KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Wednesday, April 29, 2015

MASHAUZI: NYIMBO ZANGU ZA DANSI ZIMEPOKELEWA VIZURI

MTUNZI na mwimbaji nyota wa muziki wa taarab nchini, Isha Ramadhani 'Mashauzi' amekiri kuwa, uamuzi wake wa kuimba nyimbo za miondoko ya dansi umepokelewa vizuri na mashabiki wake.

Isha, ambaye kwa sasa anamiliki na kuliongoza kundi la taarab la Mashauzi Classic, amesema amekuwa akipata pongezi nyingi kutoka kwa mashabiki baada ya kurekodi nyimbo hizo.

Nyimbo hizo, ambazo zimekuwa zikipigwa mara kwa mara kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini ni 'Nimlaumu Nani' na 'Nimpe Nani'.

"Wapo wanaonisifia na wanaonibeza kutokana na uamuzi wangu huo. Lakini binafsi nampenda sana mtu anayesema ukweli kutoka moyoni mwake,"alisema Isha alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni nchini.

Ameongeza kuwa kila kundi lake la Mashauzi Classic linapofanya maonyesho kwenye kumbi za burudani, mashabiki wamekuwa wakimuomba aimbe nyimbo hizo na kuzifurahia.

Kutokana na mafanikio hayo, Isha amesema anatarajia kurekodi albamu yake binafsi yenye nyimbo sita za muziki wa dansi.

"Nataka kuwapa mashabiki burudani yenye vionjo tofauti," alisisitiza mwanamama huyo mwenye mwili tipwatipwa, lakini anayejituma katika kulishambulia jukwaa kwa minenguo yake maridhawa na murua.

Isha amesema katika nyimbo zake mbili za awali za miondoko hiyo, ameimba sauti zote pekee yake baada ya kutengenezewa 'mipigo' ya ala katika studio za Gift.

"Nilimfuata prodyuza na kumuomba anitengenezee 'beats' za wimbo wa kwanza wa Nimlaumu nani, akanitengenezea beats mbili. Niliporejea nyumbani, nikaanza kutengeneza mashairi.

"Kesho yake nikaenda studio na kuanza kuurekedi. Ajabu ni kwamba baadhi ya mashairi yalinijia nikiwa studio, tofauti na yale niliyokuwa nimeyaandaa. Lakini mwisho wa siku ukatoka wimbo mzuri,"alisema mwanamama huyo, ambaye ni shabiki mkubwa wa klabu ya Yanga.

Isha amesema amekuwa na uhusiano mzuri na wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, na baadhi yao wamekuwa wakimkubali kutokana na umahiri wake wa kuimba nyimbo za miondoko tofauti.

No comments:

Post a Comment