KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, May 10, 2017

ALLY J AITOSA FIVE STARS NA KUREJEA JAHAZI MODERN TAARAB




KIONGOZI wa kundi la muziki wa taarab la Five Stars, Ally J, ameamua kuliacha kundi hilo na kujiunga na kundi lake la zamani la Jahazi.

Ally J, ambaye ni mmoja wa wapapasaji mahiri wa kinanda nchini, amesema uamuzi wake huo umelenga kukuza na kuendeleza fani ya taarab, ambayo imeanza kupwaya.

Msanii huyo alisema ni kweli kwamba, aliwahi kuapa huko nyuma kuwa hatarudi tena kwenye kundi la Jahazi, lakini kuwa na mkataba wa kufanya hivyo.

Alikiri kuwa uamuzi wa kiongozi wa zamani wa Jahazi, Mzee Yussuf, kuachana na taarab baada ya kurejea kutoka Hijja, Makka, umeudhoofisha muziki huo.

"Kwamba sitarajii kurudi Jahazi, yalikuwa maneno tu. Nilipoona wanahitaji mtu wa aina yangu na baada ya kunifuata, nilizungumza nao tukakubaliana,"alisema Ally J, ambaye pia ni mmoja wa watunzi mahiri wa muziki wa taarab nchini.

Mpiga kinanda huyo alisema yeye si mgeni katika kundi la Jahazi kwa vile aliwahi kulitumikia miaka ya nyuma, likiwa chini ya Mzee Yussuf na kwamba aliondoka kwa hiari yake bila kugombana na mtu yeyote.

Ally J alisema anamshukuru Mungu kwamba alipokelewa vizuri Jahazi na kwamba, kurejea kwake hakumaanisha kwamba kundi hilo halina wasanii wengine wazuri wa kiwango chake.

"Si kwamba Jahazi haina wapigaji wazuri, isipokuwa walitaka mtu anayeifahamu vyema mipigo ya Jahazi,"alisema Ally J.

Aliongeza kuwa binafsi anazo njia zake za kimuziki kama ilivyo kwa Jahazi na vikundi vingine vya taarab, lakini hilo haliwezi kumfanya ashindwe kwenda sambamba na kundi hilo kwa wakati huu.

Alisema iwapo ataamua kubadilisha mipigo ya kimuziki ya Jahazi na kuanzisha mipigo ya Five Stars Modern Taarab, atakuwa ameiondoa kwenye reli na kufanya kitu tofauti na kile walichokizoea.

"Mimi na wenzangu kina Jumanne Ulaya na wengine niliowakuta Jahazi, tutakaa na kuona tufanye nini ili kuliendeleza kundi hili kimuziki,"alisema Ally J.

Mtaalamu huyo wa kupapasa kinanda alisema, karibu nyimbo zote alizoshiriki kupiga ala hiyo alipokuwa Jahazi ni nzuri hivyo anaamini ataendelea kutumia ujuzi wake kufanya vizuri zaidi.

Hata hivyo, Ally J amekiri kuwa uamuzi wake wa kurejea Jahazi haukuwafurahisha wasanii na mashabiki wengi wa muziki huo kwa vile kila mmoja ana mtazamo wake.

"Jambo la muhimu ni kwamba nahitaji kufikiria, sio kufikiriwa. Haya ni maisha na maamuzi yangu. Hakuna mdau yeyote wa taarab aliyewahi kunisaidia matatizo yangu ya kimaisha. Tuache maneno maneno, tupige muziki. Tutengeneze nyimbo nzuri,"alisema.

Alisema tayari ameshatunga nyimbo mbili mpya ndani ya kundi la Jahazi, ambazo ni Nataka Jibu na Jicho la Mungu, zilizoimbwa na Mwasiti na Mosi Suleiman.

Alikiri kuwa amekuwa akikumbana na changamoto nyingi katika muziki huo, lakini amekuwa akijitahidi kukabiliana nazo kadri ya uwezo wake.

"Ninachokifanya kwa sasa ni kufikiria nitoe kitu gani kitakachokubalika kwa mashabiki. Hii ni kwa sababu Jahazi imeshatoa nyimbo nyingi nzuri, hivyo mashabiki kwa sasa wanatarajia kuona mambo mapya sio yale yale waliyoyazoea,"alisisitiza msanii huyo.

Pamoja na kujiengua katika kundi la Five Stars Modern Taarab, Ally J alisema kundi hilo bado lipo na litaendelea kufanya maonyesho yake kama ilivyokuwa zamani, japokuwa kwa sasa halina wasanii wa kudumu.

Alisema Five Stars badi ipo na itaendelea kuwepo, isipokuwa yeye ndiye hayupo. Alisema binafsi itakapotokea kundi hilo kupata mwaliko wa kufanya maonyesho, atakuwa akishiriki iwapo kundi lake la Jahazi halitakuwa na kazi siku hiyo.