KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, August 31, 2012

HALI YA BI KIDUDE INALETA MATUMAINI


HALI ya msanii mkongwe wa taarab nchini Fatma bint Baraka ‘Bi kidude’, inaendelea vizuri licha ya kulazwa tena hospitali Jumapili iliyopita, na taarifa zimeeleza kuwa, kuna uwezekano mkubwa akaruhusiwa leo.
Mwanzoni mwa mwezi huu, msanii huyo aliugua na vipimo vya kitabibu vilibaini kuwa, anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari, lakini kabla ya kulazwa majuzi, alikuwa akiuguzwa nyumbani kwa mwanawe Bububu meli nane.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka katika hospitali ya Zanzibar Medical Group iliyopo Shangani, Mkurugenzi wa kikundi cha Tausi Taarab, Maryam Hamdan, alisema hali ya Bi Kidude inaendelea vyema  tafauti na alivyokuwa wakati akipelekwa hospitalini hapo.
 Maryam, mtu wa karibu sana na Bi Kidude, amesema awali, hali ya msanii huyo ilikuwa hairidhishi kutokana na kuvimba miguu  pamoja na tumbo.
 “Alipofikishwa hapa hakuwa katika hali nzuri kwani sukari ilikuwa ikipanda na kushuka, lakini sasa tunashukuru ameanza kupata nafuu na kama hali itaendelea vizuri kama hivi, huenda kesho (leo), atapewa ruhusa”,
"Akipimwa sukari asubuhi inakutwa iko nane na ikifika saa kumi jioni hupanda hadi 29,  jambo linalotia wasiwasi kwamba kuna chakula anachokula mchana kina sukari", aliongeza Maryam.
Naye Juma Mohammed wa HABARI MAELEZO, anaripoti kuwa, wadau wa sanaa nchini wamewatupia lawama baadhi ya wasanii wa Zanzibar kwa kumtelekeza mwenzao huyo.
Mmoja wa watu wa familia ya Bi Kidude ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema  tangu alipoanza kuugua, ni wasanii wachache mno  waliopita kwake angalau kumjulia hali licha ya kutolewa matangazo mbalimbali juu hali msanii huyo.
“Tunashangazwa sana na hawa wasanii wenzake, si wengi wanaokuja kumjulia hali… kwa namna anavyoishi nao kwa ukaribu na kupendwa na kila mmoja, hatukutarajia kama wangefanya hivi”, alilalamika mwanafamilia huyo.
Hivi karibuni, Makamu wa Kwanza wa Rais  Maalim Seif Sharif Hamad, alifanya ziara kwenda  kumjulia hali msanii huyo anayekisiwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 90, ambaye  ameitangaza sana Zanzibar kwa kuimba nyimbo mbalimbali mashuhuri zilizorekodiwa na magwiji kama Sitti Bint Sadi aliyekuwa akitamba kwa muziki wa taarab katika upwa wa Afrika Mashariki na nje.

