KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Monday, October 22, 2012

FUNGAKAZI MODERN TAARAB: WATANGAZAJI WANAZIBANIA NYIMBO ZETU
KIONGOZI wa kikundi kipya cha muziki wa taarab cha Fungazi, Karia Temba
amesema, kikundi chake kinatisha ndio sababu wapinzani wao wanafanya kampeni ili nyimbo zao zisipigwe kwenye vituo vya redio na televisheni nchini.
Karia, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Kepteni Temba, alisema mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, wamesambaza nyimbo zao kwenye vituo mbali mbali vya televisheni, lakini vingine havizipigi.
Temba, ambaye ni mchaga wa kwanza kuimba taarabu alisema, licha ya kufanyiwa hila hizo, hawawezi kukata tamaa kwa sababu lengo lao kubwa ni kufanya maajabu katika muziki huo.
Alisema kamwe hawawezi kutoa pesa ili nyimbo zao zipigwe redioni na kwenye vituo vya televisheni kwa sababu siku zote kizuri kinajiuza na kibaya kinajitembeza.
"Tumejipanga, tupo kwa ajili ya kuwapa burudani mashabiki,"alisema msanii huyo, ambaye ni ndugu wa mkali wa bongo fleva, Mheshimiwa Temba.
Alisema kabla ya kuingia kwenye gemu, waliwasoma wapinzani wao na kufahamu nini wanachokifanya, ndio sababu wamekuja kivingine na kuwashika kisawasawa.
"Watu wanafanya juhudi za kutuzuia tusitoke, lakini wasisahau kwamba tumeaga kwetu na hatufanyi muziki kwa kubahatisha,"alisema msanii huyo mwenye sauti maridhawa.
Temba alisema kundi la Fungakazi Modern Taarab linaundwa na wasanii chipukizi kutoka katika makundi mbali mbali ya muziki huo. Aliyataja makundi hayo kuwa ni Machupa Family lililotokea Mashauzi Classical na Kings Modern Taarab.
Kwa mujibu wa Temba, baadhi ya nyimbo zao mpya zinazotesa hivi sasa kwenye maonyesho yao ni Nimeiteka himaya, Usipende, Fungakazi, Maradhi ya moyo, Sweet language, Hakuna kaburi la mjinga na Usisemwe wewe nani.
Alisema wanatarajia kuizindua albamu yao hiyo mpya katika maonyesho
yatakayofanyika kwenye kumbi mbali mbali za burudani za mjini Dar es Salaam.
Fungakazi Modern Taarab wamekuwa wakirekodi nyimbo zao kwa kuwashirikisha baadhi ya wasanii nyota wa muziki wa kizazi kipya kama vile Z Anto na mwanamama mkongwe wa taarab, Khadija Omar Kopa.

No comments:

Post a Comment