KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Thursday, November 15, 2012

KALALE PEMA MARIAM KHAMISMWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Mariam Khamis 'Paka Mapepe' amefariki dunia na kuzikwa jana katika makaburi ya Magomeni Makuti wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mariam, ambaye ni mwimbaji wa kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT), alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi kutokana na matatizo ya uzazi.
Mwimbaji huyo mwenye sauti tamu na yenye mvuto, alipelekwa kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kujifungua baada ya kupatwa na uchungu.
Habari kutoka ndani ya hospitali hiyo zimeeleza kuwa, Mariam alilazimika kufanyiwa operesheni ili aweze kujifungua, lakini akafariki dunia. Mtoto wa mwimbaji huyo yuko salama.
Awali, familia ya marehemu Mariam ilipanga mazishi hayo yafanyike juzi, lakini iliamua kuyasogeza mbele hadi jana kutokana na maombi ya uongozi wa TOT.
Mkurugenzi wa TOT, Kepteni John Komba aliomba mazishi hayo yasogezwe mbele ili wasanii wenzake waweze kuhudhuria.
Wakati wa msiba huo, wasanii wa TOT walikuwepo mjini Dodoma kwa ajili ya kuwatumbuiza wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM uliomalizika kwenye ukumbi wa Kizota.
Marehemu Mariam alianza kujipatia umaarufu mkubwa baada ya kuimba kibao cha Paka Mapepe alipokuwa katika kikundi cha East African Melody kabla ya kuhamia Zanzibar Stars na baadaye Five Stars Modern Taarab.
Akiwa Five Stars, Mariam aliendelea kung'ara kutokana na vibao vyake viwili vya
Uzushi wenu haunitii doa na Ndio basi tena.
Alijiunga na TOT mwaka jana na kuibuka na kibao cha Sidhuriki na lawama, ambacho kilikuwa ni majibu kwa wasanii wenzake waliokuwa wakimlaumu kwa uamuzi wake wa kujiunga na kundi hilo.
  WASEMAVYO WASANII
Baadhi ya wasanii nyota wa muziki huo wameeleza kusikitishwa kwao kutokana na kifo hicho, ambacho wamekielezea kuwa ni pigo kubwa katika fani ya muziki wa taarab.
Mkurugenzi wa Jahazi, Mzee Yusuph alisema juzi kuwa, ameumizwa vibaya kutokana na msiba huo kwa vile Mariam alikuwa ni zaidi ya msanii kwake na kwamba alikuwa karibu mno na familia yake.
"Nashindwa kupata maneno ya kuzungumza kwa sababu kifo cha Mariam kimeniuma mno kutokana na ukaribu aliokuwa nao na familia yangu. Alikuwa zaidi ya msanii kwangu,"alisema Mzee.
"Mara nyingi nilikuwa nikimkuta nyumbani akiwa na wake zangu, akishirikiana nao kwa mambo mbalimbali. Alikuwa akishirikiana nao kwa raha na shida,"aliongeza.
Kwa mujibu wa Mzee, aliwahi kumtungia Mariam kibao cha Huliwezi bifu, ambacho kilichangia kumfanya aonekane kuwa tishio kutokana na wororo na utamu wa sauti yake.
Mpiga kinanda maarufu, Issa Kamongo alisema kifo cha mwimbaji huyo ni pigo kubwa kwa sababu alikuwa na sauti tamu, inayoweza kumsahaulisha binadamu yoyote matatizo aliyonayo.
  MANENO YA MWISHO
Alipohojiwa na Burudani kwa mara ya mwisho mwaka jana baada ya kujiunga na TOT, Mariam alisema hajutii uamuzi wake huo na kwamba hajioni kama amepotea njia kufanya hivyo.
Mariam alisema uamuzi wake huo umelenga kutafuta maslahi bora zaidi na pia kujiandaa kwa maisha yake ya baadaye.
Alisema hakuondoka Five Stars kwa kufukuzwa bali alifanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe kwa vile maisha ni kutafuta na ahangaikaye siye sawa na mkaa bure.
“Unajua linapotokea jambo, huwa yanasemwa mengi, lakini huo ndio ukweli wenyewe,”alisema.
Mariam alisema ameamua kujiunga na TOT kwa sababu ajira yake ni ya uhakika tofauti na vikundi vingine vya mitaani.
Alisema wasanii wote wanaounda kundi la TOT hawategemei mapato ya milangoni kulipana mishahara na hata wasipofanya maonyesho, malipo yao kwa mwezi yapo pale pale.
“Nawaomba mashabiki wangu wasichukie kwa sababu maisha ni kutafuta, wakubali matokeo,”alisema.
Mwimbaji huyo mwenye sura yenye mvuto alikiri kuwa, tangu alipojiunga na TOT, yalisemwa mengi juu yake, lakini hajali na anayachukulia kama changamoto katika maisha yake.
“Wengine wanasema nimekwenda TOT kujimaliza kiusanii, wengine wanasema nitakufa, lakini mimi sijali. Tangu nilipozaliwa, nilishatia saini mbele ya Mungu kwamba nitakufa siku fulani,”alisema.
Alisisitiza kuwa, ili msanii aweze kukomaa kiusanii, anapaswa kutembea katika vikundi mbalimbali kama ilivyo kwa waimbaji nyota wa muziki huo, Khadija Omar ‘Kopa’, Sabah Salum na wengineo.
“Hata mimi utafika wakati nitakuwa hivyo na kuamua kutulia kama wakongwe hao,”alisisitiza.

No comments:

Post a Comment