KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Monday, September 17, 2012

REHEMA TAJIRI, MWANAMUZIKI ALIYEAMUA KUJITOSA KWENYE TAARAB


BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwanadada Rehema Tajiri ameibuka upya, lakini safari hii ameamua kujitosa kwenye muziki wa miondoko ya zouk na taarab.
Rehema, ambaye alianza kuchomoza kimuziki mwaka 2002, anatarajia kurekodi albamu ya zouk kwa ajili ya kuuaga muziki wa dansi kabla ya kuhamia kwenye mipasho.
Mwanamama huyo ameamua kujitosa kwenye taarab kwa kile anachodai kuwa, muziki huo una mvuto mkubwa ikilinganishwa na dansi na kwamba ameshaanza kufanya vizuri katika kikundi cha Jahazi Korongwe chenye maskani yake Temeke, Dar es Salaam.
Kikundi hicho ni maalumu kwa ajili ya kupiga nyimbo za kuiga za vikundi mbali mbali vya taarab na kwa Rehema, amekuwa akipendelea zaidi kuimba nyimbo za Mwanahawa Ally wa kundi la East African Melody, Leila Rashid na Khadija Yussuf wa kundi la Jahazi.
Akizungumza na Uhuru mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Rehema alisema anaamini kuwa, huo ni mwanzo tu wa safari yake ndefu katika muziki huo kwa vile lengo lake kubwa ni kuimba nyimbo zake mwenyewe za taarab.
Mama huyo wa watoto wawili alisema amekuwa kimya kwa muda mrefu kutokana na kutingwa na masomo na pia matatizo ya kifamilia. Hata hivyo, alisema kwa sasa anamshukuru Mungu kwamba ameweza kuvivuka vikwazo vingi vilivyokuwa vikimkwaza katika kazi yake hiyo.
Rehema alianza kung’ara kimuziki baada ya kuibuka na albamu yake ya kwanza inayojulikana kwa jina la Sumu ya Ndoa. Alirekodi albamu hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya wanamuziki nyota waliokuwa wakiunda bendi ya Msondo Ngoma, wakiwemo marehemu Moshi William na Maneno Uvuruge.
Baadhi ya vibao vilivyokuwemo kwenye albamu hiyo ni pamoja na Maisha Vijijini, Binadamu hawana wema, Karibu shemeji na muziki ni kazi.
Rehema alisema alipata mafanikio makubwa kutokana na mauzo ya albamu hiyo kwa vile aliweza kuwalipa wanamuziki alioshirikiana nao pamoja na kupata faida kidogo.
Alirekodi albamu yake ya pili mwaka 2005, inayojulikana kwa jina la Ni wako tu, lakini safari hii hakuwatumia wanamuziki maarufu. Alimtumia mwanamuziki mwingine nyota wa kike, Dotnata.
Baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Sirudi nyuma, Namsaka mbaya wangu, Penzi la uongo na Nicheze na nani.
“Katika albamu hii, sikutaka kuwashirikisha wanamuziki wengine kwa sababu mara ya kwanza nilisakamwa sana na maneno. Wapo waliodai kuwa, nyimbo zote za kwenye albamu ya kwanza nilitungiwa na marehemu Moshi, wengine wakazua uongo kwamba alikuwa mpenzi wangu wakati si kweli,”alisema Rehema.
“Na hata nilipomshirikisha Dotnata, walimwengu hawakukosa maneno ya kuzungumza. Na nilipotengeneza video ya wimbo wangu kwa kumshirikisha Dokta Cheni, pia yakasemwa maneno mengi. Ndio sababu niliamua kuwa kimya kwa muda,”aliongeza mwanamuziki huyo.
Rehema, ambaye ni mke wa zamani aliyekuwa kipa namba moja wa Yanga, marehemu Sahau Kambi alisema, albamu yake itakayofuata hivi karibuni itakuwa ya muziki wa zouk.
Alisema ameshaanza maandalizi kwa ajili ya kurekodi albamu hiyo, lakini hakuwa tayari kuzitaja nyimbo zitakazokuwemo ndani yake. Alisema atazitangaza baada ya kuzikamilisha.
Baada ya albamu hiyo, Rehema alisema itakayofuata itakuwa ya taarab, ambayo atarekodi kwa kushirikiana na wasanii mbali mbali nyota wa muziki huo.
