Tuesday, February 19, 2013
FIVE STARS MODERN TAARAB CHASUKWA UPYA
KIKUNDI cha taarab cha Five Stars kimewanyakua nyota wapya wa muziki huo kutoka katika vikundi mbalimbali kwa lengo la kujiimarisha.
Miongoni mwa wasanii hao wapya ni pamoja na waimbaji wakongwe, Mwanahawa Ally, Sabah Salum, Maua Tego, Mosi Suleiman na mpiga kinanda Thabiti Abdul.
Mbali na kuajiri nyota hao, kundi hilo pia limeupiga chini uongozi wote wa zamani na kuweka viongozi wapya.
Kwa sasa, kundi hilo ambalo lilitamba vilivyo mwaka juzi kabla ya wasanii wake 14 kufariki dunia kwa ajali ya gari, lipo chini ya mkurugenzi, Maalim Sharrif Mambo maarufu kwa jina la Shacks.
Wasanii wa zamani wa kundi hilo waliofariki dunia kwa ajali ni Issa Kijoti, Sheba Juma, Tizzo Mgunda, Omary Hashim, Omary Haji, Hajji Mzania, Nassoro Madenge, Husna Mapande, Hamisi Omary, Maimuna Makuka, Hassan Ngeleza, Ramadhani Maheza na Ramadhani Mohamed.
Kiongozi wa kundi hilo, Ally J aliwaambia waandisi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, wameamua kulisuka upya kundi hilo ili kuhimili ushindani wa taarab uliopo sasa.
Wasanii wengine wapya waliojiunga na kundi hilo ni Jumanne Ulaya, Yussuf Tego, Mariam Mohamed, Mariam Omary na Hammer Q.
Jay alisema wasanii hao wameingia mkataba wa miaka miwili na Five Stars kila mmoja na kundi hilo linatarajiwa kuingia kambini wakati wowote kwa ajili ya kuandaa albamu mpya.
Kwa upande wake, Shacks alisema kundi lake halina uhasama na kundi lolote na kwamba ujio wao umelenga kuongeza ushindani katika muziki wa taarab na kusaka fedha kwa kutoa vitu vya uhakika.
Alisema tayari wamefanya makubaliano na Jahazi Modern Taarab ili kutochukuliana wasanii. Katika makubaliano hayo, viongozi wa makundi hayo mawili hawatapokea msanii kutoka kundi lingine.
Mbali na kuingia mkataba huo, Shacks alisema makundi hayo mawili yamekubaliana kushirikiana katika kuendeleza muziki wa taarab.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment