KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Sunday, August 21, 2016

JK, MAKAMU WA RAIS SAMIA WAONGOZA MAZISHI YA MAREHEMU SHAKILA SAIDI

HII ni picha aliyopiga kwa mara ya mwisho marehemu Bi Shakila Saidi alipohudhuria mkutano mkuu maalumu wa CCM uliofanyika Julai 23, mwaka huu mjini Dodoma
Rais mstaafu Jakaya Kikwete akitia saini kitabu cha maombolezo baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu Bi Shakila Saidi, Mbagala Charambe, Dar es Salaam jana.
MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan akitia saini kitabu cha maombolezo baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu Bi Shakila Saidi
MKE wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete akitia saini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye akimkaribisha Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan nyumbani kwa marehemu Bi Shakila Saidi
Makamu wa Rais akiwafariji baadhi ya ndugu wa marehemu
WAZIRI Nape akiteta jambo na mmiliki wa blogu ya Michuzi, Ankal Muhidin Issa Michuzi. Katikati ni Mwenyekiti wa Chama Cha Muziki wa Dansi, Athumani Msumari
BAADHI ya waumini wa dini ya kiislamu wakijiandaa kuuswalia mwili wa marehemu Bi Shakila
MAKAMU wa Rais akishiriki kwenye dua ya kumuombea marehemu Shakila
JENEZA lenye mwili wa Bi Shakila likipelekwa makaburini. PICHA KWA HISANI YA BLOGU YA MICHUZI NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS

Saturday, August 20, 2016

MKONGWE WA TAARAB NCHINI BI SHAKILA SAIDI AFARIKI DUNIA



Bi Shakila Tatu Said Msengi muimbaji maarufu wa Taarab, hatunae tena. Jioni leo ameanguka ghafla na alipokimbizwa hospitali moja jirani na kwake Mbagala Charambe alipofika huko Bi Shakila alikata roho.

Bi Shakila alikuwa mzaliwa wa peke yake kwa baba na mama yake, alizaliwa tarehe 14 June 1947, tarehe moja na mwanamuziki mwingine mkongwe Mabruk Khamis wa Kilimanjaro Band anaejulikana kwa jina la Babu Njenje.

Mama yake Babu Njenje alikuwa na tatizo la kutoa maziwa hivyo Babu Njenje alianza kwa kunyonyeshwa na mama yake wa Bi Shakila.

Kwa kadri ya maelezo yake mwenyewe Bi Shakila alianza muziki akiwa na miaka 6, alipokuwa na umri wa miaka 12, aliteuliwa kumuimbia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipotembelea Pangani, wakati wa kutafuta Uhuru.

Na ni baada ya hapa ambapo aliweza kusikika na Bwana Khatibu ambaye aliweza kumshawishi kujiunga na kundi la Taarab lililokuwa pale Pangani lililoitwa Taarab Kijamvi, hakukaa sana katika kundi hilo akalazimika kuhamia Tanga kumfuata Bwana Khatib ambaye walibahatika kuzaa watoto watano.

Huko Tanga alijiunga na kundi la Shaabab Al Watan. Katika kundi hili hakupata nafasi ya kuimba katika kadamnasi, hivyo baada ya muda si mrefu Bi Shakila akiambatana ma mumewe walihamia kundi lililokuwa likimilikiwa na Mzee Kiroboto lililoitwa Young Noverty.
Pamoja na Bi Shakila kupata uzoefu mkubwa wa kuimba mbele za watu kundi hili lilikuwa ni kutumbuiza bure katika vikao vya kahawa.

Hatimae kundi hili lilikufa na zaidi ya nusus ya wasanii kujiunga na kundi la Black Star lililokuwa la mwarabu mmoja aliyekuwa anafanya kazi bandarini aliyeitwa Hassan Awadh na hapo ndipo Bi Shakila alipoanza kufahamika, na akapewa nyimbo kama Jongoo Acha Makuu, Mpenzi Amini, Majuto Yamenipata.

Sifa zake zikaanza kuenea Afrika Mashariki. Mwaka 1972 tajiri mwingine Mwarabu aliyeitwa Sudi Said akanunua vyombo vipya vizuri na kuanzisha kundi la Lucky Star Musical Club, hapo Bi Shakila na wenzie tisa walihama Black Star na kuhamia Lucky Star.

Kwa kuwa kundi lilianzishwa wakati Bi Shakila alikuwa mja mzito, mtoto aliyezaliwa alimuita Lucky kwa ajili ya tukio hilo. Nyimbo nyingi zinazofahamika hadi leo za Bi Shakila zilirekodiwa wakati yuko kundi hili.

Mapenzi Yamepungua, Kifo cha Mahaba. Macho Yanacheka. Bi Shakila aliendelea na kundi hili hadi mwaka 1984, Baada ya kifo cha mumewe alipumzika kwa muda kasha akahamia Dar es salaam ambapo alijiunga na kundi la JKT alilodumu nalo mpaka alipostaafu.
CHANZO CHA HABARI: BLOGU YA KITIME

Monday, August 15, 2016

MZEE YUSSUF AACHANA NA MUZIKI WA TAARAB, AAMUA KUMREJEA ALLAH



Gwiji wa mziki wa taarabu nchini Mzee Yusuf ‘Mfalme wa Taarab’ amethibitisha kuwa ameachana na kazi hiyo takribani miezi miwili iliyopita.

Taarifa zilizoenea katika mitandao ya kijamii hasa kuanzia jana zimeeleza kuwa mwanamziki huyo ameachana na mziki na kuamua kumrudia Mungu.

Akizungumza, mmiliki huyo wa bendi ya Jahazi Modern Taarab amethibitisha kuwa taarifa hizo ni za kweli: “Nashangaa taarifa hizi zinasemwa leo. Ni suala la muda mrefu… takribani miezi miwili iliyopita na sababu ni kuwa nimeamua kumrudia Allah,” Mzee Yusuf alisema.

Mwimbaji huyo wa huyo wa taarabu mzaliwa wa Zanzibar alipoulizwa kuwa ni suala gani lililomsukuma hata achukue maamuzi hayo magumu, alijibu kwa kifupi, “ndivyo tunavyofundishwa na viongozi wa dini.”

Yusuph aliyetamba na vibwagizo kama “Nichumu, nikisi….mwaaaa,” katika baadhi ya nyimbo zake, amesema familia yake imeupokea uamuzi wake kwa mtazamo chanya na kwamba inamuunga mkono.

“Kwa sasa nitaimba kaswida zenye mafundisho ya dini,” amesema nyota huo huku akiahidi kufanya mkutano rasmi kuelezea suala hilo.

Mfalme huyo aliyeonekana kuwa ni gwiji wa taarabu ya kisasa (modern taarab) amezaliwa visiwani Zanzibar mwaka 1977. Aidha amejihusisha na sanaa nyingine kama maigizo.

Ni mshindi wa tuzo katika tasnia ya muziki wa taarab zikiwemo ya Kilimanjaro Music Award 2014-15.

    Kikundi bora cha mwaka taarab – Jahazi Modern Taarab
    Mtunzi bora wa mwaka taarab- Mzee Yussuf
    Mwimbaji bora wa kiume taarab – Mzee Yussuf