KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Thursday, August 8, 2013

FIVE STARS, MASHAUZI CLASSIC, DAR MODERN TAARAB KUTOA BURUDANI IDD EL FITR


Mwanahawa Ally-Five Stars
Isha Mashauzi-Mashauzi Classic
Mwimbaji wa Dar Modern Taarab

KUMBI mbalimbali za burudani za mjini Dar es Salaam kesho na keshokutwa zinatarajiwa kuwaka moto wakati vikundi mbalimbali vya taarab vitakapofanya maonyesho ya kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitr.

Kikundi cha taarab cha Five Stars kitasherehekea sikukuu hiyo siku ya Idd Mosi kwa kufanya onyesho katika kitongoji cha Kigogo Fresh kilichopo Pugu, Ilala, Dar es Salaam.

Kiongozi wa kundi hilo, Ally J alisema juzi kuwa, siku ya Idd Pili, kundi hilo litatoa burudani kwenye ukumbi wa Roshi Garden ulioko Mwandege, Mbagala, Dar es Salaam wakati siku ya Idd Tatu itahanikiza maraha Kibiti, Rufiji mkoani Pwani.

Ally J alisema katika maonyesho hayo, kundi hilo litatambulisha kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la Habari ya mjini.

Kundi la muziki wa taarab la Dar Modern litasherehekea siku ya Idd Mosi kwa kushusha burudani nzito kwenye kiota kipya cha maraha kinachojulikana kwa jina la Serengeti Golden Paradise Resort, Mbagala, Mbande, Dar es Salaam.

Meneja wa hoteli hiyo, Wambura  Sungura alisema juzi kuwa, kundi hilo limeahidi kuporomosha vibao vyake vipya zaidi ya vitano, vitakavyokuwemo kwenye albamu yao mpya.

Sungura amewataka wakazi wa Mbagala na vitongoji vya jirani kufika kwa wingi kwenye ukumbi huo ili kupata burudani adhimu kutoka katika kundi hilo, ambalo lilikuwa kimya kwa zaidi ya miezi miwili.

Kwa mujibu wa Sungura, kabla ya burudani hiyo, kutakuwepo na onyesho ya utangulizi la muziki wa disco kwa ajili ya watoto. Alisema onyesho hilo litaanza saa sita mchana na kuhitimishwa saa kumi na moja jioni.

Kundi la Mashauzi Classic linaloongozwa na Isha Mashauzi limeamua kukwea basi kwenda Morogoro kuwapa burudani ya kusherehekea sikukuu hiyo mashabiki wake katika kitongoji cha Mji Mpya.

Mashauzi alisema juzi kuwa, siku ya Idd Pili kundi hilo litahamishia burudani zake kwenye ukumbi wa City Pub mjini Mbeya wakati Iddi Tatu litamwaga lazi kwenye ukumbi wa Garden Park ulioko Mafinga mkoani Iringa.

Katika maonyesho hayo, Mashauzi alisema kundi hilo litatambulisha nyimbo zake nne mpya, zinazotarajiwa kuwemo kwenye albamu yao mpya, itakayokuwa na nyimbo sita.

Alizitaja nyimbo hizo, watunzi wakiwa kwenye mabano kuwa ni Asiyekujua hakuthamini (Isha na Saida), Bonge la bwana (Hashim Said), Ropokeni yanayowahusu (Saida) na Ni mapenzi tu (Zubeda Maliki).

Monday, August 5, 2013

AMIN-T MOTO BADO IPO HAI

MKURUGENZI wa kikundi cha taarab cha T Moto, Amin Salmin amesema kundi hilo bado lipo hai na limezidi kujiimarisha.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Salmin alisema wamepanga kuliimarisha kundi lao kwa kuongeza wasanii wengine sita kutoka makundi mbalimbali.

Salmin alisema wasanii hao watatoka katika vikundi vya Jahazi na Kings Modern Taarab, lakini hakuwa tayari kutaja majina yao.

Kwa mujibu wa Salmin, wasanii wanne watatoka Jahazi na wengine wawili kutoka Kings Modern Taarab.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa kundi la G5 taarab, Hamisi Slim amesema kundi lake lipo katika maandalizi ya kuipua nyimbo mpya nne.

Mbali na kupika nyimbo nne, Slim alisema kundi lake linatarajia kuendelea kujiimarisha kwa kuongeza wasanii wawili wapya. Hakuwa tayari kutaja majina yao.

Saturday, August 3, 2013

KHADIJA KOPA: BAADA YA KUFIWA NA MUME WANGU, NIMEGUNDUA NAPENDWA

MALKIA wa Mipasho Afrika Mashariki, Khadija Kopa amesema baada ya kufiwa na mumewe kipenzi, Jafari Ally, amegundua kuwa anapendwa na watu wengi tofauti na alivyokuwa akifikiria.
 Akistorisha na mwandishi wetu, Khadija alisema kuwa kipindi alipokuwa kwenye matatizo alishangazwa na ukaribu ulioonyweshwa na watu hata ambao hakuwatarajia na ameijua nafasi yake kwenye jamii.

 “Nimesaidiwa na asasi mbalimbali, vikundi pamoja na watu wengi, huku wengine wakiniambia kuwa nikitaka msaada niwapigie ingawa sijafanya hivyo, nimefarijika sana kuona napenda kiasi hiki,” alisema mwanamama huyo ambaye anatarajia kumaliza eda Oktoba 16, mwaka huu kabla ya kurejea…