Ni utunzi na uimbaji wake Mfalme Mzee Yussuf, ngoma kali ambayo inakuwa zawadi nzuri ya kufungia mwaka 2014 na kufungua 2015.
Kazi hii imefanyika katika studio za Sound Crafters, Temeke jijini Dar es Salaam, chini ya producer Enrico. Ndani ya wimbo huu utakutana na mipini mikali ya Mohamed Mauji aliyetambaa vizuri na gitaa lake la solo huku kwenye kinanda kazi kubwa ikiwa imefanywa na Chid Boy.
Kama ilivyo kawaida ya Mzee Yussuf kwenye ngoma ambapo hufunika na vionjo vikali, humu nako ametisha sana, utakutana na vitu vya “Songa Ugali Tule” na vikorombwezo vingine kibao.
Je huu ndio wimbo wa mwisho wa Mzee Yussuf? Sahau kabisa hiyo kitu. Mzee Yussuf ameiambia Saluti5 kuwa lolote linaweza kutokea.
“Ningependa kuacha kuimba mwaka huu, lakini ni mapokeo ya kazi hii ndiyo yatakayoamua, nitaangalia mashabiki wanaipokea vipi, nitaangalia pia namna malengo yangu mengine yatakavyokuwa.
Ninatamani “Mahaba Niue” uwe wimbo wangu wa mwisho, lakini sisemi kuwa huu ni wimbo wangu wa mwisho,” alisema Mzee Yussuf katika maongezi yake na Saluti5
No comments:
Post a Comment