KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, March 29, 2013

SHAKILA: MWASISI WA TAARAB ALIYESIMAMA JUKWAANI KWA ZAIDI YA MIAKA 40


“'Macho yanacheka, moyo unaliaaa, macho yanacheka aeeh, moyo unalia, nikimkumbuka wangu my dear ''
Hayo ni baadhi ya maneno yaliyo katika wimbo aliouimba Bi Shakila alipokuwa na Bendi ya JKT miaka 1980 -1990, ambao ulijizolea umaarufu mkubwa ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki.

Mkongwe huyo aliolewa mwaka 1960 alipokuwa na umri wa miaka 11 na mwanamume ambaye alizaa naye mtoto mmoja.

Shakila Said Khamis maarufu kwa jina la Bi Shakira  ni mmoja wa waasisi wa muziki wa Taarabu nchini, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Waimbaji wa Taarabu Tanzania.

Katika mahojiano na Starehe, Bi Shakila alieleza kuwa alianza kuimba taarabu sambamba na marehemu Saada Binti Saad, mwaka 1960 baada tu ya kuolewa na baadaye moja kwa moja alijiunga katika Bendi ya JKT aliyoitumikia kwa zaidi ya miaka 40.

"Nilianza muziki mwaka 1960 kabla ya Uhuru na nimekuwa huko kwa miaka mingi. Kabla ya kuanza muziki, nilimkuta marehemu Saada Binti Saad, Bi Kidude yeye nilimkuta akiwa tayari amejiunga na ngoma za Unyago, alikuwa bibi yangu na mtu wa karibu sana na mimi wakati huo nilikuwa na miaka sita.”

Hayo ni baadhi ya maelezo ya awali Bi Shakila katika mahojiano na Starehe nyumbani kwake Charambe, Dar es Salaam, kabla ya mfululizo ufuatao wa maswali na majibu na mwandishi wa makala haya.

Mwandishi: Hali yako kiuchumi kwa sasa ikoje?

Bi Shakila: Sina pesa, kiwango ninachokipata kama kiinua mgongo hakinitoshi kabisa. Nalipwa Sh80,000 kwa mwezi na NSSF, matumizi yangu kwa siku ni zaidi ya Sh15,000 kwa siku. Nilistaafu mwaka 2009, lakini mpaka sasa huwa naendelea na kazi yangu pale JKT mara chache na kama tukifanya shoo huwa napewa nauli Sh3000 inayonisaidia kunirudisha nyumbani. Kwa sasa hali yangu ni mbaya kiuchumi.

Mwandishi: Katika kipindi chote cha kazi yako hukuweza kujiwekea vitega uchumi, kama ndivyo sababu ni zipi?

Bi Shakila: Zamani muziki ulikuwa kama starehe, tulilipwa ujira mdogo na hata kukiwa na shoo tulipata ujira mdogo. Kwa sasa muziki ni ajira, tena kubwa kuliko ofisini, lakini umri umeshaenda sana na sisi wakongwe tunatamani haya yangekuwepo hapo nyuma, hii ndiyo sababu ya mimi kushindwa kuweka vitega uchumi.

Mwandishi: Unadhani Serikali inaweza kukusaidia?

Bi Shakila: Kabisa, sisi wakongwe hatuthaminiwi na tunatupwa jalalani, lakini watoto wadogo wavuta unga ndiyo wanasaidiwa, Msanii Ray C alienda mwenyewe kuvuta unga akijua kabisa ni kinyume cha sheria, lakini Serikali imemsaidia, kwa nini na sisi tusiangaliwe? Sisi ni dhahabu, wapo kina Mzee Gurumo, Small, Bi Kidude hivi sasa ni wagonjwa na wanahitaji msaada ila hawasaidiwi mpaka tufe ndiyo waje kutuzika?

Mwandishi: Pole! Wewe huamka saa ngapi na nini majukumu yako ya kutwa nzima?

Bi Shakila: Naamka saa 11 alfajiri kwa ajili ya kuanza kuandaa unga wangu wa vitumbua na maandazi, baada ya hapo naanza kupika. Alhamdulilahi, nina wateja kidogo wanaoniungisha. Saa4 asubuhi namaliza, napumzika kidogo na kuanza kuanza kutengeneza visheti hadi saa 12 jioni. Naoga, napumzika na wanangu tunazungumza mawili matatu kisha naenda kulala hadi kesho tena. Kama ninakwenda mazoezi JKT, basi siku hiyo ratiba yangu huvurugika kidogo. Biashara ya vitumbua nimeifanya kwa miongo minne sasa.

Mwandishi: Kwa kulinganisha na wakati wenu, unadhani taarabu ya sasa inakua?

Bi Shakila: Taarabu kwa sasa hakuna. Kwa sasa kuna rusha roho, mipasho, kiduku na  khanga moja. Vitu hivi vimevamia na kuiharibu taarabu yetu. Zamani taarabu ilikuwa na ustaarabu na waimbaji tuliimba kwa staha na maneno yalikuwa ya kuburudisha na kusifia kitu fulani si sasa hivi. Hii wanaita Morden Taarabu mimi siikubali kabisa.

Mwandishi: Maisha yako ya ndoa yalikuwaje?

Bi Shakila: Niliozwa nilipokuwa na miaka 11. Mume aliyenioa kwa ndoa aliniacha mwaka mmoja baadaye kwa kuwa tulitofautiana kwa mengi. Aliniacha nikiwa na mtoto mmoja mchanga, hapo ndipo nilipoanza balaa hilo. Niliolewa tena na mume mwingine huyu niliishi naye miaka 18 na kuzaa naye watoto watano, mwaka 1975 alifariki, iliniuma sana nikakaa eda.
Baadaye niliolewa na mume mwingine, huyu nikazaa naye watoto watano na baadaye tuliachana. Nikaolewa tena kwa mara ya nne, nikazaa watoto wawili, nilipokuwa na mimba ya huyu mtoto wa mwisho mwaka 1993, mume akaniacha. Mwanangu wa mwisho Shani nilimzaa Ijumaa ya tarehe 27 Machi 1993. Tangu hapo niliwachukia wanaume na sijataka kuolewa tena mpaka leo.

Mwandishi: Waimbaji wa muziki wa taarabu waume kwa wanawake huoa sana au kuolewa na kuachika, tatizo ni nini?

Bi Shakila: Sijui, kwa kweli mimi siyo kwamba nilikuwa nikiacha wanaume, hapana ila walikuwa wakiniacha wao. Kwa upande wangu nahisi ilitokana na kuwa mwanamuziki na wakati huo muziki ulichukuliwa kama uhuni. Lakini huenda kuna sababu nyingine ambazo mimi sizijui.

Mwandishi: Tangu kustaafu umeshafikiria kufanya kazi ya muziki ukiwa mwenyewe?

Bi Shakila: Ndiyo, tangu nimestaafu nilianza kufanya kazi nikiwa na mwanangu na mpaka sasa nipo mwishoni kumalizia albamu yangu ya Mama na Mwana itakayokuwa na nyimbo nane. Kati ya hizo tano zimekamilika ikiwamo ya Mama na Mwana.

MAKALA HII NI KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI.

Thursday, March 7, 2013

ALLY STAR AVUNJA UKIMYA



BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwimbaji taarab mkongwe nchini, Ally Hemed Star ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Mvuvi Kinda.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Ally alisema amekirekodi kibao hicho kwa mtindo wa zing zong, nje ya kundi lake la Tanzania One Theatre (TOT-Plus).

Ally alisema kibao hicho kitakuwemo kwenye albamu yake binafsi, anayotarajia kuizindua hivi karibuni, ambayo ameirekodi kwa mtindo huo.

Alisema anaushukuru uongozi wa TOT Plus kwa kumruhusu kurekodi nyimbo zake binafsi kwa lengo la kujiongezea mapato.

Mkongwe huyo wa taaab alisema, muziki huo kwa sasa unalipa, tofauti na miaka ya nyumba ndio sababu si rahisi kwa msanii kutunga wimbo na kumpa msanii mwingine auimbe.

"Enzi zetu, msanii akitunga wimbo, alikuwa anafikiria ampe nani aimbe na atampatia mwimbaji, ambaye anaendana na wimbo huo kutokana na maudhui yake,"alisema.

"Lakini siku hizi, mtu akitunga wimbo mzuri, hataka kumpa mwingine kwa hofu ya kumpatia sifa na umaarufu,"aliongeza.

Ally alisema kutokana na muziki wa taarab kuwa na malipo mazuri hivi sasa, kila msanii anataka kutoka kivyake kwa lengo la kujiongezea mapato.

Ally alianza kupata umaarufu katika taarab wakati alipokuwa akiimbia kikundi cha Bima Modern Taarab kabla ya kutua Muungano Cultural Troupe na baadaye TOT Plus.

SIJAITOSA MASHAUZI CLASSIC-THABITI


MSANII nyota wa muziki wa taarab nchini, Thabit Abdul amesema uamuzi wake wa kujiunga na kikundi cha taarab cha Five Stars hauna maana kwamba amekitosa kikundi chake cha Mashauzi Classic.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Thabiti alisema amejiunga na Five Stars kwa makubaliano maalumu na kwamba bado ataendelea kuitumikia Mashauzi Classic.
Thabit, ambaye ni mmoja wa wapiga vinanda mahiri nchini alisema, uongozi wa Five Stars umemruhusu kufanya maonyesho na kikundi cha Mashauzi Classis kila atakapokuwa na nafasi.
Alisema kwa sasa yeye si msanii wa kupiga muziki jukwaani kwa muda mrefu kwa sababu kazi yake kubwa ni kutunga, kutengeneza muziki na kupiga ala.
"Katika kikundi cha Mashauzi Classic, sina kawaida ya kupiga nyimbo nyingi stejini. Naweza kupiga wimbo mmoja ama mbili tu kwa sababu wapo vijana wanaofanya kazi hiyo,"alisema.
Alipoulizwa atawezaje kuvitumikia vikundi vyote viwili iwapo vitakuwa na maonyesho kwa wakati mmoja, Thabit alisema kikundi chake cha kazini ni Five Stars.
"Inapotokea hivyo, lazima nikitumikie kikundi cha Five Stars, ambacho nina mkataba nacho,"alisisitiza.
Thabit ni mmoja wa wakurugenzi wa Mashauzi Classic, kinachoongozwa na mwimbaji machachari wa kike, Isha Mashauzi.
Hata hivyo, msanii huyo wiki iliyopita alitangaza kujiunga na Five Stars, ambacho kimesukwa upya baada ya kupata uongozi mpya. Wasanii wengine waliojiunga na kikundi hicho ni Mwanahawa Ally, Sabah Salum, Hammer Q, Maua Tego na Mosi Suleiman.