Pamoja na kurudi kwenye gemu kivingine, Rehema pia ameamua kuwa mwanasiasa na hivi karibuni alichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa UWT mkoa wa Dar es Salaam na mjumbe wa baraza la UWT la wilaya ya Temeke.
Aliibuka wa pili katika uchaguzi wa mkoa baada ya kuzoa kura 448 wakati katika uchaguzi wa wilaya, aliibuka kinara kwa kuzoa kura 538.
Rehema alisema hii ni mara yake ya pili kujitosa katika uchaguzi wa jumuia hiyo, mara ya kwanza ikiwa miaka mitano iliyopita, ambapo kura hazikutosha.
Mwanamama huyo alisema ameamua kujitosa kwenye siasa kwa lengo la kufuata nyayo za baba yake, marehemu Hamisi Tajiri, ambaye aliwahi kushika nyadhifa kadhaa za uongozi za CCM katika ngazi ya tawi na kata.
Marehemu Tajiri, ambaye alikuwa mmoja wa waigizaji magwiji wa maigizo wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) miaka ya 1970 hadi 1980, pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA).
“Nimeamua kujitosa kwenye siasa kwa lengo la kufuata nyayo za baba yangu na pia kutetea haki za akina mama,”alisema Rehema.
Kwa mujibu wa Rehema, uamuzi wake huo hauna lengo la kutaka kuwania ubunge ama udiwani katika uchaguzi mkuu ujao, bali kuwatumikia wanawake wenzake.
“Nataka kuwanasua akina mama, hasa wa vijijini, ambao wanatumika zaidi katika kazi za kilimo na kijamii kuliko akina baba,”alisisitiza.
Hata hivyo, alikiri kuwa kazi hiyo ni ngumu na inahitaji moyo kutokana na ukweli kwamba, ni hulka kwa akina mama kutokuwa na utamaduni wa kupendana zaidi ya kusemana.
Alisema kutokana na mapenzi yake katika kuwainua kina mama, hata nyimbo nyingi anazotunga zimekuwa zikizungumzia maisha yao na matatizo yanayowakuta katika jamii.
Pamoja na kujitosa kwenye siasa, Rehema alisema hatarajii kuitumia fani ya muziki kumbeba kama ilivyo kwa wanasiasa wengine. Alisema atatumia nguvu ya marehemu baba yake na ushawishi alionao kwa wanawake wenzake.
Rehema amewahi kutunga wimbo wa kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa nafasi nyingi za uongozi kwa wanawake na pia kwa uongozi wake mzuri na uliotukuka kwa watanzania.
Alisema kwa sasa, ameshatunga nyimbo mbili kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao mkoani Dodoma, lengo likiwa kuwahamasisha wanachama wake kuchagua viongozi wenye uwezo wa kukivusha na kukifikisha chama mbali zaidi.
Amewashukuru waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari kwa kumpa ushirikiano mkubwa katika kipindi chote alichokuwa kwenye fani hiyo na kusisitiza kuwa, bila wao asingeweza kufika alipo sasa.
“Kwa moyo wa pekee, nawashukuru sana waandishi wa habari, walifanyakazi kubwa sana ya kunitangaza hadi nikafahamika nchi nzima. Bila wao, nisingekuwa Rehema ninayejulikana sasa,”alisema.
“Pia nawaomba mashabiki wangu wasiwe na wasiwasi wowote. Najua hawajaniona kwa muda mrefu, lakini nipo, nilikuwa nasoma na pia nilipatwa na matatizo ya kifamilia, lakini sasa mambo yapo safi,”alisema.
Rehema alisema baadhi ya mashabiki wake walikuwa wakimtumia barua pepe na wengine kuwasiliana naye kwenye facebook kutaka kujua alipo. Alisema alishindwa kujibu meseji zingine kutokana na matatizo aliyokuwa nayo.
“Lakini nawapenda sana wote. Watarajie kuniona tena kwenye muziki hivi karibuni na pia kwenye ulingo wa kisiasa,”aliongeza.

No comments:

Post a Comment