KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, July 19, 2013

KINGS MODERN TAARAB YAJIANDAA KUTOA ALBAMU MPYA



KIKUNDI cha taarab cha Kings Modern kipo katika maandalizi ya kutoa albamu mpya ya nyimbo za taarab.

Wasanii wanaotarajiwa kuibuka na nyimbo mpya kwenye albamu hiyo ni
Aisha Salum Othuman 'Vuvuzela', Salha Abdala, Kibibi Yahaya na Sophia.

Mkurugenzi wa Kings Modern Taarab, Hamis Majaliwa amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha kuwa, albamu hiyo inakuwa moto wa kuotea mbali.

"Tunawaomba mashabiki wetu wakae mkao wa kula na kutegemea mambo mazuri na makubwa kutoka kwetu,"alisema.

"Ni album, ambayo italeta gumzo kwa sababu wapenzi wengi wa taarab wamekuwa wakisubiri kusikia wataimba nini hawa wasanii wapya, hasa Aisha Vuvuzela na Salha,"aliongeza.

Kings Modern Taarab kwa sasa inajumuisha wasanii 13 wakiwemo Aisha Othuman,Salha Abdallah, Kibibi Yahaya, Amina Myalu, Sophia,Anif Juma,Mzaka Nudu,Ibrahim Kamungu,Maneno Goma ,Dogras, Hassan Ally na Mrisho Rajab

JUMA MGUNDA 'JINO MOJA WA JAHAZI' AFARIKI



ALIYEKUWA mpiga gita la besi wa kikundi cha taarab cha Jahazi, Juma Mgunda 'Jino Moja' amefariki dunia.

Mgunda alifariki dunia Jumatano iliyopita kwenye hospitali ya Temeke, Dar es Salaam.
Msanii huyo alikuwa amelazwa kwenye hospitali hiyo kwa muda mrefu kutokana na kuugua ugonjwa wa kifua kikuu.

Mgunda alijipatia umaarufu mkubwa katika fani ya taarab kutokana na kupiga gita hilo kwa umahiri mkubwa katika nyimbo za Daktari wa mapenzi.

Katika sehemu ya wimbo huo, kiongozi wa Jahazi, Mzee Yusuph anasikika akimtaja kwa majina ya 'Juma Mgunda Jini Moja.'

Marehemu Mgunda alizikwa jana katika makaburi ya Tandika, Dar es Salaam.