Friday, November 23, 2012
RAHMA, NYOTA MPYA YA TAARAB INAYONG'ARA JAHAZI
NA MOHAMMED ISSA
RAHMA Machupa ni muimbaji chipukizi wa taarab anayeibukia kwa kasi katika tasnia ya muziki huo hapa nchini.
Muimbaji huyo, anayetokea kwenye familia ya wanamuziki, katika siku za hivi karibuni ameonyesha uwezo mkubwa katika kundi lake la Jahazi Morden Taarab 'Wana wa nakshinakshi'.
Akizungumza na liwazozito mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Rahma anasema kipaji chake cha uimbaji kilianza kuibuka akiwa katika shule ya sekondari ya Sinza.
Anasema akiwa katika shule hiyo alikuwa akishiriki kuimba nyimbo mbalimbali kwa kushirikiana na wanafunzi wenzake hususan wakati wa sherehe.
Rahma, anasema mwaka 2010 baada ya kuhitimu kidato cha nne katika shule hiyo alijiunga na kundi la Mashauzi Classic chini ya Isha Mashauzi 'Jike la Simba'.
Anasema baada ya kujinga na kundi hilo na kuonyesha uwezo mkubwa, alitunga wimbo unaofahamika kama 'Sijamuona kati yenu wa kunirusha roho'
Rahma anasema wimbo huo, ulikonga vilivyo nyoyo za wapenzi wa burudani na kuanzia hapo jina lake lilianza kusikika kila kona ya mtaa.
Anasema pamoja na kuachia kibao hicho, hakufanikiwa kukaa sana kwenye kundi hilo kutokana na sababu mbalimbali na ndipo alipojiunga na Jahazi.
Muimbaji huyo mwenye umbo la wastani na sauti maridhawa, anasema baada ya kujiunga na Jahazi chini ya 'Mfalme' Mzee Yussuf aliendelea kuonyesha uwezo wake wa uimbaji.
"Kwa kweli baada ya kujiunga na Jahazi kipaji changu kimezidi kukua na kadri siku zinavyokwenda nazidi kujipatia umaarufu kwa mashabiki wangu.
"Juhudi na uwezo mkubwa nilizozionyesha katikan kundi la Jahazi ndio zimemshawishi Yussuf kunipa wimbo katika albamu yetu mpya itakayozinduliwa hivi karibuni," anasema.
Anasema kutokana na uwezo na umahiri alionyesha akiwa na kundi hilo, amekabidhiwa wimbo unaofahamika kama nipe stara.
Rahma anasema wimbo huo, ni miongoni mwa nyimbo zitakazokuwemo kwenye albamu mpya ya Jahazi itakayozinduliwa mwezi ujao.
Anasema kwa mara ya kwanza wimbo huo, atautambulisha kwa mashabiki wake kesho katika ukumbi wa Buliaga Temeke, Dar es Salaam.
"Nimejipanga vya kutosha katika utambulisho ya wimbo wangu huo, nawaahidi wapenzi na mashabiki wangu sitowaangusha," alijigamba muimbaji huyo.
Anasema akiwa katika kundi hilo atatumia uwezo wake wote kufikia lengo lake la kuwa muimbaji bora na mwenye uwezo mkubwa kama walivyo waimbaji wengine.
Rahma, anasema binafsi anavutiwa sana na muimbaji mkongwe wa taarab Rukia Ramadhani kutokana na uimbaji wake na tungo zake maridhawa.
Anasema mbali na muimbaji huyo, anavutiwa na Hadija Yussuf na Leila Rashid na kwamba anatamani siku moja awe na uwezo kama walionao waimbaji hao.
Akimzungumzia Mzee Yussuf, Rahma anasema ni muimbaji mahiri asiyependa makuu na hana upendeleo ndani ya kundi lake.
Anasema Yussuf, amekuwa na mchango mkubwa kwa waimbaji wake na kwamba anawafundisha mambo mengi hususan ya muziki.
Rahma, anasema matarajio yake ni kumiliki kundi lake la muziki na kuwa muimbaji bora ndani na nje ya nchi.
Pamoja na kuwa muimbaji bora, anaelekeza nguvu zake kwenye elimu na kwamba anafikiria kurudi darasani kuendelea na masomo mpaka afike chuo kikuu.
Muimbaji huyo, anasema amezaliwa miaka 22 iliyopita jijini Dar es Salaam na ni mtoto wa mwisho kati ya wanane katika familia yao.
Wednesday, November 21, 2012
SALHA ABDALLA: SIMUHOFII MWIMBAJI YEYOTE WA TAARAB
MWIMBAJI chipukizi wa muziki wa taarab nchini, Salha Abdalla amesema hana mpango wa kukihama kikundi chake cha Dar Modern Taarab kwa vile ameridhika kwa anachokipata.
