KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, November 6, 2013

VIKUNDI VYA TAARAB VYAUNDA UMOJAHATIMAYE wasanii na viongozi wa vikundi vya taarab nchini, wameamua kuanzisha
umoja kwa lengo la kuzungumzia matatizo yao.

Lengo lingine la kuanzishwa kwa umoja huo ni kutetea maslahi yao na kupanga
mikakati ya kupanua soko la muziki huo.

Mkurugenzi wa kundi la East African Melody, Ashraf Mohamed amesema
wanatarajia kukutana hivi karibuni kuzungumzia matatizo yao.

Ashraf alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, vikundi vyao
vimekuwa vikitumika kuwanufaisha watu wengine.

Amesema wakati wasanii wamekuwa wakiumia vichwa kutunga, kuimba na kupiga
nyimbo nyingi za taarabu, wanaonufaika ni wajanja wengine.

"Tunadhani huu ni  wakati wa bendi za taarab kujiendesha kibiashara kwani makosa
tunayoyafanya sisi viongozi, yanawaumiza sana wasanii wetu, hivyo ni bora tuamke
ili tupange mambo yetu kwa pamoja,"amesema.

Kiongozi huyo amesema japokuwa wamechelewa kuchukua uamuzi huo, lakini
wanao muda wa kutosha wa kuweza kurekebisha mwenendo na mwelekeo wao.

FIVE STARS SASA KUITWA VIP MODERN TAARABUONGOZI wa kikundi cha taarab cha Five Stars, umeamua kubadili jina la kundi hilo
na kujiita VIP Modern Taarab.

Habari kutoka ndani ya kundi hilo zimeeleza kuwa, uamuzi huo umelenga kubadili
mwelekeo na kukifanya kikundi hicho kiwe na mwelekeo mpya.

Hata hivyo, viongozi wa kundi hilo hawakuwa tayari kusema lolote kuhusu uamuzi
huo kwa vile jambo hilo limefanywa kuwa siri kubwa.

Lakini habari za uhakika zimeeleza kuwa, tayari uongozi umeshalipitisha jina hilo na
baadhi ya wadau wa taarab wamelisifu kwa madai kuwa ni zuri.

Kundi la Five Stars lilijipatia sifa kubwa wakati lilipoanzishwa kutokana na kuibuka na
vibao vyenye mvuto, ambavyo viliwapa homa viongozi wa vikundi vingine.