KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Saturday, August 11, 2012

KHADIJA KOPA: HAKUNA ANAYEWEZA KUNIFIKIA KWA UIMBAJI TAARAB

KWA umbo, Khadija Omar Kopa ni mnene. Rangi yake ni nyeusi yenye mng’ao. Uso wake hujawa na tabasamu muda wote utadhani hajui kitu kinachoitwa kukasirika.
Licha ya kuwa na umbile hilo, Khadija ni mwepesi wa kuunyonganyonga mwili wake atakavyo awapo stejini, akiimba nyimbo za muziki wa taarab. Sauti yake nayo ni maridhawa na yenye mvuto wa pekee.
Sifa hizo ndizo zilizomfanya mwanamama huyo apachikwe jina la ‘Malkia wa Mipasho’ nchini. Waliompa jina hilo hawakubahatisha, walitambua vyema kwamba uwezo wake katika fani hiyo ni mkubwa.
Mwanamama huyo alianza kuvuma kimuziki miaka 20 iliyopita alipokuwa katika kikundi cha taarab cha Culture cha Zanzibar, ambako aling’ara kwa vibao vyake kama vile ‘Kadandie’, ‘Wahoi’ na ‘Daktari’.
Anakiri kwamba, akiwa katika kundi hilo, aliweza kujifunza mambo mengi kuhusu muziki wa taarab ikiwa ni pamoja na utunzi wa nyimbo, uimbaji bora na upangiliaji wa muziki.
"Culture ni chuo, ambacho nilianza kujifunza uimbaji na utungaji wa mashairi, nilipata uzoefu wa kutosha na mashabiki walinikubali," alisema Khadija alipokuwa akizungumza na mwandishi wa makala hii hivi karibuni mjini Dar es Salaam.
Baada ya kutoka Culture, mwimbaji huyo alitua katika kundi la TOT mwaka 1992 akiwa mmoja wa waanzilishi wake, ambapo alianza kung’ara kwa kibao cha ‘Tx mpenzi’, ‘Ngwinji’, ‘Wrong number’, ‘Mtie kamba mumeo’ na nyinginezo.
“Kule Culture ni kama vile nilikuwa nasafisha nyota yangu, lakini baada ya kujiunga na TOT ndipo hasa mambo yangu yalipoanza kuwa mazuri,”alisema.
Khadija alikorofishana na uongozi wa TOT mwaka 1993 baada ya yeye na mwimbaji mwenzake, Othman Soud kuamua kuondoka kinyemela na kwenda Dubai, ambako walishiriki kuanzisha kundi la East African Melody.
Mara baada ya kurejea nchini kutoka Dubai, mwanamama huyo alilazimika kujiunga na kikundi cha Muungano Cultural Troupe kwa vile uongozi wa TOT uligoma kumpokea.
Kujiunga kwa Khadija na Othman katika kikundi cha Muungano kulisababisha kuwepo kwa ushindani mkali kati ya vikundi hivyo viwili, ambavyo vilifanya maonyesho kadhaa kwa ajili ya kuonyeshana nani mkali.
Akiwa Muungano, Khadija aling’ara kwa vibao vyake murua kama vile ‘Homa ya Jiji’, ‘Kiduhushi’ na ‘Umeishiwa’. Pia kulizuka ushindani mkali kati yake na marehemu Nasma Khamis ‘Kidogo’, ambaye alichukuliwa na TOT kutoka Culture kwa lengo la kuziba pengo lake.
"Nilipojiunga na Muungano nililiwezesha kundi hilo kuwa juu na tuliwapa wakati ngumu kweli wapinzani wetu TOT,”alisema mwimbaji huyo.
Mwaka 1998, mwanamama huyo aliamua kurejea TOT, akibadilishana na Nasma, ambaye aliamua kuhamia Muungano, hali iliyoongeza ushindani mkali kati ya vikundi hivyo.
Khadija anasema alikuwa akihama mara kwa mara kutoka kundi moja hadi jingine kutokana na matatizo ya uongozi na maslahi duni. Alisema msanii siku zote hufurahia kazi yake pale anapopata maslahi mazuri.
Mwimbaji huyo alisema kwa sasa anajivunia umaarufu aliojijengea nchini kutokana na uimbaji wake maridhawa na kuongeza kuwa, muziki huo umemwezesha kutembelea mikoa yote ya Tanzania.
"Usifanye mchezo, taarab hivi sasa inalipa, lakini ukiwa unamiliki kundi lako. Amini usiamini, taarab ipo juu kuliko muziki mwingine wowote ule," anasema mwanamama huyo.
Khadija alisema kwa sasa anajiandaa kuzindua wimbo wake mpya, utakaojulikana kwa jina la 'Top in Town'. Alisema amechelewa kuuzindua wimbo huo kutokana na kukosa wadhamini.
Mwimbaji mwenye sura yenye mvuto na mwili tipwatipwa alisema, wimbo huo umeshakamilika na kuanza kupigwa kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini.
"Ninachokifanya hivi sasa ni kuutambulisha wimbo huu kwa mashabiki wangu. Nikipata mdhamini nitauzindua rasmi kwa onyesho maalumu," alisema.
Gwiji huyo wa mipasho alisema, licha ya kuwepo kwa ushindani mkubwa katika muziki wa taarab hivi sasa, bado anaamini yeye ndiye malkia wa muziki huo na hakuna mwimbaji anayeweza kumfikia.
"Ninachowaambia wapinzani wangu ni kwamba, waparamie miti yote, lakini wajihadhari na mbuyu. Hawawezi kunifikia hata kwa bahati mbaya," alijigamba Gwiji huyo anayependwa na mashabiki wengi kutokana na uchangamfu wake awapo stejini.
Khadija alilielezea soko la muziki wa taarab hivi sasa kuwa ni kubwa, tofauti na miaka ya nyuma na kuongeza kuwa, muziki huo umekuwa na manufaa makubwa kwa wasanii.
Mwimbaji huyo mahiri alisema kwa sasa hana mpango wa kuhama katika kikundi cha sanaa za maonyesho cha Tanzania One Theatre (TOT) na ameahidi kuwapa raha zaidi ya muziki huo mashabiki wake.
Mbali na kutembelea mikoa yote nchini, Khadija alisema muziki huo umemwezesha kusafiri katika nchi kadhaa za Ulaya, Arabuni na Afrika. Alizitaja nchi hizo kuwa ni Marekani, Ufaransa, Ureno, India, Comoro, Kenya, Zimbabwe na Oman.
Mwimbaji huyo alisema pia kuwa, muziki wa taarab umemwezesha kujenga nyumba mbili katika kisiwa cha Unguja na pia kuendesha maisha yake bila matatizo.
Khadija, ambaye alizaliwa miaka 47 iliyopita katika kisiwa cha Unguja,
amebahatika kupata watoto wanne, lakini mmoja, ambaye alikuwa amerithi kipaji chake, Omar Kopa alifariki dunia mwaka juzi.
Anakiri kwamba kifo cha Omar kilikuwa pigo kubwa kwake na familia yake kwa sababu alikuwa na kipaji cha hali ya juu cha muziki. Anasema alikuwa akisaidiana naye katika utunzi wa nyimbo.

No comments:

Post a Comment