KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Thursday, October 24, 2013

KHADIJA KOPA: NARUDI UPYA NA MAMBO MAPYA



HATIMAYE mwimbaji nyota wa nyimbo za muziki wa taarab nchini, Khadija Omar Kopa amemaliza eda na anatarajiwa kurudi ulingoni Oktoba 30 mwaka huu.

Khadija, ambaye alifiwa na mumewe Juni mwaka huu, alimaliza eda wiki iliyopita nyumbani kwa mumewe, Bagamoyo mkoani Pwani.

Mwanamama huyo kwa sasa amerejea nyumbani kwake Mwananyamala, Dar es Salaam, ambako ndiko alikokuwa akiishi kabla ya kuolewa.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Khadija alisema amealikwa kufanya onyesho maalumu Oktoba 30 mwaka huu kwenye ukumbi wa Villa Park ulioko Mwanza.

Khadija alisema baada ya onyesho hilo, atapanda tena stejini Novemba 3 mwaka huu katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Dar Live ulioko Mbagala mjini Dar es Salaam.

Alisema baadhi ya mashabiki wake wameandaa onyesho la Dar Live kwa lengo la kumchangia kutokana na msiba mzito alioupata wa kufiwa na mumewe.

Mume wa msanii huyo, Jaffari Ali Yusuf alifariki dunia nyumbani kwake Bagamoyo baada ya kuugua kwa muda mfupi na kuzikwa huko huko.

Kutokana na kifo hicho cha mumewe, Khadija alilazimika kuacha kufanya maonyesho ya taarab ili kukaa eda kwa miezi minne kwa mujibu wa taratibu za kisheria za kiislamu.

Khadija amewashukuru wakazi wa Bagamoyo kwa kumpa ushirikiano wa hali ya juu katika muda wote aliokuwa akiishi na mumewe katika wilaya hiyo ya kihistoria.

Malkia huyo wa mipasho alisema, baada ya kufiwa na mumewe, amegundua kwamba anapendwa na watu wengi tofauti na alivyokuwa akifikiria.

Khadija alisema kipindi chote alichokuwa kwenye matatizo, alishangazwa na ukaribu ulioonyweshwa na watu, ambao hakuwatarajia na ameijua nafasi yake kwenye jamii.

 “Nimesaidiwa na asasi mbalimbali, vikundi pamoja na watu wengi na wengine walikuwa wakiniambia nikitaka msaada, niwapigie ingawa sijafanya hivyo. Nimefarijika sana kuona napendwa kiasi hiki,” alisema mwanamama huyo, ambaye alimaliza eda Oktoba 16, mwaka huu.

Alisema itamchukua muda kidogo kuweza kupanda tena jukwaani kutokana na hali aliyonayo na kuongeza kuwa, anataka atakapotoka, aonekane mtu mpya na mwenye mambo mapya.

Kwa mujibu wa Khadija, katika onyesho lake la kwanza, anatarajia kutoka na wimbo mpya, unaojulikana kwa jina la Mwanamke kujiamini.

Alisema alitunga wimbo huo kabla ya kifo cha mumewe, lakini alichelewa kuutoa kutokana na kutingwa na mambo mengi.

"Nataka kwanza nitulize akili yangu. Namuomba Mungu anirejeshee nguvu upya ili nikitoka, nitoke kivingine,"alisema mwimbaji huyo wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT).

Khadija, ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema, baada ya onyesho la Dar Live, anatarajia kufanya onyesho lingine la kuwaaga wakazi wa Bagamoyo.

"Onyesho hili litakuwa maalumu kwa ajili ya kuwaaga wakazi wa Bagamoyo kutokana na kuishi nao vizuri muda wote niliokuwepo hapa na mume wangu,"alisema mwanamama huyo.

Khadija alisema anamshukuru Mungu kuona kuwa, bado yuko imara na amewaomba mashabiki wake, wamuombee dua ili aweze kurudi upya.

"Hii ni kazi yangu inayoendesha maisha yangu na ya familia yangu, nataka nitakaporudi ulingoni, niwe mpya, nitoke angalau na nyimbo mbili mpya, nawaomba mashabiki wangu waniombee kwa Mungu ili nirudi upya,"alisema.

Khadija alisema katika maonyesho hayo, anatarajia kuimba nyimbo zake mpya na za zamani na kuwaomba mashabiki wampokee kwa mikono miwili.

"Unajua ukiwa kwenye eda, unarudi nyuma sana, hivyo nahitaji muda kidogo wa kupanga mambo yangu upya ili nijue nitatoka vipi,"alisema mwimbaji huyo, ambaye aliwahi kung'ara kwa vibao vya Daktari, Wahoi na Kadandie wakati alipokuwa kikundi cha Culture cha Zanzibar.