KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, April 17, 2013

BI KIDUDE HATUNAYE, KUZIKWA LEO Z'BAR


Na Aboud Mahmoud, Zanzibar
MSANII mkongwe wa fani ya muziki wa taarab nchini, Fatuma Binti Baraka, maarufu kwa jina la Bi Kidude amefariki dunia.
Bi Kidude alifariki dunia leo saa 6:45 mchana nyumbani kwa mtoto wa ndugu yake, maeneo ya Bububu, Zanzibar baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya msiba huo kuhamishiwa nyumbani kwake maeneo ya Rahaleo, mmoja wa wajukuu wa marehemu, Omar Ameir alisema, marehemu Bi Kidude alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa idi na sukari.
"Bi Kidude alikuwa akiugua kwa muda mrefu na kutibiwa katika hospitali mbalimbali hapa nchini. Mara ya mwisho alitibiwa katika hospitali ya KMKM,"alisema.
Kwa mujibu wa Ameir, mazishi ya Bi Kidude yanatarajiwa kufanyika kesho mchana kijiji kwake Kitumba, Wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.
Hali ya afya ya Bi Kidude ilianza kuzorota kuanzia mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha alazwe katika hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam.
Wakati alipolazwa kwenye hospitali hiyo, watu wengi walikuwa wakipishana kwenda kumsalimia, wengine wakitoka nje ya nchi.
Jambo moja kubwa, ambalo Bi Kidude alikuwa akililaani vikali wakati huo ni taarifa za kuzushiwa kufariki dunia.
“Watu wamenizushia kufa na wewe hukuja kuniona, ulifikiri nimekufa? Mi mzima, si unaniona, cheki,”alisema Bi Kidude huku akiuvuta
mkono wa mwandishi wa makala hii kwa nguvu, akiuminya ‘kibaunsa’ kuonyesha nguvu za misuli yake, kwamba yeye yuko mzima.
Bi Kidude alilazwa kwenye hospitali hiyo kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya sukari, ambayo alikuwa akiugua kwa kwa muda mrefu, lakini yalimzidia kutokana na kukiuka taratibu za vyakula.
“Kweli nilikuwa naumwa, ngozi yote ilivuka hii, nilikonda sana, ila sasa Alhamdulillah mi mzima, naweza kuondoka,”alisema.
Muda wote, ambao Bi Kidude amekuwa akiugua, alikuwa akiuguzwa na watoto wa ndugu zake. Hakubahatika kuzaa.
Ndugu wote watatu, ambao ni wadogo zake Bi Kidude, walishafariki dunia. Alikuwa anakula matunda ya watoto wa ndugu zake hao, ambao ndio waliokuwa wakimlea.
Baada ya kutolewa katika hospitali hiyo, Bi Kidude hakuruhusiwa kufanyakazi yoyote ya saa. Alitakuwa kupumzika. Pia alipigwa marufuku na madaktari kuvuta sigara.
Bi Kidude alikuwa gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, katika fani ya mwambao, ambayo hujulikana kwa jina la taarabu. Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa vionjo kutoka nchi za Kiarabu na Kiafrika, umetikisa sana katika mwambao wa Afrika Mashariki, yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Marehemu Bi Kidude alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo, Zanzibar katika familia ya watoto saba (7). Baba yake, Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi.
Wakati wote wa uhao wake, hakuwa akifahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa alichojua ni kwamba, alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha na kwamba ilikuwa kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.
Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo, walimpigia hesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 100.
Bi Kidude alianza uimbaji tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba enzi hizo, Sitti Binti Saad.
Wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kwenda kumuona Sitti na kwa vile alikuwa karibu na Bi Kidude, yeye ndiye aliyewapeleka nyumbani kwake na kupata nafasi ya kumsikia akiwaimbia.
Alipokuwa na umri wa miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara. Alifanya hivyo
baada ya kulazimishwa kuolewa.
Hata hivyo, alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa, aliolewa japokuwa ndoa hiyo  haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata. Hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930.
Akiwa Misri, aling'ara katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940, aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake za uimbaji.
Enzi za uhai wake, Bi Kidude hakuwa akitegemea kazi moja tu ya kuimba. Alikuwa akifanya biashara zingine kama vile kuuza 'wanja' na 'hina', ambavyo alivitengeneza mwenyewe.
Mkongwe huyo pia alikuwa mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba. Zaidi ya hayo, alikuwa mwalimu mzuri wa 'Unyago' na aliwahi kuanzisha chuo chake. Aliwahi kutamba kuwa,
katika wanafunzi wake wote, hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Marehemu Bi Kidude amewahi kutembelea nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza. Pia amewahi kupata tuzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) 1999.
Mwaka jana, mkongwe huyo alipata tuzo ya WOMAX. Miongoni mwa nyimbo alizowahi kuimba na kumpatia umaarufu ni Muhogo wa Jang'ombe.
Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Quraan.

No comments:

Post a Comment