THABITI Abdul |
KHADIJA Yussuf |
AISHA Vuvuzela |
JUMANNE Ulaya |
RAHMA Machupa |
HATIMAYE kikundi cha muziki wa taarab cha Jahazi, kimesambaratika baada ya wasanii wake zaidi ya wanane, kuhama na kujiunga na kikundi cha Wakali Wao Modern Taladance.
Habari kutoka ndani ya Jahazi zimeeleza kuwa, uamuzi wa wasanii hao kuhama, umelenga kuheshimu matakwa ya kiongozi wa zamani wa kundi hilo, Mzee Yussuf, kutaka jina hilo lisiendelee kutumika.
Kwa mujibu wa habari hizo, Mzee Yussuf aliwaeleza wasanii wa kundi hilo kuwa, kuendelea kutumia jina la Jahazi ni sawa na kuendelea kumshirikisha na dhambi wakati alishatangaza kuachana na muziki wa taarab na kumrudia Mungu.
Miongoni mwa wasanii wa Jahazi, waliojiunga na Wakali Wao Modern Taladance ni pamoja na Khadija Yussuf, Rahma Machupa, Aisha Vuvuzela, Mwasiti, Miriam, Mgeni Kisoda, Jumanne Ulaya na Mohamed Ali 'Mtoto Pori'.
Akihojiwa na Uhuru mwishoni mwa wiki, Khadija alikiri kuondoka kwake Jahazi, akiwa amefuatana na wasanii wengine kadhaa. Alisema wamefikia uamuzi huo kwa sababu kuendelea kwao kuwepo Jahazi ni kuzidi kumpa dhambi kaka yake, Mzee Yussuf.
"Jahazi ilikuwa Mzee Yussuf. Kwa vile ameamua kumrudia Mungu, tuliona ni bora kikundi kivunjwe ili kuepuka kumshirikisha katika dhambi,"alisema.
Aliongeza: "Nimeondoka Jahazi na kijiji changu. Mfalme Mzee Yussuf alikuwa ndiye kila kitu. Ameondoka na sasa hakuna wa kuiongoza."
Khadija alisema hajutii uamuzi wake huo kwa sababu yeye na wenzake wanajiamini kikazi na watashirikiana vyema na wenzao waliowakuta Wakali Wao kuupaisha muziki wa taarab.
"Mashabiki wetu watarajie makubwa kutoka kwetu kwa sababu ukali wetu ni ule ule, hatujatetereka kimuziki,"alisisitiza mwanamama huyo, ambaye amewahi kuimbia vikundi vya East African Melody na Zanzibar Stars.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wakali Wao Modern Taladance, Thabiti Abdul, alithibitisha kuwepo kwa muungano kati ya vikundi hivyo viwili.
Thabiti alisema awali, uongozi uliokuwa umebaki Jahazi, baada ya Mzee Yussuf kuachana na muziki, ulimfuata na kumuomba ajiunge na kikundi hicho akiwa ndiye mkurugenzi mkuu.
"Lakini baada ya majadiliano ya muda mrefu kati yetu, ikaonekana ni vizuri wasanii waliokuwa Jahazi waje kwangu ili tuwe kitu kimoja kwa kuwa mwenye bendi yake alikuwa hataki jina hilo liendelee kutumika,"alisema.
Thabiti, ambaye ni mmoja wa wapiga kinanda maarufu nchini, akitokea bendi ya Twanga Pepeta International, alisema lengo la muungano wao, ambao wameuita kwa jina la 'Mbili kwa moja', ni kuendeleza muziki wa taarab.
"Niliukubali mpango huu kwa sababu baada ya Mzee Yussuf kujitoa, Jahazi ilikuwa kama imekufa. Japokuwa ilikuwa ikiendelea na maonyesho, haikuwa Jahazi iliyozoeleka,"alisema.
Thabiti alisema mikakati waliyonayo ni kuhakikisha Wakali Wao, kinakuwa kikundi bora na maarufu katika muziki wa taarab nchini kama ilivyokuwa Jahazi enzi za Mzee Yussuf.
"Hakuna kushindwa, tunataka tushinde. Lazima tufike kule ilikokuwa Jahazi,"alisisitiza msanii huyo, ambaye pia ni mtunzi mahiri wa nyimbo za muziki huo.
Kwa mujibu wa Thabiti, katika maonyesho yao, watakuwa wakiimba nyimbo zote za Jahazi, zilizoimbwa na wasanii waliopo kwenye kikundi hicho, akiwemo Khadija Yussuf.
Thabiti alisema kikundi pekee kilichokuwa kikimuumiza kichwa kilikuwa Jahazi, lakini kwa kuwa hakipo, haoni kikundi kingine kitakachomsumbua.
"Mimi na Mzee Yussuf ndio tuliokuwa tukisumbuana. Hata kwenye tuzo za wasanii bora wa muziki wa taarab, tulikuwa tukibadilishana kuzinyakua. Kwa hiyo naweza kusema kuwa, kwa sasa nimebaki peke yangu,"alisema.
Thabiti alisema kwa kuwapata wapiga ala mahiri, kina Mgeni Kisoda, Jumanne na waimbaji kina Khadija, Rahma Machupa, Mwasiti, Miriam na Mtoto Pori, anaamini Wakali Wao itakuwa kwenye matawi ya juu.
Naye Mtoto Pori alisema yeye na wasanii wengine wote kutoka Jahazi, waliojiunga na Wakali Wao, wamefanya hivyo kwa moyo safi, bila kushawishiwa na mtu.
"Tuliona kwa kuwa mwanzilishi wa kikundi hataki jina lake liendelee kutumika, tusiendelee kumbebesha dhambi. Tuliangalia upepo, tukaona ni bora tuondoke,"alisema mwimbaji huyo machachari.
Aliongeza: "Pia, tuliona hakuna anayependa kuwa masikini kwa sababu ni kitu kibaya. Unaamka asubuhi, hujui wapo pa kwenda."
Utambulisho wa wasanii hao wapya ndani ya Wakali Wao Modern Taladance, umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, kwenye ukumbi utakaotangazwa baadaye.