KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Thursday, August 8, 2013

FIVE STARS, MASHAUZI CLASSIC, DAR MODERN TAARAB KUTOA BURUDANI IDD EL FITR


Mwanahawa Ally-Five Stars
Isha Mashauzi-Mashauzi Classic
Mwimbaji wa Dar Modern Taarab

KUMBI mbalimbali za burudani za mjini Dar es Salaam kesho na keshokutwa zinatarajiwa kuwaka moto wakati vikundi mbalimbali vya taarab vitakapofanya maonyesho ya kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitr.

Kikundi cha taarab cha Five Stars kitasherehekea sikukuu hiyo siku ya Idd Mosi kwa kufanya onyesho katika kitongoji cha Kigogo Fresh kilichopo Pugu, Ilala, Dar es Salaam.

Kiongozi wa kundi hilo, Ally J alisema juzi kuwa, siku ya Idd Pili, kundi hilo litatoa burudani kwenye ukumbi wa Roshi Garden ulioko Mwandege, Mbagala, Dar es Salaam wakati siku ya Idd Tatu itahanikiza maraha Kibiti, Rufiji mkoani Pwani.

Ally J alisema katika maonyesho hayo, kundi hilo litatambulisha kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la Habari ya mjini.

Kundi la muziki wa taarab la Dar Modern litasherehekea siku ya Idd Mosi kwa kushusha burudani nzito kwenye kiota kipya cha maraha kinachojulikana kwa jina la Serengeti Golden Paradise Resort, Mbagala, Mbande, Dar es Salaam.

Meneja wa hoteli hiyo, Wambura  Sungura alisema juzi kuwa, kundi hilo limeahidi kuporomosha vibao vyake vipya zaidi ya vitano, vitakavyokuwemo kwenye albamu yao mpya.

Sungura amewataka wakazi wa Mbagala na vitongoji vya jirani kufika kwa wingi kwenye ukumbi huo ili kupata burudani adhimu kutoka katika kundi hilo, ambalo lilikuwa kimya kwa zaidi ya miezi miwili.

Kwa mujibu wa Sungura, kabla ya burudani hiyo, kutakuwepo na onyesho ya utangulizi la muziki wa disco kwa ajili ya watoto. Alisema onyesho hilo litaanza saa sita mchana na kuhitimishwa saa kumi na moja jioni.

Kundi la Mashauzi Classic linaloongozwa na Isha Mashauzi limeamua kukwea basi kwenda Morogoro kuwapa burudani ya kusherehekea sikukuu hiyo mashabiki wake katika kitongoji cha Mji Mpya.

Mashauzi alisema juzi kuwa, siku ya Idd Pili kundi hilo litahamishia burudani zake kwenye ukumbi wa City Pub mjini Mbeya wakati Iddi Tatu litamwaga lazi kwenye ukumbi wa Garden Park ulioko Mafinga mkoani Iringa.

Katika maonyesho hayo, Mashauzi alisema kundi hilo litatambulisha nyimbo zake nne mpya, zinazotarajiwa kuwemo kwenye albamu yao mpya, itakayokuwa na nyimbo sita.

Alizitaja nyimbo hizo, watunzi wakiwa kwenye mabano kuwa ni Asiyekujua hakuthamini (Isha na Saida), Bonge la bwana (Hashim Said), Ropokeni yanayowahusu (Saida) na Ni mapenzi tu (Zubeda Maliki).

No comments:

Post a Comment