KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Sunday, June 25, 2017

EID MUBARAKA WASOMAJI WANGU WAPENZI WA BLOGU YA RUSHAROHO


EID MUBARAK



Mikono tupeane
Rehema tutakiane
Upendo tushikamane
Toba tuhimizane
Makosa tusameheane
Yarabi tupe baraka zako
Utukubalie swaumu zetu
Amina yarabi Amina

KHADIJA: SIKUKATAA KUMPA MKONO LEILA WAKATI WA MSIBA. ASEMA HUO NI UZUSHI, MZEE YUSSUF ASIMULIA KILICHOTOKEA



MWIMBAJI  nyota wa muziki wa taarab nchini, Khadija Yussuph, amekanusha madai kuwa alikataa kupeana mkono na mke mkubwa wa kaka yake, Leila Rashid wakati wa msiba wa mke mdogo, Chiku.

Khadija amesema madai hayo hayana msingi wowote kwa sababu asingeweza kufanya kitu kama hicho kwenye msiba na kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akihojiwa katika kipindi cha Ng'aring'ri, cha Clouds TV leo, Khadija alisema kifo cha wifi yake, Chiku, ambaye ni mke mdogo wa kaka yake, Mzee Yussuph kilimchanganya na kumpa uchungu mkubwa.

"Kumbuka kulikuwa na watu wengi na ulikuwa msiba, nisingeweza kukataa kupeana naye mkono. Ingekuwa kwenye harusi labda ingeweza kutokea, lakini sio kwenye msiba.

"Na mimi nilikuwa nimechanganyikiwa sana. Nakumbuka nilimuona kwa mbali wakati anafika, lakini sikumbuki kama alinifuata na kunipa mkono, sio kweli hata kidogo,"amesema Khadija, ambaye alikuwa akiimba kundi moja na kaka yake, Mzee Yussuph na wifi yake, Leila.

Khadija amewataka mashabiki wake wapuuze madai hayo kwa kuwa yamelenga kumchafua kwa vile bado anamtambua Leila kuwa ni mke halali wa kaka yake, ikiwa ni pamoja na kuzaa naye watoto wawili.

Aidha, amewataka mashabiki wa muziki huo kumuombea Mzee Yussuph awe na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu, ambacho mkewe amemuachia watoto wadogo wawili.

Chiku alifariki dunia wiki iliyopita baada ya kufanyiwa operesheni ya uzazi kwenye Hospitali ya Amana, Dar es Salaam. Mazishi yake yalifanyika kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Akizungumzia uamuzi wa Mzee Yussuph kuachana na muziki wa taarab na kumrudia Mungu, ikiwa ni pamoja na kwenda kuhiji Makka, Khadija alikiri kuwa anajisikia kupwaya kwa vile alizoea kuimba naye pamoja.

Alisema uamuzi huo wa Mzee Yussuph umemfanya ajihisi upweke kila anapojihusisha na muziki huo stejini kwa vile alimzoea kama kaka, kiongozi na msanii mwenzake.

Kwa upande wake, Mzee Yussuph alisema hana hakika iwapo Khadija alikataa kupeana mkono na Leila wakati wa msiba wa mkewe mdogo, Chiku.

Alisema kama ni kweli Khadija alifanya kitendo hicho ni kosa kubwa mbele ya Mungu, hivyo anamuombea msamaha kwake na kwa mashabiki wa muziki huo.

Hata hivyo, alisema katika siku za hivi karibuni, Khadija alikuwa na uhusiano mzuri na Leila, ikiwa ni pamoja na kuchati ama kuzungumza kwa simu, tofauti na miaka kadhaa iliyopita, ambapo hawakuwa wakielewana.

Kuhusu msiba wa mkewe mdogo Chiku, msanii huyo nyota wa zamani wa taarab alisema baada ya kupata taarifa za kifo chake, alichanganyikiwa kwa kuwa hakutarajia.

Alisema mara baada ya kupata taarifa hizo, alimpigia simu mkewe mkubwa, Leila ambaye naye alichanganyikiwa na kumuuliza iwapo anaruhusiwa kuhudhuria kwenye msiba.

Amesema maneno ambayo hawezi kuyasahau kutoka kwa Leila ni pale alipompa pole na kisha kutuma ujumbe mfupi kwenye simu ya mkononi ukisema 'Jamani Chiku, mbona mapema hivi.'

Sunday, June 18, 2017

MKE WA PILI WA MZEE YUSSUPH AFARIKI KWA UZAZI AMANA




Aliyekuwa mfalme wa muziki wa Taarab Alhaj Mzee Yusuf, amefiwa na mke wake wa pili, Chiku Khamis Tumbo.

Mzee Yusuf amenukuliwa katika moja ya vyombo vya habari leo akisema kuwa, mkewe alifariki jana kwenye Hospitali ya Amana, Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo wa zamani wa kundi la Jahazi, alisema alimpeleka mkewe Amana, jana saa 10 alasiri, kwa ajili ya kujifungua na kwa bahati mbaya opereshini (upasuaji) iliyofanywa jioni, haikwenda salama na ikampoteza mkewe na mtoto aliyezaliwa.

Mazishi ya Chiku yanatarajiwa kufanyika leo jioni kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam. Marehemu Chiku ameacha watoto wawili.