KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, April 17, 2013

BURIANI MANJU HAJI MOHAMED


HATIMAYE safari ya miaka 55 ya msanii nguli na mkongwe wa fani ya muziki wa taarab nchini, Haji Mohamed Omar ilikoma Jumatatu iliyopita baada ya kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa sukari.
Marehemu Haji, ambaye alikuwa mkurugenzi wa kundi la East African Melody, alifariki dunia saa nne asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, ambako alipelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kutojisikia vizuri.
Mazishi ya Haji yalifanyika juzi Zanzibar na kuhudhuriwa na mamia ya watu, wakiwemo wasanii mbalimbali wa muziki huo.
Kifo cha Haji ni pengo kubwa katika muziki wa taarab, hasa ile ya kisasa. Licha ya kuwa mmoja wa waanzilishi wa kundi la East African Melody, alikuwa mtunzi na mwimbaji mzuri wa muziki huo.
Marehemu Haji ni uzao wa mwasisi wa taarab visiwani Zanzibar, hayati Sitti binti Saad na amewahi kupanga muziki katika nyimbo nyingi za East African Melody.
Haji amekuwa msanii wa pili wa kundi la East African Melody kupoteza maisha katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Januari mwaka huu, msanii mwingine nyota wa kikundi hicho, Lamania Shaaban naye alipoteza maisha kutokana na ugonjwa wa sukari.
Kundi la East African Melody lilianzishwa 1990 nchini Oman. Miongoni mwa waasisi wa kundi hilo ni Haji, Lamania, Peter Dawo, Ashraf Mohamed, Mlamali Adam na Mahmoud Al-Alawi.
Waimbaji wa mwanzo wa kundi hilo ni pamoja na Zuhura Shaaban, Rukia Ramadhani, Sihaba Muchacho, Khadija Yussuf, Khadija Kopa na Othman Soud.
Marehemu Haji alianza kupata umaarufu baada ya kuibuka na kibao chake cha kwanza katika kundi hilo kinachojulikana kwa jina la Majamboz na Mavituz.
Kwa kawaida, marehemu Haji alikuwa mpole, lakini alikuwa mcheshi kwa mtu alizomzoea. Ni kiongozi aliyeweza kuwafanya wasanii wa East African waishi kama ndugu kwa kusaidiana kimaisha.
Wakati kundi hilo lilipohamishia maskani yake katika Jiji la Dar es Salaam likitokea Zanzibar, Haji ndiye aliyewashawishi viongozi wenzake kununua nyumba maeneo ya Magomeni Mapipa, Dar es Salaam na kuwa makao makuu yao.
Katika upande mmoja wa nyumba hiyo, waliishi wasanii wa kike na upande mwingine waliishi wasanii wa kiume. Nyumba hiyo pia ilitumika kwa ajili ya mazoezi ya kundi hilo.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii nyumbani kwake mtaa wa Livingstone, Kariakoo, Dar es Salaam 2002, Haji alisema waliamua kuhamishia maskani yao Tanzania Bara kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mashabiki.
Miongoni mwa nyimbo za East African Melody, ambazo marehemu Haji alishiriki kuzitayarisha ni pamoja na Kinyago cha Mpapure, Bure yako, Pata leo, Hatusemani hatuchekani, Halo yako, Kama wewe hakuna, Penzi, Kipo kinachonivutia.
Marehemu Haji pia ndiye mtunzi wa nyimbo za Taxi Bubu, Shecky lesi, Sorry kwa huyu siye, Mnikome na Joho la Mungu.
Mmoja wa viongozi wa kundi hilo, Mlamali amekiri kuwa, kifo cha Haji ni pengo jingine kubwa, ambalo itakuwa vigumu kuzibika baada ya kumpoteza msanii wao mwingine Lamania.
"Ni kweli vifo vya Lamania na Haji ni pengo kubwa kwa East African Melody, lakini hatuna budi kusonga mbele,"alisema.
Kwa mujibu wa Mlamali, kundi hilo kwa sasa litakuwa chini ya Peter Dawo, ambaye atarithi cheo cha ukurugenzi, akisaidia na Ashraf.
Marehemu Haji alisoma elimu ya msingi katika shule ya Vikokotoni na kuhitimu darasa la sita 1976. Alisoma masomo ya sekondari katika shule ya Forodhani na kumaliza 1980.
Alianza kujifunza muziki katika vikundi vidogo vya muziki huo vya Zanzibar kabla ya kujiunga na kikundi kikongwe cha Ikhwan Safaa kabla ya kutua East African Melody.

No comments:

Post a Comment