Salha amesema tabia ya wasanii kuhamahama kutoka kundi moja hadi jingine, haiwezi kuwaletea maendeleo zaidi ya kuwashusha kiusanii.
Mwanadada huyo amesema binafsi anakipenda na kukiheshimu kikundi cha Dar Modern Taarab kwa sababu ndicho kilichomlea na kumkuza katika fani ya muziki wa taarab.
Salha alisema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha Star TV mjini Mwanza.
Mwimbaji huyo mwenye sauti maridhawa na sura yenye mvuto alisema wakati alipojiunga na Dar Modern Taarab, hakuwa akifahamu kuimba, kutunga na kuimudu steji, lakini kwa sasa anaweza kuvimudu vyema vitu hivyo.
"Hivi sasa simuhofii mwimbaji yoyote wa kike kwa sababu nina uwezo wa kuimba, kutunga nyimbo na hata kuimiliki steji,"alisema mwimbaji huyo mwenye macho ya mwito.
Salha alisema hajawahi kuhama katika kikundi hicho kwa sababu ameshawaona wasanii wengi wakihama kutoka kikundi kimoja hadi kingine, lakini hawana mabadiliko yoyote makubwa kimaisha.
Amewataka wasanii wa muziki huo wajifunze kuridhika kwa kidogo wanachokipata kwa sababu maisha ni safari ndefu inayohitaji uvumilivu na subira.
"Mimi hapa Dar Modern Taarab nimefika, sina tamaa kwa sababu zinaweza kunifikisha pabaya. Ukiwa na tamaa, kuna siku unaweza usijue wapi unakoelekea,"alisisitiza mwimbaji huyo asiye na makeke.
Kwa sasa, Salha anatamba kwa kibao chake kinachojulikana kwa jina la Nauvua ushoga huku akiwa anajiandaa kuipua vibao vingine viwili vipya, vinavyojulikana kwa jina la Hasidi hana sababu na Kuomba Mungu sichoki.
Alisema kibao cha Hasidi hana sababu kinazungumzia watu wenye tabia ya kuzungumza mambo ya wenzao bila kuwa na uhakika nayo huku wakitambua wazi kwamba si ya kweli.
Alisema kibao cha Kuomba Mungu sichoki kinazungumzia dhamira aliyonayo ya kuendelea kumtegemea Mola katika kutafuta riziki huku akimuomba amwepushe na marafiki wanafiki.
Katika moja ya beti za wimbo huo, Salha anasikika akisema: "Unaweza kula, kunywa naye na kucheka naye, kumbe mbaya wako ndiye huyo huyo."
Salha ametoa mwito kwa wasanii wa kike nchini, kuzinduka na kuacha kuzubaa. Pia amewataka waache tabia ya kuwachuna wanaume kwa sababu maradhi yamekuwa mengi na kufanya hivyo ni kujikomoa wenyewe.
"Tuache kufuatilia fulani anafanya nini, tuwe na wivu wa maendeleo,"alisema Salha, ambaye tangu alipojiunga na Dar Modern Taarab, hajawahi kutoa mguu wake nje.
"Mimi nashangaa sana, sijui kwa nini sisi wanawake hatuna tabia ya kuombeana mema. Tunapenda kufurahia pale mwenzetu mmoja anapofikwa na balaa,"alisema.
"Tunapaswa kupendana, tusaidiane na kuombeana mema. Huwezi kujua Mungu amekuandikia nini,"alisisitiza.
BI KIDUDE KUENDELEA KUTUNZWA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KAMPUNI ya Sauti za Busara Zanzibar imesema, haitaachana na mwimbaji mkongwe wa muziki wa taarabu nchini, Fatuma Binti Baraka, maarufu zaidi kwa jina la Bi Kidude.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Yusuf Mahmoud alisema juzi mjini hapa kuwa, wataendelea kumuenzi msanii huyo mkongwe kwa vile bado wanathamini mchango wake katika kuendeleza muziki huo.
"Tunapenda kuwahakikishia watanzania wote kwamba, kampuni yetu itaendelea kumsaidia Bi Kidude katika maisha yake yote,"alisema Mahmoud.
Mkurugenzi huyo alisema pia kuwa, kampuni yake ipo tayari kukabidhi fedha za Bi Kidude kwake mwenyewe ama kwa mtu yeyote, ambaye atampendekeza.
Alisema cha msingi ni makabidhiano hayo kufanyika kisheria, yakiwahusisha mashahidi wakiwemo wanasheria, mwakilishi kutoka serikalini na waandishi wa habari ili kuepuka utata.
