Monday, May 19, 2014
BURIANI JUMA BHALO, GWIJI WA TAARAB ASILIA
Na John Kitime
Mfalme wa Taarab nchini Kenya ambaye pia amejijengea jina katika nchi za Afrika Mashariki, Mohamed Khamis Juma Bhalo, amefariki dunia. Bhalo amefariki dunia usiku wa Jumamosi akiwa nyumbani kwake eneo la mji wa zamani Mombasa, baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Juma Bhalo alizaliwa 1942 huko Shela katika wilaya ya Malindi. Mwaka1954, alijiunga na shule ya msingi ya Sir Ali bin Salim , wakati huohuo familia yake ilihakikisha anahudhuria Madrassa ili kupata elimu ya dini.
Bhallo mwenyewe aliwahi kusema hamu yake ya kuimba ilimuanza katika wakati huu na sauti yake kuwa na mvuto kutoka kipindi hiki alipokuwa Madrassa Akiwa na miaka 9 tayari muda wake mwingi ulitumika kusikiliza santuri, na akili yake ilianza kupenda sana muziki.
Hakumaliza elimu ya msingi kwa kuwa wazazi wake walishindwa kulipa ada ya shule. Mwaka 1957 alihamia Mombasa na kupata kazi Forodhani, akiwa Mombasa alianza kukutana na kushirikiana na wanamuziki wa Taarab wa Mombasa.
Hakuipenda sana kazi ya Forodha hivyo 1959 akahamia Tanga kwa mjomba wake, na hapo akajiunga na kundi maarufu la Taarab wakati ule lililoitwa Young Noverty, hapa alipata ujuzi mkubwa wa muziki wa Taarab.
Alirudi kwao Malindi kwa muda mfupi na hatimae kurudi tena Tanga 1962 na kujiunga na kundi la Young Stars Taarab.
Mwaka 1966 alirudi Mombasa na kuanzisha kundi la Bhalo and Party, kundi ambalo amedumu nalo mpaka Mauti yake.
Mwaka 2007 baada ya zaidi ya miaka 50 ya kuwemo katika muziki wa Taarab, Juma Bhalo ambaye wapenzi wake walimuita Profesa na hata Mfalme wa Taarab alitangaza kuacha kufanya maonyesho ya wazi ya taarab, alitangaza hilo siku alipopiga katika harusi ya mwanae.
Alistaafu kazi hiyo kwa maneno yafuatayo:
"Waswahili wasema kiwate kitu kabla hakijakuata. Kwa hivyo kama mulivyo nishuhudiya usiku huu nlivyowatumbuiza ambavyo ni kama kawaida yangu basi leo hii usiku huu kabla hawajaja watu wakasema ahhhhh Bhalo ashazeeka hawezi tena kuimba kwa hivyo najiuzulu ningali bado niko fiti. Kwa hivyo siimbi tena hadharani kikazi. Nawashkuru kwa ushabik wenu na musijali Mungu akiniwezesha Kasseti mpya ntawatoleya".
Taarab yake iliegemea sana muziki wa kihindi na hivyo kuwa tofauti na taarab nyingine
MUNGU AMLAZE PEMA PROFESA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment