KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Sunday, September 23, 2012

MWANAHAWA APAGAWISHA MASHABIKI DAR LIVE

Mwimbaji mkongwe wa taarab, Mwanahawa Ally (juu) akiimba wakati wa onyesho la usiku wa dhahabu lililofanyika jana kwenye ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala, Dar es Salaam. Picha ya chini ni waimbaji wa kundi la East African Melody wakiimba wakati wa onyesho hilo.

KHADIJA KOPA AMTUNGIA WIMBO MUMEWE

Mwimbaji nyota wa taarab nchini, Khadija Kopa akiwa na mumewe kabla ya kupanda stejini katika moja ya maonyesho yake.
Khadija Omar Kopa akilishambulia jukwaa akiwa sanjari na mabinti zake

Mwimbaji nyota wa taarab nchini, Khadija Omar Kopa ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Nampenda mume wangu.
Kibao hicho alichokiimba kwa tashtiti ya hali ya juu kimeshaanza kutikisa anga za muziki kwa kupigwa mara kwa mara kwenye vituo mbalimbali vya redioni nchini.
Katika kibao hicho, Khadija anaelezea umuhimu wa wanawake kuwapenda na kuwaheshimu waume ama wapenzi wao badala ya kuwakashifu.
Anasema yeye binafsi anampenda mumewe na kumpatia kila anachokihitaji na kwamba katu hawezi kumuhini chochote.

MDOGO WAKE MASHAUZI AFUATA NYAYO

Binti mdogo Saida, ambaye ni mdogo wake wa nne wa Isha Mashauzi, ameanza kuonyesha cheche katika uimbaji wake na kuleta tegemeo la  kufikia upeo wa dada yake. Salma ni mmoja wa waimbaji katika kundi la Mashauzi Classic

Monday, September 17, 2012

JOKHA KASSIM AKANA KUWAPIGA VIJEMBE MZEE YUSSUF NA LEILA RASHID


"KUPIGANA vijembe katika tungo za taarab hakujaanza leo wala jana, tangu enzi za marehemu Leila Khatib, ambaye alikuwa akirushiana maneno na Khadija Kopa."
"Sisi waimbaji chipukizi tumerithi kwao. Siwezi kushangaa kusikia mtu anampiga vijembe mwenzake kwenye nyimbo za taarab," ndivyo alivyoanza mazungumzo yake mwimbaji taarab mwenye sura na sauti yenye mvuto, Jokha Kassim,ambaye kwa sasa yupo katika kundi la T-Moto.
Jokha alitoa ufafanuzi huo kutokana na kuwepo kwa madai kuwa, nyimbo zake nyingi anaziomba zimelenga kuwapiga vijembe, mkurugenzi wa kikundi cha Jahazi, ambaye pia ni mumewe wa zamani, Mzee Yussuf na mkewe wa sasa, Leila Rashid.
Baadhi ya mashabiki wa muziki huo wanadai kuwa, tangu Jokha alipoachana na Mzee, amekuwa akitunga nyimbo zenye mwelekeo wa kumpifa vijembe mumewe huyo pamoja na mkewe Leila, ambaye pia ni mwimbaji wa Jahazi.
Mzee alibahatika kuzaa na Jokha mtoto mmoja wa kiume, anayejulikana kwa jina la Yussuf na waliwahi kufanyakazi pamoja katika makundi mbali mbali ya muziki huo.
Jokha alisema kwa kawaida, muziki wa taarab ni wa malumbano na majibizano na kwamba imekuwa ikifanyika hivyo tangu enzi na enzi.
Alisema tangu akiwa mdogo, waimbaji wengi wa muziki huo walikuwa wakiimba nyimbo za kujibimizana hivyo haoni ajabu kwa waimbaji wa sasa nao kufuata mkondo huo.
"Nakumbuka marehemu Leila Khatib alikuwa akipigana vijembe sana na Khadija Kopa. Lakini lengo lao halikuwa baya, ilikuwa ni njia fulani ya kuvuta mashabiki kwenye maonyesho yao,"alisema.
"Hivyo hata sisi tumerithi kutoka kwao hao, ambao tunaamini ni wakongwe kwetu na wanaheshimika kwenye tasnia ya muziki wa taarab,"alisisitiza Jokha.
Hata hivyo, mwimbaji huyo alisema si kweli kwamba nyimbo nyingi anazoimba zimewalenga Yussuf na Leila. Alisema lengo lake ni kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu masuala mbali mbali.
Jokha alisema majibizano kwenye taarab ni mambo ya kawaida na kwamba kufanya hivyo kunaleta changamoto kwa mashabiki na vikundi vya muziki huo.
Alisema kibao chake kipya kinachojulikana kwa jina la 'Domo la udaku' hakimlengi mtu yeyote kama baadhi ya mashabiki wanavyodai. Alisema mpangilio wa mashairi ya wimbo huo yamekuwa yakileta tafsiri mbaya, ambapo wengi wanaamini kuna mtu aliyekusudiwa.
Jokha alisema lengo lake katika kutunga wimbo huo ni kuielimisha jamii juu ya mambo mbali mbali kama ulivyo wajibu kwa msanii.
Mwimbaji huyo mwenye macho yenye mvuto pia alisema kwa sasa anajiandaa kuachia kibao kingine kipya, ambacho alitamba kwamba kitakuwa moto wa kuotea mbali.
Akizungumzia maisha yake ya sasa baada ya kujiunga na T-Moto, alisema mambo yanamwendea vizuri na kipaji chake kinazidi kuongezeka.
Alisema tayari wamesharekodi albamu inayoitwa 'Aliyeniumba hajakosea', ambayo imekuwa gumzo mkubwa kwa mashabiki wa muziki huo.
Jokha alisema baada ya albamu hiyo, wanatarajia kuipua albamu zingine mbili zitakazojulikana kwa majina ya Mimi staa na Domo la udaku.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zitakazokuwemo kwenye albamu hizo kuwa ni Mwanamke hashuo na Wewe si daktari wa mapenzi.

REHEMA TAJIRI, MWANAMUZIKI ALIYEAMUA KUJITOSA KWENYE TAARAB


BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwanadada Rehema Tajiri ameibuka upya, lakini safari hii ameamua kujitosa kwenye muziki wa miondoko ya zouk na taarab.
Rehema, ambaye alianza kuchomoza kimuziki mwaka 2002, anatarajia kurekodi albamu ya zouk kwa ajili ya kuuaga muziki wa dansi kabla ya kuhamia kwenye mipasho.
Mwanamama huyo ameamua kujitosa kwenye taarab kwa kile anachodai kuwa, muziki huo una mvuto mkubwa ikilinganishwa na dansi na kwamba ameshaanza kufanya vizuri katika kikundi cha Jahazi Korongwe chenye maskani yake Temeke, Dar es Salaam.
Kikundi hicho ni maalumu kwa ajili ya kupiga nyimbo za kuiga za vikundi mbali mbali vya taarab na kwa Rehema, amekuwa akipendelea zaidi kuimba nyimbo za Mwanahawa Ally wa kundi la East African Melody, Leila Rashid na Khadija Yussuf wa kundi la Jahazi.
Akizungumza na Uhuru mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Rehema alisema anaamini kuwa, huo ni mwanzo tu wa safari yake ndefu katika muziki huo kwa vile lengo lake kubwa ni kuimba nyimbo zake mwenyewe za taarab.
Mama huyo wa watoto wawili alisema amekuwa kimya kwa muda mrefu kutokana na kutingwa na masomo na pia matatizo ya kifamilia. Hata hivyo, alisema kwa sasa anamshukuru Mungu kwamba ameweza kuvivuka vikwazo vingi vilivyokuwa vikimkwaza katika kazi yake hiyo.
Rehema alianza kung’ara kimuziki baada ya kuibuka na albamu yake ya kwanza inayojulikana kwa jina la Sumu ya Ndoa. Alirekodi albamu hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya wanamuziki nyota waliokuwa wakiunda bendi ya Msondo Ngoma, wakiwemo marehemu Moshi William na Maneno Uvuruge.
Baadhi ya vibao vilivyokuwemo kwenye albamu hiyo ni pamoja na Maisha Vijijini, Binadamu hawana wema, Karibu shemeji na muziki ni kazi.
Rehema alisema alipata mafanikio makubwa kutokana na mauzo ya albamu hiyo kwa vile aliweza kuwalipa wanamuziki alioshirikiana nao pamoja na kupata faida kidogo.
Alirekodi albamu yake ya pili mwaka 2005, inayojulikana kwa jina la Ni wako tu, lakini safari hii hakuwatumia wanamuziki maarufu. Alimtumia mwanamuziki mwingine nyota wa kike, Dotnata.
Baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Sirudi nyuma, Namsaka mbaya wangu, Penzi la uongo na Nicheze na nani.
“Katika albamu hii, sikutaka kuwashirikisha wanamuziki wengine kwa sababu mara ya kwanza nilisakamwa sana na maneno. Wapo waliodai kuwa, nyimbo zote za kwenye albamu ya kwanza nilitungiwa na marehemu Moshi, wengine wakazua uongo kwamba alikuwa mpenzi wangu wakati si kweli,”alisema Rehema.
“Na hata nilipomshirikisha Dotnata, walimwengu hawakukosa maneno ya kuzungumza. Na nilipotengeneza video ya wimbo wangu kwa kumshirikisha Dokta Cheni, pia yakasemwa maneno mengi. Ndio sababu niliamua kuwa kimya kwa muda,”aliongeza mwanamuziki huyo.
Rehema, ambaye ni mke wa zamani aliyekuwa kipa namba moja wa Yanga, marehemu Sahau Kambi alisema, albamu yake itakayofuata hivi karibuni itakuwa ya muziki wa zouk.
Alisema ameshaanza maandalizi kwa ajili ya kurekodi albamu hiyo, lakini hakuwa tayari kuzitaja nyimbo zitakazokuwemo ndani yake. Alisema atazitangaza baada ya kuzikamilisha.
Baada ya albamu hiyo, Rehema alisema itakayofuata itakuwa ya taarab, ambayo atarekodi kwa kushirikiana na wasanii mbali mbali nyota wa muziki huo.
Pamoja na kurudi kwenye gemu kivingine, Rehema pia ameamua kuwa mwanasiasa na hivi karibuni alichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa UWT mkoa wa Dar es Salaam na mjumbe wa baraza la UWT la wilaya ya Temeke.
Aliibuka wa pili katika uchaguzi wa mkoa baada ya kuzoa kura 448 wakati katika uchaguzi wa wilaya, aliibuka kinara kwa kuzoa kura 538.
Rehema alisema hii ni mara yake ya pili kujitosa katika uchaguzi wa jumuia hiyo, mara ya kwanza ikiwa miaka mitano iliyopita, ambapo kura hazikutosha.
Mwanamama huyo alisema ameamua kujitosa kwenye siasa kwa lengo la kufuata nyayo za baba yake, marehemu Hamisi Tajiri, ambaye aliwahi kushika nyadhifa kadhaa za uongozi za CCM katika ngazi ya tawi na kata.
Marehemu Tajiri, ambaye alikuwa mmoja wa waigizaji magwiji wa maigizo wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) miaka ya 1970 hadi 1980, pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA).
“Nimeamua kujitosa kwenye siasa kwa lengo la kufuata nyayo za baba yangu na pia kutetea haki za akina mama,”alisema Rehema.
Kwa mujibu wa Rehema, uamuzi wake huo hauna lengo la kutaka kuwania ubunge ama udiwani katika uchaguzi mkuu ujao, bali kuwatumikia wanawake wenzake.
“Nataka kuwanasua akina mama, hasa wa vijijini, ambao wanatumika zaidi katika kazi za kilimo na kijamii kuliko akina baba,”alisisitiza.
Hata hivyo, alikiri kuwa kazi hiyo ni ngumu na inahitaji moyo kutokana na ukweli kwamba, ni hulka kwa akina mama kutokuwa na utamaduni wa kupendana zaidi ya kusemana.
Alisema kutokana na mapenzi yake katika kuwainua kina mama, hata nyimbo nyingi anazotunga zimekuwa zikizungumzia maisha yao na matatizo yanayowakuta katika jamii.
Pamoja na kujitosa kwenye siasa, Rehema alisema hatarajii kuitumia fani ya muziki kumbeba kama ilivyo kwa wanasiasa wengine. Alisema atatumia nguvu ya marehemu baba yake na ushawishi alionao kwa wanawake wenzake.
Rehema amewahi kutunga wimbo wa kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa nafasi nyingi za uongozi kwa wanawake na pia kwa uongozi wake mzuri na uliotukuka kwa watanzania.
Alisema kwa sasa, ameshatunga nyimbo mbili kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao mkoani Dodoma, lengo likiwa kuwahamasisha wanachama wake kuchagua viongozi wenye uwezo wa kukivusha na kukifikisha chama mbali zaidi.
Amewashukuru waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari kwa kumpa ushirikiano mkubwa katika kipindi chote alichokuwa kwenye fani hiyo na kusisitiza kuwa, bila wao asingeweza kufika alipo sasa.
“Kwa moyo wa pekee, nawashukuru sana waandishi wa habari, walifanyakazi kubwa sana ya kunitangaza hadi nikafahamika nchi nzima. Bila wao, nisingekuwa Rehema ninayejulikana sasa,”alisema.
“Pia nawaomba mashabiki wangu wasiwe na wasiwasi wowote. Najua hawajaniona kwa muda mrefu, lakini nipo, nilikuwa nasoma na pia nilipatwa na matatizo ya kifamilia, lakini sasa mambo yapo safi,”alisema.
Rehema alisema baadhi ya mashabiki wake walikuwa wakimtumia barua pepe na wengine kuwasiliana naye kwenye facebook kutaka kujua alipo. Alisema alishindwa kujibu meseji zingine kutokana na matatizo aliyokuwa nayo.
“Lakini nawapenda sana wote. Watarajie kuniona tena kwenye muziki hivi karibuni na pia kwenye ulingo wa kisiasa,”aliongeza.

Thursday, September 13, 2012

UNAFAHAMU LOLOTE KUHUSU TAUSI WOMEN MUSICAL CLUB? SUBIRI KUSOMA HABARI ZAKE HIVI KARIBUNI

Wasanii wa kikundi cha (Tausi Women Musical Club) wakicharaza ala ya Muziki wakati wa uzinduzi wa kikundi hicho uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Ali Mohamed Shein, katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel.(22/10/2011)

Watoto waliozaliwa katika familia za wanamuziki wa Taarab,Neema Suri,(kulia) na Nabil Mohamed wakionesha vipaji vyao katika fani ya kupiga udi katika uzinduzi wa kikundi cha Wanawake cha Taarab,kiitwacho (Tausi Women Musical Club),uzinduzi wa kikundi hicho umefanywa na Rais wa zanzibar Dk Ali Mohamed Shein,katika ukumbi wa salama Bwawani Hotel juzi.(22/10/2011).

Tuesday, September 11, 2012

VIDEO ZA ALBAMU TATU ZA DAR MODERN TAARAB ZAKAMILIKA


KIKUNDI cha Dar Modern Taarab kimekamilisha kazi ya kurekodi video za albamu zake tatu ilizozizindua hivi karibuni kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine iliyopo Magomeni, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa kundi hilo, Mridu Ally alisema wiki hii kuwa, video hizo za albamu zote tatu zilikamilika wiki iliyopita.
Mridu alisema picha za video hizo zilipigwa katika maeneo mbali mbali ya Jiji la Dar es Salaam na Bagamoyo na lengo lilikuwa kuzipa vionjo tofauti.
Mkurugenzi huyo alitamba kuwa, video hizo ni moto wa kuotea mbali na kuongeza kuwa, anaamini zitakuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wao.
"Video za albamu zote tatu tumezitengeneza kwa umakini mkubwa na utaalamu wa hali ya juu, kilichobakia ni kuanza tu kuzisambaza kwa mawakala wetu,"alisema.
Mridu alisema tayari baadhi ya video hizo zimeshaanza kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni nchini kabla ya kuanza kuwafikia mashabiki.
Albamu hizo tatu, ambazo zilizinduliwa kwa mpigo ni Ndugu wa mume, Toto la Kiafrika na Ninauvua ushoga.

VIDEO YA DUNIA DUARA IPO TAYARI


VIDEO ya kibao cha Dunia Duara ya kundi la muziki wa taarab la Kings Modern Taarab, inatarajiwa kuanza kuonekana hivi karibuni kwenye vituo mbali mbali vya televisheni nchini.
Akizungumza na Spoti Leo, Mkurugenzi wa kundi hilo, Majaliwa Hamisi alisema kazi ya kurekodi video hiyo inatarajiwa kukamilika wiki hii.
Kibao hicho kipo kwenye albamu ya My Heart ya kundi hilo na kimeimbwa na mwimbaji mkongwe, Mwanahawa Ally, ambaye kabla ya kurejea Kings Modern alikuwa akiimbia kundi la T-Moto.
Mwanahawa, ambaye amewahi kupachikwa majina ya Kinyago cha Mpapure na Chipolopolo, alikiri hivi karibuni kuwa, hakuwa na furaha alipokuwa kwenye kundi la T-Moto kama ilivyo awapo Kings Modern.
Kibao cha My Heart kimeimbwa na Young Hassan Ally wakati kibao cha Full Style kimeimbwa na Hanifa Mpita, aliyejiunga na kundi hilo hivi karibuni akitokea Mashauzi Classics.
Kwa mujibu wa Majaliwa, kibao cha Riziki mwanzo wa chuki kilichoimbwa na mshindi wa shindano la Bongo Star Search mwaka jana, Mariam ndicho pekee, ambacho hakijatengenezewa video.
"Karibu vibao vyote vilivyomo kwenye albamu yetu mpya vimeshatengenezewa video zake, isipokuwa Riziki mwanzo wa chuki,"alisema.
CHANZO CHA HABARI: SPOTI LEO

ALBAMU YA SHAKILA YA MAMA NA MWANA YAJA


ALBAMU binafsi ya mwimbaji mkongwe wa taarab nchini, Shakila Saidi ya Mama na Mwana, imechelewa kukamilika baada ya binti yake kupatwa na matatizo.
Shakila kwa kushirikiana na binti yake wa kwanza, Mwape Kibwana walitarajia kutoa albamu hiyo, ambayo tayari walishaanza kurekodi nyimbo zake, lakini wameshindwa kuikamilisha baada ya binti huyo kuugua.
Shakila alisema wiki hii kuwa, binti yake huyo alikumbwa na matatizo ya uja uzito na kusababisha washindwe kukamilisha kazi hiyo kwa muda waliopanga.
"Binti yangu, ambaye nimeshirikiana naye kurekodi albamu hiyo amepata matatizo wakati wa uja uzito, ikawa bahati mbaya tumeshindwa kukamilisha kazi hiyo," alisema Shakila.
Naye Mwape alisema wanatarajia kuendelea na kazi hiyo baada ya afya yake kutengemaa. Alisema anaamini kazi hiyo itakamilika baada ya muda si mrefu.
Kwa mujibu wa Mwape, wanatarajia kukamilisha kazi hiyo baada ya kurejea kutoka Dodoma, ambako wamealikwa kwenda kutioa burudani.
CHANZO CHA HABARI: SPOTI LEO

Monday, September 3, 2012

BI KIDUDE MUZIKI SASA BASI


Kulia kwangu ni Bi Hidaya, anayemuuguza Bi Kidude hospitalini, tukizungumza huku tukipiga soga na mgonjwa pia ambaye yuko mbele yetu jioni ya leo, Hindu Mandal. 

Na Mahmoud Zubeiry
HALI ya afya ya msanii mkongwe nchini, Fatuma Binti Baraka, maarufu kama Bi Kidude inaendelea vizuri katika hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam alipolazwa na wakati wowote kuanzia kesho anaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani, ila familia imemstaafisha rasmi sanaa.
BIN ZUBEIRY alifika katika wadi namba 202 hospitali ya Hindu Mandal, jioni hii kumjulia hali Bi Kidude, mwimbaji maarufu na mkongwe haswa wa muziki wa Taarabu duniani na ‘alhamdulillah’, Bi Mkubwa anaendelea vizuri.
Watu wanapishana kuingia na kutoka kumsalimia Bi Kidude, wengine wakitoka nje ya nchi, baadhi mashabiki wake na baadhi ndugu na jamaa.
Lakini jambo moja tu Bi Kidude analaani vikali ni taarifa za kuzushiwa kufariki dunia mwishoni mwa wiki. “Watu wamenizushia kufa Zubeiry, na wewe hukuja kuniona, ulifikiri nimekufa? Mi mzima, si unaniona, cheki,”alisema Bi Kidude na kuuvuta mkono wa BIN ZUBEIRY kwa nguvu akiuminya ‘kibaunsa’ kuonyesha nguvu za misuli yake, kwamba yeye yuko mzima.
Bi Kidude alikuwa mcheshi wakati anazungumza na watu mbalimbali waliomtembelea hospitali na alimuambia BIN ZUBEIRY kwamba anasumbuliwa na maradhi ya sukari, ambayo ni maradhi yake kwa muda mrefu, ila yalimzidia kwa kukiuka taratibu za vyakula.
“Kweli nilikuwa naumwa, ngozi yote ilivuka hii, nilikonda sana, ila sasa Alhamdulillah mi mzima, mi mzima, naweza kuondoka,”alisema.
Mwonekano wa Bi Kidude ni mtu mwenye afya njema japokuwa amelala kitandani wadi namba 202, Hindu Mandal na sasa anainuka kwenda mwenyewe msalani.
Amezuiwa kuvuta sigara tangu alazwe hospitalini hapo na inaonekana kwa hamu ya sigara anaomba aondoke hata sasa hivi. Amewekewa waangalizi wawili, wa kike na wa kiume, wote wakiwa ni wanafamilia.
Hidaya Abdi Omar, mkwe wa Kidude ambaye ni mmoja wa waangalizi wake hospitalini hapo amesema kesho Bi Mkubwa huyo atafanyiwa vipimo ambayo kama vitakuwa namna ambavyo madaktari wa hospitali hiyo wanataka, ataruhusiwa.
Hidaya ni mke wa mtoto wa mdogo wake wa kiume Bi Kidude, aitwaye, Abdallah Baraka ambaye hivi sasa ni marehemu. “Bi Kidude hakubahatika kuzaa, lakini ndugu zake wamezaa, mimi ni mke wa mtoto wa kaka yake Bi Kidude, na kwa sasa ndiye naishi na huyu bibie kulingana utu uzima na hali yake pia,”anasema Hidaya.
Hidaya anasema msimamo wa familia umekwishapita kwamba Bi Mkubwa huyo sasa hataruhusiwa kufanya kazi yoyote ya sanaa, atakuwa wa kupumzika tu acheze na wajukuu.
“Hatapanda tena jukwaani popote, sasa basi tena, akae tu apumzike, familia imekwishaamua,”alisema. Familia hiyo hiyo imeamua Bi Kidude asipigwe picha yoyote akiwa wadini.
Ndugu zake wote watatu ambao ni wadogo zake Bi Kidude wamekwishafariki dunia na kwa sasa Bi Kidude anakula matunda ya watoto wa ndugu zake hao, ambao kwa sasa ndio wanamlea.
Hakuna promota yeyote wa tamasha au kiongozi wa serikali, au chombo chochote cha sanaa aliyekwenda kumjulia hali Bi Kidude wadini, zaidi baadhi ya wasanii wanapiga simu tu na kwa hilo wala Bi Mkubwa huyo hajali, watu wanaokwenda kumuona na kumfariji kwake wanatosha.
Bi Kidude alianza kusumbuliwa na maradhi mwezi uliopita, lakini baadaye akapata ahueni na kufanya mahojiano hadi na vyombo vya habari, lakini ghafla mambo yakabadilika tena na amerudi hospitali, ila kwa sasa unaposoma habari hii yuko vizuri Hindu Mandal.
Bi Kidude ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, katika fani ya muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.
Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
Bi Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti Binti Saad. Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
Bi Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya 'wanja' na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Quraan.
CHANZO CHA HABARI: BIN ZUBEIRY

Sunday, September 2, 2012

JAHAZI WAJA NA ALBAMU MPYA

Mmoja wa waimbaji wa kikundi cha Jahazi, Mariam Mwinjuma

Fatma Kassim, mmoja wa waimbaji wenye mvuto wa kundi la Jahazi

KIKUNDI cha taarab cha Jahazi kinatarajia kupakua albamu mpya hivi karibuni itakayojulikana kwa jina la Wasiwasi wako ndio maradhi yako.
Akizungumza na blogu ya rusha roho wiki hii, kiongozi wa kundi hilo, Mzee Yusuph alisema albamu hiyo itakuwa na nyimbo sita.
Mzee alisema tayari baadhi ya nyimbo zimeshakamilisha wakati zingine bado zipo kwenye hatua ya mwisho.
Kwa mujibu wa Mzee, miongoni mwa nyimbo zitakazokuwemo kwenye albamu hiyo ni Mgodi wa Dhahabu, ambao umeshaanza kusikika kwenye vituo mbali mbali vya redio nchini.
Mzee alisema amepania kufanya mabadiliko makubwa kwenye muziki wa taarab ili kuwapa mashabiki ladha tofauti badala ya ile waliyoizoea.
"Sisi kama Jahazi tunapenda tufanye kile kitu mashabiki wanapenda, hivyo tunawaahidi mambo mapya kabisa katika albamu yetu hii mpya,"alisema.
Albamu hiyo itakuwa ya tisa tangu kundi la Jahazi lilipoanzishwa mwaka 2006. Albamu zingine zilizopita za kundi hilo ni Tupendane wabaya waulizane, Wagombanao ndio wapatanao, Mpenzi chokolate, Daktari wa mapenzi, Two in one, VIP na My Valentine.

Saturday, September 1, 2012

MZEE YUSUPH AFUNGUA KAMPUNI YA KUSAMBAZA KAZI ZAKE


MSANII wa mziki wa Taarabu nchini Mzee Yussuf ameamua
kufungua kampuni yake ya usambazaji ijulikanayo kama MY
Collection kwa ajili ya kusambaza kazi zake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Meneja Mauzo wa
Kampuni hiyo Mussa Msuba amesema wameamua kufungua duka
kwa ajili ya kuuza CD NA DVD za bendi ya Jahazi inayongozwa na
Mzee Yussuf.
Duka hilo lililopo makutano ya barabara ya likoma na
Muhonda, linajihusisha na uzaji wa DVD za taarabu kwa jumla na
rejareja kwa ajili ya kuwaweka karibu wapenzi wake ili waweze
kupata burudani kupitia nyimbo zao kwa kuwaburudisha wakiwa
majumbani.
Msuba amesema kuwa Mzee Yusufu yupo mbioni kutoa albamu
yake ya mduara itakayokuwa hivi karibuni ambayo ni yake binafsi.
Mbali na hilo, bendi hiyo itatoa video yake ya Live za albamu zake
zote za Two in One,Kazi ya Mungu, Nakula ka Naksh
Naksh,tupendane, Daktari wa Mapenzi, ambazo zitakuwa madukani kwa
ajili ya kuwapa wapenzi wao burudani wakiwa majumbani mwao.
Naye Mzee Yussuf aliongeza kwa kusema ameanzisha kampuni yake
binafsi baada ya kuona kwamba kazi zake nyingi zimekuwa
zikichakachuliwa kutokana na kuwepo kwa wizi wa kazi za sanaa.
Kampuni yake imekuwa ikisambaza kazi zake kwa ajili ya kuogopa
kuibiwa kutokana na wimbi la kazi za wasanii nchini.
Duka lililopo mtaa wa Muhonda na Likoma kwa ajili ya CD za
Jahazi pekee.
Mbali na duka hilo mzee Yusufu anamiliki duka lingine la Nguo
lililopo Magomeni Mapipa kwa ajili ya kujiongezea
kipato chake.
Bendi ya Jahazi mpaka sasa imekwisha toa albam nane ambazo
zipo madukani zinauzwa kwa ajili ya watu wotekupata burudani
wakiwa majumbani mwao.
Kwa sasa bendi hiyo ipo mbioni kuachia albamu yake ya tisa
ambayo aijapewa jina inatarajiwa kuzinduliwa mwezo Octoba kwa
ajili ya kutoa burudani kwa wapenzi wao na kuwataka mashabiki
wao kuja kuangalia na kusikiliza nyimbo mpya popote pale
wanapotoa burudani zao katika kumbi mbalimbali za jijini Dar es
salaam.