KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Saturday, December 12, 2015

ZUHURA SHAABAN AANGUO KILIO, ASEMA TAARAB SASA BASI


Na Rashid Zahor

MWIMBAJI nyota na machachari wa muziki wa taarab nchini, Zuhura Shaaban, amejikuta akibubujikwa na machozi na kuapa kwamba, kamwe hatawasamehe watu wanaomzushia maneno ya uongo kwamba anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Zuhura amesema japokuwa vitabu vya dini vinasisitiza umuhimu wa binadamu kusameheana pale wanapotendeana makosa, kwake katu hawezi kuwasamehe watu hao.

Huku akitokwa na machozi kwa uchungu, Zuhura amesema kamwe katika maisha yake hajawahi kujihusisha na vitendo vya aina hiyo na roho huwa ikimuuma pale anapowasikia ama kuwaona watu wakizungumzia jambo hilo kuhusu yeye.

"Watu wananisema vibaya. Wananiweka kwenye mstari ambao mimi sipo. Roho inaniuma sana kwa sababu tangu nilipozaliwa kutoka tumboni kwa mama yangu hadi leo hii nina umri wa miaka 49, sijawahi kujihusisha na vitendo hivyo,"amesema Zuhura huku akishindwa kuyazuia machozi yaliyokuwa yakimchuruzika.

Zuhura alijikuta akiwa katika hali hiyo wiki hii, alipokuwa akihojiwa na mtangazaji Mariam wa Migomba, katika kipindi cha Muziki wa Mwambao, kilichorushwa hewani na kituo
cha televisheni cha TBC 1.

"Kama kuna mtu niliyewahi kumtamkia kuhusu kufanya naye kitendo  hicho ama niliwahi kufanya naye, ajitokeze hadharani aseme," alisema Zuhura, mwimbaji mwenye sauti yenye mvuto na macho ya kuvutia.

Aliongeza kuwa kutokana na uvumi huo, kila anapokwenda kwenye shughuli za kijamii, akiwa ameongozana na mwanamke mwenzake, baadhi ya watu humnyooshea vidole ama kukonyezana na kuanza kumzungumzia vibaya.

"Siwezi kumsamehe mtu wa aina hiyo. Sitamsamehe japo dini inatufundisha kusameheana,"alisema Zuhura, mwimbaji asiyependa makeke anapokuwa jukwaani, zaidi ya kuutikisa mwili wake taratibu kwa namna ya kuvutia.

Licha ya umaarufu alionao katika muziki wa taarab kutokana na uimbaji wake mwanana na sauti ya kuvutia, Zuhura kwa sasa ameamua kujiweka kando na muziki huo.

Moja ya sababu anazozitaja ni umri kumtupa mkono, licha ya ukweli kwamba wapo baadhi ya waimbaji nyota wa kike wenye umri mkubwa kuliko wake, kama vile Mwanahawa Ally, Khadija Kopa na Rukia Juma, ambao bado wanajihusisha na muziki huo.

"Wakati umekwenda. Katika maisha, lazima hufika wakati wewe mwenyewe unaamua hiki nitafanya, hiki sifanyi.

"Wakati ule nilikuwa mdogo, nilikuwa naweza kufanya chochote ninachokitaka, lakini kwa sasa nimeshakuwa mtu mzima, nina watoto. Baadhi ya wakati huwa wananiambia mama hilo hapana,"alisema Zuhura, mwimbaji mwenye sauti inayopanda na kushuka mithili ya mawimbi baharini.

Mwanamama huyo mwenye wajihi unaovutia na sura ya mchongo wa dafu, amesema kwa sasa ameamua kujihusisha na biashara kwa ajili ya kuendesha maisha yake na familia yake, akiwa anamiliki duka la nguo.

Amesema kwenye duka hilo lililoko visiwani Zanzibar katika kisiwa cha Unguja, anauza nguo za kinamama, vipodozi na vikolombwezo vya aina mbalimbali vinavyowahusu wanawake.

"Nimeamua kuingia kwenye biashara. Nauza nguo na vitu vya kike. Naendesha maisha yangu na watoto kwa njia hiyo,"amesema Zuhura.

Akizungumzia maendeleo ya muziki wa taarab kwa sasa, Zuhura alisema umepoteza maana na mvuto kutokana na kutoka nje ya mipaka na kuwa muziki wenye kelele nyingi.

Alisema wakati ulipoanzishwa mtindo wa modern taarab, akiwa na kikundi cha East African Melody, hawakutokana moja kwa moja nje ya muziki wa taarab kama ilivyo sasa.

"Vikundi vya sasa hivi vimetoka nje kabisa ya taarab, kuanzia kwenye ushairi na mipigo ya nyimbo,"amesema mwanamama huyo.

Amewataka wasanii wakongwe wa muziki huo, ambao bado wanaendelea kujihusisha na taarab, wakae chini na kutafakari wapi walikotoka, walipo na wanakokwenda.

Alisema kama miaka ya nyuma waliweza kupiga muziki wa kiasili wa taarab na kuongeza madoido kidogo, haoni kwa nini wasiendelee kufanya hivyo kwa sasa ili wasipoteze asili ya taarab.

"Siku hizi waimbaji wa taarab hawaimbi, wanapiga kelele,"alisema.

Kwa mujibu wa Zuhura, wapo waimbaji wengi wazuri hivi sasa kuliko hata enzi zao, lakini wanakosa miongozo mizuri ya kuimba nyimbo za muziki huo kwa namna ya kuvutia.

Ameutaja wimbo ambao anaamini aliutendea haki katika kuuimba na hadi leo bado unamvutia kuwa ni 'Siadhiriki', aliourekodi wakati akiwa katika kikundi cha East African Melody.

Katika maisha yake ya usanii, Zuhura hajawahi kutunga wimbo wa taarab zaidi ya kutungiwa na watunzi mahiri wa nyimbo hizo. Anasema hiyo ni kwa sababu hana kipaji cha utunzi.

"Katika kipindi chote nilichokuwa nikiimba taarab kwenye vikundi mbalimbali, sikuwa natilia maanani na kuuweka rohoni muziki huo. Kuna watu waliogundua kwamba nina kipaji na ndio waliokuwa wakinihamasisha kuimba,"alisema.

Amesema vivyo hivyo hakuwahi kumfundisha kuimba msanii yoyote wa kike kwa kuwa hata naye hakuwahi kufundishwa kufanya hivyo.

Mbali na kikundi cha East African Melody, Zuhura amewahi kuimbia vikundi vya Zanzibar Stars na Zanzibar One. Kwa sasa anaimba muziki wa kwenye sherehe tu, hasa za harusi visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment