Sunday, July 20, 2014
MASHAUZI CLASSIC KUZINDUA ALBAMU MPYA IDDI MOSI
KIKUNDI cha Taarab cha Mashauzi Classic, chini ya uongozi wake Isha Mashauzi, siku ya Idd Mosi kitafanya onyesho la uzinduzi wa albamu yake mpya ya 'Asiyekujua hakuthamini.'
Onyesho hilo litakaloanza saa tatu usiku, limepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Buzuruga Plaza na kiingilio kitakuwa sh. 10,000 kwa mtu mmoja.
Katika onyesho hilo, kutakuwepo wasanii machachari wenye sauti za kuvutia kama vile Isha Mashauzi (mkurugenzi), Hashim Said, Thania Msomali, Saida Ramadhani na Zubeidah Andunje.
DAR MODERN TAARAB KUZINDUA ALBAMU YAKE MPYA IDDI MOSI
Kundi zima la Dar Modern Taarab limeachia Albam yake mpya kabisa inayokwenda kwa jina la "Ubinadamu kazi."
Uzinduzi wa albam hii utafanyika siku ya Idd Mosi pale kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.
WAIMBAJI WAWILI WASIMAMISHWA KAZI MASHAUZI CLASSIC
KIKUNDI cha muziki wa taarab cha Mashauzi Classic chenye maskani yake mjini Dar es Salaam, kimewasimamisha wasanii wake wawili kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kundi hilo zimeeleza kuwa, wasanii waliosimamishwa ni Thania Msomali na Fatma Seif.
Fatma amewahi kuimba nyimbo iitwayo 'Mdomo wako utakuponza' uliomo kwenye albami ya 'Si bure una mapunngufu'.
Kwa mujibu wa habari hizo, kisa cha Fatma kusimamishwa ni kutohudhuria onyesho la kundi hilo na kudaiwa kuonekana katika kundi lingine la muziki huo la Gusagusa siku hiyo.
Alipoulizwa kuhusu adhabu hiyo, Fatma alisema: “Mimi siku hiyo sikwenda kazini kwa sababu nilikuwa naumwa. Kiongozi wangu alinipigia simu kuniambia nihudhurie kwenye onyesho nikamwambia siwezi kwa sababu naumwa."
"Akaniacha, siku ya pili yake akanipigia simu tena kuniulizia hali yangu, nikamwambia bado nipo nyumbani tu, lakini cha kushangaza akanitumia ujumbe wa kunisimamisha kazi miezi mitatu. Kesho yake akanitumia ujumbe tena kuwa nimeachishwa kabisa kazi, hivyo niko huru kutafuta bendi yoyote, kwa kweli imeniuma sana maana sijui kama ndo hili tatizo la mimi kuugua,"alisema.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi aliochukua, Fatma alisema: "Sijachukua uamuzi wowote na hivi sasa nipo tu nyumbani, bado akili yangu haijatulia, hivyo sijajua kitu cha kufanya, acha kwanza nitulie."
Kwa upande wake, akizungumzia adhabu hiyo, Thonia alisema: “Mimi nilikuwa naumwa na nilitoa taarifa kwa uongozi, nimeenda hospitali kufanyiwa uchunguzi, nikaonekana (akataja ugonjwa), hivyo nikaandikiwa dawa ambazo niliendelea kuzitumia."
"Baada ya kama wiki mbili, nikawa najisikia vizuri na nikaamua kwenda kuripoti kazini, lakini cha kushangaza kidogo nikaambiwa niendelee kupumzika kwanza mpaka nipone ndo niende. Nimekaa nyumbani tena baada ya siku kadhaa, Mashauzi walikuwa wanapiga Mango Garden, nikaomba tena nihudhurie kazini, lakini nikaambiwa nisubiri tu ila nikaomba basi niende kuangalia onyesho nikaruhusiwa ila sikuimba,"alisema.
"Sasa kinachoniweka njia panda ni kuwa, hali yangu ni nzuri, nimeimarika ki-afya na nina hamu ya kuimba ila nikiuelezea uongozi wangu kuwa nataka kuripoti kazini, wanasema nisubiri tu sasa nitasubiri hadi lini!? Kwa kweli sijajua muafaka upo wapi na hatma yangu sijajua maana naendelea kusubiri tu na wala sijaelezwa kitu,” alisema.
Kiongozi wa wasanii katika kundi la Mashauzi Classic, Hashim Said alisema: "Fatma tulimuondoa katika bendi kwa utovu wa nidhamu. Alitega kuja kazini kwa kisingizio cha kuumwa.
Yote hayo yametokana na siku hiyo ilikuwa ni Alhamisi na bendi tuliigawa mara mbili, baadhi walikwenda Mwanza kikazi na baadhi wakabaki DSM. Waliokwenda Mwanza waliambatana na Mkurugenzi, waliobaki Dsm walibaki na mimi pale Mango Garden kikazi akiwemo Fatma."
"Lakini cha kushangaza, Fatma alinitumia ujumbe muda wa saa moja usiku akidai anaumwa! Nikamuuliza huu ugonjwa umeanza saa hizi kwa kuwa ni muda wa kuja kazini? Nikamwambia lazima aje kazini sababu waimbaji waliokuwapo ni wachache,"alisema.
"Kinachoonekana ni kuwa Fatma alimaindi suala la yeye kubakishwa Dsm! La kushangaza zaidi kazini hakuja na akaonekana huko Mbagala akiwa na bendi hizi za mitaan akiimba, hapo ndipo nilipomsimamisha kazi. Kibaya zaidi alishindwa kuomba msamaha. Uongozi ukaamua kumuondoa katika bendi sababu hatuwezi kuwa na msanii asiyekuwa na uzalendo na bendi yake,"alisema.
"Thania naye tumemsimamisha kutokana na kiwango chake kila kukicha kinashuka na tumempa nafasi ya kufanya mazoezi zaidi ili akiwa vizuri basi atarudi kazini, "aliongeza.
JAHAZI YAFUNIKA UZINDUZI WA ALBAMU YA CHOZI LA MAMA
Mzee Yusuf (kulia) akiongea jambo kabla ya uzinduzi wa "Chozi la Mama". Katikati ni Aisha Abushily 'Mama wa madikodiko' kutoka Kenya.
Meneja wa Jahazi Modern Taarab, Mohammed Rashid Mauji 'Father Mauji' pamoja na shabiki wa Jahazi wakizindua albamu mpya iitwayo "Chozi la Mama" ndani ya ukumbi wa Dar Live.
KIKUNDI cha muziki wa taarab cha Jahazi hivi karibuni kilifunika katika uzinduzi wa albamu yake mpya inayokwenda kwa jina la Chozi la Mama.
Uzinduzi wa albamu hiyo ulifanyika kwenye ukumbi wa Dar Live ulioko Mbagala, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki.
Kama ilivyo kawaida, wimbo uliobeba jina la albamu hiyo uliimbwa na Mzee Yusuph, ambaye pia aling'ara katika kikao cha Wasiwasi wako.
Subscribe to:
Posts (Atom)