KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, December 21, 2012

ALBAMU MPYA YA JAHAZI KUZINDULIWA DESEMBA 30KIKUNDI cha taarab cha Jahazi kinatarajia kupakua albamu mpya ya Wasiwasi wako katika onyesho litakalofanyika Desemba 30 mwaka huu kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.
Akizungumza na blogu ya rusha roho leo, kiongozi wa kundi hilo, Mzee Yusuph amesema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya uzinduzi huo yameshakamilika.
Kwa mujibu wa Mzee, albamu hiyo itakuwa na nyimbo sita, ambazo amejigamba kuwa zote zitakuwa moto wa kuotea mbali.
Mzee alisema tayari nyimbo zote sita zimeshakamilisha na baadhi zimeshaanza kupigwa na kusikika kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Wasiwasi wako aliouimba yeye mwenyewe, Kazi mnayo ulioimbwa na Ahmed Ally  na Sitaki Shari ulioimbwa na mahabuba wake, Leila Rashid.
Alizitaja nyimbo nyingine kuwa ni Nipe Stara ulioimbwa na Rahma Machuppa, Hata bado hamjanuna ulioimbwa na Fatma Ally na Mambo bado ulioimbwa na Khadija Yussuf.
Mzee alisema amepania kufanya mabadiliko makubwa kwenye muziki wa taarab ili kuwapa mashabiki ladha tofauti badala ya ile waliyoizoea.
"Sisi kama Jahazi tunapenda tufanye kile kitu mashabiki wanapenda, hivyo tunawaahidi mambo mapya kabisa katika albamu yetu hii mpya,"alisema.
Alisema wakati wa onyesho hilo, wanatarajia kuuza CD na DVD za albamu hiyo kwa mashabiki ili wakapate starehe zaidi majumbani kwao.
Albamu hiyo itakuwa ya tisa tangu kundi la Jahazi lilipoanzishwa mwaka 2006. Albamu zingine zilizopita za kundi hilo ni Tupendane wabaya waulizane, Wagombanao ndio wapatanao, Mpenzi chokolate, Daktari wa mapenzi, Two in one, VIP na My Valentine.

No comments:

Post a Comment