Kampuni hiyo imeelezea msimamo wake huo siku chache baada ya kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za msanii huyo, ambazo zilikuwa zikihifadhiwa na Sauti za Busara.
Kutolewa kwa taarifa hiyo kulitokana na taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba, kampuni hiyo ilidhulumu fedha za msanii huyo.
Thursday, November 15, 2012
KALALE PEMA MARIAM KHAMIS
MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Mariam Khamis 'Paka Mapepe' amefariki dunia na kuzikwa jana katika makaburi ya Magomeni Makuti wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mariam, ambaye ni mwimbaji wa kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT), alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi kutokana na matatizo ya uzazi.
Mwimbaji huyo mwenye sauti tamu na yenye mvuto, alipelekwa kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kujifungua baada ya kupatwa na uchungu.
Habari kutoka ndani ya hospitali hiyo zimeeleza kuwa, Mariam alilazimika kufanyiwa operesheni ili aweze kujifungua, lakini akafariki dunia. Mtoto wa mwimbaji huyo yuko salama.
Awali, familia ya marehemu Mariam ilipanga mazishi hayo yafanyike juzi, lakini iliamua kuyasogeza mbele hadi jana kutokana na maombi ya uongozi wa TOT.
Mkurugenzi wa TOT, Kepteni John Komba aliomba mazishi hayo yasogezwe mbele ili wasanii wenzake waweze kuhudhuria.
Wakati wa msiba huo, wasanii wa TOT walikuwepo mjini Dodoma kwa ajili ya kuwatumbuiza wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM uliomalizika kwenye ukumbi wa Kizota.
Marehemu Mariam alianza kujipatia umaarufu mkubwa baada ya kuimba kibao cha Paka Mapepe alipokuwa katika kikundi cha East African Melody kabla ya kuhamia Zanzibar Stars na baadaye Five Stars Modern Taarab.
Akiwa Five Stars, Mariam aliendelea kung'ara kutokana na vibao vyake viwili vya
Uzushi wenu haunitii doa na Ndio basi tena.
Alijiunga na TOT mwaka jana na kuibuka na kibao cha Sidhuriki na lawama, ambacho kilikuwa ni majibu kwa wasanii wenzake waliokuwa wakimlaumu kwa uamuzi wake wa kujiunga na kundi hilo.
WASEMAVYO WASANII
Baadhi ya wasanii nyota wa muziki huo wameeleza kusikitishwa kwao kutokana na kifo hicho, ambacho wamekielezea kuwa ni pigo kubwa katika fani ya muziki wa taarab.
Mkurugenzi wa Jahazi, Mzee Yusuph alisema juzi kuwa, ameumizwa vibaya kutokana na msiba huo kwa vile Mariam alikuwa ni zaidi ya msanii kwake na kwamba alikuwa karibu mno na familia yake.
"Nashindwa kupata maneno ya kuzungumza kwa sababu kifo cha Mariam kimeniuma mno kutokana na ukaribu aliokuwa nao na familia yangu. Alikuwa zaidi ya msanii kwangu,"alisema Mzee.
"Mara nyingi nilikuwa nikimkuta nyumbani akiwa na wake zangu, akishirikiana nao kwa mambo mbalimbali. Alikuwa akishirikiana nao kwa raha na shida,"aliongeza.
Kwa mujibu wa Mzee, aliwahi kumtungia Mariam kibao cha Huliwezi bifu, ambacho kilichangia kumfanya aonekane kuwa tishio kutokana na wororo na utamu wa sauti yake.
Mpiga kinanda maarufu, Issa Kamongo alisema kifo cha mwimbaji huyo ni pigo kubwa kwa sababu alikuwa na sauti tamu, inayoweza kumsahaulisha binadamu yoyote matatizo aliyonayo.
MANENO YA MWISHO
Alipohojiwa na Burudani kwa mara ya mwisho mwaka jana baada ya kujiunga na TOT, Mariam alisema hajutii uamuzi wake huo na kwamba hajioni kama amepotea njia kufanya hivyo.
Mariam alisema uamuzi wake huo umelenga kutafuta maslahi bora zaidi na pia kujiandaa kwa maisha yake ya baadaye.
Alisema hakuondoka Five Stars kwa kufukuzwa bali alifanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe kwa vile maisha ni kutafuta na ahangaikaye siye sawa na mkaa bure.
“Unajua linapotokea jambo, huwa yanasemwa mengi, lakini huo ndio ukweli wenyewe,”alisema.
Mariam alisema ameamua kujiunga na TOT kwa sababu ajira yake ni ya uhakika tofauti na vikundi vingine vya mitaani.
Alisema wasanii wote wanaounda kundi la TOT hawategemei mapato ya milangoni kulipana mishahara na hata wasipofanya maonyesho, malipo yao kwa mwezi yapo pale pale.
“Nawaomba mashabiki wangu wasichukie kwa sababu maisha ni kutafuta, wakubali matokeo,”alisema.
Mwimbaji huyo mwenye sura yenye mvuto alikiri kuwa, tangu alipojiunga na TOT, yalisemwa mengi juu yake, lakini hajali na anayachukulia kama changamoto katika maisha yake.
“Wengine wanasema nimekwenda TOT kujimaliza kiusanii, wengine wanasema nitakufa, lakini mimi sijali. Tangu nilipozaliwa, nilishatia saini mbele ya Mungu kwamba nitakufa siku fulani,”alisema.
Alisisitiza kuwa, ili msanii aweze kukomaa kiusanii, anapaswa kutembea katika vikundi mbalimbali kama ilivyo kwa waimbaji nyota wa muziki huo, Khadija Omar ‘Kopa’, Sabah Salum na wengineo.
“Hata mimi utafika wakati nitakuwa hivyo na kuamua kutulia kama wakongwe hao,”alisisitiza.
Tuesday, November 13, 2012
Mariam Khamis wa TOT afariki dunia
Mwimbaji nyota wa taarab nchini, Mariam Khamis amefariki dunia.
Habari kutoka kwa ndugu wa marehemu zimesema kuwa, Mariam alifariki dunia leo asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa habari hizo, Mariam amefariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi.
Habari kamili kuhusu kifo cha mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la Five Stars Modern Taarab zitafuata baadaye.
00000
Haya ni mahojiano ya mwisho kati ya Mariam gazeti la Burudani yaliyochapishwa kwenye gazeti la Burudani, mtandao wa liwazozito. blogspot.com na ramozaone.blogspot.com mwaka jana.
MWIMBAJI nyota wa taarab nchini, Mariam Khamis amesema hajapotea njia kutokana na uamuzi wake wa kujiengua kutoka katika kundi la Five Stars Modern Taarab na kujiunga na kundi la Tanzania One Theatre (TOT).
Mariam alisema mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, uamuzi wake huo umelenga kutafuta maslahi bora zaidi na pia kujiandaa kwa maisha yake ya baadaye.
Alisema hakuondoka Five Stars kwa kufukuzwa bali alifanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe kwa vile maisha ni kutafuta na ahangaikaye siye sawa na mkaa bure.
“Unajua linapotokea jambo, huwa yanasemwa mengi, lakini huo ndio ukweli wenyewe,”alisema.
Mariam, ambaye aliwahi kutamba kwa kibao chake cha ‘Paka mapepe’ alisema, ameamua kujiunga na TOT kwa sababu ajira yake ni ya uhakika tofauti na vikundi vingine.
Alisema wasanii wote wanaounda kundi la TOT hawategemei mapato ya milangoni kulipana mishahara na hata wasipofanya maonyesho, malipo yao kwa mwezi yapo palepale.
Tayari mwimbaji huyo mwenye sauti maridhawa, ameshatungiwa wimbo unaojulikana kwa jina la ‘Sidhuriki kwa lawama’, na unatarajiwa kuanza kusikika hewani hivi karibuni.
“Nawaomba mashabiki wangu wasichukie kwa sababu maisha ni kutafuta, wakubali matokeo,”alisema.
Mwimbaji huyo mwenye sura yenye mvuto alikiri kuwa, tangu alipojiunga na TOT, yamesemwa mengi juu yake, lakini hajali na anayachukulia kama changamoto katika maisha yake.
“Wengine wanasema nimekwenda TOT kujimaliza kiusanii, wengine wanasema nitakufa, lakini mimi sijali. Tangu nilipozaliwa, nilishatia saini mbele ya Mungu kwamba nitakufa siku fulani,”alisema.
Alisisitiza kuwa, ili msanii aweze kukomaa kiusanii, anapaswa kutembea katika vikundi mbalimbali kama ilivyo kwa waimbaji nyota wa muziki huo, Khadija Omar ‘Kopa’, Sabah Salum na wengineo.
“Hata mimi utafika wakati nitakuwa hivyo na kuamua kutulia kama wakongwe hao,”alisisitiza.
Mbali na kuimbia kundi la Five Stars, Mariam pia aliwahi kung’ara alipokuwa katika vikundi vya East African Melody na Zanzibar Stars.Baadhi ya vibao alivyotamba navyo katika vikundi hivyo ni pamoja na ‘Huliwezi bifu’, ‘Raha ya mapenzi’ na ‘Ndo basi tena’.
Subscribe to:
Posts (Atom)