KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Sunday, September 29, 2013

MWASITI AJIENGUA TOT PLUS



Mwasiti Suleiman (kulia) akiwa na waimbaji wenzake wa TOT katika moja ya maonyesho ya kikundi hicho.

MWIMBAJI Mwasiti Suleiman wa kikundi cha taarab cha Tanzania One Theatre (TOT Plus) ameamua kujiengua katika kikundi hicho.

Mwasiti amesema mjini Dar es Salaam leo kuwa, ameamua kujiengua TOT Plus kwa sababu ya maslahi duni.

Amesema amekuwa akifanyakazi katika kikundi hicho kwa zaidi ya miaka tisa na kuongeza kuwa, hakuwahi kuajiriwa zaidi ya kufanyakazi kama kibarua.

Amesema katika miaka miwili ya kwanza, hakuwa akilipwa chochote na kwamba katika miaka saba iliyofuata, alikuwa akilipwa posho.

Mwasiti amesema kwa sasa ameamua kufanyakazi katika kampuni moja ya Wakorea, ambayo hakutaka kuitaja, lakini pia amekuwa akijihusisha na muziki huo katika vikundi vya mitaani.

Mwanadada huyo amesema haoni tofauti yoyote katika maisha yake ya sasa na wakati alipokuwa akifanyakazi TOT Plus na kwamba muziki haikuwa ajira pekee ya kuendesha maisha yake.

"Nilipo naweza hata kuuza vitumbua au maandazi kwa sababu zote ni kazi. Kila siku tunapishana na akina mama wakifanyakazi mbalimbali na wanaishi,"amesema mwanamama huyo mwenye mwanya wa kuvutia.

Alisema hakuwahi kugombana na mtu yoyote kwa kipindi chote alichokuwa TOT Plus na kwamba aliwaaga viongozi wake huku akiwaeleza wazi kwamba maslahi duni ndiyo yaliyomkimbiza.
Amesema anaweza kuwa tayari kurudi katika kikundi hicho iwapo tu atahakikishiwa ajira na maslahi mazuri.

Mwanadada huyo amesema pia kuwa, yupo tayari kujiunga na kikundi kingine cha taarab iwapo kitamuhakikishia ajira na maslahi mazuri.

Friday, September 27, 2013

MZEE YUSUPH KUSTAAFU MUZIKI 2015


MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Mzee Yusuph amesema anatarajia kustaafu kazi hiyo katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Mzee, ambaye ni kiongozi wa kikundi cha Jahazi. amesema uamuzi wake huo umelenga kuwapa nafasi vijana kuonyesha vipaji vyao.

"Ni vigumu sana kuacha muziki wakati kikundi chako kipo juu, lakini kwa kuwa nimeshaamua, lazima nitekeleze hilo,"amesema Mzee alipozungumza na blogu ya

"Sina muda mrefu mbele, nitaweka kipaza sauti pembeni ili kuwapisha vijana waendeleze tasnia hii,"aliongeza.

Mtunzi na mwimbaji huyo mwenye sauti yenye mvuto, amesema uamuzi wake huo unaweza kuwaumiza mashabiki wake, lakini hana lingine la kufanya zaidi ya kuutekeleza.

"Kwangu mimi ni maamuzi magumu sana kwa vile nitakiacha kitu ninachokipenda na mashabiki wamenizoea, lakini itabidi wakubaliane na maamuzi haya,"alisema mwimbaji huyo, ambaye pia amepachikwa jina la Mfalme.

Kwa mujibu wa msanii huyo, baada ya kustaafu muziki, atalazimika kukivunja kikundi chake cha Jahazi na kumpatia kila msanii haki anayostahili kwa ajili ya kuendeleza maisha yake.

"Ningependa wasanii nitakaowaacha, watafute bendi zingine za kufanyakazi kwa kipindi hicho ili waendelee kuimba na kukuza zaidi vipaji vyao,"alisisitiza.

THABITI ABDUL AMWACHA SOLEMBA ISHA MASHAUZI


MKURUGENZI msaidizi wa kikundi cha taarab cha Mashauzi Classic, Thabiti Abdul amejiengua katika nafasi hiyo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kundi hilo zimeeleza kuwa, Thabiti ameshawasilisha barua ya kujitoa kwenye  kundi hilo kwa mkurugenzi wake, Isha Mashauzi.

Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Abdul au Isha kuhusu uamuzi wake huo.

Thabiti ni mmoja wa wasanii wanaounda kundi la Five Stars Modern Taarab, lakini amekuwa akishiriki mara kwa mara kwenye maonyesho ya Mashauzi Classic.

Hivi karibuni, Isha alikaririwa akisema kuwa, Thabiti bado yupo kwenye kundi hilo na amekuwa akishiriki kwenye maonyesho mbalimbali.

Habari kamili kuhusu uamuzi huu utazipata hivi karibuni kupitia kwenye blogu yako ya Rusha Roho.

ISHA: SIPENDI KUUMIZWA KIMAPENZI


KIONGOZI wa kikundi cha muziki wa taarab cha Mashauzi Classic, Isha Mashauzi amesema kamwe katika maisha yake hapendi kuumizwa kimapenzi na mwanaume.

Isha amesema anapoachana na mwanaume, huwa hageuki nyuma na kwamba mapenzi kwake ni kitu cha kupita.

"Nikiacha nimeacha, sipendi kuumizwa, kazi yangu mwenyewe inaumiza,"alisema Isha alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Ng'aring'ari kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Clouds TV mwishoni mwa wiki iliyopita.

Isha amesema amewahi kutongozwa na wanaume wengi, lakini kutokana na msimamo alionao kimapenzi, wamebaki kuwa rafiki zake baada ya kuwaeleza ukweli wa mambo.

"Wapo zaidi ya wanaume wanne, ambao walinitongoza na kunitaka kimapenzi, lakini niliwaeleza wazi kwamba, kwa vile kila mmoja ana mkewe nyumbani, siwezi kujihusisha nao katika suala hilo. Hivi sasa ni rafiki zangu wakubwa, huwezi kuamini,"alisema.

Hata hivyo, Isha ametahadharisha kuwa, mwanamke anapoamua kumtolea nje mwanaume, anapaswa kuwa makini ili kuepuka kujiingiza katika matatizo.

Alisema wapo wanaume wanaopenda vibaya na wanaoweza kufanya lolote pale wanapokataliwa kimapenzi, ikiwa ni pamoja na kuua ama kujiua.

"Hata kama humpendi, mchukulie taratibu, usimweleze kwa pupa, wewe ni mwanadamu, siyo ng'ombe, hujui anakupenda vipi,"alisema mwanamama huyo, ambaye alianza kupata umaarufu katika muziki wa taarab alipokuwa kundi la Jahazi.

Isha amekiri kuwa, aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Jumanne Tevez, ambaye alipiga naye picha za video ya wimbo wake wa Nakupenda kwa dhati, lakini hawakuwahi kupata mtoto.

Anasema anajuta kumtambulisha Tevez kwa watu wengine kwa sababu baadhi yao walitumia nafasi hiyo kumtaka kimapenzi kwa lengo la kumkomoa.

Licha ya kuachana na Tevez baada ya mpenzi wake huyo wa zamani kuoa mwanamke mwingine, Isha amesema bado wanaendelea kuwasiliana na kuwa na urafiki wa kawaida.

"Hata mkewe tuna uhusiano mzuri na wakati mwingine huwa tunapigiana simu kujulikana hali, namwita wifi naye ananiita wifi,"alisema Isha.

Isha amesema katika maisha yake, kamwe hawezi kupigana na mwanamke mwenzake kwa ajili ya kugombania mapenzi. Alisema tabia hiyo imepitwa na wakati.

Ametoa mwito kwa wanawake wa Kitanzania kujenga utamaduni wa  kupendana na kukosoana badala ya kujengeana chuki bila ya sababu za msingi.

Amesema inapendeza mwanamke anapomuonea mwenzake wivu wa kimaendeleo kwa kufanya kile kilichomvutia kutoka kwa mwenzake hata kama atakuwa anamuiga.

Isha amesema licha ya mkurugenzi mwenzake wa Mashauzi Classic, Thabiti Abdul kuhamia kundi la Five Stars, bado amekuwa akiendelea kufanya maonyesho na kundi hilo.

"Thabiti bado tuko naye, anakuja mazoezini, anapiga kinanda na gita kwenye maonyesho, kwa ujumla bado tuko naye,"alisema.

Isha amesema kwa sasa kundi lake la Mashauzi Classic linajiandaa kuipua albamu mpya, itakayokuwa na nyimbo sita. Amesema albamu hiyo itajulikana kwa jina la Asiyekujua hakuthamini.
Albamu hiyo itakuwa ya pili kwa Mashauzi Classic tangu kundi hilo lilipoanzishwa miaka miwili iliyopita.

Albamu ya kwanza inajulikana kwa jina la Si bure una mapungufu, iliyofuatiwa na Viwavi Jeshi. Albamu hizo mbili zilikuwa na nyimbo nne kila moja.

Tuesday, September 17, 2013

MWIMBAJI AHMED MGENI WA ZANZIBAR STARS AFARIKI DUNIA



MWIMBAJI  wa kikundi cha taarabu cha Zanzibar Stars, Ahmed Mgeni, amefariki dunia.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mmoja wa ndugu wa marehemu, alisema Mgeni alifariki jana saa kumi na mbili asubuhi katika hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar.

Alisema marehemu alikuwa akisumbuliwa na kichwa na alianza kuugua tangu mwezi wa nne mwaka huu lakini baadae alipata nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Alisema, hali ya marehemu ilibadilika ghafla juzi na kukimbizwa hosipitali kabla ya mauti kumfika na kusema alizikwa jana katika makaburi ya Mwanakwerekwe, Zanzibar.

Akiwa na kundi la Zanzibar Stars, marehemu aliwahi kutamba na nyimbo mbalimbali na mapema mwaka huu alianzisha kundi lake la muziki wa taarabu lililoitwa Nia Njema.