KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Monday, January 7, 2013

MZEE YUSSUF, KHADIJA NI VILIO, MASHABIKI WASHIKWA NA SIMANZI

Richard Bukos na Shakoor Jongo
Ndugu wanapogombana shika jembe ukalime, wakipatana nenda ukavune, ngano hiyo ilidhihirika kwa kaka na dada, Mzee Yusuf ‘Mfalme’ na Khadija Yusuf ambao mwaka jana walikosana kiasi cha kunyimana salamu na kusemeana mbovu kwenye vyombo vya habari.

Mzee na Khadija, Ijumaa iliyopita kwenye onesho la uzinduzi wa albamu mpya ya Kundi la Jahazi Modern Taarab, My Valentine, waliangua vilio vilivyoambatana na machozi, walipokuwa wakiimba pamoja wimbo “Undugu Hazina Yetu.”

Ndugu hao wa damu walipokuwa wanaangusha vilio, mashabiki ambao walihudhuria onesho hilo kwenye Ukumbi wa PTA, Temeke, Dar, walitafsiri kuwa mashairi ya wimbo huo yaliwachoma, hivyo kuwakumbusha walipokuwa katika ‘bifu’ zito.

Mwanzoni mwa mwaka jana, Khadija alilikacha Kundi la Jahazi linalomilikiwa na Mzee, kisha kwenda kushiriki kuanzisha Five Stars Modern Taarab na akiwa huko, alidaiwa kumpiga madongo mengi kaka yake.

Katika tukio la Ijumaa, aliyeanza kumwaga machozi ni Khadija kabla ya Mzee kuguswa, naye kuangusha kilio chenye ujazo wa kutosha.
Wakati wawili hao wakilia, baadhi ya watu wa karibu walifika kuwasaidia ili waendelee kuimba.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Khadija ambaye machozi yalikuwa mengi kutokana na kuzidiwa na hisia za uchungu, hivyo watu hao kulazimika kumuondoa ukumbini haraka.

Khadija, alipotolewa ukumbini, alipandishwa kwenye gari ambalo liliondoka naye, kabla ya kumrejesha baada ya nusu saa kuendelea kuwajibika jukwaani.
Mwanamuziki huyo, hivi karibuni alirejea Jahazi baada ya kupata suluhu na Mzee, hivyo kuliacha Kundi la Five Stars Taarab kwenye mataa.

Awali, Mzee ndiye aliyeanza kupanda jukwaani, akamkaribisha Khadija na kuanza kuimba Undugu Hazina Yetu lakini wimbo haukufika katikati, wawili hao walikumbatiana kabla ya kuangusha vilio.

Wakizungumza ukumbini hapo, Khadija na Mzee walisema kuwa safari ndefu ya maisha yao iliwakumbusha mbali na kuwataka walimwengu kutoingilia ugomvi wao, kwani wao ni ndugu na hata wakitofautiana, mwisho wa siku wataelewana.

Tukio la Mzee na Khadija likiwa halijapoa, ukumbi wa PTA uliingia kwenye mshikemshike wa aina yake baada ya wanenguaji wawili wa Kundi la Kanga Moja kucharukiana na kupeana mkong’oto.

Tifu la wanenguaji hao ambapo mmoja wao tulimnasa kwa jina la Rehema, lilizua patashika, hasa baada ya kuwa wagumu kuamulika.
Juhudi za walinzi na waratibu wa ‘shoo’ hiyo ya Jahazi, zilisaidia kuwatuliza wanenguaji hao, lakini baada ya kuamuliwa, Rehema aliangusha kilio huku akijiapiza kulipa kisasi.

(Habari, Picha kwa hisani ya gazeti la Amani)

No comments:

Post a Comment