KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Monday, May 26, 2014

DK SHEIN AKICHANGIA KIKUNDI CHA ZANZIBAR MODERN TAARAB SH. MILIONI NANE

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la  Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein akipokea album mbili za nyimbo kutoka kwa Mkurugenzi wa kikundi cha muziki wa taarab cha  Zanzibar Modern Taarab, Abdalla Ali, alipokuwa akiwa mgeni rasmi katika sherehe za kikundi hicho kutimiza miaka saba tangu
kuanzishwa kwake. Katika sherehe hiyo, Rais alikichangia kikundi hicho shillingi za kitanzania milioni nane. Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani, Zanzibar.[Picha na Ramdhan Othman,Ikulu.]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wasanii wa kikundi cha muziki wa taarab cha Zanzibar Modern Taarab, alipokuwa mgeni rasmi katika sherehe za kikundi hicho kutimiza miaka saba tangu kuanzishwa kwake. [Picha na Ramdhan Othman,Ikulu.]

Monday, May 19, 2014

BURIANI JUMA BHALO, GWIJI WA TAARAB ASILIA



Na John Kitime

Mfalme wa Taarab nchini Kenya ambaye pia amejijengea jina katika nchi za Afrika Mashariki, Mohamed Khamis Juma Bhalo, amefariki dunia. Bhalo amefariki dunia usiku wa Jumamosi akiwa nyumbani kwake eneo la mji wa zamani Mombasa, baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Juma Bhalo  alizaliwa 1942 huko  Shela katika wilaya ya Malindi. Mwaka1954, alijiunga na shule ya msingi ya Sir Ali bin Salim , wakati huohuo familia yake ilihakikisha anahudhuria Madrassa ili kupata elimu ya dini.

Bhallo mwenyewe aliwahi kusema hamu yake ya kuimba ilimuanza katika wakati huu na sauti yake kuwa na mvuto kutoka kipindi hiki alipokuwa Madrassa Akiwa na miaka 9 tayari muda wake mwingi ulitumika kusikiliza santuri, na akili yake ilianza kupenda sana muziki.

Hakumaliza elimu ya msingi kwa kuwa wazazi wake walishindwa kulipa ada ya shule. Mwaka 1957 alihamia Mombasa na kupata kazi Forodhani, akiwa Mombasa alianza kukutana na kushirikiana na wanamuziki wa Taarab wa Mombasa.

Hakuipenda sana kazi ya Forodha hivyo 1959 akahamia Tanga kwa mjomba wake, na hapo akajiunga na kundi maarufu la Taarab wakati ule lililoitwa Young Noverty, hapa alipata ujuzi mkubwa wa muziki wa Taarab.

Alirudi kwao Malindi kwa muda mfupi na hatimae kurudi tena Tanga 1962 na kujiunga na kundi la Young Stars Taarab.

Mwaka 1966 alirudi Mombasa na kuanzisha kundi la Bhalo and Party, kundi ambalo amedumu nalo mpaka Mauti yake.

Mwaka 2007 baada ya zaidi ya miaka 50 ya kuwemo katika muziki wa Taarab, Juma Bhalo ambaye wapenzi wake walimuita Profesa na hata Mfalme wa Taarab alitangaza kuacha kufanya maonyesho ya wazi ya taarab, alitangaza hilo siku alipopiga katika harusi ya mwanae.
Alistaafu kazi hiyo kwa maneno yafuatayo: 

"Waswahili wasema kiwate kitu kabla hakijakuata. Kwa hivyo kama mulivyo nishuhudiya usiku huu nlivyowatumbuiza ambavyo ni kama kawaida yangu basi leo hii usiku huu kabla hawajaja watu wakasema ahhhhh Bhalo ashazeeka hawezi tena kuimba kwa hivyo najiuzulu ningali bado niko fiti. Kwa hivyo siimbi tena hadharani kikazi. Nawashkuru kwa ushabik wenu na musijali Mungu akiniwezesha Kasseti mpya ntawatoleya".

Taarab yake iliegemea sana muziki wa kihindi na hivyo kuwa tofauti na taarab nyingine

MUNGU AMLAZE PEMA PROFESA

Monday, May 5, 2014

KUMBUKUMBU YA MAREHEMU MOHAMED SLEYUM ZAHOR



SLEYUM MOHAMED ZAHOR (1922-2003)
HATIMAYE leo umetimiza miaka 11 tangu ulipofariki dunia mwaka 2003
baada ya kuugua kwa muda mrefu na kuzikwa katika makaburi ya Kigilagila,
Kiwalani, Dar es Salaam.
Kifo chako kimetuachia pengo na upweke mkubwa. Tunazikosa simulizi zako, maono yako, ucheshi wako, busara zako na hekima zako.
Unakumbukwa
sana na mke, Bibi Fatuma Rashid na watoto wako, Rashid, Pili, Amisa,
Shani, Asha, Saumu, Nuru na Hilali pamoja na wajukuu zako wote.
Hakika
sisi zote ni waja wa Mwenyezi Mungu na kwake lazima tutarejea.
Tunaamini maandiko ya kwamba kila chenye roho, lazima kitaonja mauti.
Mungu ailaze roho yako mahali pema, peponi. Amin