Wednesday, November 21, 2012
BI KIDUDE KUENDELEA KUTUNZWA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KAMPUNI ya Sauti za Busara Zanzibar imesema, haitaachana na mwimbaji mkongwe wa muziki wa taarabu nchini, Fatuma Binti Baraka, maarufu zaidi kwa jina la Bi Kidude.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Yusuf Mahmoud alisema juzi mjini hapa kuwa, wataendelea kumuenzi msanii huyo mkongwe kwa vile bado wanathamini mchango wake katika kuendeleza muziki huo.
"Tunapenda kuwahakikishia watanzania wote kwamba, kampuni yetu itaendelea kumsaidia Bi Kidude katika maisha yake yote,"alisema Mahmoud.
Mkurugenzi huyo alisema pia kuwa, kampuni yake ipo tayari kukabidhi fedha za Bi Kidude kwake mwenyewe ama kwa mtu yeyote, ambaye atampendekeza.
Alisema cha msingi ni makabidhiano hayo kufanyika kisheria, yakiwahusisha mashahidi wakiwemo wanasheria, mwakilishi kutoka serikalini na waandishi wa habari ili kuepuka utata.
Kampuni hiyo imeelezea msimamo wake huo siku chache baada ya kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za msanii huyo, ambazo zilikuwa zikihifadhiwa na Sauti za Busara.
Kutolewa kwa taarifa hiyo kulitokana na taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba, kampuni hiyo ilidhulumu fedha za msanii huyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment