KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, November 21, 2012

SALHA ABDALLA: SIMUHOFII MWIMBAJI YEYOTE WA TAARAB



MWIMBAJI chipukizi wa muziki wa taarab nchini, Salha Abdalla amesema hana mpango wa kukihama kikundi chake cha Dar Modern Taarab kwa vile ameridhika kwa anachokipata.
Salha amesema tabia ya wasanii kuhamahama kutoka kundi moja hadi jingine, haiwezi kuwaletea maendeleo zaidi ya kuwashusha kiusanii.
Mwanadada huyo amesema binafsi anakipenda na kukiheshimu kikundi cha Dar Modern Taarab kwa sababu ndicho kilichomlea na kumkuza katika fani ya muziki wa taarab.
Salha alisema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha Star TV mjini Mwanza.
Mwimbaji huyo mwenye sauti maridhawa na sura yenye mvuto alisema wakati alipojiunga na Dar Modern Taarab, hakuwa akifahamu kuimba, kutunga na kuimudu steji, lakini kwa sasa anaweza kuvimudu vyema vitu hivyo.
"Hivi sasa simuhofii mwimbaji yoyote wa kike kwa sababu nina uwezo wa kuimba, kutunga nyimbo na hata kuimiliki steji,"alisema mwimbaji huyo mwenye macho ya mwito.
Salha alisema hajawahi kuhama katika kikundi hicho kwa sababu ameshawaona wasanii wengi wakihama kutoka kikundi kimoja hadi kingine, lakini hawana mabadiliko yoyote makubwa kimaisha.
Amewataka wasanii wa muziki huo wajifunze kuridhika kwa kidogo wanachokipata kwa sababu maisha ni safari ndefu inayohitaji uvumilivu na subira.
"Mimi hapa Dar Modern Taarab nimefika, sina tamaa kwa sababu zinaweza kunifikisha pabaya. Ukiwa na tamaa, kuna siku unaweza usijue wapi unakoelekea,"alisisitiza mwimbaji huyo asiye na makeke.
Kwa sasa, Salha anatamba kwa kibao chake kinachojulikana kwa jina la Nauvua ushoga huku akiwa anajiandaa kuipua vibao vingine viwili vipya, vinavyojulikana kwa jina la Hasidi hana sababu na Kuomba Mungu sichoki.
Alisema kibao cha Hasidi hana sababu kinazungumzia watu wenye tabia ya kuzungumza mambo ya wenzao bila kuwa na uhakika nayo huku wakitambua wazi kwamba si ya kweli.
Alisema kibao cha Kuomba Mungu sichoki kinazungumzia dhamira aliyonayo ya kuendelea kumtegemea Mola katika kutafuta riziki huku akimuomba amwepushe na marafiki wanafiki.
Katika moja ya beti za wimbo huo, Salha anasikika akisema: "Unaweza kula, kunywa naye na kucheka naye, kumbe mbaya wako ndiye huyo huyo."
Salha ametoa mwito kwa wasanii wa kike nchini, kuzinduka na kuacha kuzubaa. Pia amewataka waache tabia ya kuwachuna wanaume kwa sababu maradhi yamekuwa mengi na kufanya hivyo ni kujikomoa wenyewe.
"Tuache kufuatilia fulani anafanya nini, tuwe na wivu wa maendeleo,"alisema Salha, ambaye tangu alipojiunga na Dar Modern Taarab, hajawahi kutoa mguu wake nje.
"Mimi nashangaa sana, sijui kwa nini sisi wanawake hatuna tabia ya kuombeana mema. Tunapenda kufurahia pale mwenzetu mmoja anapofikwa na balaa,"alisema.
"Tunapaswa kupendana, tusaidiane na kuombeana mema. Huwezi kujua Mungu amekuandikia nini,"alisisitiza.

 

No comments:

Post a Comment