Tuesday, February 3, 2015
THANIA MSOMALI AJA NA 'HIVI NDIVYO NILIVYO'
MIEZI michache baada ya kujiengua katika kundi la Mashauzi Classic, mwimbaji machachari na mwenye sauti maridhawa ya ndege mnana, Thania Msomali ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Hivi ndivyo nilivyo.
Katika kibao hicho, ambacho kimeshaanza kuteka hisia za mashabiki, Thania anasimulia jinsi alivyo na kwamba yuko tofauti na vile watu wanavyomfikiria.
Thania alianza kung'ara kimuziki alipokuwa katika kundi la Five Stars, baadaye akajiunga na kundi la T-Moto kabla ya kutua Mashauzi Classic, kundi linaloongozwa na Isha Ramadhani 'Mashauzi'.
Binti huyo jamali na mwenye sauti murua na adhimu, anakiri kuwa kipaji chake kiligunduliwa na mpiga kinanda Omary Kisira, ambaye ndiye aliyempika na kumfanya awive kisawasawa.
Thania alijiengua mwenyewe kutoka kundi la Mashauzi Classic baada ya kuona kwa sasa anaweza kusimama peke yake.
Binti huyo amesema kibao hicho ni maandalizi ya ujio wa albamu yake ya kwanza, anayotarajia kuitoa mwaka huu.
Amesema alianza maandalizi ya kutoa albamu mpya muda mrefu uliopita, lengo likiwa ni kutoa kitu kilichokamilika na chenye ladha isiyomithilika kwa utamu.
"Sikukurupuka kurekodi kibao hiki, nilijiandaa vyema ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya kutosha,"alisema.
Thania kama msanii mchanga, amekubaliana na changamoto zote atakazokumbana nazo, pia anawasihi wasanii wote kupendana na kusaidiana pale unapoona mwenzako amekwama au anakwenda sivyo, hata mawazo tu.
"Napenda kuwashukuru wale wote waliofanikisha kwa mimi kuwepo hapa nilipo:- Walimu wangu Fikirini Urembo na Kibibi Yahaya, vilevile nitakuwa mwizi wa fadhila kukosa kutoa shukrani zangu kwa walimu wangu waliopita ambao ni Ally Jay, Shaibu wa Mwamvita pamoja na Kali Kiti Moto Mafya.
"Pongezi kubwa ziwaendee Amin Salmin, Mkurugenzi wa T-Moto pamoja na Ismail Suma Ragger, Meneja wa Mashauzi Classic.
Amewaomba wapenzi wote wa taarab kumpokea na wausikilize kwa makini wimbo wake huo ili wajue kaimba nini na zaidi ya yooote, huu ni mwanzo tu, yaani mvua za rasharasha masika inakuja, ni mvua ya mawe kama si elnino.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment