alijibu kuwa, ni kile kitendo cha mtu kutoka aendako na kwenda kumzushia maneno ya uongo kwa Mzee.
"Kinachoniuma zaidi ni kwamba afadhali hayo maneno ningekuwa nimeyasema, lakini sijafanya hivyo.
Hawa watu wanapaswa kutambua kwamba kuna Mungu na mimi na Mzee Yussuf tumezaliwa baba mmoja mama mmoja, atakapozikwa Mzee Yussuf ndipo nitakapozikwa mimi,"alisema Khadija huku machozi yakianza kumlengalenga.
"Kusema kweli maisha ninayoishi na Mzee Yussuf hivi sasa ni tofauti na huko nyuma tulikotoka. Inaniuma sana,"alisema Khadija na kuangua kilio kikali, ambacho kilisababisha mtangazaji wa kipindi hicho naye machozi kumlenga.
Mapema Khadija alisema kuna kikundi cha watu ndani ya Jahazi, ambacho kimekuwa kikimchonganisha yeye na wifi yake, Leila Rashid, ambaye ni mke wa pili wa Mzee.
Alisema watu hao wamekuwa wakipeleka maneno ya umbeya kwa Leila wakidai kuwa yeye ndiye ameyasema na vivyo hivyo wamekuwa wakija kwake na kumweleza maneno kama hayo.
"Kuna wakati Leila amekuwa akinitumia meseji zenye maneno machafu. Ninapomjibu anakasirika. Sielewi tunachogombea ni kipi,"alisema Khadija.
"Binafsi sina tatizo na Leila na sioni kwa nini tugombane. Sielewi na ninashangaa. Lakini hii yote ni kwa sababu kuna watu ndani ya Jahazi wanaotuchonganisha kwa makusudi,"aliongeza.
Khadija alisema kwa sasa anajiandaa kuibuka na kibao chake kipya kitakachojulikana kwa jina la Na bado. Alisema kibao hicho kitazinduliwa katika onyesho maalumu litakalofanyika Desemba 30 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment