Monday, May 11, 2015
DAR MODERN TAARAB KUFANYA ZIARA MIKOA SITA
KIKUNDI cha taarab cha Dar Modern, kinatarajia kufana ziara katika mikoa sita nchini kwa lengo la kutambulisha ujio wake mpya katika muziki huo.
Ziara hiyo, iliyopewa jina la Modenika na Dar Modern, italifikisha kundi hilo katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Dodoma, Morogoro na Dar.
Mratibu wa ziara hiyo, Emmanuel Simon, alisema wiki hii kuwa, ziara hiyo itaanzia mkoani Mbeya, ambako kundi hilo litafanyika onyesho lake la kwanza Mei 20 mwaka huu katika mji mdogo wa Kyela.
Mei 22, mwaka huu, kundi hilo litafanya onyesho lingine katika mji mdogo wa Mpanda ulioko mkoani Katavi, wakati siku inayofuata, litahanikiza maraha katika mji wa Sumbawanga ulioko mkoani Rukwa.
Kwa mujibu wa Emmauel, baada ya maonyesho hayo, kundi hilo litarejea Dar es Salaam, ambako Mei 29, litafanya onyesho kwenye ukumbi wa Travertine ulioko Magomeni.
Mei 30, kundi hilo litakuwa kwenye ukumbi wa Royal Village ulioko mjini Dodoma na siku inayofuata, litamaliza ziara yake hiyo mjini Kilosa mkoani Morogoro kwa kufanya onyesho kwenye ukumbi wa Babylon.
Emmanuel amewataka mashabiki wa taarab kujitokeza kwa wingi kushuhudia maonyesho hayo, ikiwa ni pamoja na ujio mpya wa kundi hilo kwa vile limewaandalia mambo mazuri.
KHADIJA KOPA: NILIWAHI KUVUMISHIWA NIMEMUUA LEILA KHATIBU NA OMAR KOPA
Lakini kwa mashabiki wa taarab wa visiwa vya Zanzibar,
jina la Khadija Kopa lilikuwa maarufu. Ni kutokana na uimbaji wake mahiri na
sauti yake maridhawa, kupitia vibao vilivyompa sifa na umaarufu mkubwa, kama
vile Kadandie, Daktari na Wahoi, alivyoviimba akiwa katika kikundi cha Culture.
Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyoufanya uongozi wa TOT Plus,
kumfuata Khadija visiwani Zanzibar na kumuomba ajiunge na kikundi hicho ili
kukipa sura na mwonekano mpya, tofauti na taarab iliyozoeleka Tanzania Bara.
Kwa umbo, Khadija Omar Kopa ni mnene. Rangi yake ni
nyeusi yenye mng’ao. Uso wake hujawa na tabasamu muda wote utadhani hajui kitu
kinachoitwa kukasirika.
Licha ya kuwa na umbile hilo, Khadija ni mwepesi wa
kuunyonganyonga mwili wake atakavyo awapo stejini, akiimba nyimbo za muziki wa
taarab. Sauti yake nayo ni maridhawa na yenye mvuto wa pekee.
Sifa hizo ndizo zilizomfanya mwanamama huyo apachikwe
jina la ‘Malkia wa Mipasho’ nchini. Waliompa jina hilo hawakubahatisha,
walitambua vyema kwamba uwezo wake katika fani hiyo ni mkubwa.
Akiwa TOT Plus mwaka 1992, Khadija ambaye ni mmoja wa
waanzilishi wa kundi hilo, alidhihirisha kwamba halikukosea kumfungia safari
visiwani humo baada ya kuanza kung’ara kwa vibao kama ‘Tx mpenzi’, ‘Ngwinji’,
‘Wrong number’, ‘Mtie kamba mumeo’ na nyinginezo.
Hata hivyo, miaka miwili baadaye, Khadija alikorofishana
na uongozi wa TOT Plus baada ya yeye na mwimbaji mwenzake, Othman Soud kuamua
kuondoka kinyemela na kwenda Dubai, ambako walishiriki kuanzisha kundi la East
African Melody.
Baada ya kurejea nchini kutoka Dubai, mwanamama huyo
alilazimika kujiunga na kikundi cha Muungano Cultural Troupe kwa vile uongozi
wa TOT uligoma kumpokea.
Kujiunga kwa Khadija na Othman katika kikundi cha
Muungano, kulisababisha kuwepo kwa ushindani mkali kati ya vikundi hivyo
viwili, ambavyo vilifanya maonyesho kadhaa ya pamoja kwa ajili ya kuonyeshana
nani mkali.
Akiwa Muungano, Khadija aling’ara kwa vibao vyake murua
kama vile ‘Homa ya Jiji’, ‘Kiduhushi’ na ‘Umeishiwa’. Pia kulizuka ushindani
mkali kati yake na marehemu Nasma Khamis ‘Kidogo’, ambaye alichukuliwa na TOT
kutoka Culture kwa lengo la kuziba pengo lake.
Akizungumza mjini Dar es Salaam hivi karibuni, Khadija
alikiri kwamba asingeweza kufika mahali alipo bila ya kupata msaada mkubwa
kutoka kwa Othman.
“Othman ndiye aliyekuwa mtunzi wa nyimbo zote nilizoimba
tangu nikiwa Culture na TOT. Hata TOT waliponifuata Zanzibar, niliwaambia
kwamba nisingeweza kujiunga na kikundi hicho bila ya Othman kwa sababu bila
yeye nisingeweza kufanya lolote la maana,”alisema Khadija.
Kwa sasa, Othman ni askari wa Jeshi la Magereza visiwani
Zanzibar na uamuzi wake wa kuacha kujihusisha na muziki wa taarab ulimfanya
Khadija aanze kuchacharika na kutunga nyimbo zake mwenyewe.
Khadija anakiri kuwa ushindani wa kimuziki uliokuwepo
kati ya TOT na Muungano ulisaidia kwa kiasi kikubwa kuinua hadhi ya muziki huo.
Anasema haitatokea kwa vikundi viwili vya taarab nchini kuwa na ushindani kama
huo.
“Kila tulipofanya maonyesho ya pamoja, kumbi zilifurika.
Iwe Dar es Salaam, Morogoro au Mwanza, mashabiki walikuwa wakifurika ukumbini
kutushuhudia.
“Ni ushindani uliosababisha mashabiki wetu wajenge
uhasama mkubwa, lakini sisi wasanii tulikuwa kitu kimoja. Wengine walidhani
mimi na Nasma tulikuwa na uadui kutokana
na nyimbo tulizoimba, kumbe tulikuwa marafiki wakubwa na tulisaidiana kwa kila
hali,”alisema Khadija.
Khadija amekiri kuwa ushindani wa taarab umepungua
katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kuwepo kwa utitiri wa vikundi vya
muziki huo.
Aidha, alisema maonyesho ya vikundi vya taarab yamekuwa
yakifanyika kuanzia Jumatatu hadi Jumapili hivyo kuwafanya wasanii wake kuchoka
na kukosa ubunifu.
“Kinachosikitisha zaidi ni kuona kuwa baadhi ya vikundi
vya mitaani vimekuwa vikiimba nyimbo za vikundi vingine na maonyesho yamekuwa
yakifanyika bure hadi mashabiki wanachoka.
“Utakuta kikundi kimoja kinafanya onyesho mtaa huu,
kingine kinafanya onyesho mtaa wa pili. Huyu akisikia mwenzake amekwenda
kufanya maonyesho Lindi na mwingine naye anakwenda huko huko,”alisema Khadija.
Akizungumzia madai ya kuwepo kwa uhusiano kati ya muziki
wa taarab na ushoga, Khadija alisema si kweli kwa sababu kumjua shoga
kunahitaji ushahidi wa uhakika.
“Ushoga ni nafsi ya mtu kupenda kitu, si maumbile au
mwonekano wake,”alisisitiza mwanamama huyo.
Mwimbaji huyo pia alieleza kusikitishwa kwake na tabia
ya baadhi ya mashabiki wa muziki huo, hasa wanawake, kucheza kwa kukata viuno
na pia kuvaa mavazi yanayowaonyesha wakiwa nusu uchi.
Alisema japokuwa kukata viuno ni asili ya mwafrika,
lakini uvaaji wa mavazi ya nusu uchi si wa kistaarab, umepitiliza na unachangia
kushusha hadhi ya muziki huo na kuufanya uonekane kuwa wa kihuni.
“Tatizo hili halipo kwenye muziki wa taarab pekee, hata
hip hop na bongo fleva, utakuta wacheza shoo wamevalishwa nguo za nusu uchi.
Mbona wanaume hawavai nguo za aina hiyo, wanawavalisha watoto wa kike?” Alihoji
msanii huyo.
Amesema imefikia hatua hivi sasa, mzazi hawezi kutazama
televisheni akiwa na watoto wake, vinginevyo analazimika kuwa na ‘remote’
mkononi ili kukitokea tukio la aibu, aweze kuzima televisheni mara moja ama
kukimbilia nje ili kuepuka aibu.
Khadija amekiri kuwa umaarufu kwa wasanii ni mzuri,
lakini wakati mwingine umekuwa ukiwasababishia madhara ya aina mbalimbali,
ikiwa ni pamoja na kuzushiwa mambo ya uongo.
“Binafsi niliwahi kuzushiwa kwamba nimemuua mwanangu
Omar Kopa kwa lengo la kujiongezea umaarufu baada ya kuonekana amenizima. Pia
Leila Khatib alipokufa, niliambiwa kwamba mimi ndiye niliyemuua,”alilalamika.
Aliongeza kuwa, mbaya zaidi siku ambayo Leila alizikwa,
hakuweza kuhudhuria kwenye mazishi kutokana na yeye kufiwa na bibi yake, hali
iliyozidisha uvumi huo.
“Ukiwa msanii mzuri, unageuzwa kama malaika mtoa roho.
Msanii mwenzako akiumwa, unaogopa hata kwenda kumuangalia,” alisema.
Khadija amekielezea kifo cha aliyekuwa mkurugenzi wa
kikundi cha TOT Plus, Kepteni mstaafu, John Komba kuwa ni pigo kubwa katika fani
ya sanaa nchini.
Amesema si rahisi kwa pengo la Kepteni Komba kuzibika
kutokana na vipaji alivyokuwa navyo, isipokuwa anaweza kutokea msanii
atakayeleta ahuni.
“Kuziba pengo lake si rahisi, litabaki kama
lilivyo,”alisisitiza msanii huyo, ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa TOT.
Miongoni mwa mafanikio ya Khadija kutokana na muziki huo
ni pamoja na kutembelea nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Marekani. Pia
amefanikiwa kuanzisha kundi lake linalojulikana kwa jina la Ogopa Kopa Classic
Music.
Moja ya malengo yake ni kurekodi upya nyimbo zake zote
alizowahi kuziimba akiwa katika vikundi mbalimbali. Kikundi hicho kinaundwa na
wasanii wasiozidi 10, akiwemo mtoto wake wa mwisho wa kiume, anayefahamika
zaidi kwa jina la Black Kopa.
Iwapo mipango yake hiyo itafanikiwa, Khadija amesema
anatarajia kuanzisha miradi mbalimbali ya kikundi kwa lengo la kuwaongezea wasanii
mapato. Pia amepanga kuwashawishi wasanii wake wajiunge na mifuko ya hifadhi ya
jamii ili kujiwekea akiba kwa maisha yao ya baadaye.
Khadija hakuwa tayari kuzungumzia kwa kirefu ndoa yake
na mumewe, aliyefariki mwaka juzi mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, ambaye inadaiwa
alikuwa na umri mdogo kuliko yeye.
Alisema halikuwa jambo la ajabu kwake kuolewa na
mwanaume mwenye umri mdogo kwa sababu hata Mtume Muhammad na mkewe Khadija,
walifunga ndoa wakiwa wanatofautiana kwa miaka mingi.
“Mume wangu alikuwa anajua kunitunza. Nikienda kwenye
maonyesho alikuwa akinifuata, tunarudi nyumbani pamoja, sijui kama naweza
kumpata mume mwingine bora kama yeye. Kama atajitokeza, itabidi nimchunguze
sana,”alisema Khadija huku akitabasamu.
Khadija ametoa mwito kwa wasanii wa muziki wa taarab
kuwa na umoja kama ilivyo kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya, ikiwa ni
pamoja na kurekodi nyimbo pamoja.
“Inasikitisha kuona sisi wasanii wa muziki wa taarab
hatuna uwezo wa kufanya hivyo. Bongo fleva wanaungana na kuimba pamoja, lakini
sisi hatuna uwezo huo. Mbaya zaidi hatuna mapromota na mameneja wa kutuvusha
kutoka hapa tulipo,”alilalamika.
Subscribe to:
Posts (Atom)