KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Tuesday, October 23, 2012

TAARAB YA ASILI NI URITHI USIOSTAHILI KUPOTEANa Sammy Makilla
KWENYE miaka ya hivi karibuni kumekuwa na jitihada zenye mwelekeo potofu katika vyombo vya habari mbalimbali kupotosha maana na dhana halisi ya taarabu na kile ambacho taarabu inastahili kuwa na kuitwa.
Baada ya Watanzania kugeukawavivu wa kila kitu ikiwemo kupiga ala za muziki na kutaka mteremko katika kila jambo wale waliozuka na mitindo inayotumia mashairi, au tungo zenye vina na mizani, au isivyo hivyo wakaona urahisi ni kuita miziki yao 'modern taarab'. Miziki hiyo ninakaata sio taarabu bali inastahili kuitwa mipasho, kiduku,  rusha na roho, au mnanda na vitu kama hivyo, lakini kamwe sio taarabu.
Muziki wa taarabu una asili na fasili yake katika  watu wa Pwani na visiwani na maeneo ya mwambao wa Afrika Mashariki.Umeathirika kwa kiasi kikubwa na muziki wa Mashariki ya Kati, India na kaswida za Kiislamu.
Sifa moja kubwa ya muziki wa taarabu tofauti na wengi wanavyofikiri sio maneno na mpangilio wake, bali ala za muziki huo na mipangilio yake na ule ufundi wa kila mwanataarabu kuwa bingwa au stadi katika kupiga chombo fulani. Taarabu isipokuwa na ala hizi sio taarabu ni igizo tu  kwa kiasi fulani la kitu kama taarabu. Taarabu kwa kawaida ni kitulizo cha fikra ndani ya nyumba na katika hadhara isiyoshawishiwa na usasa na umagharibi kiasi cha kupuuza maadili na mila za wahusika.
Ala za taarabu ni nyingi na swahiba wangu Ali Salehe ambaye sio tu shabiki wa taarabu bali ni mtunzi pia wa nyimbo za taarab anaweza baadaye kunipokea hapa na kuelezea zaidi kwanini tunastahili kuwekeza kwenye taarab asilia, kama eneo la utamaduni linalostahili kuhifadhiwa na kuenziwa.
Taarabu kama walivyoiendelza kina  Siti binti Sadi, Bi Kidude, Juma Bhalo na kina Sheikh Ilyas, Machapurala bila kuwasahau mamia ya wanawake na wanaume wa Kizanzibar na Kimrima waliochangia maendeleo ya  tasnia hii adimu, lakini iliyo na  sifa ya kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa mwambao ya Pwani ya Afrika Mashariki na usiostahili kuachiwa kupotea.
Taarabu ni muziki wa enzi na enzi.  Ni sehemu ya utamaduni endelevu na hususan katika mikoa ya  pwani ya Afrika Mashariki. Taarabu ni ustaarabu, utaratibu, upole na uungwana.  Taarabu ni kitulizo cha mawazo na gundi ya kuunganisha familia kama sio ukoo mzima.  Sifa ambayo si mipasho, sio rusha roho sio mnanda unayo.
Taarabu kiasili sio muziki wa kucheza bali wa kutazama, kusikiliza, kutafakari na kutunza. Huu ni muziki uliokuwa ukisikilizwa na watu wenye fikira, busara na hekima kuwapa muda wa kuwaza na kuwazua juu ya hili au lile. Muziki wa kupayuka, kujiona, msshauzi, kusemana, kutukanana, kuumbuana na wenye nyimbo ambazo hazina staha, usiri wala taadibu ya kuimbwa katika mafumbo hauwezi kuitwa taarab.
Ni muziki ambao kwa kawaida una ala takriban ya ishirini. Na kwa wapenzi halisi wa taarabu hufuatilia upigaji wa kila ala na ufundi au ugwiji wa yule anayetumia ala husika. Aidha, mashairi ya taarab hayaangalii tu mlingano wa vina na mizani bali maudhui na mantiki ya kile kilichomo tena kikiwe kwenye mafumbo kuweza kusomeka vyema na wanaosikiliza wimbo husika.
Ni muziki ambao hutungwa kwa mafumbo na kwa namna ambayo hauzui familia nzima, yaani, babu, bibi, baba, mama, kaka na dada wote kujumuika kwa pamoja bila kutokea chochote ambacho kinaweza kuwafanya washindwe kuzungumza au kutazamana. Taarab kiasili uliunga pamoja familia za wakazi wa mji husika. Tofauti na hiyo inayoitwa 'modern taarab' ambayo kwa kiasi kikubwa inazivunja familia katika kila mji na kijiji.
Siti bint Saad  (1928) ndiye nyota wa kwanza wa taarab ambaye kwa mara ya kwanza badala ya kuimba kwa Kiarabu aliimba kwa Kiswahili. Alifyatua mamia ya santuri za nyimbo India na wapenda muziki wa enzi hizo hakuna aliyekosa wimbo wake nyumbani.
Muziki wa taarab asili hauna tofauti na 'Classical Music' wa Ulaya au 'Country Music' wa Marekani. Miziki hiyo ilikuwepo, imekuwepo na itakuwepo bila kubadilika wala kuitwa kwa jina jingine wala kupigwa kwa namna nyingine tofauti na ilivyokuwa, ilivyo sasa na itakavyokuwa kesho. Ni sehemu ya kudumu ya utamduni wa watu na sio kitu cha kupita na kusahaulika.
Aina hizo za miziki pamoja na kuzuka kwa miziki ya kila aina Ulaya na Marekani bado inatambulika kwa nembo na jina lake. Country ni country na classical ni classical. Hapajakuwapo muziki mwingine uliopewa umodern kuhusiana na miziki hii, hakuna kitu kama modern country au modern classic.
Rouget katika Music and Trance anafafanua kwamba  neno taarabu linatokana na neno la kiarabu  'tariba' likiwa na maana ya hisia za kusisimka, kudhihirisha au kutaka kufanya kitu Fulani, kama vile kuimba au kucheza taarab.
Kama jitihada zinavyofanyika kukarabati na kutunza maeneo kama vile Mji Mkongwe Zanzibar, Bagamoyo na Kilwa ili iendelee  kuwepo basi upo umuhimu pia wa wanaohusika katika serikali zetu kuhakikisha kuwa muziki wa taarab asili na wanamuziki wake wanakumbukwa na kuenziwa na kisha kizazi kipya kinajengwa ili kuendeleza muziki huu  kwa faida ya vizazi vijavyo. Kwa maana, ukweli ni kwamba taarabu asili ikipotea ndio utakuwa mwisho wa taarabu hapa Afrika Mashariki.
Kwanini tuhifadhi taarab asilia
Kwa bahati mbaya wengi tumezoea kuchukulia vitu kama ardhi, fedha, nyumba, magari kuwa ndio rasilimali tu. Lakini muziki wa kiasili nao ni rasilimali muhimu kimaendeleo na kisaikolojia. Bila urithi wa namna hii tutakuwa ni taifa lipolipo tu ambalo si jambo zuri.
Pamoja na mambo mengine kuifufua, kuitunza na kuiendelza taarab asili ni jambo lenye faida kadhaa ikiwemo kuendeleza mila na utamaduni wetu, kuzileta familia pamoja mara kwa mara, kujenga maadili bora katika jamii, kuwa na muziki usioendana kinyume na maadili ya dini, kukuza na kuendeleza ushairi na Kiswahili, kuwa kivutio kwa wageni wa leo na kesho na kuzienzi  na kuendeleza ala asili za muziki na upigaji wake.
Ninatoa wito maalumu pia kwa vyombo vya habari kuacha kuuchanganya umma juu ya muziki wa taarabu. Tafadhali Bi Hindu, Dida, Mzee Chapuo, Bi Chau, Miriam wa Migomba, Kristina wa Mbezi kwa kuturahisisishia hili na kubaini kwamba Afrika Mashariki kuna taarabu moja tu, nayo ni taarabu asilia ambayo kwa kawaida hupigwa na vyombo vingi, hutumia mafumbo na usiri katika nyimbo zake na hauchezwi achilia mbali kunenguliwa na kutingishiwa mawowowo.
Miziki inayojiita modern taarau iitwe kwa majina yao yanayostahili kama ni kiduku basi kiduku, au rusha roho basi rusha roho fulani, kama ni mipasho basi ni ‘Mipasho’ na kama ni mnanda uitwe ‘Mnanda’ na miziki hii isiruhusiwe kutumia mgongo wa taarabu kujijenga isipostahili.
Nikiri kuwa nilitaka sana nitembelee Lamu, Malindi, Mombasa, Tanga na Zanzibar kuzungumza na wakereketwa wenzangu wa taarabu asili kabla ya kuandika makala haya, lakini haikuwezekana. Ninaamini, hata hivyo kupitia makala haya ujumbe unaweza kufika kwa kiasi fulani.
Ninawashauri wanaharakati wa kulinda na kuendeleza utamaduni wetu kuangalia uwezekano wa haya yafuatayo: Kusaidia juhudi binafsi zilizopo za kufufua na kuendeleza vikundi vya taarabu kupitia vilabu na vyuo vya  upigaji ala za asili za taarab (mathalani juhudi za Bi Hamndani, Zanzibar), Kushirikiana na Unescokuhifadhi taarabu asili kwa kutumia Teknohama; Kuwatafuta wanataarab asilia waliko na kuwaunganisha ili kuufufua  na kuchochea kuwepo kwa muziki huo kiasili na kuongeza vionjo viwili vitatu vya kuvutia familia zaidi kuliko mtu mmoja mmoja.
Aidha, kusaidia vikundi vilivyopo, lakini havina ala za kutosha za muziki toka Misri na Uarabuni, kuenzi Ushairi katika vyombo vya habari kukuza vipaji vya washairi chipukizi na  kuchukulia Taarabu asili kama urithi usiostahili kupotea kwa msaada wa Unesco na wapenda utamaduni wetu wengineo.
Pepe: sammy.i.makilla@gmail.com

No comments:

Post a Comment