KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, January 29, 2014

ALLY J AKABIDHIWA FIVE STARS


ALIYEKUWA mmiliki wa kikundi cha muziki wa taarab cha Five Stars, Shaks amesema, ameamua kumkabidhi kundi hilo msanii Ally J.

Shaks alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, Ally J hakuwa mmiliki wa kundi hilo, isipokuwa alikuwa miongoni mwa wasanii waanzilishi na alikabidhiwa jukumu la uongozi.

"Wakati nalinunua kundi hili, Ally J alikuwa miongoni mwa wasanii niliowakuta na alikuwa miongoni mwa waanzilishi, hakuwahi kuwa mmiliki,"alisema.

Shaks alitoa ufafanuzi huo baada ya Ally J kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni akisema kuwa, Five Stars haiwezi kufa.

Majigambo hayo ya Ally J yalikuja baada ya Shaks kutangaza kulivunja kundi hilo wiki mbili zilizopita.

"Kwa sasa Ally J ana uwezo na haki ya kusema chochote kuhusu Five Stars kwa sasa nilimpa umiliki wa kundi hilo bure bila kumuuzia,"alisema Shaks.

Hata hivyo, Shaks alisema Ally J hana haki ya kuwamiliki wasanii wa kundi hilo kwa vile alishavunja mikataba yao na kuwaruhusu kujiunga na vikundi vingine.

MWANAHAWA: SIWEZI KUACHA KUIMBA TAARAB


MWIMBAJI mkongwe wa nyimbo za muziki wa taarab nchini, Mwanahawa Ally, amesema hawezi kuacha muziki huo kwa sasa kwa sababu ndio unaomwezesha kuendesha maisha yake.

Mwanahawa alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, sauti yake ndiyo kipaji alichopewa na Mungu kinachomwingizia kipato chake cha kila siku.

Mwanamama huyo, aliyejiunga na kikundi cha Dar Modern Taarab hivi karibuni alisema, ataachana muziki baada kujiona hawezi kuimba kama ilivyo kawaida yake.

"Labda itokee nimepatwa na ugonjwa ambao utanifanya nishindwe kabisa kuimba, lakini kwa sasa sifikirii kabisa kuacha muziki wa taarab,"alisisitiza.

Mwanahawa ni miongoni mwa wasanii wa kundi la Five Stars Modern Taarab waliopata ajali mwaka juzi mkoani Morogoro na kunusurika kufa. Katika ajali hiyo, wasanii tisa walipoteza maisha.

Kwa sasa, Mwanahawa na kundi lake la Dar Modern Taarab, wanajiandaa kwa uzinduzi wa albamu yao mpya, utakaofanyika Februari 14 mwaka huu.

KHADIJA KOPA KUANZISHA KUNDI LAKE LA TAARAB?



KUNA habari kuwa, mwimbaji nyota wa muziki wa taarab hapa nchini, Khadija Omar Kopa, anafanya mipango ya kuanzisha kikundi chake cha muziki huo.

Habari za uhakika kutoka kwa watu wa karibu na msanii huyo zimeeleza kuwa, tayari Khadija ameshaagiza vyombo vipya vya muziki kutoka China.

Kwa mujibu wa habari hizo, vyombo hivyo vinatarajiwa kutua nchini wakati wowote kabla ya kundi hilo kuingia kambini kwa lengo la kuandaa nyimbo mpya.

Kwa sasa, Khadija ni mwimbaji na Mkurugenzi Msaidizi wa kikundi cha sanaa za maonyesho cha Tanzania One Theatre (TOT).

Mbali na kuwa msanii wa TOT, Khadija pia amekuwa akirekodi nyimbo zake binafsi na kufanya maonyesho kwa kujitegemea.

THABIT ABDUL AIPELEKA MODERN TARADANSI STUDIO


KUNDI jipya la muziki wa taarab la Modern Taradansi, linaloongozwa na Thabiti Abdul, limeingia studio kurekodi nyimbo zake mpya tatu.

Akizungumza na Burudani wiki hii, Thabiti alisema wamerekodi nyimbo hizo kwenye studio za Sound Crafters, zilizoko Temeke, Dar es Salaam.

Thabiti, ambaye ni mtunzi na mpiga kinanda hodari nchini alisema, wamerekodi nyimbo hizo kwa lengo la kukitambulisha rasmi kikundi hicho.

Hata hivyo, Thabiti hakuwa tayari kutaja majina ya nyimbo hizo kwa madai kuwa, watazitangaza rasmi mwishoni mwa wiki hii.

Kiongozi huyo wa Modern Taradansi, pia hakuwa tayari kutaja majina ya wasanii wanaounda kikundi hicho kwa madai kuwa, watajulikana siku ya utambulisho.

"Kwa sasa ni mapema kuwataja wasanii wanaounda kundi letu na pia nyimbo zetu mpya. Tutafanya hivyo siku ya utambulisho,"alisema.

DAR MODERN TAARAB SASA INATISHA, YANYAKUA NYOTA WAPYA KADHAA

Mwamvita Shaibu
Zubeda Mlamali

BAADA ya kujiimarisha kwa kunyakua wasanii mbalimbali wapya wa taarab kutoka katika vikundi vingine, kikundi cha Dar Modern kimeingia studio kurekodi albamu yake ya pili.

Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo, zilirekodiwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye studio za Sound Crafters zilizoko Temeke, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na kikundi hicho wiki hii imeeleza kuwa, albamu hiyo mpya itakuwa na nyimbo saba zilizoimbwa na wasanii tofauti.

Kwa mujibu wa taarifa, lengo la kurekodi albamu hiyo ni kutambulisha ujio mpya wa kikundi hicho baada ya kutumia fedha nyingi kunyakua waimbaji nyota kutoka vikundi mbalimbali maarufu vya muziki huo.

"Lengo letu ni kuifanya Dar Modern Taarab itishe na iwe na kikosi kizuri baada ya kunyakua wasanii wazuri,"imeeleza taarifa hiyo iliyotiwa saini na mmoja wa viongozi wa kundi hilo, Adam Mlamali.

Miongoni mwa waimbaji wapya wanaounda kundi hilo ni pamoja na mkongwe, Mwanahawa Ally, Mwamvita Shaibu, Husna Mlamali, Zubeda Mlamali na Mossy Suleiman.

Vibao vipya vilivyorekodiwa na kikundi hicho ni Oh my honey (Hassan Vocha), Naenda kwa mume wangu (Husna Mlamali), Sikuamini macho yangu (Mwamvita Shaibu), Malipo duniani (Zubeda Mlamali), Siwanyimi uzuri (Mwanahawa Ally).

Mlamali hakutaka kutaja jina la wimbo ulioimbwa na Mossy kwa madai kuwa, wanataka iwe 'sapraisi' kwa mashabiki wao.

"Huu wimbo utakuwa sapraisi kwa mashabiki wakati tutakapozindua albamu yetu,"alisema Mlamali.
Kwa mujibu wa Mlamali, uzinduzi wa albamu hiyo umepangwa kufanyika Februari 14 mwaka huu, kwenye ukumbi wao mpya wa Dar Modern Hall ulioko Magomeni, Dar es Salaam.

Monday, January 27, 2014

KWENYE PICHA MNAPENDEZA, LAKINI MH....

Ni tangazo la Jahazi. Lakini pia picha ya wanafamilia, Mzee Yussuf, mkewe Leila Rashid na dada mtu, Khadija Yussuf. Leila ni mke wa Mzee na pia wifi ya Khadija.

Kwenye picha mnapendeza, lakini haifurahishi kusikia Khadija na Leila hawaelewani, wanagombana mara kwa mara. Haipendezi.

PENZI MARIDHAWA LA HAMMER Q NA SALHA

HAWA ni waimbaji nyota wa nyimbo za muziki wa taarab, Hammer Q na Salha. Kuna wakati walikuwa kundi moja la Dar Modern Taarab. Baadaye Hammer Q alihama na kwenda Five Stars Modern Taarab. Walifunga ndoa mwaka jana. Kumbe walianza mapenzi tangu zamani kabla ya Salha kuolewa. Alipoachika wakaamua kukumbusha ya zamani, lakini si kwa kuibia bali kufunga ndoa. Nimeipenda picha yenu na hongereni sana. Kusema kweli mnapendeza. Hayo macho ya Salha usiseme.

Monday, January 20, 2014

JAHAZI MODERN TAARAB YAPAGAWISHA MASHABIKI DAR LIVE

Mwimbaji na kiongozi wa kundi la Jahazi Modern Taarab akiwapagawisha mashabiki wakati wa onyesho hilo.
Mzee Yussuf na wacheza shoo wa Jahazi wakiwajibika jukwaani
 
 
Mwimbaji wa kundi la Jahazi, Leila Rashid akiwajibika jukwaani. Leila ni mke wa Mzee Yussuf

Mashabiki wa Jahazi wakijimwayamwaya wakati wa onyesho hilo

Mpiga kinanda Chid Boy akifanya vitu vyake

Mashabiki hawa walishindwa kuvumilia, walipandwa midadi na kupagawishwa na muziki wa Jahazi. (Picha zote na Mussa Mnally wa Global Publishers)

Thursday, January 9, 2014

JAHAZI YAFAFANUA SABABU ZA KUPELEKA UZINDUZI MOROGORO



KIKUNDI cha taarab cha Jahazi kimefafanua kuwa, kimetoa ufafanuzi
kuhusu uamuzi wake wa kuuchagua mkoa wa Morogoro kuwa mwenyeji
wa utambulisho wa nyimbo zake mpya.
Taarifa iliyotolewa na kikundi hicho wiki hii imeeleza kuwa, onyesho la
utambulisho wa nyimbo hizo, zitakazokuwemo kwenye albamu mpya,
litafanyika Januari 31 mwaka huu kwenye ukumbi wa Tanzanite Complex.
Mmoja wa viongozi wa Jahazi, Mohamed Mauji amesema wameamua
kuuchagua mji wa Morogoro kwa vile wanao mashabiki wengi huko.
Mauji, ambaye ni mpiga gita mahiri la solo, amesema mji wa Morogoro ni
ngome yao ya pili kwa ukubwa baada ya Dar es Salaam.
"Mara zote Jahazi imekuwa ikitambulisha nyimbo zake mpya Dar es
Salaam, na baadaye kuzitambulisha mikoani, lakini safari hii tumeamua
kuanzia Morogoro,"alisema.