Tuesday, August 28, 2012

ISHA MASHAUZI: SIJAWAHI KUHUSIANA KIMAPENZI NA THABIT ABDUL AU MZEE YUSUPH



MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Isha Ramadhani amesema hafikirii kuolewa kwa sasa kwa sababu lengo lake kubwa ni kukiimarisha kikundi chake cha Mashauzi Classic. Isha alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipohojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Channel Five. Makala hii ya ana kwa ana inaeleza mengi zaidi kuhusu mahojiano hayo kama yalivyonukuliwa na mwandishi wetu.
SWALI: Kwa nini wanawake wengi wanashindwa kudumu kwenye ndoa zao kwa muda mrefu?
JIBU: Si kweli kwamba wanaoshindwa ndoa, wanaume ndio wanaokuwa wakorofi.
Wakati mwingine ni wanawake wenyewe. Kila mmoja anakuwa na mtazamo wake.
Mi mwenyewe napenda kuolewa, lakini kwa sasa kutokana na kazi yangu, nimeona ni bora niimarishe bendi ndipo baadaye nifikirie suala la kuolewa, maana ndoa ni suala la majaliwa, unaweza kufikiria utaolewa, lakini kumbe usiolewe. Kwa hiyo baadaye naweza kufikiria kuolewa, lakini kwa sasa napumzika kidogo.
SWALI: Inawezekana hayo yote yametokea kwa sababu uliolewa mapema sana?
JIBU: Naweza kusema sikuolewa mapema sana kwa sababu sina ndoa moja. Nina ndoa mbili.
SWALI: Kwa maana hiyo inawezekana wewe ndiye unayetafuta bucha?
JIBU: Unajua kumpata mpenzi wa kweli ni sawa na kuingia kwenye pori kumsaka mnyama mkali, ambaye binadamu tunaogopa. Inategemea, unaweza ukabahatisha, lakini pia unaweza ukakosa. Lakini yote mawili yanawezekana, ni sawa na bahati nasibu. Ni sawa na kupapasa kizani, utakachoibuka nacho ndicho hicho hicho.
SWALI: Wanawake wengi maarufu huwa wameolewa, wakaachika ama wanakuwa na wachumba wengi sana. Hili likoje kwako?
JIBU: Mimi kwa upande wangu, naweza kusema wakati nilipoolewa kwa mara ya kwanza, nilikuwa sijulikani. Waliokuwa wananijua ni familia yangu na marafiki zangu na ndugu zangu. Nilipokuja kuolewa mara ya pili, nilikuwa najulikana, lakini kutokana na hitilafu zangu mimi na yeye, hatukuweza kudumu kwa muda mrefu.
Si kwamba niliachika kwa sababu ya umaarufu, la hasha au ukiwa maarufu unakuwa na wapenzi wengi, hapana. Naweza kukwambia kwa sasa nina mpenzi mmoja, huwezi kuamini, lakini ni ukweli kutoka moyoni mwangu. Nampenda ananipenda, namjali ananijali.
Wapo wanaosumbua kwa sababu wapo wanaokuja kwa nia nzuri, anaomba namba yako ya simu, anasema oooh, nitakuhitaji, lakini mwisho wa siku anakusumbua, oooh nakupenda, ooh kila ninapokuona kwenye TV, napenda kukuona vile kama unavyocheza, lakini tuwe wawili tu.
Lakini hayo yote yanategemea na wewe mwenyewe, ukiwa na tamaa, ukiona ana chapaa, unajikuta unakwenda, lakini kwa mtu kama mimi sidhani kama ninayo tamaa ya pesa kwa sababu mimi mwenyewe najua kutafuta.
SWALI: Kuna mtazamo kwamba mwanamke anapomiliki bendi, lazima kunakuwa na mwanaume nyuma yake, ambaye ndiye anayemuunga mkono. Kuna ukweli wowote kuhusu msemo huu?
JIBU: Hicho kitu sikikatai, inawezekana kabisa kipo kwa sababu haiwezekani mtu kuja kuwekeza kwako bila sababu maalumu, inawezekana kabisa mtu akaja kuwekeza kwako kwa sababu maalumu, akijua kuna kitu ambacho atakipata.
SWALI: Hivi asili yako hasa ni wapi kwa sababu ulivyo, unaonekana kuwa ni mtanzania, lakini umechanganya marashi fulani. Hebu tueleze kwenu hasa ni wapi?
JIBU: Mimi na taarabu ni vitu viwili tofauti, lakini yote haya ni kwa sababu ya kutafuta maisha. Mimi hasa chimbuko langu kwa wazazi wangu, hasa upande wa baba, wametokea Burundi. Kwa hiyo mimi jina langu halisi, ambalo linatambulika katika ukoo, naitwa Mlundi.
Kwa hiyo baada ya wazazi wetu kutoka kule Burundi, wakawa wanaishi Tanzania. Ndio sababu najiita mkuria wa kwanza kuimba taarabu. Kwa hiyo Musoma ndiko hasa nilikokulia, lakini kiasili hasa, mimi siyo mtu wa Musoma, asili ya wazazi wangu ni Burundi.
Baada ya hapo, wazazi wangu wakaamua kuhamishia maisha yao Dar es Salaam. Ni kuanzia hapo, nilisoma Dar es Salaam na kukulia Dar es Salaam. Kwa hiyo hata kuolewa, niliolewa Dar na walionilea, baadhi yao ni watu wa Pemba.
Mama yangu alikuwa msanii, kwa hiyo kila alipokuwa akitoka, tuseme saa mbili usiku, alikuwa akiniacha kwa majirani zetu, ambao wengi walikuwa Wapemba, ndio sababu na mimi nilikuwa naitwa Mpemba kwa sababu hata lafudhi yangu ilikuwa kama ya kwao, lakini mimi si mpemba hata kidogo, sihusiki nao kwa lolote.
SWALI: Kwa hiyo ile stori kwamba wewe na Mzee Yusuph ni ndugu haina ukweli wowote?
JIBU: Hapana, mimi na Mzee Yusuph hatuna undugu wowote.
SWALI: Kwa nini muziki wa taarab unaitwa mipasho?
JIBU: Ni kwa sababu tunaimba vitu, ambavyo ni vya kweli, ndio maana wakaita mipasho, ingawaje mtu akisikia wimbo ukiimbwa, anadhani kaambiwa yeye, ndio sababu wanasema anayejishuku, hajiamini.
SWALI: Kwa nini unaitwa Mashauzi? Una dharau sana?
JIBU: Mimi nasema anayenizungumzia, mara nyingi anakuwa hanitambui. Mimi ni mtu ambaye napenda sana kucheka na watu, napenda kutaniana na watu, naweza nikafika sehemu, watu wasiponiona, labda siku mbili au tatu, wanaweza kunipigia simu wakaniuliza, inakuwaje mbona hatukuona? Isha tumekumiss sana, hebu njoo mahali fulani. Kwa hiyo mtu anayenizungumzia kwa mwelekeo huo, hanijui kiundani.
SWALI: Hivi wewe huwa unaandika maishairi ya muziki?
JIBU: Unajua unaweza kukaa na mtu mahali, lakini huwezi ukajua hisia zake zikoje. Wewe unaweza kuzungumza kitu, lakini hujui kwamba hicho kitu mimi kimenigusa. Kwa hiyo ninapoona hivyo, namtumia ujumbe mkurugenzi wangu, ambaye ni Thabiti Abdul na kumweleza kwamba kuna mtu amezungumza kitu hiki na kile kimenigusa sana, naomba unitungie mashairi na yeye atafanya hivyo.
Kwa mfano, kuna wakati tulipokuwa tumekaa pale nje, kuna mtu alisema neno kuhusu mimi, nikamwambia kama nimekukera, hama mji. Inapokuwa hivyo, namweleza mkurugenzi wangu kwamba kuna hiki na kile na yeye anaandika, anaweka muziki na sauti, nyimbo inakuwa imekamilika. Baadaye ananifuata na kuniambia wimbo umekamilika kwa hiyo kazi yangu inakuwa ni kuweka vikorombwezo vya chini. Mara nyingi hivyo huwa vinatoka kichwani.
SWALI: Taarabu ina mashabiki wengi sana, lakini mara nyingi wanakuwa wale, ambao mwonekano wao ni tofauti na wengine na kwa wanawake, inakuwa ni wale, ambao wameshindikana katika familia zao. Kwa nini inakuwa hivyo?
JIBU: Hakuna uhusiano isipokuwa vile vitu vinavyoimbwa, wao ndio wanakuwa wanapenda. Wanakuwa wanapenda kupashana, kuchambana, labda niseme hivyo.
Lakini nikirudi kwenye swali la awali, si watu wote wanaopenda taarabu wanakuwa ni watu walioshindikana. Sasa hivi naweza kusema kwamba taarabu inapendwa hata na akina baba, ambao ni marijali, wanapenda watoto, wanapenda wasichana, utakuta mtu anakwenda klabu huku akiwa anamjua mwimbaji taarabu.
Zamani wanaume walikuwa wanahisi kwamba mwanamke akipenda taarabu, huenda ni shangingi na vivyo hivyo mwanaume akipenda taarabu, alikuwa akionekana namna gani vipi.
SWALI: Hivi inakuwake mwanaume, ambaye namna gani vipi anaweza kuwachukua shoga zake wa kike wanne au hata watano, akajiweka katikati yao na kucheza kama vile naye ni mwanamke ama shughuli ni ya kwake. Inakuwaje kitu kama hicho kinatokea?
JIBU: Niseme tu kwamba, awali ya yote namshukuru Mungu kwamba sisi wanawake bado tunaendelea kuzaa. Lakini huwa nasikia uchungu sana ninapoona kitu kama kile, lakini huwezi kusikia uchungu, ukamfuata mtu na kumweleza acha maana jibu atakalokupa, ukirudi nyumbani unaweza kutafuta maji ili ushushie.
Wale ni watu ambao wanakuwa wameshaamua kuishi maisha ya aina fulani. Kuna wengine ukionyeshwa na kuambiwa huyu ni dizaini fulani, unaweza kukataa.
SWALI: Mara ya mwisho kulia ilikuwa lini?
JIBU: Siku kama nne hivi zilizopita.
SWALI: Nini hasa kilitokea?
JIBU: Naweza kusema ni sababu ya mapenzi.
SWALI: Unataka kusema ni maumivu? Ulilizwa?
JIBU: Hapana hapana, unajua wakati mwingine furaha nayo inaweza kuleta kilio. Lakini sikulia kwa kuumizwa, nililia kwa kujiumiza kwa maana kwamba nilipatwa na kitu kama wivu fulani hivi.
SWALI: Kuna wasanii fulani wa kundi la taarab la Five Stars walipata ajali ya barabarani kule Morogoro mwaka jana. Ulijisikiaje baada ya kupata taarifa hizo?
JIBU: Ukweli ni kwamba kila chenye roho lazima kitaonja mauti, lakini mauti yanapomfika mtu wa karibu yako, huwa yanaumiza sana, na hasa ukikumbuka ajali yenyewe jinsi ilivyotokea, ni kitu ambacho tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Binafsi siwezi kusema kwamba nilishuhudia, lakini nilikuwa mmoja kati ya watu wa mwanzo kupata taarifa za ajali ile kuliko watu wengine. Ah, inasikitisha sana.
SWALI: Kuna taarifa kwamba matiti yako yametengenezwa na wachina na wewe ulikuwa mtu wa mwanzo kuyatengeneza. Je, kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizo?
JIBU: Asante sana kwa swali lako. Naweza kusema kwamba, huyo mchina mwenyewe mimi huwa nakutana naye barabarani. Mimi nilivyo ndivyo jinsi nilivyoumbwa na Mungu. Kama nimejaaliwa au vinginevyo, siwezi kujua. Lakini sijawahi kwenda mahali popote kuomba ama kutaka umbo langu liboreshwe.
Sijui huyo aliyeandika kwenye gazeti kwamba aliniona au vipi au aliamua tu kufanya hivyo ili auze gazeti lake, lakini sijawahi kufanya kitu kama hicho kwa sababu mimi ni mtoto wa kiislamu na dini yetu inazuia kufanya kitu kama hicho.
SWALI: Unazungumziaje kuhusu masuala ya dini na muziki? Unadhani dini yako inaruhusu wewe kujishughulisha na muziki?
JIBU: Kazi ya muziki ni kazi kama zilivyo kazi zingine, lakini si mbaya mtu kama mimi nikipata muda wakati mwingine kujihusisha na muziki kwa sababu siku zote, kabla sijapanda jukwaani, huwa namuomba Mungu kwa maana hiyo, ukimkumkuka Mungu, siku sote ndivyo atakavyozidi kukujalia na kukuwezesha kufanikiwa katika mambo yako.
SWALI: Hivi jina la Mashauzi limetokea wapi?
JIBU: Jina hilo limetokana na mashabiki. Zamani nilikuwa najulikana zaidi kwa jina la Mama Afrika kwa sababu nilikuwa napenda sana kuvaa kiafrika. Nilipokuwa nikienda kwenye kitchen part, nilikuwa najulikana zaidi kwa jina hilo kwa sababu wakati huo nilikuwa nafanyakazi kama MC.
SWALI: Kwa maana hiyo, kabla hujaanza kuimba ulikuwa MC?
JIBU: Ni kweli kabisa kwamba kabla ya kuanza kuimba taarabu nilikuwa MC. Ilikuwa miaka hiyo kabla sijaanza kuganga njaa.
SWALI: Kila mtu anajijua thamani yake, wewe binafsi unaijua thamani yako?
JIBU: Ni kweli, kwa sasa naijua thamani yangu kwa sababu nilivyokuwa huko nyuma sio sawa na nilivyo hivi sasa.
SWALI: Kwa hiyo thamani yako huwa unaiona?
JIBU: Thamani naiona kwa sababu bila ya wewe mwenyewe kuiona thamani yako, hakuna mtu mwingine anayeweza kuiona.
SWALI: Bangi vipi? Nasikia ndio zako hizo (kuvuta)?
JIBU: Hicho kitu mimi situmii kabisa. Katika vitu ambavyo sijawahi kukifanya ni kuvuta bangi. Muziki mimi upo kwenye damu kwa hiyo siwezi kuunogesha kwa kitu chochote zaidi ya kusema naanza kwa kutaja jina la Mwenyezi Mungu na sasa nakwenda kazini.
SWALI: Gari lako la kwanza kumiliki lilikuwa la aina gani?
JIBU: Gari langu la kwanza lilikuwa Lexas. Ukweli hiyo ni ndoto kubwa niliyokuwa nayo kwa sababu mimi huwa sipendi kitu cha kununuliwa kwa sababu mtu anaweza kukufanyia hivyo, baadaye akaja na kukueleza kitu kingine.
Sasa ikitokea mtaani watu wameshazoea kukuona na kitu fulani, halafu baadaye hicho kitu huna, utakuwa huna mahali pa kuuweka uso wako.Nilikaa na gari hiyo kwa muda wa kama mwaka mmoja na miezi mitatu hivi.
SWALI: Ni kweli kwamba wasanii wa taarab, hasa wa kike wana tabia ya kutembea na waume za watu?
JIBU: Unajua mapenzi ni kitu, ambacho hakiingiliwi. Na mapenzi ni siri, ingawaje sasa hivi imekuwa dhahiri na ndio sababu baadhi yetu tumekuwa tukishutumiwa kwamba unatembea na mume wa mtu, lakini kama tungekuwa tunafanya siri, sidhani kama kuna mtu angekuja kugundua hicho kitu. Kila mtu anataka ajionyeshe kwamba mimi nilikuwa natembea na fulani.
SWALI: Kuna kipindi ulishutumiwa kwa kutimua wasanii wote wa kike kwenye kikundi chako na stori iliyozagaa mjini ni kwamba ulikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Thabiti Abdul. Hebu tueleze mahusiano yako na Thabiti, kuna ukweli wowote kuhusu hilo?
JIBU: Usinione nacheka, nafanya hivyo kwa sababu umeniambia nifunguke. Mimi Thabiti sina mahusiano naye yoyote zaidi ya kazi. Nimemtambua Thabiti miaka mingi iliyopita. Alianza kazi ya sanaa siku nyingi, tangu mimi nikiwa mdogo. Mimi ni mdogo sana kwa Thabiti. Nilikuwa nikimuona akifanyakazi na mama yangu na sehemu nyingine.
Mwaka 2009 wakati nikiwa Jahazi, baada ya kuona mambo yanakwenda longo longo ama mrama, nikaamua kutengeneza albamu yangu mimi kama mimi. Nilianza kushirikiana na watu kama akina Ally J, Fikirini pamoja na Mussa, lakini baadaye nikasema hata, wacha nimshirikishe na huyu mtu ili niweze kupata kitu kizuri zaidi. Ndipo hapo nilipoanza mahusiano ya kikazi na Thabiti Abdul.
Ikaenda hivyo kwa muda mrefu, lakini waswahili wanasema kila mtu na mtuwe ama kila shetani na mbuyu wake. Jinsi tulivyokuwa tumeshibana kikazi, ndivyo watu walivyoanza kututafsiri kivingine. Unajuwa hakuna kitu kizuri kama unapomuelekeza mtu kitu, akaweza kukifanya vile unavyotaka ama kufundisha mtu, lakini akawa haelewi. Kila alichokuwa akikifanya, mimi nilikuwa naelewa. Vile vitu vikamfanya anielewe ndipo tukashikana mpaka kumaliza albamu yangu ya kwanza.
Kamwe hatujawahi kuunganisha viungo vyetu vya uzazi kwa sababu kila mmoja anaye wa kuunganisha naye. Lakini ndio hivyo tena, stori zimeshaenea mjini, lakini nilishawahi kusema kwamba, hakuna kitu chochote kinachoendelea kati yangu mimi na Thabiti.
SWALI: Huko nyuma ulikuwa katika kikundi cha Jahazi kinachoongozwa na Mzee Yusuph, lakini baada ya kutokea purukushani, ukaamua kuanzisha bendi yako na sasa upo na Thabiti, mnafanya kazi kama wakurugenzi. Kitu gani kilitokea kati yako na Mzee Yusuph?
JIBU: Hakuna kitu chochote kibaya kilichotokea kati yangu na Mzee Yusuph. Wakati naanza kufanya zing zong, nilimwambia nahitaji kufanya kitu fulani kutokana na majukumu yaliyonibana na akaniambia sawa. Nikaanza kutengeneza albamu zangu.
Nilipoanza kutengeneza albamu ya pili, ndipo nilipoanza kuona utamu wa vimeo. Ilikuwa kila nikipita huku na kule, naulizwa wewe ndiye Isha Ramadhani, tunakuomba siku fulani tuna kitchen party, uje kutumbuiza. Tunataka ile mama nipe radhi, na nikienda huko naulizwa tukupe shilingi ngapi, wakati mwingine nilipotaka kiasi kidogo cha pesa, waliniongeza, oooh tutakupa shilingi laki mbili.
Kwa hiyo ikafika kipindi nikasema hebu wacha nijaribu, lakini nikaona kwa nini nijaribu, bora nithubutu, kwa kweli nikaweza na sasa nasonga mbele.
SWALI: Kwa hiyo wewe na Mzee Yusuph hamna uhusiano wowote wa kimapenzi?
JIBU: Kusema ule ukweli, Mzee Yusuph ni kama baba yangu, ingawaje kuna watu huwa wanapenda kutuona tukigombana, lakini mimi siwezi kuwa mjinga kiasi hicho. Namshukuru hata yeye mwenyewe ananielewa mimi ni nani na ninataka kufanya nini.
SWALI: Kitu gani kinachokufurahisha katika maisha yako? Dhahabu, maisha mazuri, matiti yako kusimama vizuri kifuani au nywele? Ni kipi kinachokufanya uwe na furaha?
JIBU: Kitu kinachonifurahisha katika maisha yangu ni kuwa na furaha na yule ninayempenda na pia niwe na furaha na familia yangu, nisiwaudhi wazazi wangu wote wawili, bila wao mimi nisingekuwepo, wangeweza kuninyonga miaka mingi iliyopita. Napenda sana kuwa na furaha kila wakati ndio maana huwa sipendi kujiudhi.

Tuesday, August 21, 2012

CHID BENZ AMPA SHAVU KHADIJA KOPA


Kitu kimoja kizuri sana kumhusu Chidi Benz ni jinsi anavyoweza kuthubutu. Msanii anapoweza kuthubutu ina maana kwamba anakua katika sanaa yake na ni sehemu ya ubunifu.
Kama utakumbuka,siku za nyuma kidogo Chidi aliwahi kuthubutu kukutanisha Hip Hop/Bongo Fleva na muziki wa pwani katika kibao Mashaalaah alichoshirikiana vyema na Mzee Yusuph. Mambo yakaenda swadakta.Mashalaah ni mojawapo ya track nzuri mpaka hivi leo.
Katika muendelezo huo huo, hapa Chidi Benz anamshirikisha Malikia wa Mipasho,Bi.Khadija Omar Kopa.Wimbo unaitwa Nampenda Sana.

Monday, August 20, 2012

MAALIM SEIF AMTEMBELEA BI KIDUDE

Na Khamis Haji, OMKR
MSANII mkongwe hapa nchini Fatma Baraka Khamis ‘Bi Kidude’, amewajia juu baadhi ya watu walioeneza uvumi kwamba amefariki dunia.
Bi. Kidude amesema anasikitishwa sana na kitendo hicho cha kuzushiwa kifo wakati bado ni mzima na anafanya shughuli zake kama kawaida.
Msanii huyo alitoa ya moyoni jana, wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, wakati alipomtembelea nyumbani kwa mwanawe huko Kihinani, Wilaya ya Magharibi, ikiwa ni katika ziara zake za kuwatembelea wazee mbalimbali wanaosumbuliwa na maradhi.
Alisema kuwa, kitendo cha watu hao licha ya kumsikitisha yeye binafsi, pia kimesababisha usumbufu na hofu kubwa miongoni mwa jamii na baadhi ya watu ambao walilazimika kufunga safari kuja Zanzibar kutoka nchi mbalimbali.
“Kuna watu wameeneza taarifa za uongo kwamba nimekufa, wapo watu waliofunga safari kutoka nchi tafauti kuja Zanzibar, lakini walipofika walishangaa kuniona nipo hai”, alisema msanii huyo maarufu wa muziki wa taarab hapa Zanzibar na Afrika Mashariki.
Bi. Kidude alieleza kuwa anasumbuliwa na maradhi ya miguu, lakini amekuwa akifanya shughuli zake nyingi za kawaida.
Katika ziara yake ya kuwatembelea wagonjwa na watu wazima iliyoanza juzi, pia aliwafariji, mzee Khamis Makungu wa kijiji cha Ndijani, mzee Abdulrazak Mukri wa Mkunazini, mzee Ali Haji Pandu wa Mpendae na Sheikh Habib Ali Kombo wa Kiembesamaki.

Sunday, August 19, 2012

Wapenzi wasomaji wa blogu huu mpya ya Rusha Roho,

EID MUBARAK
Mikono tupeane
Rehema tutakiane
Upendo tushikamane
Toba tuhimizane
Makosa tusameheane
Yarabi tupe baraka zako
Utukubalie swaumu zetu
Amina yarabi Amina

BI KIDUDE YU HOI KITANDANI

Bi. Kidude yu hoi kitandani kwa kuumwa...........
Licha ya kuwa ametoa mchango mkubwa wa sanaa katika tasnia ya muziki hapa nchini, wasanii na
waandaaji wa matamasha mbali mbali waliokuwa wakimtumia wamemtelekeza msanii maarufu Bi Fatma Binti Baraka (Bi. Kidude) kutokana na hali yake ya kuumwa, ambapo hadi sasa yupo kitandani na
hajiwezi.
Ankal naomba uwafikishie ujumbe huu wasanii wote na waandaaji wa matamasha waliokuwa
wakifanya kazi na bi Kidude kwani anaumwa sana.
Mdau wa Globu ya Jamii Zanzibar

Wednesday, August 15, 2012

Mwanne aja na Dume Mashauzi


MWIMBAJI  wa muziki wa taarab, Mwanne Othman Sekuru, ambaye anatamba katika  wimbo  wa Vifuu Tundu alioshirikishwa na AT, ambao  pia ulipenya katika  tuzo za muziki za Kilimanjaro 2012, anatarajia
kuipua kibao kingine baada ya sikukuu ya Idd El Fitr.
Akizungumza mjini Dar es Salaam leo, Mwanne alisema wimbo huo unakwenda kwa jina la  ‘Midume Mashauzi.
Mwanne amewataka mashabiki wake kukaa mkao wa kupata raha kwani katika wimbo huo, ameachia  madongo, ambayo kama mtu atakuwa na tabia hizo, yatakuwa ni sawa kwake.
"Wimbo huo umetungwa na Mohammed Omari Mkwinda ‘Meddy’, ambaye mara baada ya kuutunga akaniletea, nami nikaweka maneno ya kutia nakshi,"alisema.
Aliyataja baadhi ya maneno hayo kuwa ni 'Watashindana, lakini watashindwa wenyewe', 'Huna thamani kama mkia wa mbuzi', 'Hufuniki wala hufukuzi nzi’.
Mbali ya kuwa  mwimbaji katika kundi la Jahazi Modern Taarab, Mwanne pia ni mtangazaji wa kipindi cha ‘Tamtam za Mwambao’ kinachorushwa katika kituo cha redio ya East Africa ‘EATV’.

Tuesday, August 14, 2012

T MOTO TAARAB KUIPUA VIBAO SITA VIPYA


KIKUNDI cha muziki wa taarab cha Tanzania Moto Modern Taarab 'T-Moto'  kinatarajia kuipua vibao vipya sita baada ya kukaa kimya kwa muda.
Meneja na Ofisa Mipango wa bendi hiyo, Kaisi Mussa Kaisi, alisema jana kuwa, kwa sasa wapi katika maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kurekodi nyimbo hizo.
Kaisi alisema nyimbo hizo, ambazo zimetungwa katika ubora wa juu, zinatarajia kuteka soko na kulipandisha hadhi kundi hilo ambalo lipo katika mikakati ya kuliteka soko la muziki huo.
Alisema mara baada ya kurekodi nyimbo hizo, zitasambazwa na kupigwa katika redio na kisha kufuatia uzinduzi wa albamu utakaofanyika baadae mwaka huu.
Alizitaja baadhi ya nyimbo hizo kuwa ni  ‘Domo la Udaku’ (Jokha Kassim), ‘Behind The Cine’, ‘Wewe sio Daktari wa mapenzi’  ‘Mwanamke Hashuo’,  ‘Jipangeni Upya’ na   ‘Ubaya'. 
Baadhi ya waambaji watakaoimba nyimbo hizo ni Johka Kassim, Nyawana Fundikira, Nassor Hussein, Shinuna Kassim, Mwanahawa Chipolopolo na Aisha Masanja.

Sunday, August 12, 2012

TOT KUVAMIA TANGA IDDI EL FITRI


KIKUNDI cha taarab cha Tanzania One Theatre (TOT) kinatarajiwa kuvamia mkoani Tanga na kufanya maonyesho kadhaa wakati wa sikukuu ya Idd El Fitr.
Katibu wa TOT, Gasper Tumaini amesema leo kuwa, watayatumia maonyesho yao mjini Tanga kutambulisha albamu zao mbili mpya za Full Stop na Mjini Chuo Kikuu.
Tumaini amesema baada ya maonyesho yao ya Tanga, kundi hilo linaloongozwa na Malkia wa Mipasho nchini, Khadija Omar Kopa litafanya ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Mwanza, Shinyanga, Geita, Mara na baadaye kuhitimisha ziara yao katika mikoa ya Tabora na Singida.
Akielezea ratiba yao ya Tanga, Tumaini alisema siku ya Iddi Mosi, watafanya onyesho kwenye ukumbi wa Bandari, Iddi Pili watarindima kwenye Uwanja wa Mkwakwani na Iddi Tatu kwenye ukumbi wa White House uliopo Muheza.
Mbali na Khadija, waimbaji wengine wa TOT wanaotarajiwa kuhanikiza maraha katika maonyesho hayo ni Ally Stars, Abdul Misambano, Mwanamtama Amir, Mariam Khamis na Mwasiti Suleiman.

Saturday, August 11, 2012

DIAMOND APIGA HESABU ZA KUIMBA TAARAB

BAADA ya kutamba kwa muda mrefu katika muziki wa kizazi kipya nchini, msanii nyota wa muziki huo, Naseeb Abdul ‘Diamond’ amesema anafikiria kujitosa katika muziki wa taarab.
Diamond alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, amefikia uamuzi huo kutokana na kuvutiwa na muziki huo wa taarab.
Mshindi huyo wa tuzo mbalimbali za muziki za Kilimanjaro amesema, anajua uamuzi wake huo utawashangaza mashabiki wengi, lakini ni jambo la kawaida kwa msanii.
Diamond alisema hadi sasa anaamini hana mpinzani katika muziki wa kizazi kipya na hakuna msanii anayeweza kufikia kiwango chake hapa nchini.
“Najua watu watanishangaa na kuniona mtu wa ajabu, lakini nimefanya hivyo kwa sababu sina mpinzani katika muziki wa kizazi kipya,”alisema.
Diamond alisema ameamua kupiga miondoko tofauti ya muziki kutokana na kipaji alichonacho katika fani hiyo, ambayo imempatia umaarufu mkubwa.
Kutokana na kipaji chake hicho, Diamond alisema hakuna kitu anachoshindwa kukifanya katima muziki.
“Bado sijaanza rasmi kupiga muziki wa taarab, ninachokifanya kwa sasa ni kufanya tathmini ya soko lake ili kuona kama unaweza kuniletea mafanikio kama ilivyo kwa muziki wa bongo fleva,”alisema msanii huyo.
“Naweza kufanya kila aina ya muziki kwa sababu nina kipaji cha kuimba nyimbo aina zote, hivyo endapo nitafikia muafaka, naweza kufanya kitu hicho ingawa mashabiki wangu watashtuka sana,” alisema.
Diamond alikiri kuwa, muziki wa kizazi kipya umemfanya ajulikane sehemu nyingi duniani, ikiwa ni pamoja na kupata manufaa mbalimbali kimaisha kwa kuishi kwenye nyumba nzuri na kumiliki magari ya kifahari.
Msanii huyo mwenye haiba ya kuvutia alisema, kwake muziki ni kazi kama zilivyo kazi zingine hivyo amekuwa akifanya kazi zake kwa malengo.
Alisema siri kubwa ya muziki wake kuwateka mashabiki wengi ndani na nje ya nchi ni kufanyakazi zake kwa kujituma na pia kujiwekea malengo.
"Sifanyi muziki kwa ajili ya kujifurahisha, kutafuta pesa na kuwaacha mashabiki wangu wabaki na kiu ya burudani,”alisema Diamond.
“Ninapofanya muziki nahakikisha kuwa, nakata kiu ya mashabiki wangu kwa kuwapa burudani wanayoihitaji,”aliongeza.
Katika kufanikisha hilo, Diamond alisema amekuwa na utaratibu wa kushirikiana na watu mbali mbali kwa vile anaamini sio rahisi kuweza kufanya kila kitu peke yake.
Alisema miongoni mwa watu, ambao wamekuwa wakimpa ushirikiano mkubwa katika kazi zake ni wacheza shoo kwa vile wamekuwa wakibuni vionjo vipya kila kukicha.
"Siwezi kuwa na ubahili ninapofanya kazi na hili ndilo lililonifanya nizidi kusonga mbele katika kazi ya muziki. Ili upate ni lazima utoe na ili uwafurahishe mashabiki wako ni lazima uzingatie kanuni hizo,”alisema.

FELLA AFYATUA ALBAMU YA TAARAB


KIONGOZI wa kundi la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family, Saidi Fella amesema yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha albamu yake ya muziki wa taarab.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Fella alisema tayari amesharekodi nyimbo tano za muziki na yupo katika maandalizi ya kuzindua albamu hiyo.
Fella alisema hadi sasa bado hajaipa jina albamu hiyo na kwamba amerekodi nyimbo zake akiwa na bendi yake ya Mkubwa na Wanawe, aliyoianzisha hivi karibuni.
“Ninachokifanya kwa sasa ni kuandaa maonyesho, ambayo nitaimba nyimbo hizo nikiwa na bendi yangu,”alisema kiongozi huyo na mwasisi wa TMK Wanaume Family.
Fella alisema ameamua kushika kipaza sauti na kuimba kwa lengo la kuongeza ujuzi wake baada ya kufanya vizuri katika muziki wa kizazi kipya.
Mkongwe huyo alisema baada ya uzinduzi wa albamu yake, atakuwa tayari kupanda jukwaa moja na kikundi chochote cha muziki huo kwa lengo la kufanya maonyesho ya pamoja.
“Cha msingi ni kujadili tu mambo ya maslahi, nikiridhika nitaimba,”alisema.
Kwa mujibu wa Fella, katika albamu yake hiyo mpya, amewashirikisha baadhi ya waimbaji nyota wa muziki huo kama vile Hassan Kumbi, Maua Tego, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ na Khadija Omar Kopa.

BANZA STONE AJA NA KIBAO KIPYA CHA TAARAB


MWIMBAJI na mtunzi mahiri wa nyimbo za muziki wa dansi nchini, Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ ameingia studio kurekodi kibao chake cha pili cha taarab.
Banza, ambaye kwa sasa ni mwanamuziki wa bendi ya Extra Bongo, alitarajiwa kuingia studio jana kurekodi wimbo huo chini ya usimamizi wa Thabiti Abdul.
Kibao hicho cha Banza kinajulikana kwa jina la Play Boy na kinatarajiwa kuanza kusikika hewani hivi karibuni.
Huo utakuwa wimbo wa pili kwa Banza baada ya kung’ara katika wimbo wake wa kwanza wa ‘Kuzaliwa mjini’, ambao pia ulitungwa na Thabit, ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa kikundi cha Mashauzi Classic.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Thabiti alisema ni kweli ameamua kumtungia Banza wimbo mwingine wa taarab baada ya kupata hamasa kutoka kwa mashabiki wa muziki huo.
“Mashabiki wengi walikuwa wanataka Banza aendelee kuimba nyimbo za taarab. Wamekuwa wakinilaumu kwa kumweka kimya kwa muda mrefu,”alisema Thabiti.
“Nami nimeona ni kweli, kwa vile wimbo wa Kuzaliwa mjini ulipokelewa vyema na mashabiki, ni vyema aendelee kuimba taarab,”aliongeza.
Mbali na kusumbuliwa na mashabiki, Thabiti alisema Banza mwenyewe naye amekuwa akimpigia simu mara kadhaa akimuomba amtungie wimbo mwingine wa taarab.
“Banza mwenyewe alikuwa akinisumbua, anasema nilipomtungia wimbo wake wa kwanza, nilikuwa kama nimembeeb, hivyo anataka aendelee kuimba taarab,”alisema Thabiti.
Kwa mujibu wa Thabiti, wimbo wa Kuzaliwa mjini, aliutunga miaka sita iliyopita, lakini hadi sasa bado unawavutia mashabiki wengi kutokana na maudhui ya wimbo na mipigo ya ala.
Banza amewahi kupigia bendi mbalimbali za muziki wa dansi nchini, lakini iliyomweka kwenye chati ya juu kimuziki ni Twanga Pepeta International.
Baadaye alijiunga na bendi ya TOT Plus, ambayo aliiongoza kwa miaka takriban mitano kabla ya kuanzisha bendi yake binafsi ya Bambino Sound.
Mtunzi huyo mahiri wa nyimbo za muziki wa dansi pia aliwahi kuimbia bendi ya Twanga Chipolopolo na Rufita Jazz kabla ya kujiunga na Extra Bongo, inayoongozwa na Ally Choki.
Ndani ya bendi hiyo, Banza amekuwa akitamba na kibao chake kinachojulikana kwa jina la Falsafa ya Maisha. Pia amekuwa akiimba nyimbo alizowahi kutamba nazo katika bendi mbalimbali.
Hivi karibuni, msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, Hamisi Ramadhani H-Baba aliamua kumshirikisha Banza kurekodi wimbo wake mpya wa Sina Raha. Kibao hicho kimo kwenye albamu mpya ya msanii huyo inayojulikana kwa jina la Shika hapa, acha hapa.

OMAR NA MAUA TEGO, KAKA NA DADA WANAOTAMBA KATIKA TAARAB

TANGU muziki wa taarab ulipoanza kupigwa hapa nchini, hasa katika visiwa vya Zanzibar, imewahi kutokea kwa baadhi ya vikundi kuwa na wasanii wa familia moja.
Imewahi kutokea kwa baadhi ya vikundi kama vile TOT mama kuimba na mwanawe, kama ilivyokuwa kwa Khadija Kopa na marehemu Omar Kopa.
Pia imetokea kwa mwimbaji Eshe Mashauzi wa Jahazi Modern Taarab kurekodi albamu kwa kushirikiana na mama yake, Rukia Juma, ambaye aliwahi kuimbia kundi la TOT.
Kiongozi wa Jahazi, Mzee Yusuph naye amewahi kuimba kundi moja na dada yake, Khadija Yussuf wakiwa East African Melody na Jahazi kabla ya kutengana na kila mmoja kuamua kuwa kivyakevyake.
Na sasa wapo waimbaji ndugu wawili, Omar Tego na Maua Tego, ambao ni waanzilishi na wamiliki wa kundi la Coast Modern Taarab, ambalo limetokea kuteka hisia za mashabiki wengi wa muziki huo kutokana na nyimbo zake nzuri.
Kundi la Coast lilianzishwa mwaka 1998. Wakati lilipoanzishwa, kundi hilo halikuweza kupata umaarufu kutokana na kutokuwa na waimbaji mahiri na wenye mvuto. Lilipiga muziki wake kwenye kumbi za vichochoroni.
Lakini hivi sasa, kundi hilo limepata umaarufu mkubwa kutokana na vibao vyake vitamu vinavyoimbwa na Maua na kaka yake, Omar. Vibao hivyo vimekuwa vikipigwa mara kwa mara kwenye vituo vya radio na televisheni hapa nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam hivi karibuni, ndugu hao walikiri kuwa, muziki huo umewawezesha kupata mafanikio makubwa.
Wakati kundi hilo lilipoanzishwa, Maua alianza kung’ara kwa vibao vyake vya ‘Kayaona mambo’ na ‘Full kujiachia’. Vibao hivyo ndivyo vilivyomsafishia nyota na kumfanya afahamike kwa mashabiki. Hata hivyo, Maua alikihama kikundi hicho siku miezi michache baadaye na kuhamia Zanzibar Stars. Alisema sababu kubwa iliyomfanya ahame ni kutafuta maslahi mazuri zaidi.
Pamoja na kujiunga na kundi hilo, hakufanikiwa kurekodi nalo wimbo wowote. Lakini anakiri kwamba, lilimwezesha kuongeza ujuzi zaidi wa muziki huo kutokana na kuundwa na wanamuziki kadhaa wakongwe.
Alirejea Coast mwaka 2004 akiwa ameiva kiusanii. Alitaja baadhi ya sababu zilizomfanya aondoke Zanzibar Stars kuwa ni pamoja na kukithiri kwa majungu na maslahi madogo.
"Ukubwa wa pua sio wingi wa makamasi. Ni kweli Zanzibar Stars ni kundi kubwa, lakini kwangu halikuwa na maslahi, nilinyimwa nafasi ya kurekodi nyimbo zangu ndio sababu nikaachana nalo,”alisema.
Mara baada ya kurejea Coast, aliibuka na kibao cha ‘Kuvuja kwa pakacha, nafuu ya mchukuzi’, ambacho kililiweka kundi hilo kwenye chati ya juu na kumfanya azidi kufahamika kwa mashabiki.
Kwa sasa, Maua anajiandaa kuachia kibao cha ‘Damu nzito’, ambacho atakiimba kwa kushirikiana na kaka yake, Omar. Pia anatarajia kuibuka na kibao kingine cha ‘Gubu la mawifi’.
Maua alisema yeye na kaka yake, Omar wanapenda na hawajawahi kugombana na ndio sababu wamemudu kufanyakazi pamoja kwa muda mrefu.
Mwanamama huyo mwenye watoto wawili, anavutiwa na waimbaji Mwanahawa Ally na Omar, ambaye pia ni maarufu kwa jina la Special One.
Naye Omar, ambaye ana uwezo wa kuimba, kupiga kinanda, gita la solo na kutunga nyimbo amesema albamu ya ‘I’m Crazy for you’, waliyeirekodi mwanzoni mwa mwaka 2004 ndiyo iliyowapa umaarufu zaidi.
"Kwa kweli baada ya kuachia albamu hiyo, mashabiki wengi walinikubali sana na ndio ilikuwa mwanzo wa jina langu kusikika kwenye masikio ya mashabiki wa muziki huu," anasema.
Hivi karibuni, aliachia albamu yake ya pili inayojulikana kwa jina la ‘Chongeni furniture, ambayo hadi sasa ipo kwenye chati ya juu katika muziki huo.
Mwanamuziki huyo, ambaye ni kipenzi cha mashabiki wengi, anasema amepiga hatua kubwa kupitia muziki huo na anaamini ataendelea ‘kutesa’ kwa kipindi kirefu.
Omar amekiri kuwa, muziki huo umemwezesha kujulikana sana hapa nchini na pia kunufaika kimaisha, tofauti na wakati alipoanza muziki huo miaka ya 1990. Kwa sasa, Omar amejenga nyumba na anamiliki gari la kutembelea.
“Nimetokea mbali sana, awali nilikuwa nikipiga muziki kule Temeke tu, lakini hivi sasa nafahamika karibu mikoa yote Tanzania na nina wapenzi wengi," anasema mwanamuziki huyo mwenye umbo la kuvutia.
Omar anavutiwa zaidi na uimbaji wa Eshe Mashauzi na Khadija Kopa.

MWANAHAWA:SIWEZI KUACHA KUIMBA TAARAB

MWIMBAJI mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Mwanahawa Ally amesema kwa sasa hategemei kurudi katika kundi lake la Jahazi kutokana na mambo waliyomfanyia.
Amesema hivi sasa anaendelea na kazi yake ya uimbaji katika kundi la East African Melody la jijini Dar es Salaam na tayari amesharekodi kibao kinachoitwa 'Rabi nilinde na wenye nia mbaya'.
Mwanahawa aliyasema hayo juzi alipozungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa makala hii na kuongeza kuwa, hataki kuendelea kufanyakazi zake kwa kutegemea Jahazi.
Alisema yeye ni mwimbaji mzoefu na anayesifika ndani na nje ya nchi na kwamba kipaji chake ni cha kuzaliwa na si cha kutegemea kundi au mtu. Alisema uwezo alionao ndio uliomfikisha hapo alipo.
"Kwangu mimi Jahazi ni kama kundi la kawaida, siwezi kulipapatikia wala sina haja nalo, kipaji na uwezo nilionao unanitosha na unanifanya nitambe,"alisema mwanamama huyo mwenye umri unaokadiwa kuwa zaidi ya miaka 60.
"Nimeanza kazi hii ya uimbaji wakati hao waimbaji wa Jahazi hawajazaliwa na hadi sasa nipo kwenye fani na ninawika, siwezi kubembeleza mtu na wala sijaona cha kubembeleza," alisema gwiji huyo wa mipasho mwenye sauti ya kuvutia.
Alisema baada ya kujiondoa Jahazi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kutoelewana na baadhi ya waimbaji pamoja na uongozi wa kundi hilo, amerudi katika kundi la East African Melody, ambako anaimba kama kibarua.
Muimbaji huyo aliyewahi kutamba na wimbo wa 'Kinyago cha Mpapure' na kujipatia umaarufu mkubwa alisema, akiwa katika kundi hilo, anafanya shughuli zake bila kuingiliwa na mtu.
Alisema kutokana na uwezo mkubwa wa uimbaji alionao, hawezi kubabaishwa na kundi lolote na anajiamini kwamba anaweza kufanyakazi sehemu yoyote.
Mwimbaji huyo, mwenye umbo kubwa na sauti ya kuvutia alisema, hajafikiria kuachana na kazi ya uimbaji kwani ni sehemu ya maisha yake na anaipenda kuliko kazi nyingine yoyote.
"Bado sijafikiria siku ya kuacha kuimba, kazi hii ndio iliyoniweka mjini hadi sasa, ninaendesha familia yangu kwa kazi hii, kwa hiyo bado ninaiheshimu sana," alisema mwimbaji huyo, anayetamba na kibao cha 'Roho mbaya siyo mtaji' alichokiimba akiwa Jahazi.
Mkongwe huyo wa mipasho pia alisema hana mpango wa kuhamia katika kundi la Fiver Stars 'Watoto wa Bongo' hata kama ataombwa kujiunga na kundi hilo.
Alisema mawazo yake ameyaelekeza kwenye makundi makongwe, likiwemo Melody kutokana na kusheheni waimbaji wenye umri unaoendana naye.
"Hata nikiombwa niende Fiver Stars, siwezi kwenda kwa sasa, watanisumbua tu, kiwango changu hakiendani nao," alisema mwimbaji huyo aliyenusurika kufa katika ajali ya gari akiwa na kundi hilo hivi karibuni.
Ajali hiyo ilitokea Machi 21 mwaka huu baada ya basi dogo aina ya Toyota Coaster walilokuwa wakisafiria kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam, kulivaa lori lililokuwa limeegeshwa kando mwa barabara na baadae kupinduka na kusababisha vifo vya wasanii 13 wa kundi la Fiver Stars, akiwemo mwimbaji nyota wa kundi hilo Issa Kijoti.
Ajali hiyo ilitokea saa 2.30 usiku, ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, umbali wa kilomita sita kutoka lango kuu la kuingia hifadhini, ambapo wasanii wengine sita waliokuwa kwenye gari hilo walijeruhiwa.
Mwanahawa aliambatana na kundi hilo kama mwimbaji mwalikwa na katika ajali hiyo, aliumia mkono na kupelekwa Kenya kwa matibabu.
Akizungumzia afya yake baada ya ajali hiyo, Mwanahawa alisema anaendelea vizuri na anafanya shughuli zake kama kawaida.
Alisema katika maisha yake hawezi kuisahau ajali hiyo, na ndio kubwa aliyowahi kukumbana nayo tangu kuzaliwa.
"Itachukua muda mrefu kuisahau ajali kama ile ambayo ilipoteza roho za wasanii wezewtu 13 kwa mpigo, ninamuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu pahala pema peponi Amina," alisema.

ISHA MASHAUZI:MUZIKI WA TAARAB UNALIPA


‘MAMA nipe radhi, kuishi na watu kweli kazi, Mama nipe usia, nipe usia unifae katika dunia’.Hiyo ni baadhi ya mashairi yanayopatikana katika wimbo wa ‘Mama nipe radhi’ ulioimbwa na mwimbaji anayechipukia kwa kasi hapa nchini, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’.
Wimbo huo wenye mashairi ya kuvutia, umelenga kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana kuhusumaisha na jinsi mtoto anavyotakiwa kuishi vizuri katika jamii iliyomzunguka.
Mwimbaji huyo hivi karibuni alizindua albamu yake ya kwanza, inayoitwa ‘Mama na Mwana’ katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni mjini Dar es Salaam.
Albamu hiyo inazo nyimbo nne,‘Maneno si mkuki’, ‘Mama nipe radhi’, ‘Kila mtu na mtuwe’ na
‘Tugawane ustarabu’.
Isha alifanya uzinduzi wa albamu hiyo, akisindikizwa na vikundi vya taarab vya Jahazi, Coast Modern Taarab, Baikoko kutoka Tanga , Hadija Kopa, Mc Babu Ayubu, Hassani Ally na Ahmed Mgeni kutoka Zanzibar Stars.
Katika onyesho hilo, mashabiki waliokuwa wamefurika ukumbini walilipuka mayowe ya kushangilia muda wote kutokana na kuguswa na mashairi ya nyimbo zilizoimbwa na mwanadada huyo.
Isha, ambaye ni mwimbaji wa kikundi cha Jahazi, alipanda jukwaani saa 7.05 usiku, akiwaamesindikizwa na mama yake mzazi, Rukia Juma na kuimba kibao cha ‘Mama nipe radhi’.
Utamu wa mashairi ya nyimbo zake, sauti yake nyororo na madoido yake anapokuwa stejini, nimiongoni mwa mambo yaliyompatia sifa kubwa mwanadada huyo na kumfanya aibuke kuwamwimbaji tishio.
Isha amekuwa mwimbaji wa kwanza chipukizi wa kike kutoa albamu yake binafsi, nje ya kundi lake la Jahazi kwa lengo la kujiongezea kipato.
Akizungumza na Burudani wakati wa onyesho hilo, Ishe alisema uamuzi wake wa kutoa albamu hiyo yenye nyimbo nne haumaanishi kwamba anataka kulipa kisogo kundi lake la Jahazi, bali anataka kujipima uwezo wake wa uimbaji.“Najua wengi wanaweza kuhisi kwamba nimehama Jahazi.
Lakini ukweli ni kwamba bado mimi ni mwimbaji wa Jahazi na sina mpango wa kuhama,”alisema.Isha alianza kujihusisha na muziki huo kutokana na kuvutiwa na uimbaji wa mama yake. Alijitosarasmi kwenye taarab mwaka 2007.
“Nilikuwa nikihusudu sana kuimba tangu nikiwa shule ya msingi ya Mnazi Mmoja. Naweza kusema kipaji changu kilianza kuonekana tangu nikiwa shule, ambako nilikuwa nikiimba kwaya,”alisema.
Kikundi chake cha kwanza kilikuwa Wazazi Culture Troupe, kilichokuwa na maskani yake Kariakoo, mjini Dar es Salaam. Anasema akiwa katika kikundi hicho, alikuwa akiimba nyimbo mbalimbali, lakini hakubahatika kurekodi nacho.
Mwishoni mwa mwaka 2007, alijiunga rasmi na kundi la Jahazi Modern Taarab ‘Wana wanakshinakshi’, linachoongozwa na mwimbaji mahiri nchini, Mzee Yusuf.
Anasema mara yake ya kwanza kupanda stejini na kuimba na kundi la Jahazi, ilikuwa kwenye onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa bwalo la maofisa wa polisi, Oysterbay, Dar es Salaam. Katika onyesho hilo, aliimba wimbo wa ‘Hayanifiki’.
“Kwa kweli nilijisikia faraja kubwa, sikuwa na hofu yoyote ile, mashabiki walinikubali vilivyo, si unajua mambo yangu,” alisema.
Isha anakiri kwamba, kibao cha ‘Hayanifiki’ ndicho kilichompandisha chati na kudhihirisha uwezo wake katika fani hiyo. Wimbo huo umetungwa na Mzee.
Miaka miwili baadaye, alifanikiwa kutunga wimbo wake mwenyewe, unaotambulika kwa jina la ‘Ya wenzenu midomo juu.’ Wimbo huo unapatikana kwenye albamu ya ‘VIP’, ambayo ni ya nne kwa Jahazi.
“Wimbo huo ulinifanya niwe juu, mashabiki waliupenda sana na hadi leo wanaupenda, namshukuru Mzee kwa kutunga wimbo ule, ambao ni guzo kwa mashabiki wengi,” anasema.
Mwimbaji huyo anakiri kwamba, muziki wa taarab una manufaa makubwa kwao hivi sasa, tofauti na miaka ya nyuma.
Alisema binafsi amekuwa akipata fedha za kumwezesha kuishi vizuri na kupata mahitaji menginemuhimu kutokana na muziki wa taarab.Alizitaja faida zingine alizozipata kutokana na muziki huo kuwa ni pamoja na kusafiri katika nchimbalimbali kama vile Uingereza na Arabuni.
“Hivi sasa nimenunua kiwanja kwa ajili ya kujenga nyumba na naendesha duka na kuuzavinywaji,”alisema.
Aliwataja waimbaji taarab wanaomvutia kuwa ni pamoja na mama yake, Rukia na Mzee kutokana na tungo zao maridhawa pamoja na sauti yenye mvuto.Amewataka wasanii wa muziki huo kupendana na kufanyakazi kwa ushirikiano ili waweze kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
Mwimbaji huyo alizaliwa Februari 3, 1982 mkoani Mwanza na ni mtoto wa kwanza kati ya watoto watano katika familia yake.Alisoma shule ya msingi Mnazi Mmoja, Dar es Salaam kuanzia mwaka 1990 hadi 1996 alipomaliza darasa la saba.
Licha ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari, alijikuta akiishia kidato cha pili shuleni hapo kutokana na matatizo mbalimbali.Isha, ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Mara, hivi sasa ameolewa na ana watoto wawili. Anaishi na familia yake maeneo ya Tandale, Dar es Salaam.

KHADIJA KOPA: HAKUNA ANAYEWEZA KUNIFIKIA KWA UIMBAJI TAARAB

KWA umbo, Khadija Omar Kopa ni mnene. Rangi yake ni nyeusi yenye mng’ao. Uso wake hujawa na tabasamu muda wote utadhani hajui kitu kinachoitwa kukasirika.
Licha ya kuwa na umbile hilo, Khadija ni mwepesi wa kuunyonganyonga mwili wake atakavyo awapo stejini, akiimba nyimbo za muziki wa taarab. Sauti yake nayo ni maridhawa na yenye mvuto wa pekee.
Sifa hizo ndizo zilizomfanya mwanamama huyo apachikwe jina la ‘Malkia wa Mipasho’ nchini. Waliompa jina hilo hawakubahatisha, walitambua vyema kwamba uwezo wake katika fani hiyo ni mkubwa.
Mwanamama huyo alianza kuvuma kimuziki miaka 20 iliyopita alipokuwa katika kikundi cha taarab cha Culture cha Zanzibar, ambako aling’ara kwa vibao vyake kama vile ‘Kadandie’, ‘Wahoi’ na ‘Daktari’.
Anakiri kwamba, akiwa katika kundi hilo, aliweza kujifunza mambo mengi kuhusu muziki wa taarab ikiwa ni pamoja na utunzi wa nyimbo, uimbaji bora na upangiliaji wa muziki.
"Culture ni chuo, ambacho nilianza kujifunza uimbaji na utungaji wa mashairi, nilipata uzoefu wa kutosha na mashabiki walinikubali," alisema Khadija alipokuwa akizungumza na mwandishi wa makala hii hivi karibuni mjini Dar es Salaam.
Baada ya kutoka Culture, mwimbaji huyo alitua katika kundi la TOT mwaka 1992 akiwa mmoja wa waanzilishi wake, ambapo alianza kung’ara kwa kibao cha ‘Tx mpenzi’, ‘Ngwinji’, ‘Wrong number’, ‘Mtie kamba mumeo’ na nyinginezo.
“Kule Culture ni kama vile nilikuwa nasafisha nyota yangu, lakini baada ya kujiunga na TOT ndipo hasa mambo yangu yalipoanza kuwa mazuri,”alisema.
Khadija alikorofishana na uongozi wa TOT mwaka 1993 baada ya yeye na mwimbaji mwenzake, Othman Soud kuamua kuondoka kinyemela na kwenda Dubai, ambako walishiriki kuanzisha kundi la East African Melody.
Mara baada ya kurejea nchini kutoka Dubai, mwanamama huyo alilazimika kujiunga na kikundi cha Muungano Cultural Troupe kwa vile uongozi wa TOT uligoma kumpokea.
Kujiunga kwa Khadija na Othman katika kikundi cha Muungano kulisababisha kuwepo kwa ushindani mkali kati ya vikundi hivyo viwili, ambavyo vilifanya maonyesho kadhaa kwa ajili ya kuonyeshana nani mkali.
Akiwa Muungano, Khadija aling’ara kwa vibao vyake murua kama vile ‘Homa ya Jiji’, ‘Kiduhushi’ na ‘Umeishiwa’. Pia kulizuka ushindani mkali kati yake na marehemu Nasma Khamis ‘Kidogo’, ambaye alichukuliwa na TOT kutoka Culture kwa lengo la kuziba pengo lake.
"Nilipojiunga na Muungano nililiwezesha kundi hilo kuwa juu na tuliwapa wakati ngumu kweli wapinzani wetu TOT,”alisema mwimbaji huyo.
Mwaka 1998, mwanamama huyo aliamua kurejea TOT, akibadilishana na Nasma, ambaye aliamua kuhamia Muungano, hali iliyoongeza ushindani mkali kati ya vikundi hivyo.
Khadija anasema alikuwa akihama mara kwa mara kutoka kundi moja hadi jingine kutokana na matatizo ya uongozi na maslahi duni. Alisema msanii siku zote hufurahia kazi yake pale anapopata maslahi mazuri.
Mwimbaji huyo alisema kwa sasa anajivunia umaarufu aliojijengea nchini kutokana na uimbaji wake maridhawa na kuongeza kuwa, muziki huo umemwezesha kutembelea mikoa yote ya Tanzania.
"Usifanye mchezo, taarab hivi sasa inalipa, lakini ukiwa unamiliki kundi lako. Amini usiamini, taarab ipo juu kuliko muziki mwingine wowote ule," anasema mwanamama huyo.
Khadija alisema kwa sasa anajiandaa kuzindua wimbo wake mpya, utakaojulikana kwa jina la 'Top in Town'. Alisema amechelewa kuuzindua wimbo huo kutokana na kukosa wadhamini.
Mwimbaji mwenye sura yenye mvuto na mwili tipwatipwa alisema, wimbo huo umeshakamilika na kuanza kupigwa kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini.
"Ninachokifanya hivi sasa ni kuutambulisha wimbo huu kwa mashabiki wangu. Nikipata mdhamini nitauzindua rasmi kwa onyesho maalumu," alisema.
Gwiji huyo wa mipasho alisema, licha ya kuwepo kwa ushindani mkubwa katika muziki wa taarab hivi sasa, bado anaamini yeye ndiye malkia wa muziki huo na hakuna mwimbaji anayeweza kumfikia.
"Ninachowaambia wapinzani wangu ni kwamba, waparamie miti yote, lakini wajihadhari na mbuyu. Hawawezi kunifikia hata kwa bahati mbaya," alijigamba Gwiji huyo anayependwa na mashabiki wengi kutokana na uchangamfu wake awapo stejini.
Khadija alilielezea soko la muziki wa taarab hivi sasa kuwa ni kubwa, tofauti na miaka ya nyuma na kuongeza kuwa, muziki huo umekuwa na manufaa makubwa kwa wasanii.
Mwimbaji huyo mahiri alisema kwa sasa hana mpango wa kuhama katika kikundi cha sanaa za maonyesho cha Tanzania One Theatre (TOT) na ameahidi kuwapa raha zaidi ya muziki huo mashabiki wake.
Mbali na kutembelea mikoa yote nchini, Khadija alisema muziki huo umemwezesha kusafiri katika nchi kadhaa za Ulaya, Arabuni na Afrika. Alizitaja nchi hizo kuwa ni Marekani, Ufaransa, Ureno, India, Comoro, Kenya, Zimbabwe na Oman.
Mwimbaji huyo alisema pia kuwa, muziki wa taarab umemwezesha kujenga nyumba mbili katika kisiwa cha Unguja na pia kuendesha maisha yake bila matatizo.
Khadija, ambaye alizaliwa miaka 47 iliyopita katika kisiwa cha Unguja,
amebahatika kupata watoto wanne, lakini mmoja, ambaye alikuwa amerithi kipaji chake, Omar Kopa alifariki dunia mwaka juzi.
Anakiri kwamba kifo cha Omar kilikuwa pigo kubwa kwake na familia yake kwa sababu alikuwa na kipaji cha hali ya juu cha muziki. Anasema alikuwa akisaidiana naye katika utunzi wa nyimbo.

MWANAHAWA ALLY AJIENGUA T-MOTTO, AREJEA EAST AFRICAN MELODY


MWIMBAJI mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Mwanahawa Ally amesema katika maisha yake ya usanii, hajawahi kutunga wimbo wa taarab.
Mwanahawa (61) amesema hajawahi kufanya hivyo kwa sababu utunzi wa nyimbo za taarab ni kazi ngumu na inahitaji kuwa na kipaji cha aina yake.
Mkongwe huyo wa taarab alisema hayo wiki hii alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Raha Zetu kilichorushwa hewani na kituo cha redio cha Clouds.
“Kutunga wimbo ni kazi ngumu, tofauti na watu wanavyofikiria kwani nyimbo nzuri ni lazima iwe na mashairi yenye vina vinavyolingana,”alisema mwanamama huyo.
“Tangu nianze kuimba taarab huu ni mwaka wa 45 na sijawahi kutunga nyimbo yangu mimi mwenyewe. Natungiwa tu na watu wengine, siwezi hata kujaribu, mashairi yana kazi ngumu,” aliongeza.
Mwanahawa, ambaye kwa sasa anafanyakazi katika kikundi cha East African Melody, amesema amerejea kikundi hicho baada ya kushindwa kuelewana na uongozi wa T Motto.
Alisema ameamua kujiondoa T Motto kwa hiari yake baada ya kuona mkurugenzi wake, Amin Salmin ameshindwa kukiendesha kwa mafanikio.
“Wakati waliponifuata, walinieleza kwamba nitalipwa shilingi milioni mbili na kusaini mkataba wa mwaka mmoja, lakini hadi sasa sijui kama huo mkataba uliandikwa na sijawahi kulipwa mshahara wowote,”alisema.
“Nasikia tu matangazo ya redio na televisheni yakieleza kwamba nipo T Motto, lakini sijawahi kumuona mkurugenzi wake hata siku moja na sidhani kama anafahamu nina shida gani,”aliongeza.
Mwanahawa alisema, anahisi kundi hilo lilitaka kuleta ushindani katika muziki wa taarab, lakini halikuwa limeandaliwa vyema ama kujipanga vizuri.
Alisema tangu aliporekodi wimbo mmoja na kundi hilo na kushiriki kwenye uzinduzi, hajawahi kuitwa kwenye onyesho lolote na haelewi iwapo bado lipo ama limekufa.
Mkongwe huyo amewahi kuimbia vikundi mbalimbali vya taarab kama vile Jahazi, Five Stars, Zanzibar Stars na East African Melody.

LEILA: SIONI TATIZO KUFANYAKAZI NA MUME WANGU


“NILIANZA kumfahamu Mzee Yusuf katika ukumbi wa Equator Grill uliopo Mtoni kwa Azizi Ally, Temeke, Dar es Salaam. Nilipenda sana jinsi alivyokuwa anapiga kinanda wakati huo, ” anasema mwimbaji nyota wa taarab wa kundi la Jahazi, Leila Rashid.
Anasema kipindi hicho alikuwa akihudhuria maonyesho mbalimbali yaliyokuwa yakifanywa na kikundi cha taarab cha Zanzibar Stars, ambacho Yusuf alikuwa mmoja wa wasanii wake, akiwa anapiga kinanda.
Leila, ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa mwimbaji tangu akiwa mdogo anasema, alikuwa na kawaida ya kwenda kwenye ukumbi huo kila Zanzibar Stars ilipokuwa ikifanya onyesho.
“Nilikuwa na ndoto ya kuimba taarab tangu nilipokuwa mdogo na nilikuwa nikivutiwa sana na uimbaji wa Sabah Salum ‘Muchacho’ kutokana na uimbaji wake mzuri,” anasema.
Leila anasema alikuwa akitumia muda mwingi akiwa nyumbani kwao kuimba nyimbo mbalimbali za waimbaji nyota wa muziki huo kwa lengo la kupima uwezo wake kama anaiweza fani hiyo.
Mwimbaji huyo mwenye sura na umbo la kuvutia, ambaye wajihi wake unashabihiana na mwanamke wa kisomali, anasema siku ya kwanza kuanza kufahamiana na Yusuf, alijihisi mwenye furaha kubwa.
“Kwa kweli siku ya kwanza kufahamamiana na Yusuf nilijihisi mwenye furaha sana na niliamini ataweza kunisadia kukuza kipaji changu cha uimbaji nilichokuwa nacho,” anasema.
Baada ya kufahamiana na kuwa karibu na Yusuf, Leila anasema mwimbaji huyo gwiji wa taarab alimshawishi ajiunge na kikundi cha Zanzibar Stars, ambacho kilikuwa kikiwika wakati huo.
Leila, ambaye kwa sasa anasikika kila kona ya nchi kutokana na uimbaji wake mzuri, anasema ushauri aliopewa na Yusuf aliusikiliza na kuufanyia kazi.
Anasema alijiunga na Zanzibar Stars miaka tisa iliyopita na wimbo wake wa kwanza ndani ya kikundi hicho unajulikana kwa jina la ‘Riziki atoae Mola’.
Mwimbaji huyo mwenye bashasha anasema, baada ya kurekodi wimbo huo, hakufanikiwa kutoa wimbo mwingine kutokana na ubinafsi uliokuwepo katika kundi hilo.
Anasema mara yake ya kwanza kupanda kwenye steji alikuwa na hofu, lakini alifanikiwa kuimba vizuri na kushangiliwa na mashabiki wengi.
Leila, mwimbaji mwenye sauti nyororo na macho ya kuvutia anasema, aliamua kuondoka Zanzibar Stars kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ubinafsi na uchache wa maslahi.
Anasema licha ya kwamba kipindi hicho Zanzibar Stars ilikuwa inatamba kwa nyimbo za taarab, maslahi yalikuwa madogo, hali iliyosababisha waimbaji wengi mahiri kuhama.
Mwimbaji huyo anasema, mwaka 2006 alijiunga na kundi jipya la Jahazi Morden Taarab ‘Wana wa nakshinakshi’ chini ya Mkurugenzi wake Mzee Yusuf.
Anasema kuanzishwa kwa kundi hilo, ambalo linaongozwa na mume wake, Yusuf kulimfanya afahamike ndani na nje ya nchi hii.
“Jahazi ndiyo imenifanya nifahamike kila kona ya nchi hii, nadhani kama si kundi hili, hadi sasa ningekuwa sifahamiki,” anasema.
Leila anasema wimbo wa ‘Maneno ya mkosaji’, ambao ulikuwa wa kwanza kuimba katika kundi hilo, ulimpandisha chati na kumpa umaarufu mkubwa na kusisitiza kuwa, kwa sasa anajiona yupo kwenye chati ya juu.
“Sidhani kama kuna mwimbaji anayeweza kujaribu kusimama na mimi kwa sasa, niko juu na nimeiva kila idara,” anajigamba mwimbaji huyo.
Akizungumzia maendeleo ya muziki wa taarab nchini, Leila anasema upo juu na unazidi kukua kadri siku zinavyosonga mbele kutokana na kuwa na mashabiki wengi zaidi.
Mwimbaji huyo, ambaye ni mama wa watoto wawili anasema, haoni tatizo kufanyakazi katika kundi moja na mumewe kwa sababu ameshaizoea tabia ya mumewe.
Leila anasema ataendelea kuheshimiana na mume wake kwa kipindi chote watakachoendelea kuwa pamoja huku akisisitiza kuwa, hakuna anayeweza kuwatenganisha kwa vile anampenda kuliko kitu kingine chochote.
“Nampenda sana mume wangu ndio maana hata anapotaka kuoa mke mwengine, huwa nampa ruksa kwani najua kufanya hivyo ni sheria kwa mujibu wa dini yetu,” anasema.
Hata hivyo, mwimbaji huyo anayependa kutabasamu muda wote anasema, hafurahishwi kuona Yusuf na mdogo wake Khadija, ambaye ni mwimbaji wa kundi la Five Stars Modern Taarab wametofautiana.
Anasema ni vyema wanandugu hao wawili waishi kama awali na waendelee kufanyakazi katika kundi moja kwa vile kugombana kwao hakutoi sura nzuri mbele ya jamii.
Leilah, ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wa ‘Ubinadamu kazi’, anasema kupitia fani hiyo, ameweza kusafiri katika mikoa mingi nchini na pia nje ya nchi. Alizitaja baadhi ya nchi alizowahi kutembelea kuwa ni Uingereza, Oman, Dubai, Nairobi na Burundi.
Mwimbaji huyo amekitaja kibao cha ‘Kwa hilo hujanikomoa’ kuwa ndicho kilichomfanya apendwe zaidi na mashabiki kutokana na kukiimba kwa umahiri mkubwa.
Ametoa mwito kwa serikali kuwasaidia waimbaji wachanga ili waweze kuonyesha vipaji vyao. Pia amewataka wasanii wenzake wa muziki huo, kuwa na upendo na kuacha majungu miongoni mwao.

TAARAB YA SASA BIFU TUPU-KHADIJA KOPA

MTUNZI na mwimbaji nyota wa muziki wa taarab nchini, Khadija Omar Kopa amesema vikundi vya muziki huo kwa sasa vimetawaliwa na chuki binafsi miongoni mwa viongozi wake.
Khadija amesema chuki hizo pia zimetawala miongoni mwa wasanii, ambao baadhi yao wamekuwa hawaelewani na kuchukiana kwa sababu zisizokuwa na msingi.
Mwanamama huyo, ambaye ni kiongozi wa kikundi cha taarab cha Tanzania One Theatre (TOT), alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC 1.
“Bifu la sasa ni bifu kweli kweli, sio la kutungiana nyimbo tu, utakuta kikundi fulani cha taarab hakielewani na kikundi kingine na hata wasanii wake nao hawaelewani, ‘ alisema.
Khadija alisema bifu la aina hiyo kamwe haliwezi kuleta maendeleo ya muziki huo, badala yake litaufanya muziki huo udumae na kupoteza umaarufu kwa mashabiki.
Alisema wakati vikundi vya TOT na Muungano vilipokuwa kwenye chati ya juu miaka ya 1990 hadi mwanzoni mwa 2000, viongozi na wasanii wake walikuwa na uhusiano mzuri na wa karibu na kamwe hawakuwa na bifu.
Alisema bifu la vikundi hivyo wakati huo lililenga kutafuta pesa na kuviletea maendeleo, halikuwa bifu la kuchukiana na kujengeana uhasama kama ilivyo sasa kwa baadhi ya vikundi vya muziki huo.
“Wakati ule tulikuwa tunatunga nyimbo za kujibishana, lakini lengo letu lilikuwa ni kutafuta pesa,”alisema Khadija, ambaye ni miongoni mwa waimbaji wakongwe wa muziki huo wanaotesa hadi sasa.
Khadija alisema ilikuwa kawaida ya vikundi hivyo viwili vilivyokuwa vikiongozwa na John Komba na Norbert Chenga kuandaa maonyesho makubwa ya taarab na kuhudhuriwa na mashabiki wengi kuliko hivi sasa.
Alisema waliweza kufanya maonyesho ya aina hiyo katika viwanja vikubwa kama vile wa Uhuru, Dar es Salaam, Jamhuri-Morogoro na ukumbi wa Vijana-Dar es Salaam, ambapo walipata pesa nyingi.
“Katika baadhi ya maonyesho, tuliweza kupata shilingi milioni 30 kwa onyesho moja na kwa wakati ule zilikuwa pesa nyingi sana,”alisema mwanamama huyo.
Khadija alisema baadhi ya wakati, Komba na Chenga walipoona kikundi kimoja kikitetereka kimuziki, walikuwa wakikutana na kupanga mikakati ya kukiinua.
“Mbinu walizokuwa wakizitumia kuinuana ni kuandaa kitu fulani cha pamoja na kutoleana lugha za kiushindani, zisizokuwa na matusi na mashabiki walikuwa wakishawishika kirahisi kujitokeza kuhudhuria maonyesho yetu,”alisema.
Licha ya kikundi cha TOT kutosikika sana kwa sasa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, Khadija bado anang’ara kimuziki kutokana na tungo zake mbalimbali, ambazo zimetokea kuteka hisia za mashabiki wa muziki huo. Baadhi ya tungo hizo ni kama vile Top in town.
Akizungumzia utunzi wa nyimbo za taarab, Khadija alikiri kuwa ni kazi ngumu na inayohitaji uvumilivu na kujituma. Alisema binafsi amekuwa akitunga nyimbo zake nyingi nyakati za usiku.
“Ninapoamua kutunga wimbo, huwa nakesha usiku kucha nikiandika mashairi. Naandika, nafuta, naandika tena hadi alfajiri,”alisema.
Aliongeza kuwa, kazi ya kutia muziki katika nyimbo zake huwa sio ngumu kwa vile huwaelekeza wapigaji wa ala upigaji anaoutaka nao hufanya hivyo.
Hata hivyo, Khadija alisema wakati mwingine anapokuwa stejini, hufanya vitu tofauti na alivyourekodi wimbo wake kutokana na kupandwa na mzuka.
Khadija alianza kupata umaarufu alipokuwa katika kikundi cha Culture cha Zanzibar, ambako aling’ara na vibao vyake kama vile Wahoi, Daktari na Kadandie.
Baadaye alihamia Bara, ambako alijiunga na kikundi cha TOT wakati kilipoanzishwa mwaka 1993 kabla ya kuwa miongoni mwa waanzilishi wa kikundi cha East African Melody. Pia aliwahi kuimbia kikundi cha Muungano.

MZEE YUSUPH AMZAWADIA ISHA MASHAUZI PIPI YA KIJITI

SHANGWE, vifijo, hoihoi na nderemo vilitawala mwishoni mwa wiki iliyopita wakati vikundi vya taarab vya Jahazi na Mashauzi Classic vilipofanya onyesho la pamoja.
Onyesho hilo la aina yake, lilifanyika katika ukumbi wa hoteli ya Travertine uliopo Magomeni mjini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki.
Kivutio kikubwa katika onyesho hilo walikuwa kiongozi wa Jahazi, Mzee Yussuf ‘Mfalme’ na kiongozi wa Mashauzi Classic, Isha Mashauzi ‘Jike la Simba’.
Isha, ambaye ni mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za taarab, alitumia onyesho hilo kumuomba radhi Yussuf kutokana na kitendo chake cha kujiengua katika kundi hilo bila kuaga.
Baada ya kujiengua katika kundi la Jahazi, Isha ambaye alikuwa miongoni mwa waimbaji tegemeo na kipenzi cha mashabiki wengi wa kundi hilo, alianzisha kundi lake la Mashauzi Classic.
Mashabiki walianza kufurika kwenye ukumbi huo kuanzia saa tatu usiku na hadi ilipotimia saa nne, walifurika pompni. Kundi la Jahazi lilikuwa la kwanza kupanda stejini na kuanza kutoa burudani.
Kama kawaida yake, kundi hilo lilianza kuporomosha nyimbo zake mpya na zile zinazotamba katika viunga vya burudani hivi sasa na kuwafanya mashabiki kuachia viti vyao na kujimwaga ukumbini kucheza.
Ilipotimia saa sita usiku, ndipo kundi la Mashauzi Classic lilipopanda stejini na kuanza kutoa burudani kwa mashabiki.Ni wakati huo, mwimbaji tegemeo wa kundi hilo, Mashauzi alipopanda stejini na kushangiliwa kwa mayowe mengi na mashabiki.
Akiwa stejini, Mashauzi alimwomba Yussuf ampatie zawadi aliyomuandalia. Kupanda jukwaani kwa Yussuf kuliamsha shangwe na nderemo katika ukumbi huo, ambapo Isha alipata nafasi ya kuzungumza na kiongozi huyo wa Jahazi.
Kabla ya Isha kusema lolote, Yussuf alitoa pipi ya kijiti na kumkabidhi mwimbaji huyo, aliyemlea katika medani ya muziki wa taarab.
"Siku zote zawadi ya mtoto ni pipi, kwa hiyo nakukabidhi zawadi yako mwanangu, nadhani umeipenda," alisema Yussuf huku akishangiliwa na mashabiki wengi.
Isha alipokea zawadi hiyo kwa heshima na kusema amefarijika na ameipokea kwa mikono miwili.
"Nakushukuru baba yangu kwa zawadi uliyonipatia, nimeipokea kwa mikono miwili na roho safi. Siku zote zawadi ya mtoto huwa pipi kwa hiyo nimeipokea," alisema.
Kwa mujibu wa Isha, hana ugomvi na Yussuf wala mwimbaji yeyote wa kundi la Jahazi na kuahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa kundi hilo linalosadikiwa kuwa na mashabiki wengi hapa nchini.
Alisema aliondoka katika kundi hilo kwa ajili ya kwenda kutafuta maisha na kwamba muda wowote anaweza kurudi na anaamini hawezi kuzuiliwa na mtu yoyote. Isha aliambatana na mama yake mzazi, Rukia Juma.
"Niliondoka kwenda kutafuta maisha, lakini muda wowote maisha yakinishinda, nitarejea nyumbani. Ng'ombe akivunjika mguu malishoni, hurejea zizini kusaidiwa," alisema.
Kwa upande wake, Yussuf alimuhakikishia muimbaji huyo kwamba Jahazi ni nyumbani kwake na anaweza kurejea wakati wowote atakapojisia kufanya hivyo.
"Mtu kwao anaweza kuondoka na kurudi wakati wowote na wewe unaweza kurudi wakati wowote unapohitaji kurudi, karibu na nitakupokea kwa mikono miwili," alisema.
Yussuf alisema amefarijika mno kumuona mtoto wake aliyemfundisha muziki anakiri kosa na kuomba radhi hadharani bila ya kushinikizwa na mtu yoyote.
Alisema kitendo alichofanya muimbaji huyo ni cha kiungwana na kinahitaji kuigwa na wasanii wengine na kwamba ni wachache wenye moyo kama wa Isha.
Yussuf alimpa ofa maalumu muimbaji huyo ambapo alimwambia atakuwa miongoni mwa watakaomsindikiza katika uzinduzi wa albamu mpya ya Jahazi ya 'Mpenzi Chokleti' itakayozinduliwa Desemba 24, mwaka huu.
Baada ya Isha kutoa maneno mafupi ya kumuomba radhi kiongozi huyo wa Jahazi, alimkabidhi zawadi maalumu ya ngao iliyochorwa kwa ustadi mkubwa.
Ngao hiyo ina nembo ya kundi la Jahazi, picha ya Yussuf na Isha huku maandishi yake yakiwa na ujumbe mbalimbali.
Tukio lililowavutia mashabiki wengi katika usiku huo maalumu uliopewa jina la 'Usiku wa baba na mwana' ni pale Isha alipopanda jukwaani akiwa amevalia jezi za timu ya Yanga.
Muimbaji huyo alisema ameamua kuvaa jezi za klabu hiyo kwa sababu ya kusherehekea ushindi wa Yanga dhidi ya Simba na pia kumpongeza Yussuf, ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo.
"Kwa vile baba yangu ni Yanga, nimeamua kuvaa jezi za klabu ya baba yangu kuonyesha mapenzi niliyonayo kwake. Yanga oyeeeeeee," alisema.
Wimbo wa 'Mpenzi Chokleti' ulioimbwa na Yussuf ndio uliofunika katika onyesho hilo na kuacha gumzo kwa mashabiki kutokana na kupangiliwa sauti na ala kwa utaalamu mkubwa.

DIDA: MTANGAZAJI WA REDIO ALIYEJITOSA KWENYE TAARAB


JINA la Khadija Shaibu 'Dida' si jina geni kwenye masikio ya mashabiki wa muziki wa taarab, hasa wanaosikiliza vipindi vya muziki huo kupitia kwenye vituo mbalimbali vya radio nchini.
Ni mtangazaji maarufu na mwenye mbwembwe nyingi kila anapotangaza kipindi cha muziki huo kupitia kituo cha radio cha Times FM. Na sasa ameamua kuwa mwimbaji wa muziki huo, ambao ulianza kumvutia tangu akiwa mdogo.
Umaarufu wa Dida, mama wa mtoto mmoja, mwenye umbo dogo,lugha ya tashtiti na yenye mvuto wa aina yake, tayari ameshaipua kibao kimoja cha muziki huo kinachojulikana kwa jina la ‘Waniache miaka 800’.
Dida alikizindua kibao hicho mwishoni mwa wiki iliyopita katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine iliyopo Magomeni, Dar es Salaam, akisindikizwa na kundi maarufu la muziki huo la Jahazi.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii hivi karibuni mjini Dar es Salaam, Dida alisema ameamua kujitosa kwenye muziki huo kutokana na mapenzi makubwa aliyonayo katika fani hiyo.
"Huwezi kuamini, katika utoto wangu nilikuwa sipendi kabisa taarab na ilikuwa haiko kwenye damu, lakini baada ya kuwa mtangazaji, hasa wa kipindi cha taarab, nimetokea kuupenda tu,”alisema Dida.
"Nimeona kwa vile nimepata uzoefu wa kutosha kutokana na kuutangaza kwa muda mrefu muziki huo, nami niachie tungo yangu ili kujipima uwezo wangu," aliongeza.
Awali, Dida alipanga kumshirikisha kiongozi wa kundi la Jahazi, Mzee Yusuph katika kuimba wimbo huo, lakini mpango huo ulikufa kimya kimya na kuamua kuuimba yeye mwenyewe.
"Nilitaka kumshirikisha Mzee Yusuph kwa sababu bila ya unafiki,yeye yupo juu kwa sasa. Pia ndiye aliyenishauri mambo mengi hadi nikafanikisha kutunga wimbo huo," alisema.
Dida alisema anaamini wimbo huo utafanya vizuri na unaweza kuwa wimbo bora wa mwaka wa taarab.Mtangazaji huyo alijigamba kuwa, wimbo huo umesheheni vionjo vingi na siku ya uzinduzi alisindikizwa na kundi zima la Jahazi linalotamba na albamu yao ya sita ya 'My Valentine'.
Akizungumzia kazi yake ya utangazaji, Dida alisema kwake ni kipaji alichojaliwa kuwa nacho na Mwenyezi Mungu na alibaini kuwa nacho baada ya kumaliza masomo ya sekondari.
"Utangazaji kwangu ni kipaji nilichokipata ukubwani, nakumbuka nilipokuwa mdogo, sikuwa na kipaji chochote, hata mimi nashangaa, sielewi ilikuwaje," alisema.
Amemtaja mmoja wa watangazaji waliomvutia na kumfanya ajitose katika fani huyo kuwa ni marehemu Amina Chifupa 'Mpakanjia', aliyejizolea umaarufu mkubwa enzi za uhai wake kupitia kituo cha radio cha Clouds.
Kupitia kazi yake hiyo, Dida alisema amejikuta akipata maadui wengi, hasa wanawake wanaodhani kuwa anawapiga vijimbe anapokuwa akiendesha kipindi chake.Alisema baadhi ya wanawake hao humuandama kwa matusi kwa kumtumia ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake ya mkononi, ambao anakiri kuwa, mara nyingi humuathiri kisaikolojia.
"Usione hivi, navumilia mambo mengi, tangu nianze kutangaza, nimejikusanyia maadui kibao, wengi ni wanawake wenzangu, lakini hiyo ni changamoto kwangu na nitazidi kusonga mbele," alisema.
Dida alisema maneno yake wakati anapotangaza kipindi cha mipasho hayalengi kumchafua mtu ama kumpiga vijembe yeyote, isipokuwa ni katika kukiboresha na kuwapa burudani wasikilizaji wake.
Mwanamipasho huyo amelitaja tukio ambalo hawezi kulisahau katika maisha yake kuwa ni la kuvumishiwa kuwa anajihusisha na dawa za kulevya, jambo ambalo amekana katakata kuhusika nalo.
"Siwezi kuusahau uvumi huo katika maisha yangu kwa sababu ulilenga kunichafua, lakini yote namuachia Mungu, najua atawabainisha wote walionienezea uvumi huo," alisema.
Amewaasa waimbaji chipukizi wa taarab nchini kuwa, watunge nyimbo zenye maadili na zenye kuleta ujumbe kwa jamii na waachane na majungu ili waweze kusonga mbele.
Amewashauri pia watangazaji wenzake, wawe na ushirikiano , wapendane na wasitupiane vijembe visivyo na msingi ili waweze kuendeleza taaluma yao hiyo.
Dida alizaliwa mwaka 1982, katika Hospitali ya Ocean Road, mjini Dar es Salaam. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Ubungo na sekondari ya Makongo, Dar es Salaam. Kidato cha tano na sita alisoma mkoani Tanga na baada ya hapo alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Dar es Salaam (DSJ). Mwanamama huyo hajaolewa, lakini anaye mtoto mmoja na anaishi Kijitonyama, Dar es Salaam.

MZEE YUSUPH ATANGAZA BINGO YA MILIONI MOJA

KIONGOZI wa kikundi cha muziki wa taarab cha Jahazi, Mzee Yusuph ameahidi kutoa bingo ya sh. milioni moja kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa ya kuuzwa kwa CD feki za albamu yao mpya.
Akizungumza mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Mzee alisema ameamua kutoa zawadi hiyo kwa lengo la kupambana na tatizo lililokithiri la wizi wa kazi za sanaa nchini.
Mzee alisema kwa sasa, albamu yao mpya ya Mpenzi Chokolate inapatikana kwenye CD za kusikiliza na kwamba albamu ya video itafuata hivi karibuni.
Alisema albamu hiyo inauzwa na kusambazwa na kampuni yake binafsi ya Mzee Classic na kwamba hawajatoa tenda hiyo kwa kampuni nyingine.
Kiongozi huyo alisema kwa yeyote anayetaka kuuza albamu hiyo kwa jumla ama reja reja, afike ofisini kwake Magomeni Mapipa, Dar es Salaam jirani na hoteli ya Butiama.
“Natangaza zawadi ya shilingi milioni moja kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa kuhusu mahali zinapouzwa ama zinakotengenezwa CD feki,”alisema.
Mzee pia amewataka mashabiki wa taarab waepuke kununua CD feki kwa vile kufanya hivyo ni kuwatajirisha wezi wa kazi za sanaa na kuwaacha wasanii wakiendelea kuwa hohehahe.
“Ni kweli COSOTA (Chama cha Hatimiliki Tanzania) inajitahidi kupambana na tatizo hili, lakini haiwezi kufanyakazi hiyo peke yake,”alisema Mzee.
“Hawa watu ni wezi, si kwa kazi za Jahazi tu, bali bendi zote za muziki wa dansi na za wacheza filamu. Polisi wamekubali kushirikiana nasi, hivyo lazima tupambane nao,”aliongeza.
Mzee alisema baada ya kuwapata wezi hao, watakachokifanya kwanza ni kuwaelimisha ili waache kuuza CD feki, badala yake wauze CD orijino na kwamba wapo tayari kuingia nao makubaliano maalumu.
Kiongozi huyo wa Jahazi alisema wamejipanga vyema kuhakikisha kwamba, wanauanza mwaka 2012 kwa kuendelea kuwa nambari moja katika muziki wa taarab nchini.
Alisema watafanya hivyo kwa kuendelea kutoa kazi nzuri na zenye viwango na kuwaridhisha mashabiki ili nao watambue kwamba, wanaujua vyema muziki huo na wanafanya vizuri.
Alipoulizwa ni kwa nini ameacha kupiga kinanda hivi sasa katika nyimbo za kundi hilo, Mzee alisema taarifa hizo si za kweli kwa vile bado anaendelea kuutumia ujuzi wake huo.
Alisema katika nyimbo tano zilizomo kwenye albamu yao mpya ya Mpenzi Chokolate, amepiga kinanda kwenye nyimbo tatu.
“Hawa wasanii wanaotajwa kwamba wapo juu yangu katika kupiga kinanda hawana lolote. Mimi ndiye mwalimu wa Thabiti Abdul na Ally J katika kupiga kinanda,”alisema.
Kwa mujibu wa Mzee, alianza kupiga kinanda tangu akiwa kikundi cha East African Melody miaka ya mwanzoni mwa 1990 na kujigamba kuwa, yeye ndiye mwasisi wa taarab ya kisasa.
“Mimi ndiye niliyemwingiza Thabiti kwenye taarab, nilianza kumfundisha tangu nikiwa Melody na ndiye niliyempeleka TOT. Alikuja kwangu kuiba ujuzi.
“Na wakati naanza kupiga kinanda, Ally J alikuwa bado mdogo, na ndiye niliyekuwa nikimpa ujiko wakati alipokuwa Jahazi. Sasa kama wao wanajiona wapo juu zaidi, sawa, lakini nasema hawaniwezi,”alisisitiza.
Mzee alisema yupo tayari kupambana na Thabiti na Ally J kwa lengo la kutafuta nani mkali kati yao, lakini hahitaji kuwepo kwa mwandaaji wa pambano hilo kwa vile lengo si kufanya biashara.
“Nitaondoka kwenda Marekani hivi karibuni (Januari 17), nitakaporudi, nitakuwa tayari kukutanishwa na vijana hawa ili tuonyeshane nani mkali,”alisema.

KHADIJA KOPA AICHANACHANA JAHAZI

MOJA ya matatizo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya muziki wa taarab hapa nchini ni kuwepo kwa chuki, uhasama na kupigana vijembe miongoni mwa wasanii wa fani hiyo.
Matatizo hayo kwa kiasi kikubwa yamesababisha wanamuziki wengi washindwe kupiga hatua mbele kimaendeleo, badala yake huishia njiani.
Hali hiyo imesabisha waimbaji wengi wa muziki huo waliowahi kutamba hapa nchini miaka ya nyuma hivi sasa kutoonekana tena kwenye tasinia hiyo.
Mbali na kutoweka kwa baadhi ya wasanii, matatizo hayo yamesababisha soko la muziki huo kushuka kadri siku zinavyosonga mbele. Umaarufu wa wasanii wa muziki huo umekuwa ukibaki na kuishia hapa hapa nchini.
Hali hiyo imeonekana kumgusa na kumkera sana mkongwe wa muziki huo nchini, Khadija Omar Kopa, ambaye ameeleza kinagaubaka sababu zinazochangia kuzorota kwa maendeleo ya muziki huo.
“Hakuna kingine zaidi ya waimbani kujengeana chuki, majungu na kupigana vijembe,”alisema Khadija wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Ladha za Pwani, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha C2C.
Khadija alisema katika siku za hivi karibuni, kumezuka baadhi ya waimbaji, ambao wamekuwa wakipika majungu kwa wenzao kwa lengo la kuwadhoofisha, hali inayorudisha nyuma maendeleo na maudhui ya muziki huo.
Mwanamama huyo aliyejengeka kimwili alisema, lengo la muziki wa taarab ni kuelimisha, kufurahisha na kutoa ujumbe kwa jamii na si kujengeana chuki, fitina na majungu kama ilivyozoeleka hivi sasa.
Mkongwe huyo wa mipasho aliyewahi kujizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchini alisema, kinachoshangaza ni kwamba tabia hiyo hufanywa na waimbaji chipukizi na baadhi ya vikundi vilivyoibuka hivi karibuni.
"Nawasikitikia sana hawa waimbaji chipukizi kwa kujiingiza kwenye matatizo. Badala ya kuendeleza vipaji vyao, wao wanaendeleza malumbano," alisema.
Mwimbaji huyo mwenye macho yenye mvuto na sauti ya kubembeleza alisema binafsi ameshangazwa na kukerwa zaidi na kikundi cha taarab cha Jahazi Modern kutokana na vitendo wanavyomfanyia.
Alisema baadhi ya waimbaji na viongozi wa kundi hilo wamejenga chuki za waziwazi dhidi yake, bila sababu yoyote, hali inayomweka kwenye wakati mgumu.
Khadija alisema mara kadhaa anapoalikwa kufanya maonyesho kwa kushirikiana na kundi hilo, viongozi na wasanii wake humfanyia vituko vya kila aina, ambavyo humfanya wakati mwingine ashindwe kuimba.
"Mara kwa mara ninapoalikwa kuimba pamoja na Jahazi, huwa sipewi ushirikiano. Hunifanyia vituko vingi sana,”alisema.
Mkongwe huyo wa taarab, aliyeanza kung’ara akiwa katika kundi la Culture la Zanzibar, alisema binafsi hana bifu na uongozi ama msanii yeyote wa kundi hilo na kwamba anawaheshimu.
Gwiji huyo wa kundi la taarab la Tanzania One Theatre (TOT Plus), anayetamba na wimbo wa Top in Town alisema, kutokana na vituko anavyofanyiwa na uongozi wa kundi hilo, analiona kama vile limeamua kumdhalilisha na kumvunjia heshima.
Akitoa mfano alisema, katika tamasha la Mitikisiko ya Pwani lililofanyika mwishoni mwa mwaka jana katika ukumbi wa Daimond Jubilee, Dar es Salaam, alilazimika kuimba kwa tabu baada ya Jahazi kuondoa stejini baadhi vyombo vyao.
Kwa mujibu wa Khadija, kuna siku alikodiwa na mfanyabiashara Abbas Shentemba kuimba akiwa na waimbaji wengine pamoja na kundi la Jahazi, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kuwekewa ngumu na viongozi wa kundi hilo.
"Nakumbuka nilialikwa pamoja waimbji wengi, akiwemo Mohamed Iliyas na Afua Suleiman, lakini sikuweza kuimba kutokana na kubaniwa na uongozi wa Jahazi na kila nilipokuwa namkumbusha msimamizi wa onyesho hilo, alinijibu kwa kejeli,”alisema.
"Alianza kupanda jukwaani Afua, wakati anapanda Mohamed Iliyas, nilimtuma mpiga kinanda mmoja wa Jahazi akamwambie yule msimamizi kwamba akiteremka Iliyas nipande mimi, lakini wakampa majibu ya kebehi,”aliongeza.
Akisimulia zaidi mkasa huo, nguli huyo wa mipasho alisema, siku hiyo alipata taarifa mapema kwamba hawezi kuimba na alimfuata aliyemkodi na kumuuliza, lakini alimpa majibu kwamba lazima aimbe.
Alisema baada ya Iliyas kuteremka stejini, alipanda Mzee Yusuf na kuanza kuimba na hapo ndipo alipoamini maneno aliyoambiwa mapema kwamba hawezi kuimba siku hiyo.
“Baada ya Mzee Yusuf kupanda stejini, nilimfuata aliyenialika na kumuaga na yeye akakubali, kwa maana hiyo niliondoka bila kuimba,”alisema Khadija.
"Mimi binafsi ni mtu wa watu, kwa hiyo naomba kama Jahazi nimewakosea kitu, wanambie ili niwaombe radhi na mimi kama wamenikosea waniombe radhi,”aliongeza.
"Namheshimu kila mtu, sijawahi kugombana na yeyote, naona Jahazi wanajisumbua kwa sababu kwangu ni watoto wadogo sana," alisema.
Mkongwe huyo wa mipasho amewatahadharisha waimbaji chipukizi kwa kuwataka wasibweteke na kuvamia mambo yasiyowahusu badala yake waonyeshe vipaji vyao.Alisema waimbaji wengi chipukizi wanalewa sifa na kusahau wajibu wao.
Khadija, ambaye alizaliwa miaka 47 iliyopita katika mtaa wa Makadara, Zanzibar amewahi kuimba pia kwenye vikundi vya East African Melody na Muungano.

KHADIJA YUSUPH:SINA UGOMVI NA MZEE YUSUPH

MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Khadija Yussuf ameanika hadharani sababu za kuondoka kwake katika kundi la Jahazi Modern Taarab, linaloongozwa na kaka yake, Mzee Yussuf.
Akizungumza mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Khadija alisema alijiengua katika kundi hilo kwa sababu ya maslahi duni si vinginevyo.
Khadija alisema si kweli kwamba aliondoka katika kundi hilo kutokana na kushindwa kuelewana na Mzee, hasa katika mambo ya maslahi.
Mwanamama huyo tipwatipwa alijiengua katika kundi la Jahazi mwaka mwishoni mwa mwaka jana na kujiunga na kundi jipya la Five Stars Modern Taarab.
"Sina ugomvi wowote na Mzee, yeye ni kaka yangu, tunaheshimiana sana na tunaelewana sana, lakini nilihama katika kundi lake kutokana na uchache wa maslahi," alisema.
Mwimbaji huyo anayependwa na mashabiki wengi kutokana na sauti yake maridhawa alisema, yupo tayari kufanya maonyesho na kaka yake iwapo atatakiwa kufanya hivyo.
Alisema tangu ajiunge na kundi la Five Stars, linaloongozwa na Ally Jay, mambo yake yamekuwa mazuri na hana matatizo kama alivyokuwa Jahazi.
"Hivi sasa mambo yangu yanakwenda vizuri, tofauti na nilipokuwa Jahazi, namshuruku Mungu malengo yangu yametimia," alisema.
Khadija aliwahi kutamba kwa vibao vyake vitamu kama vile Mkuki kwa Nguruwe, Zilipendwa, Hayanifiki, Hamchoki kusema, Riziki mwanzo wa chuki.
Alikiri kwamba kibao kilichompandisha chati na kumpatia umaarufu mkubwa ni Mkodombwe, alichokiimba wakati akiwa katika kundi la East African Melody.
Khadija alisema kwa sasa anajipanga upya kabla ya kuibuka na kibao chake kipya kitakachojulikana kwa jina la Ukisema cha nini.
"Ninawaahidi mashabiki wangu wakae mkao wa kula kwani niko mbioni kuachia tungo yangu mpya, ambayo bila shaka itakuwa gumzo hapa nchini," alisema.

MARIAM KHAMIS: SIJAPOTEA NJIA KUJIUNGA NA TOT

MWIMBAJI nyota wa taarab nchini, Mariam Khamis amesema hajapotea njia kutokana na uamuzi wake wa kujiengua kutoka katika kundi la Five Stars Modern Taarab na kujiunga na kundi la Tanzania One Theatre (TOT).
Mariam alisema mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, uamuzi wake huo umelenga kutafuta maslahi bora zaidi na pia kujiandaa kwa maisha yake ya baadaye.
Alisema hakuondoka Five Stars kwa kufukuzwa bali alifanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe kwa vile maisha ni kutafuta na ahangaikaye siye sawa na mkaa bure.
“Unajua linapotokea jambo, huwa yanasemwa mengi, lakini huo ndio ukweli wenyewe,”alisema.
Mariam, ambaye aliwahi kutamba kwa kibao chake cha ‘Paka mapepe’ alisema, ameamua kujiunga na TOT kwa sababu ajira yake ni ya uhakika tofauti na vikundi vingine.
Alisema wasanii wote wanaounda kundi la TOT hawategemei mapato ya milangoni kulipana mishahara na hata wasipofanya maonyesho, malipo yao kwa mwezi yapo palepale.
Tayari mwimbaji huyo mwenye sauti maridhawa, ameshatungiwa wimbo unaojulikana kwa jina la ‘Sidhuriki kwa lawama’, na unatarajiwa kuanza kusikika hewani hivi karibuni.
“Nawaomba mashabiki wangu wasichukie kwa sababu maisha ni kutafuta, wakubali matokeo,”alisema.
Mwimbaji huyo mwenye sura yenye mvuto alikiri kuwa, tangu alipojiunga na TOT, yamesemwa mengi juu yake, lakini hajali na anayachukulia kama changamoto katika maisha yake.
“Wengine wanasema nimekwenda TOT kujimaliza kiusanii, wengine wanasema nitakufa, lakini mimi sijali. Tangu nilipozaliwa, nilishatia saini mbele ya Mungu kwamba nitakufa siku fulani,”alisema.
Alisisitiza kuwa, ili msanii aweze kukomaa kiusanii, anapaswa kutembea katika vikundi mbalimbali kama ilivyo kwa waimbaji nyota wa muziki huo, Khadija Omar ‘Kopa’, Sabah Salum na wengineo.
“Hata mimi utafika wakati nitakuwa hivyo na kuamua kutulia kama wakongwe hao,”alisisitiza.
Mbali na kuimbia kundi la Five Stars, Mariam pia aliwahi kung’ara alipokuwa katika vikundi vya East African Melody na Zanzibar Stars.Baadhi ya vibao alivyotamba navyo katika vikundi hivyo ni pamoja na ‘Huliwezi bifu’, ‘Raha ya mapenzi’ na ‘Ndo basi tena’.