Wasanii na wanamichezo hao wamepewa tuzo hizo leo jioni katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.
Utoaji wa nishani hizo ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za miaka 51 ya uhuru wa Tanzania Bara, zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Wasanii na wanamichezo waliopewa nishani hizo ni kiongozi wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo, kiongozi wa zamani wa bendi ya Dar es Salaam International, marehemu Marijani Rajabu na mwimbaji mkongwe wa taarab, Fatuma Baraka 'Bi Kidude'.
Wengine ni aliyekuwa msanii maarufu wa maigizo na filamu nchini, marehemu Fundi Saidi 'Mzee Kipara' na mwanariadha mkongwe, John Steven Akwari.
Gurumo, Bi Kidude na Akwari walihudhuria hafla hiyo na kuvishwa nishani zao na Rais Kikwete wakati nishani za Marijani na Mzee Kipara zilipokelewa na watoto wao.
Nishani ya sanaa na michezo, hutolewa kwa wasanii na wanamichezo mashuhuri, ambao kazi zao za sanaa au michezo zimeipatia sifa kubwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bi Kidude hakuweza kwenda eneo la kupokea nishani kutokana na hali ya afya yake kutokuwa nzuri. Ilibidi Rais Kikwete amfuate mahali alipokuwa ameketi na kumtunukia nishani yake.
Bi Kidude, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka zaidi ya 100 ni mwimbaji taarbab mkongwe aliyedumu kwenye fani hiyo kwa zaidi ya miaka 50. Ni msanii pekee wa taarab mwenye sifa zilizotukuka kutokana na ukongwe wake na umahiri wake katika kuimba taarab.
Gurumo alianza muziki 1960 na kushiriki katika bendi mbalimbali kama vile NUTA, JUWATA, OTTU, Atomic Jacc, Kiko Kids, Jamhuri Jazz, Kilwa Jazz, Rufiji Jazz, Mlimani Park, Msondo Ngoma. Ametunga nyimbo nyingi zinazoelimisha jamii kuhusu kuheshimu na kufanyakazi kwa juhudi na maarifa, kulinda uhuru wa nchi, kudumisha usawa, haki na amani na kuwaasa wazazi kutimiza wajibu wao kwa kulea watoto na vijana kutimiza wajibu wao.
Marehemu Marijani, maarufu kama Jabali la Muziki, alifariki dunia mwaka 1995. Alitoa mchango mkubwa katika tasnia ya muziki, alishiriki kutunga na kurekodi nyimbo zaidi ya 103, ambazo zilirekodiwa RTD, nyimbo zake zilikuwa na mafunzo mengi kwa jamii na zinaendelea kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini.
Mzee Kipara mwaka 1962 alijiunga na waigizaji wa Redio Tanzania, pia ameshiriki maigizo na tamthiria nyingi za kwenye televisheni kama vile Hujafa hujaumbifa, Fukuto, Radi, Gharika, Tufani na Tetemo.
Mzee Akwari aliweka historia ya pekee nchini mwaka 1968 pale aliposhiriki mbio za marathoni za Olimpiki na kuumia goti na kutoka malengelenge, lakini aliushangaza ulimwengu alipoendelea na kumaliza mbio hizo. Alipoulizwa, alisema 'mimi sikutumwa kuja kuanza mbio, nimetumwa kumaliza mbio'. Maneno hayo yamekuwa yakitumika kama mifano duniani.
No comments:
Post a Comment