Tuesday, December 20, 2016
TMK MODERN TAARAB YAZINDULIWA KWA KISHINDO
KIKUNDI kipya cha taarab cha TMK Modern, mwishoni mwa wiki kilifanya onyesho kabambe la uzinduzi, lililofanyika kwenye ukumbi wa Dar Live, Mbagala, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki.
Katika onyesho hilo, kundi hilo lilisindikizwa na bendi ya Twanga Pepeta, Madada sita na mwimbaji nyota wa muziki huo, Leila Rashid kutoka Jahazi.
Wakiongozwa na waimbaji nyota na wakongwe, Mwanahawa Ali, Omar Tego na Maua Tego, kundi hilo liliwafanya mashabiki wafurike kwa wingi stejini kucheza muda wote wa onyesho.
Wakati huo huo, uongozi wa kundi jipya la muziki wa taarab nchini, 'Yah TMK Modern Taarab', umewataka wapenzi wa muziki huo, kuipokea bendi yao ambayo inaanza rasmi maonyesho yake ya katika kumbi mbalimbali hapa nchini.
Mkurugenzi wa kundi hilo, Said Fella amesema baada ya kufanya utambulisho wa kundi hilo mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Dar Live, sasa wanaanza rasmi maonyesho katika kumbi mbalimbali za burudani hapa nchini.
Fella alisema kundi hilo litaanza onyesho lake la kwanza Desemba 23, mwaka huu, kwenye ukumbi wa CCM Kigamboni, wakati siku ya mkesha wa Krismas watakuwa kwenye ukumbi wa Mpo Africa, ulioko
Tandika.
Alisema Desemba 25, kundi hilo litakuwa ndani ya ukumbi wa Lekam ulioko Buguruni na Desemba 26, litakuwa kwenye ukumbi wa Lanch Time, Mazense.
Fella alisema kuwa kundi hilo limejipanga kutoa burudani ya aina yake na kudhihirisha kuwa, kwa sasa ndilo moto wa kuotea mbali.
"Lengo letu ni kutoa burudani, tumejipanga kutoa burudani ya aina yake, wanamuziki wapo vizuri na kila mtu anajisikia kufanya kazi yake vizuri kabisa," alisema Fella.
Kundi hilo linaundwa na wasanii mbalimbali nguli, akiwepo Mwanahawa Ali, Fatma Mcharuko, Aisha Vuvuzela, Omar Tego, Maua Tego na wapiga vyombo kina Mohamed Mauji, Mussa Mipango, Chid Boy (kinanda) na Babu Ally Kichupa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment