KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, April 17, 2013

WASEMAVYO WASANII KIFO CHA BI KIDUDE


BAADHI ya wasanii wa filamu na muziki nchini wameeleza kusikitishwa na kifo cha msanii mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Fatuma Binti Baraka, maarufu zaidi kwa jina la Bi Kidude.
Wakizungumza na magazeti ya Burudani na Uhuru jana, wasanii hao walisema kifo cha msanii huyo mkongwe ni pigo kubwa katika tasnia ya taarab nchini.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Wilsoni Makubi alisema, kifo cha Bi Kidude ni pengo kubwa kwa wasanii kwa vile alikuwa akichukuliwa kuwa mfano wa kuigwa na wasanii.
Makubi alisema tasnia ya sanaa ilimtumia Bi Kidude katika sehemu mbili, moja katika muziki na nyingine katika filamu na kufanikisha kazi zao kuwa nzuri na za kuvutia.
Alisema msanii huyo alikuwa kiraka kwani kila alichoombwa kukifanya, alishiriki kikamilifu bila kuharibu kazi za wahusika na alijitolea kufanya kazi na wasanii wengi bila kujali aina ya kazi na umri wa wahusika.
Alisema pia kuwa, Bi Kidude alikuwa balozi wa wasanii katika nchi za nje kwa kuwa wengi waliifahamu Tanzania kupitia kazi zake na hivyo kuinufaisha kiutalii.
"Ukiangalia katika matamasha mengi yaliyokuwa yakifanyika Zanzibar kama vile ZIFF, watalii wengi walikuwa wakimfuata Bi Kidude," alisema Makubi.
Msanii nyota wa filamu nchini, Jacob Steven 'JB' alisema taarifa za kifo cha msanii huyo zilimshtua, lakini kwa vile ni kazi ya Mungu, haina makosa.
JB alisema wasanii wa Tanzania wanapaswa kujifunza mengi kupitia kwake ili kuuenzi mchango wake katika muziki wa taarab.
Mwanamuzi Judith Wambura, maarufu kwa jina la Lady JayDee, kupitia ukurasa wake wa twitter aliandika: "Mungu ni mwema na mapenzi yake yatimizwe kwa kuwa msanii huyo ameweza kufanikisha mengi katika uhai wake na hasa kuwa mfano kwa wasanii wengi."
Jay Dee alisema atamkumbuka msanii huyo kupitia wimbo wake wa 'Muhogo wa Jang'ombe', ambao aliuimba kwa mara ya pili na kuwa moja ya nyimbo zilizompatia umaarufu.
"Ukitaka kujua kama Bi Kidude alikuwa kipenzi cha watu na alisaidia mafanikio ya wasanii wengi, angalia waliofanya naye kazi jinsi kazi zilivyopata mafanikio," alisema Jay Dee.
Mkurugenzi wa kikundi cha Jahazi, Mzee Yussuf alisema, amesikitishwa na kifo cha mkongwe huyo na kumuombea mapumziko mema.
Alisema katika kumuenzi msanii huyo, atatayarisha wimbo mmoja
utakaoelezea wasifu wake na kazi zake.
Mkurugenzi wa kikundi cha taarab cha Wanawake cha Zanzibar, Maryam Mohammed Hamdan alisema, kifo cha Bi Kidude ni pigo zima kwa taifa kwa vile alikuwa kipenzi cha wengi.
Uongozi wa Tamasha la Sauti za Busara umesema, ilikuwa vigumu kwao kuamini taarifa za msiba wa msanii huyo kutokana na kuzushiwa kifo mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment